JUMANNE
YA WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo:
Mdo 4:32-37
Zab:
93: 1ab, 1cd-2, 5
Injili:
Yoh 3:7b-15
Nukuu:
“Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja
na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho
ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika,” Mdo 4:32
“Wala
hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote
waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile
vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa
mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji,” Mdo 4:34-35
“Amin, amin, nakuambia
kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala
ushuhuda wetu hamwukubali.” Yoh 3:11
“Wala
hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana
wa Adamu,” Yoh 3:13
“Na
kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu
hana budi kuinuliwa; ili kila mtu
aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye,” Yoh 3:14-15
TAFAKARI:
“Jumuiya yenye moyo moja na roho moja, husafiri pamoja na hutoa shuhuda
iliyokweli kweli daima.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni kweli iliyo wazi kwamba mafanikio ya jumuiya ya kwanza za Wakristo
yalijijenga katika msingi wa upendo wa kindugu ulio wa wazi, na malengo yaliyo
wazi na kweli kumwelekea Mungu. Jambo hili liliwafanya kushuhudia kweli kwani
maisha yao yaliakisi maisha ya jumuiya yaliyo halisi.
Moyo mmoja na roho moja
katika maisha ya jumuiya yoyote ile, ubebwa na mizania ya uaminifu na uwazi.
Kunapokuwa na uwazi na uaminifu, hata mali aliyokuwa nayo mtu, haiwezi kuwa
kikwazo katika kushirikishana. Undugu ulio wa kweli na wawazi hujengwa kwa
uaminifu na upendo wa kweli. Undugu huu huwa imara kuliko ule wa kuzaliwa.
Undugu wa kuzaliwa hukosa mshikamano kwa kuingiliwa na mazoea ya kujihesabia
haki. Ila endapo undugu huu wa kuzaliwa ukizingatia ukweli ulio uwazi,
mshikamano wa kweli, na uaminifu, undugu huu huwa imara sana. Kwa bahati mbaya
uzoefu waonyesha mambo hayawi hivyo, kwa sababu tu ya kujihesabia haki kama
mwanafamilia.
Umoja huu ujenga
ushirika wa kudumu na wenye nia moja. “Na
jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja
aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali
walikuwa na vitu vyote shirika,” Mdo 4:32. Ni katika mtazamo huu na uelewa huu,
Mt. Augustino anaijenga jumuiya yake ya kitawa kwa mfano wa jumuiya ya kwanza
ya Wakristo. Undugu huu wa Kiagustino umedumu hadi sasa.
Ndugu
yangu, umoja wa moyo mmoja na roho moja, uliondoa ubinafsi wa kujilimbikizia
mali kwani aliyeitaji alipata kadiri ya mahitaji yake. Na wale ambao walijiunga
katika jumuiya hii yenye kushirikishana mambo ya kimwili na kiroho, walijisikia
furaha na kumshuhudia Mungu wa kweli. Mungu huyu alionekana kwa kila kitu walichofanya,
na kwa kila kitu walichoshirikishana. Kwa mantiki hii, “wala
hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote
waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile
vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa
mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji,” Mdo 4:34-35.
Msimamo
huu, na dira hii ya maisha, iliwafanya wanajumuiya hii kuwa kitu kimoja na hasa
katika swala la ushuhuda. Hakuna aliyejibwatukia lililo lake. Kila kilichosemwa
kilisemwa na kuongozwa na Roho wa Bwana. Utulivu huu na mwelekeo huu wa
kimtazamo uliwafanya wanajumuiya wajue ni nani mwenye mamlaka ya kweli na
wakufikika kwa urahisi. Mitume walikuwa viongozi na waelekezaji wa ushuhuda
ulio kweli. Kitu hiki kilionekana wazi kwa wale waliokuwa chini yao. Hivyo vitu
vyote vilikuwa chini ya uongozi na usimamizi wa mitumu, Mdo 4:35.
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna aliyejiona bora kuliko mwingine, na wala muhimu kuliko
mwingine. Kila mmoja alijitoa kwa ajili ya jumuiya na maendeleo ya jumuiya. Uzuri
au ubora wa mtu ulikuwa ni ufunuo wa uzuri wa Mungu na uumbaji wake.
Tunachojifunza hapa ni kwamba, uzuri, utajiri, hekima, akili, na vipaji
vilionekana na ndivyo ilivyo, kwamba ni ufunuo wa Mungu na uzuri wake kwa vile
alivyoviumba. Kwa maana nyingine, mali yetu halali ni dhambi zetu, ambazo mara
tunapotambua udhaifu na mapungufu haya, yatupasa kupatanishwa na Mungu. Tendo
hili kwa Mkristo yeyote wenye hofu ya Mungu, ni tendo la kufanya kila mara
tukitambua kwamba Neema na Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.
Wapendwa
katika Kristo, kutokuishi kweli hii kama Wakristo, bado hatujamfahamu Kristo,
na kama tunamfahamu kwa kuzaliwa katika familia ya wakristo, basi bado tupo
kwenye mazoea na tunayo safari ndefu kiimani kweli ambayo itatuweka huru, Yoh
8:32, 36. Kwa naana hiyo hatuwezi kuyasema maneno haya ya Yesu, “Lile
tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu
hamwukubali.” Yoh 3:11. Kama hatumjui vizuri Kristo twawezaje kumshuhudia?
Yawezekana hatuna uwezo wa kuyasema kwa ufasaha, je maisha yetu yanafunua
ukweli huu wa Kristo ndani yetu? Ni changamoto kubwa!
Wapendwa, tukimjua
Kristo na kufuata mafundisho yake, tutafunuliwa yale ya mbinguni kwani yeye
anayajua kwa sababu ametoka huko na Baba anamfunulia nyakati zote. “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye
aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu,” Yoh 3:13. Kufahamu ukweli
huu, ni tendo la kuwa tayari kila siku wanafunzi wa Kristo, yaani kujifunza
kusiko kuwa na kikomo. Mtume Paulo anasema, “ndugu, sijidhanii nafsi yangu
kwamba nimekwisha kushika; ila natenda nena moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma,
nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya
mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu,” Flp 3:13-14. Kweli juu ya Kristo ni
maisha mazima ya kila siku ya Mkristo, yakiambatana na tafakari juu ya yote
tunayokutana nayo katika maisha ikiwa ni pamoja na majaribu yake. Kumbe hata
katika majaribu yetu ya maisha tunafunuliwa ukweli ambao Mungu anataka tuujue
ili nasi kesho tuwe walimu kwa wale watakao kuwa na mahangaiko na mateso kama
yetu. Majaribu hutufanya kukua na kukomaa kiimani. Tusitangulize lawama na
malalamiko hata mara moja; “kwa nini mimi haya yanatokea kwangu,” bali
tujiulize Mungu anataka kunifundisha nini katika majaribu haya.
Tunapokubali majaribu
tuyapatayo huwa tunafunuliwa kweli iliyo juu ya upeo wetu kama binadamu. Tendo
hili kama binadamu utuwezesha kuinuliwa kama Kristo alivyoinuliwa msalabani na
kuuvaa Utukufu uliotukuka. “Na kama vile
Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi
kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye
awe na uzima wa milele katika yeye,” Yoh 3:14-15. Ndugu yangu tendo hili ni la
Imani na lina uzima ndani yake. Kwa maana nyingine, tuyapokeapo majaribu yetu
na mateso yetu kwa mwono wa Mungu, huwa ni furaha kwa sababu tunajua sababu ya
mateso hayo. “Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo
hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo,” 2Kor 1:5. Je, yale utesekayo
bila kujua chanzo chake unayapa tafsiri gani katika maisha yako?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile
tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu
hamwukubali.” Yoh 3:11
Ee Yesu Mwema, nifanye mara zote kuona
maana ya mateso na mahangaiko yangu katika mtazamo wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario