JUMATANO
WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 8:1-8
Zab: 66:1-3a, 4-5, 6-7a
Injili: Yoh 6:35-40
Nukuu:
“Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika
Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao
mitume,” Mdo 8:1
“Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko
wakilihubiri neno,” Mdo 8:4
“Kwa
maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na
watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa,” Mdo 8:7
“Lakini
naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini,” Yoh 6:36
“Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,”
Yoh 6:37
“Na
mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze
hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 6:39
TAFAKARI:
“Kwa Yesu Kristo kuna uzima na ufufuo siku ya mwisho; Je, umewekeza wapi maisha
yako?”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni kweli pasipo shaka yoyote kwamba kila mmoja wetu kuna kitu ambacho
kinaongoza na kuyasukuma maisha yake. Kitu hicho ndiyo dira na sababu ya mtu
kufanya afanyavyo na kuishi aishivyo. Msukumo huo ndiyo unaotufanya kama
tulivyo. Msukumo huyo ndio unaotupa furaha na matumaini kwa yale
tunayoyatarajia. Msukumo huo wa maisha ndio unaotupa moyo wa kuendelea kufanya
tunayoyafanya. Na kwa upende mwingine, msukumo huo wa maisha huwa sababu ya
huzuni yetu ya kudumu.
Hivyo ndugu yangu
tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, kwa namna ya pekee leo tulitafakari
neno hili, “Kwa Yesu Kristo kuna uzima na ufufuo siku ya mwisho; Je, umewekeza
wapi maisha yako?” Mtume Paulo anasema jambo hili kuonyesha kile kinachosukuma
maisha yake. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu
Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Huu ndiyo msukumo
sahihi wa maisha yetu ya ufufuko, maisha mapya na Kristo. Ni maisha ya
kuutafuta ufalmwe wa Mungu kwa yale yote tuyafanyayo. Ni kumwona Kristo kwa
kila unayekutana naye, ishi naye, na kuwajibika kwako kwao kadiri ya wito wako,
nafasi yako, na vipaji na uwezo aliokujalia Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu,
msukumo huu wa maisha ndiyo sababu ya kifo dini na shahidi cha Stefano. Jumuiya
ya kwanza ya Wakristo inahujumiwa na Sauli na kutawanyika. Mitume wakisukumwa
na Kristo aliye sababu ya maisha yao, na Roho Mtakatifu, wanabaki Yerusalemu
wakitoa ushuhuda wa Kristo hadi toni la mwisho licha ya machafuko yaliyotokea
kwa sababu ya kifo cha Shahidi Stefano. “Siku
ile kukatukia adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote
wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao Mitume,” Mdo
8:1. Hata wale waliotawanyika kutokana na hujuma hii, hawakukoma kulitangaza na
kulihubiri jina hili lililopita majina yote, Yesu Kristo Mnazareti. “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko
wakilihubiri neno,” Mdo 8:4. Miongoni mwa
watu hawa ni Filipo.
Filipo analihubiri
Jina la Yesu na wengi wanaona mwanga, kweli, na uzima kwa kuponywa na kuwa
huru. “Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao,
wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa,” Mdo
8:7. Haya ndiyo mambo makuu ya Mungu kwa wale wanao mwamini na kumtegemea. Haya
ndiyo mambo makuu Mungu huyafanya kwa wale wasiokuwa na shaka naye na uwezo
wake. Mungu huyatenda makuu hayo kwa wale wasiokatishwa tamaa na vipingamizi
dhidi ya kile wanachoamini.
Wapendwa
katika Kristo, ndani na katika Kristo kuna uzima na ufufuo siku ya mwisho.
Maisha ya kweli na Kristo, ndiyo njia sahihi ya kuufikia umilele ambao ndiyo
makusudi ya uumbaji wetu. Kazi kubwa ya Kristo ni kuhakikisha walio mridhia
hawapotei hata mmoja. Ulizi ndani ya Kristo ni salama kuliko linzi nyingine
zote unazoweza kufikiria. Ni ulinzi, si tu katika usalama wa miili yetu na mali
zetu, ila roho zetu katika hali ya ufufuo na uzima wa milele. Naye Yesu
anatuhakikishia jambo hili na kusema, “Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,”
Yoh 6:37. Ndugu yangu maisha yako umeyawekeza
kwa nani? Je, kwenye utajiri wako? Je, kwa marafiki zako? Je, akili na ujanja
wako? Je, katika maisha yako ya kijanja kijanja? Je, kwenye kadi zako za benk
ya “life security?” Yote hayo utayaacha na kuondoka na Roho yako tu. Je, mbele
ya Mungu utajitetea na nini? Njia salama ni kuwekeza kwa Kristo kupitia Benk
yake-“ROHO YAKO”
Mpendwa tuliyeanza safari hii ya
tafakari pamoja upoooo? Hivi unajua mapenzi ya Mungu kupitia mwanaye Yesu
Kristo? Ndugu yangu, mapenzi yake Mungu kwako kupitia mwanaye Mpenzi ni
kukupatia uzima wa milele na ufufuo siku ya mwisho bure. Nasema bure kwa sababu
huitajiki kuununu ila kuuridhia kila siku ya maisha yako. Naye Yesu anasema, “Na mapenzi yake
aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja,
bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 6:39.
Ndugu yangu kabla
sijakuacha, jaribu kuchunguza jambo hili. Je, ni kitu gani kwa siku kinachukua
muda mwingi kwako? Kitu hicho ndicho kinachochukua uhai wako, na mwisho wa siku
ndicho kitakachokuwa hatima ya maisha yako. Kitu hicho ndicho kibebacho Imani
yako mbele ya Mungu. Swali la kujiuliza ni hili; Je, kitu hicho kinauhusiano
wowote wa karibu na Kristo? Kama hakina, umejipanga vipi kujibu maswali haya
mawili mbele ya Mungu: Swali la kwanza:-Umefanya nini na upendo wa Mwanangu
Mpenzi Yesu Kristo aliyekufa kifo cha aibu pale Msalabani kwa ajili yako? Na
swali la pili na la mwisho: Umefanya nini na vipaji nilivyokupa bure? Yesu
Kristo anasema hivi, “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila
amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua
siku ya mwisho,”Yoh 6:40. Kristo keshafanya nafasi yake, wewe na mimi je?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,”
Yoh 6:37
Ee Yesu uliye yote katika yote,
yatengeneze maisha yangu kadiri ya msukumo wako kila siku kwa kila nifanyacho.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario