ALHAMISI
WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 8:26-40
Zab:
66:8-9, 16-17, 20
Injili: Yoh 6:44-52
Nukuu:
“Tazama,
maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?,”
Mdo 8:36b
“Filipo
akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya
kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu,” Mdo 8:37
“Kisha,
walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi
asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi,” Mdo 8:39
“Hakuna
mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku
ya mwisho,” Yoh 6:44
“Mimi
ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula
hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya
uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51
TAFAKARI:
“Kwa nini nashindwa kukata shauri kuhusu maisha yangu?”
Wapendwa wana wa Mungu,
kuna msemo wa kiswahili usemao, ‘kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi.’ Msemo
huu unaendana na somo letu la leo, na kile kilichotokea Jerusalemu baada ya
kifo cha Shahidi Stefano. Jumuiya ya kwanza ilitawanjika sehemu mbalimbali,
huku ikimbeba Kristo kwa kila walichokuwa wakikifanya. Hivyo tunaona Mtume
Filipo akihubiri na mara hii akikutana na Towashi mmoja aliyekuwa amekwenda
Yerusalemu kuabudu. Bila shaka kwa namna alivyokuwa Towashi huyu alikuwa tayari
ameandaliwa na Mungu mwenyewe kwa tukio ambalo Filipo atalifanya, kama Yesu
anavyosema kwenye Injili ya leo, “Hakuna
mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku
ya mwisho,” Yoh 6:44. Ukweli ni kwamba, Filipo anamkuta Towashi huyu akisoma
chuo cha Nabii Isaya.
Baada ya mazungumzano
na kuhubiriwa kuhusu Kristo, Towashi anafikia hatua ya kukata shauri na
kuachana na maisha ya zamani na kuanza maisha mapya, na kusema, “Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia
nisibatizwe?,” Mdo 8:36b. Mpendwa
tunayesafiri wote katika tafakari hii, hakuna mtihani mgumu kwa binadamu kama
“kufanya maamuzi” na hasa maamuzi ya maisha mapya na yenye mtazamo mpya. Wengi
wetu mtihani huu umetushinda na tumebakia kudhani kwamba maisha yetu
yamelaaniwa. Kukata shauri ni hatua ya kwanza ya kukua katika maisha ya kawaida
na hasa ya kiroho.
Kukata shauri huku
kunanikumbusha rafiki yangu mmoja aliyekuwa mtaratibu sana na mwenye kuipenda
familia yake. Ila mambo hubadilika mara anapokunywa pombe. Jambo hili lilikuwa
kero sana kwa mke wake, na kila lilipotokea basi nilikuwa msuluhishi. Mara zote
jamaa huyu alikiri kuwa alifanya makosa na hivyo kuamua kuacha kunywa pombe.
Baada ya muda kama miezi
miwili mitatu hivi, jambo hili lilijirudia tena. Na mara hii nilimwuliza;
Rafiki, tatizo lipo wapi mbona unarudia kulekule ulipoamua kutokurudi? “Father,
tatizo lipo hapo, ‘naomba unisaidie. Ingewezekana kuyatoa mabango yote huko
barabarani yenye tangazo ya “KILI TIME,” ingenisaidia kuacha pombe. Ninapoliona
tangazo hili, ujue bar ifuatayo lazima niingia na kusaka kinywaji hicho kwa
uvumbi na uvumba,” Rafiki yangu alinijibu kwa upole wa hali ya juu.
Wapendwa wana wa
Mungu, mtakubaliana na mimi kwamba mabango yalioko huko barabarani hayana
tatizo. Tatizo kubwa lipo pale tunaposhindwa kufanya maamuzi ya kina na kuanza
maisha mapya kama kweli tunataka mabadiliko. Towashi baada ya kuyaona maji
aliamua kubatizwa. Filipo anamwambia, “ukiamini
kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu
Kristo ndiye Mwana wa Mungu,” Mdo 8:37. Ndugu yangu kwa nini unashindwa kukata
shauri na kuanza maisha mapya kwa kuamini utaweza ndani na katika Kristo Yesu?
Yapo mambo mengi ya kujikatalia ili ukue mwili na roho. Hapa hakuna jambo kubwa
wala dogo kama kwa kiasi fulani linakwamisha kukua kwako kimwili na kiroho.
Yawezekana, unaishi uchumba sugu, na hivyo kutoshiriki masakramenti. Uchumba
siyo ndoa! Kata shauri na anza maisha mapya. Siku hizi ukipenda na kuamua
kufunga ndoa unaweza hasa zile misa za alfajiri na baada ya tukio hilo
ukaendelea na shughuli zako za kila siku. Achana na ndoa za matarumbeta na
mbwembwe zisizo na maana. Ndoa nyingi zenye mbwembwe huishia mtindo huo huo wa
mbwembwe.
Baada
ya kazi hii muhimu aliyoifanya Filipo, Roho wa Bwana anamnyanyua na kumpeleka
mahali pengine kwa kazi yake. “Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana
akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi,”
Mdo 8:39. Nasi tunaotoa huduma za kiroho katika vituo tulivyopangiwa
tunakumbushwa hapa kwamba, tukishafanya yale tuliyotakiwa kufanya kama
watumishi, tusianze kujenga viota. Tuache viota hivyo na kwenda sehemu nyingine
mara tunapoamuriwa kufanya hivyo. Wengi pia wameshindwa mtihani huu kwa kukosa
uti kwa Roho Mtakatifu na wale waliotuweka kwenye tume hizo-Wahudumu wetu wakuu
wa Mashirika.
Wapendwa
katika Kristo, tunapomtumikia Kristo tunauhakika wa maisha yenye uzima wa
kweli. Katika maisha hayo na Kristo, wote wahudumu na wahudumiwa hustawi na
kufikia hatma yake. Ndani ya maisha haya tunapata furaha ya kweli, kwa sababu
tunayemtumikia ndiye ALFA na OMEGA. Naye Yesu Kristo anasema, “Mimi ndimi chakula
chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi
milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa
ulimwengu,” Yoh 6:51
Ndugu
yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii nikuache na neno hili; uzima wako
hasa wa hapa ulimwenguni bila Kristo hauna maana kabisa. Shughuli zako hapa
duniani bila Kristo ni upepo tu usiojua uvumako na uendako. Usalama wetu
kimwili na kiroho bila Kristo ni ndoto ya samaki kusihi jangwani. Hata kama
ndoto hiyo itatimia, kifuatacho ni Kifo tu. Wapo watu wengi miongoni mwetu,
walitamani ndoto kama hizo, na baada ya kufikia malengo ya ndoto zoa tulipigwa
mshangao mkubwa na kusema hivi: “AMEKUFA MAPEMA KWELI BILA KUFURAHIA MATUNDA
YAKE!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Tazama, maji
haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?,”
Mdo 8:36b
Tusali: Ee Yesu na
Mwakozi wangu, niwezeshe kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kuiokoa Roho,
Mwili, na Nafsi yangu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario