JUMATATU
WIKI YA 4 YA PASAKA
Somo: Mdo 11:1-18
Zab: 42:2-3; 43:3, 4
Injili: Yoh 10:1-10
Nukuu:
“Basi
mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa
Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu,” Mdo 11:1
“Sauti
ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe
najisi,” Mdo 11:9
“Ikawa
nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo,”
Mdo 11:15
“Basi
ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini
Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?” Mdo 11:17
“Yesu
aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la
kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo,”
Yoh 10:1-2
“Mimi
ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata
malisho,”Yoh 10:9
TAFAKARI:
“Wote tumeitwa kama tulivyo; Kristo ndiye Mlango.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Jumuiya ya kwanza ya Wakristo inaanza kukua na kuenea maeneo tofauti tofauti nje
ya Yerusalemu. Uwezo na Nguvu hizi unatoka na kazi ya Roho Mtakatifu Mwenyewe
ambaye jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo wamemridhia. Jumuiya ile ya Yerusalemu
inapigwa mshangao kuona hata watu wa mataifa wamelipokea nano la Mungu. “Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi
wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu,” Mdo
11:1. Ukweli ni kwamba, kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuunganisha sote kuwa kitu
kimoja mbele ya Mungu. Namna ya maisha yetu, mwelekeo wa kijiografia, na
ukabila, havina nafasi katika Kanisa la Mungu. Sote kwa Sakramenti ya ubatizo
tunafanywa wana wa Mungu, na warithi wa Ufalme wa Mungu. Ukweli huu unafunuliwa
kwa njia ya maono kupitia Mtume Petro. “Sauti
ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe
najisi,” Mdo 11:9. Vilivyoumbwa na Mungu na kutakaswa naye si najisi. Nasi
mbele za Mungu, kwa kuumbwa kwa sura na mfano wake, sote tunamastahili sawa.
Kwa mastahili haya
mbele za Mungu, hatuwezi kumwekea ukuta Roho Mtakatifu kuzitenda kazi zake.
Ukweli huu unamtokea Mtume Petro, na kusema, “Ikawa
nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo,”
Mdo 11:15. Hakuna mwenye hati miliki ya Roho Mtakatifu, bali tunapewa haki hiyo
kadiri Mungu apendavyo kugawa karama zake, na kadiri pia ya Roho Mtakatifu huyu
apendavyo. “Basi ikiwa Mwenyezi Mungu
amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi
ni nani niweze kumpinga Mungu?” Mdo 11:17
Pamoja
na nguvu hizi za Roho Mtakatifu, hatuwezi kutenganisha mahusiano haya na nafsi
nyingine katika umoja hasa ule wa kitendaji. Tunamwitaji Kristo ambaye ndiye
Mlango wa kwenda mbinguni. Kristo akiwa nafsi ya pili ya Mungu, katika utendaji
ndiye aliye mwokozi kwa kile kilichoanguka. Nafsi hii inapokuwa katika utendaji
haimaanishi kwamba kwa wakati huo nafsi nyingine hazifanyi kazi, yaani Mungu
Baba na Roho Mtakatifu. Ni vile vile Roho Mtakatifu katika utendaji,
uvitakatifuza vyote vilivyokombolewa na Kristo, na kwa namna hiyo hiyo nafsi
nyingine, yaani Mungu Baba, na Mungu Mwana hufanya kazi pamoja. Na ndiyo maana
Yesu anasema maneno haya, “Amin, amin,
nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea
penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.
Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo,” Yoh 10:1-2.
Kristo ndiye Mchungaji
wa kondoo na pia ndiye Mlango wenyewe. Kristo ndiye Mlango halisi wa kwenda
Mbinguni. “Basi Yesu aliwaambia tena, Amin,
amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo, Yoh 10:7. Anayempinga Kristo na
kutokufuata maagizo yake, ni kwa namna hiyo hiyo anajifungia mlango mwenyewe wa
kutokuiona Mbingu. Yesu anasema, “Mimi
ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata
malisho,”Yoh 10:9. Kukua kwetu kiroho kunategemea uhusiano wetu na Kristo, na
namno tunavyolishwa na neno lake. Ndugu yangu, malisho yako yako kwa nani?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mimi
ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata
malisho,”Yoh 10:9
Tusali:
Ee Yesu na Mchungaji wetu Mwema, tuonyeshe Mlango wako ili tusipotee. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario