sábado, 23 de abril de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU MARKO MWINJILI

SIKUKUU YA MWINJILI MARKO
25/4
Somo: 1Pet 5:5b-14
Zab: 89:2-3, 6-7, 16-17
Injili: Mk 16:15-20
Nukuu:
“Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5b

Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8

Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu,” 1Pet 5:10

Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16

Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18

TAFAKARI: “Unyenyekevu wa kweli katika kuhudumiana; kumwona Kristo kwa wote tunaokutana nao.”

Wapendwa wana wa Mungu, fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Neno hili unyenyekevu si geni kwetu na hata masikioni mwetu. Vipo viashirio vingi vinavyothibitisha unyenyekevu wa mtu. Leo kwa namna ya pekee na tunapoungana na Kanisa zima tukisheherekea Sikukuu ya Marko Mwinjili, tulitafakari neno hili kwa pamoja. “Unyenyekevu wa kweli katika kuhudumiana; kumwona Kristo kwa wote tunaokutana nao.” Viashirio vya mnyenyekevu wa kweli kabla ya yote, ni ile hali ya kujipokea na kujikubali katika mapungufu uliyonayo. Ni kweli kabisa hakuna binadamu aliyekamilika katika yote. Ila kutambua mapungufu yako na mazuri yako ni hatua ya msingi sana ya kusonga mbele kwa kuanza kuyarekebisha yale mapungufu. Tusipokuwa tayari kukiondoa kinyago hiki tunachojivika ambacho si chetu, maisha yote ya mtu hubakia katika hali ya vita ya ndani dhidi ya uhalisia wake, na mwisho tunakuwa washindwa wa kila kitu.

Jambo lingine la msingi kuelekea maisha ya unyenyekevu ni kuwa tayari kusikiliza zaidi ya kuongea. Binadamu licha ya kufanya tafakari ya kina ya maisha yake binafsi, kwa tendo hilo tu la tafakari halitoshi kujijua katika maana ya mizania ya kweli. Mtu mwingine nje yako na anayeona katika uhalisia wa vitu kama vilivyo, huwa msaada mkubwa sana katika ukamilisho wako, hasa pale anapokuambia kile kilicho cha kweli. Ukweli huu mara nyingi ni vigumu kuupokea kwa sababu utuanika kile ambacho hatupendi kukiona na hata kukusikia kuhusu undani wa maisha yetu. Hiki usichopenda kukiona na wala kukisikia ndicho kile ulicho. Utafaidika tu katika jambo hili kama utakuwa tayari kusikiliza. Hii ni moja ya hatua kubwa sana ya kukua kiroho ambayo itakufanya uwe kile ulicho na makusudi mazima ya uumbaji wako.

Ni mtu mwenye kiburi tu asiyekuwa tayari kupokea ukweli ulio ndani mwake. Ni hali ya kawaida mtu kupenda uzuri ulionje yake, na hivyo kupoteza uhalisia wake kwa kuyatamani yaliyo kwa wengine. Hali hii hutufanya kuwa vivuli vya wengine na kupoteza uhalisia wetu na upekee wetu. Mungu hupenda tuwe kile alichokusudia tuwe kwa sura na mfano wake. Uzuri na utofauti huu tulio nao ndiyo furaha na uzuri wa Mungu na ndiyo anavyotaka tuwe wawakilishi wake popote pale tulipo katika maisha yetu yote. Tunapokuwa kile tulicho kadiri ya makusudi yake ya uumbaji wetu tunamwakwakilisha vizuri Mungu. Mtume Petro anatuambia, “Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5b. Tunapojifungamanisha na unyenyekevu, tunakuwa sababu na makusudi ya kweli katika kutoa huduma isiyo na mawaa, na katika tendo hili la huduma kadiri ya wito na vipaji vyetu, tunajazwa neema zaidi na zaidi. Hakuna aliyefilisika kwa kumrudishia Mungu kilichochake, na kwa namna hiyo hakuna aliyekosa neema kwa kufanya yaliyo ya Mungu.

Ndugu yangu, ukifanikiwa katika hatua hii muhimu  ya pili niliyokwisha isema, utaingia hatua ya tatu ambayo ni muhimu sana katika utume wako. Hatua hii ya tatu itakufanya umwone Kristo kwa kila utakaye kutana naye na kumuhudumia. Tunao kutana nao katika  huduma zetu hawana sura moja tu na yenye kupendeza. Wapo wenye furaha na wasio na furaha, wapo wagonjwa na wenye afya, wapo walio huru na wasio huru, wapo watana shati na walio uchi, wapo walioshina na wasio na chakula, wapo walio na makazi na wasio na pakuegemeza vichwa vyao. Sura hizi na mtazamo huu wa mahangaiko ni Kristo utakayekutana naye kila siku katika utume wako.

Yeyote kati yetu atakaye mrudishia Mungu kilichochake na kupata neema za kufanya zaidi na zaidi, kwa tendo hili ni chukizo kwa yule mwovu na mtumikia mwovu. Hivyo yatupasa daima kuwa tayari dhidi ya mashambulizi ya kiroho. Kunapokuwa na mwanga, giza ujitenga, hivyo kivuli cha mwanga hakiondoki licha ya kwamba hatukioni. Ninachomaanisha hapa ni kwamba, kinyume cha mwanga ni giza, na kinyume cha giza ni mwanga. Hii ndiyo maana ya vita vya kiroho. Na hivyo Mtume Petro anasema,Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8. Hii ni changamoto kubwa sana ya kukua katika maisha ya kiroho. Je, mbele ya vita hivi vya kiroho kuna nini?

Wapendwa, ushindi wa vita hivi vya kiroho ni kuingia katika utukufu wa milele katika Kristo. Kwa maana nyingine hatutaweza kushinda vita hivi kama hatupo na Kristo na ndani ya Kristo. Na kushinda huku si kwa nguvu zetu wenyewe au jeuri na ustadi wetu katika vita, bali ni kwa neema za Mungu, ambazo tunajaliwa naye Kristo. Hivyo, Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu,” 1Pet 5:10. Tunathibitishwa au kwa maana nyingine tunahesabiwa haki si kwa matendo yetu mema tu, bali kwa neema ya Kristo mwenyewe. Tunatiwa nguvu si kwa mastahili yetu na mwono wetu, bali kwa kuyafanya yale yaliyo makusudi ya Mungu kadiri ya wito na vipaji vyetu ambavyo ni mali yake mwenyewe.

Ndugu yangu, unyenyekevu kwa upande wetu ikiwa ndiyo msingi wa mambo yote, na neema kutoka kwa Mungu, vitatuwezesha kutenda maagizo haya muhumu kwa ambayo ni agizo kwa kila mbatizwa, yaani: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Kwa vile kile tulicho ndicho tukiaminicho na kukiishi kadiri ya makusudi ya Mungu katika uumbaji wetu, ni kwa namna hiyo kile tusemacha kwa watu na kukihubiri katika kweli kitakavyokuwa hukumu ya kweli.

Mtazamo huu wa kweli katika Imani, huambatana na ishaza za kimungu. Ishara hizi ni uthibitisho wa yale tunayoyaamini na kuyatenda kwamba si kwa nguvu zetu na akili zetu,  bali ni Mungu mwenyewe ayatendaye hayo kwa vyombo vyake vya udongo ili atambulike kupitia vyombo hivyo. Na hivyo Yesu anawaambia mitume wake, Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18. Ujumbe huu na wosia huu wa mwisho wa Kristo, ndilo agizo la kila Mbatizwa.

Wapendwa wana wa Mungu, leo tunaposheherekea sikukuu hii ya Mwiinjili Marko tufanye tafiti moyo juu ya unyenyekevu wetu, na matendo yetu tuyafanyayo kila mmoja kadiri ya wito wake na vitaji vyake. Kama hakuna uhusiano wa ukweli huu, usione aibu kurudi nyumbani na kuchukua tochi, kuliko kuendelea na safari yako ndefu katika kiza kinene ambacho hujui kilichopo mbele ya safari hiyo. Nyumbani kwako kuliko na tochi hiyo ni ile hali ya kujinyenyekeza, ili uhesabiwe haki kwa kujazwa neema za kufanya zaidi na zaidi kama tunavyomsheherekea Mwiinjili Marko.

Tumsifu Yesu Kristo!

Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16


Tusali:-Ee Yesu, tujalie unyenyekevu katika kweli yako, ili tuweze kuishi kile tulicho kadiri ya wito na vipaji vyetu vilivyo mali yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario