ALHAMISI
WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo:
Mdo 5:27-33
Zab:
34:2, 9, 17-18, 19-20
Injili:
Yoh 3:31-36
Nukuu:
“Je! Hatukuwaamuru
ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza
Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu,” Mdo
5:28
“Petro
na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu,” Mdo 5:29
“Mtu
huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape
Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31
“Na
sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa
wote wamtiio,” Mdo 5:32
“Yeye
ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya
dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote,”
Yoh 3:31
“Yeye
aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli,” Yoh 3:33
“Amwaminiye Mwana
yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu
inamkalia,” Yoh 3:36
TAFAKARI:
“Maisha mapya ndani na katika Kristo ni kufanya naye agano la kudumu kwa
kutenda jambo jema kama shukrani ya upendo wake kwako maisha yako yote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
maisha ya ufufuko ni maisha mapya yenye mwono wa kiagano na yule aliyetufia kwa
sababu ya makosa yetu ili tuwe huru. Leo kwa namna ya pekee tutafakari neno
hili pamoja, “maisha mapya ndani na katika Kristo ni kufanya naye agano la
kudumu kwa kutenda jambo jema kama shukrani ya upendo wake kwako maisha yako
yote.” Mpendwa tunayesafiri wote katika tafakari hii, jumuiya ya kwanza ya
Wakristo, kama mwanzo wa maisha mapya ya ufufuko, waliweka agano la kudumu na
la milele kwa Kristo kama shukrani na upendo wao kwake.
Jambo hili halikuwatia
woga wala hofu kuusema ule ukweli walioushuhudia tangu wakati wa mafundisho
yake, mateso, kusulubiwa na ufufuko
wake. Pamoja na mateso wanayopata dhidi ya watesi wao, na makatazo juu ya jina
hili yenye nguvu la Yesu Kristo, bado hawakomi wala kushtushwa katika
kumuhubiri Kristo. “Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili?
Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu
ya mtu yule juu yetu,” Mdo 5:28. Vitusho hivi haviwababaisha kwa sababu jumuiya
hii na kila mmoja ndani ya jumuiya hii ya ufufuko, wanajua wazi ni nani wanaye
mtumikia. Naye Petro na Mitime
wakawajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu,” Mdo 5:29. Imani isipokuwa
na msingi mzuri na usio yumbishwa, haiwezi kudumu.
Yesu Kristo ndiyo
msingi wa Imani hii na yote wanayoyafanya kama jumuiya. “Jiwe walilolikataa
waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo
ni ajabu machoni petu.” Mt 21:44. Hili ndilo agano la kudumu la Wakristo wa
kwanza ndani na katika Kristo. Kristo ndiyo mwanzo na mwisho kwa kila kitu
wakifanyacho. Ujumbe huu na ukweli huu juu ya Kristo Mfufuka, Wakristo hawa wa
jumuiya ya kwanza hawaoni haya kuwaambia watesi wao. “Mtu
huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape
Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Fundisho wanalotoa kwa watesi
wao ni kwamba hata wao kama wanataka kupona na kutoka adhabu ya Mungu, yawapasa
kufanya toba ya kweli ili wapate msamaha wa dhambi zao. Mungu ni Upendo na
Huruma. Ni kwa sababu hiyo na ukweli huo juu ya Kristo, hawaachi kushuhudia na
kuhubiri habari zake. “Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na
Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio,” Mdo 5:32.
Ndugu yangu, shahidi ni
yule aliyeshuhudia jambo fulani kuwa kweli. Na ukweli huu anaujua vizuri na
yupo tayari kuuweka wazi kwa wengine ili wajue kweli hiyo. Kwa imani yetu na
kama tendo la shukrani kwa Kristo, kukubali kuwa shuhuda wa kweli ni kuingia
agano na Kristo, yaani kuyasadifu yale yote aliyoyafanya juu ya maisha yako.
Huku ni kuishi upya katika ufufuko.
Bila shaka hapo ulipo
sasa na maisha unayoishi ni agano fulani ambalo umelifanya kutokana na
utaratibu wa maisha fulani katika mapokeo fulani ya jamii kadiri ya mila na
desturi zake. Maisha hayo hayajalishi unaishi maisha ya kisakramenti kama
Sakrameti ya ndoa, Daraja Takatifu, au maisha ya Kiwakfu. Ingawa maisha hayo ni
maisha ya kimaagano na ni utaratibu ambao lengo lake kubwa ni kuiishi imani
iliyo ndani na katika Kristo, mtindo huo wa maisha ni sawa na chombo cha
kusafiria ili kufuka ng’ambo ya upande wa pili ambalo ndilo lengo msingi. Kufanya
agano la kuwa katika chombo hiki; iwe ni maisha ya ndoa, daraja Takatifu na
wakfu kama mtawa, haitoshi tu kama ilivyo. Kwa wewe kuwa mahali hapo tu kama
tendo la muda na wakati siyo ufufuko na utakatifu wenyewe. Yakupasa kufanya
zaidi ili kuleta umoja na utofauti hapo hapo ulipo, ikiwa ndicho kielelezo cha
kuupata utakatifu wako ambao ndio cheo chako cha kudumu.
Tukifanya jambo lile
lile kwa mtindo ule ule na mfanano ule ule mwisho wasiku tunapotesa hata ladha
ya kile tulichokifanyia agano kama hatua ya kwanza. “Maana mkiwapenda
wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi
hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zetu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa
mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:46-47. Yesu anakupa wewe na mimi
changamoto ya kufanya zaidi ya yale tunayoyafanya kadiri ya mfumo wa maisha
tuliyouchagua kuuishi. Agano hili ya pili ni kuzaliwa upya katika roho
Mtakatifu. Ni kuwa pale ulipofanya agano lako la kwanza, ila kufanya tofauti
zaidi na kwa kumpendaza zaidi Kristo kama shukrani ya upendo wake kwako.
Ni kufanya jambo jema
karidi ya uwezo na upendo usiojibakiza wala kujigawa. Kama unaishi katika
Sakramenti ya ndoa chagua kitu fulani kama tendo la upendo na lifanye tendo
hilo kila siku bila kukoma. Jambo hili mwisho wa siku huwa na sura mbili;
kwanza ni sadaka ya hiari na ya kumpendeza Mungu, na pili ni shukrani kwa
upendo huo wa Mungu juu ya maisha yako uliyo changua kuyaisha kama agano
msingi. Kwa upande wa maisha ya daraja Tatatifu na maisha ya wakfu, jambo hili
ni muhimu sana kufanya. Haitoshi mimi leo kuwa tu mtawa wa shirika la
Waagustino kwa kufuata taratibu za kishirika na kuziishi bila kuzivunja. Hii
haitoshi! Yanipasa kufanya kingine zaidi ndani ya maisha hayo hayo ya kitawa. Tendo hili linakuwa “fundamental Project of live,”
bila kupoteza umoja katika shirika. Umoja katika utofauti ndio uzuri wa Mungu,
na Mungu huonekana katika umoja na utofauti wetu kwani kila mmoja wetu amebeba
sura na mfano wake, Mwa 1:27.
Kuishi katika kweli hii niliyoisema ni kutambua
uhasili wa Yule tuliyejifungamanisha naye, yaani, Yesu Kristo. Maisha yako na
yangu bila Yesu Kristo hatutaweza kufanya chochote. Naye Yesu anatuambia kweli
hii waziwazi, “Mimi ni mzabibu; ninyi ni
matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi
ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Kwani mwisho wa siku siyo kuishi hapa duniani kwa muda wote, bali
maisha ya hapa duniani ni maandalizi tu ya maisha ya umilele. “Yeye ajaye kutoka juu,
huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena
mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote,” Yoh 3:31. Kuishi
ushuhuda huu katika umoja na utofauti wetu, ndiko kutiwa muhuri ikimaanisha
maisha mapya ya kiagano na Kristo yenye mwelekeo wa Kimungu na umilele. “Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia
muhuri ya kwamba Mungu ni kweli,” Yoh 3:33
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, maisha yenye uzima wa kweli ni kumwamini Mwana wa Mungu, kwani yeye ndiye
“njia, na kweli, na uzima; na mtu haji kwa Baba, ila kwa njia yake yaani Yesu
Kristo.” Yoh 14:6. Kama hatuna imani na jambo hili, hapo ulipo na maisha
unayoishi ni kama kukimbiza upepo tu. “Amwaminiye
Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya
Mungu inamkalia,” Yoh 3:36. Haya ndiyo maisha mpya ndani na katika Kristo,
ikiwa ni pamoja na kuingia agano naye kama shukrani kwa kile unachoikiishi na
kukishuhudia kila siku ya maisha yako.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Petro
na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Na sisi
tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote
wamtiio,” Mdo 5:29, 32
Ee Yesu Mshindi, tuwezeshe kutambua
kweli yako ndani ya maisha yetu ya kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario