sábado, 16 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA PASAKA YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 4 YA PASAKA YA MWAKA-C
MCHUNGAJI MWEMA

Somo I: Mdo 13:14, 43-52
Zab: 100:1-2, 3, 5
Somo II: Ufu7:9, 14b-17
Injili: Yoh 10:27-30
Nukuu:
Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu,” Mdo 13:43

Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana,” Mdo 13:45 

 “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao,” Ufu 7:9 

 “Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao,” Ufu 7:17
Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27 

Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28 

TAFAKARI: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya Pasaka ya Mwaka “C” wa Kanisa. Dominika hii ya nne kadiri ya Mpango wa Kiliturjia, na inavyojionyesha yenyewe katika tafakari nzima ya masomo ya leo, hujulikana kama “Dominika ya Mchungaji Mwema.” Yesu Kristo ndiye Mchungaji wetu Mwema kwani ni kwake tu kunaweza kuupata Uzima huo na kuufikia Umilele huo kama anavyosema,Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Hivyo kwa ukweli huu, sisi wenyewe bila Kristo Yesu hataweza kufanya lolote. Yesu anaweka bayana kweli hii anapojifananisha na Mzabibu. Naye anasema, Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Hivyo tunapoadhimisha Dominika hii ya Mchungaji mwema ni vyema kuelewa kweli hiyo kuhusu Yesu Kristo.

Yesu Kristo Mchungaji Mwema na Baba mwenye ukamilifu wa Ubaba wa Mungu Baba, ni kwake tu tunapoweza kupata ukamilifu wa Tumaini la kweli, Imani dhabiti, na Upendo wa kweli. Kwa mafundisho yake, kuishi kwake, na kuutoa uhai wake kwaajili yako na yangu angali hapa duniani, amethibitisha pasipo shaka yoyote hayo mambo makuu matatu: Imani, Tumaini, na Upendo. Mimi na wewe kila mmoja kadiri ya wito wake, vipaji vyake, na nafasi yake katika jamii husika anayoishi ni wajibu wangu kama Mkristo na Mfuasi wa Kristo kuishi kweli hii; “Kuwa Mchungaji Mwema kama alivyokuwa Kristo Yesu.” Kuwa kama Kristo-Mchungaji Mwema ni kuishi ukilenga Utukufu ukijua wazi kabla ya taji hilo la Utukufu kuna Msalaba. Huu ndio mwito wa somo letu la kwanza na la pili.

Wapendwa wana wa Mungu, kinachowatokea Paulo na Barnaba huko Perge hakina tofauti na kile kilichomtokea Yesu  huko Nazareti siku ya Sabato katika sinagogi alipopewa chuo cha Nabii Isaya na kulisoma neno ambalo ndilo lililokuwa mpango kazi wake hapa duniani, Lk 4:16-21. Yesu alitangaza mpango kazi waka na kusema, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:18-19, 21. Neno hili halikupokelewa kwa furaha, na hasa kwa Wayahudi waliokuwa na msimamo makali juu ya Masiha yule waliyekuwa wakimngoja. Fikra na mategemeo yao ilikuwa kuja kwa Masiha ambaye kwa kiasi kikubwa alibeba taswira ya kisiasa-kuwatoa katika utawala ule wa Kirumi.  Hivyo baada ya Yesu kuutoa mpango kazi wake, “Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho,” Lk 4:20. Kumkazia macho huku Yesu kulidhihirisha wazi hawakuwa tayari kuupokea ujumbe ule.

Mtume Paulo na Barnaba  huko Perge wanapatwa na maswahiba hayo hayo wakiwa kwenye sinagogi. Licha ya kwamba sinagogi lilifurika watu na kupokelewa vizuri na wenyeji (Mchanganyiko wa Wayahudi na wasio wayahudi), Wayahudi hawakufurahiswa na habari njema ile waliyoitangaza, Mdo 13:43. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana,” Mdo 13:45. Licha ya vurugu na vitisho hivi vya Wayahudi, Paulo na Barnaba waliutazama Utukufu uliokuwa mbele yao ilhali wakijua pia kuna Msalaba kama alama ya Ushindi. Ni kwa mantiki hii, Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa,” Mdo 13:46. Kwa tendo hili la Paulo na Barnaba wanatambua ni wajibu wao kufuata njia ile ya Mchungaji wetu Mwema-Yesu Kristo.

Kutokuupokea ujumbe huu wa habari njema kwa Wayahudi haikuwa sababu ya wao (Paulo na Barnaba) kukaa kimya. Hapa Paulo na Barnaba wanakumbuka na kutukumbusha pia mafundisho ya Yesu aliposema, Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule,” Mt 10:14-15. Na hiki ndicho kilichotokea baada ya Wayahudi wa Perge kukataa habari njema ya wokovu na kuleta ufitini juu ya Paulo na Barnaba: Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio,” Mdo 13:50-5. Hakika kumpiga teke chura siyo kukatiza safari yake bali kumwongezea mwendo! Na mti wenye matunda ndio upigwao mawe!

Hujuma wanazozipata Paulo na Barnaba zinakuwa chachu ya kusonga mbele na kulihubiri Neno la Uzima. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia,” Mdo 13:47. Agizo hili la kufikisha habari njema hata mwisho wa dunia ni kwa kila Mbatizwa. Na hii ndiyo ajenda mzito na mahususi Yesu aliyowaachia wanafunzi na Kanisa kwa upana wake kabla ya kupaa mbinguni akisema, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Ujumbe huu mahususi wa Ufalme wa Mungu, unaambatana na hukumu kwa Yule asiyeamini. Wajibu wangu na wako, yaani wewe uliyebatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake, ni kulihubiri na kuliishi neno la Mungu bila kukoma. Mwijili Mathayo kalihusisha tendo hili la kuhubiri neno na ufalme wa Mungu na Sakramenti ya Ubatizo. Maana yake, siyo tu kulihubiri neno la Mungu, bali na kuwavuta watu kwa Mungu na kuuonja upendo na furaha hiyo. "Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi" Mt 28:19-20. Paulo na Barnaba wanaitendea haki ajenda hii nzito na muhimu.

Wapendwa katika Kristo, “uzuri ni gharama, na penye utaratibu kuna akili.” Mimi na Wewe leo kwa kumwamini Kristo na kumfuata kila siku itukumbushe kuwa tumekombolewa kwa gharama kubwa sana-Damu ya Mwanakondoo, Yesu Kristo. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Ndugu yangu tunayesafari sote katika tafakari hii, ni wazi kwamba usichokijua thamani yake wakati mwingine ni vigumu kukithamini. Ni heshima kubwa sana tuliyopewa Mimi na Wewe kwa tendo la Yesu Kutufia pale Msalabani. Ni upendo mkubwa sana kwetu. Tendo hili kubwa na la upendo limeusadifu mwenendo mzima wa Yesu Mchungaji Mwema. Hivyo kuwa Mchungaji Mwema ni kwenda ndani kabisa ya maisha ya Kondoo zako kwa lengo la kuwainua na kuiona nuru ile uliyonayo. Kweli hii kaifanya Kristo Yesu pasipo shaka yoyote. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Hii ndiyo taswira ya Mchungaji Mwema ambaye kila Mbatizwa kadiri ya wito na maisha yake apaswa kuishi pale alipo. 

Mimi na Wewe tunapoishi hapa duniani kama sehemu ya maandalizi ya maisha ya umilele, na kuufia ukweli huu kama Kristo, tu mashahidi mbele ya Mwanakondoo katika maisha ya umilele naye Mbinguni. Huu ndio ufunuo wa Yohana kadiri ya somo letu la pili leo. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao,” Ufu 7:9. Hawa ndio wale watakao fahamika kwa mavazi yao meupe, yaani, utakatifu wao. Ni katika dhiki na taabu bila kupoteza Imani, Matumaini, na Upendo kwa ajili ya Kristo-Mwanakondoo aliye hai tunaoshwa kwa damu yake Takatifu na kuhesabiwa haki kama wateule wake na warithi wake. Yohana anaambiwa katika maono yale kwamba, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b 

Tunayo kazi moja tuu mara ya kuushinda ulimwengu huu, yaani, kumtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake. Hawa ndio wale watakao hesabiwa haki baada ya kuushinda ulimwengu huu. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao,” Ufu 7:15. Hali yetu ya kuchoka hatutakua nayo tena kwa sababu tutakuwa na miili tukuka na takatifuzwa. Hivyo walio na miili hiyo  Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote,” Ufu 7:16. Mchungaji wa kundi hili la watukuka na watakatifuzwa ni Mwana-Kondoo katika kiti chake cha enzi na cha Utukufu. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao,” Ufu 7:17. Ni raha iliyoje kuwa ndani na katika Kristo nyakati na majira yote licha ya taabu na dhiki tunazokutana nazo kila siku?

Wapendwa wana wa Mungu, furaha tunayoitegemea kutoka kwa Kristo ni tokeo la kuisikia sauti yake. Zipo sauti nyingi sana tuzisikiazo kila mmoja kadiri ya wito na mazingira yake. Ni mara ngapi umekatishwa tamaa hapo ulipo kwa kusikiliza sauti nyingine na siyo ya Kristo Mchunguji wetu Mwema? Yesu anakuambia leo wewe na mimi, kwamba, Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata,” Yoh 10:27. Je, unaiheshimu sauti yako ya ndani, yaani, dhamiri yako njema? Dhamiri njema ndiyo mwito wa Yesu pia ndani yako. Dhamiri hii njema utuongoza kwa yaliyomema (kuyatenda) ili kuifikia ile mede ya dhahabu-uzima wa milele katika Kristo Yesu, Flp 3:14. Hivyo, Kristo tu ndiye mwenye uwezo wa kutupatia uzima huo wa milele. Naye anasema,  Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28. Bila Kristo usalama wetu upo matatani. Ila ndani na katika Kristo tunauhakika wa kila kitu na hatuna cha kupoteza.

Ndugu yangu, yale yote yanayokupa matumaini hapa duniani kwayo bila Kristo hayana umilele. Yesu anatupa hakikisho la matumaini ya kweli na kusema, Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja,” Yoh 10:29-30. Ndugu yangu, vyote uvionavyo na usivyoviona kwa macho haya ya kibinadamu vipo kama vilivyo kwa sababu ya Neno, yaani Yesu Kristo. “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Ndugu yangu, kilicho chako na mali yako ni kipi zaidi ya dhambi zako?

Padre Joseph Nalia na Mungu baada ya upadirisho wake alitumwa na Askofu wake uchungaji eneo la wafugaji. Mazingira ya eneo lile yalikuwa makame sana. Mifugo ilikuwa mingi ukilinganisha na idadi ya watu. Hata hivyo watu walionekana wanyonge na wadhaifu sana licha ya wingi wa ng’ombe, kondoo na mbuzi walikuwa nao.

Padre Nalia na Mungu Joseph, alihuzunishwa sana na hali za waamini wake, na hasa kutokufika Kanisani kusali na kupata Katekesi ya kina. Alipofanya tafakari kwa nini waamini wake wapo kama walivyo, lilimjia wazo la kuwatembelea na kujua hali zao. Padre Joseph alianza kutembelea kaya baada ya kaya. Baada ya mwaka mmoja kutokana na ukubwa wa Parokia ile alifanikiwa kuwatembelea waamini wake wote.

Padre Joseph Nalia na Mungu alijifunza mambo mengi sana. Baadhi ya mambo hayo ni kama haya yafuatayo:

Moja, wengi wa waamini wake wanakosa muda wa kufika Kanisani kwa katekesi na Misa kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta malisho ya mifungo yao.

Pili, aligundua familia nyingi ni dhaifu kiafya kutokana na kutokula mlo kamili, na mara nyingine kula mlo mmoja tu kwa siku.

Tatu, Padre Nalia na Mungu aligundua ukame ule kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na wingi wa mifugo.

Nne, wingi wa mifugo ile haukuweza kubadili hali za maisha ya waamini wake: Kimwili na Kiroho. Ili kuwa ni sehemu ya sifa tu kwa mtu kuwa na ng’ombe nyingi na kumfanya kuwa na uwezo wa kuoa wanawake wengi.

Na tano, Padre Joseph aligundua kwamba karibia asilimia 96 ya waamini wake ni washirikina na wenye kuamini imani potofu.

Kwa kutambua matatizo hayo Padre Joseph alifanya yafuatayo: Kwanza aliongea na viongozi wa vijiji vyote vya Parokia ile na kuwaomba wawakutanishe watu wao wote siku ya jumamosi kwani kutakuwa na mganga maarufu. Kwa vile waliamini sana ushirikina hakuna aliyekosa kikao kile.

Wakiwa wamekwisha kupanga yote na Mseminari aliyekuja Parokiani pale kwa uchungaji namna watakavyofanya, Mseminari yule alijitambulisha kwenye kikao kile kama yeye ndiye Mganga Mashuhuri-“Mti Mkavu.” Lengo la ujio wake ni kutengeneza mvua ili kusiwe tena na tatizo la majani kwa ajili ya mifungo.

Basi Mseminari yule akiwa amevalia mavazi ya kutisha na sasa kama Mganga Mti Mkavu, alitabiri huku akitoa sauti ya kutisha, “vijiji hivi vinamatatizo sana kwa sababu mmekwenda kinyume na mizimu ya Mababu zenu. Kurudisha amani katika vijiji hivi kuanzia sana kila familia lazima itoe ng’ombe wasiopungua 10, na mbuzi wasiopungua 15. Ng’ombe na mbuzi hawa watakuwa wanachinjwa kutokana na mahitaji ya kila kijiji. Ngozi za wanyama hao zitawambwa na kutengeneza wigo kubwa ili kupunguza kasi ya upepo kwa sababu kwenye upepo huo ndiko kwenye mizumu hiyo inayoleta fujo.”

Watu wote walikaa kimya kwa hofu juu ya utabiri ule. Hivyo siku iliyofuata ng’ombe na mbuzi waliletwa parokiani pale kwa wingi. Kila kijiji kiliteua wazee watano kwa ajili ya kuchinja na kugawa nyama kwa kila kaya. Baada ya miezi mitatu afya za watu zilibadilika. Na baada ya miezi mitatu baadaye, idadi kubwa ya mifugo ilipungua na kuwafanya wakazi wale kutumia muda mwingine kwa kazi za kilimo kilichozunguka maeneo yao. Kwa vile ilikuwa kipindi cha kilimo, mvua zilianza kunyesha na hali ilibadilika.

Watoto na baadhi ya watu wazima walipata muda wa kwenda mafundisho na hata kuudhuria misa kila jumapili kwa sababu kila familia ilikuwa  na mifugo michache. Padre Joseph aliwaleta wataalam wa kilimo na kutoa elimu kuhusu kilimo cha kisasa na ufugaji wa kisasa. Baada ya miaka mitatu mambo yalibadilika kabisa. Afya za watu zilikua nzuri, na wengi waliachana na Imani potofu kwa katekesi ile aliyoitoa Padre Nalia na Mungu ya nyumba kwa nyumba.

Ndugu yangu, tujifunze kwa Padre Joseph Nalia na Mungu. Nawe pia ni Mchungaji mwema pale ulipo kadiri ya wito wako na mazingira yako ya kazi.

Tumsifu Yesu Kristo!

Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh 10:28


Tusali:-Ee Yesu Mchungaji wetu Mwema, tujalie Neema ya kutumika bila kujibakiza kila mmoja kadiri ya wito wake ili Wewe uonekane kwa kila tutakaye muhudumia kama Baba na Mchungaji mwema ukiwa Wewe ndiye kielelezo chetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario