martes, 26 de abril de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 5 YA PASAKA

ALHAMISI WIKI 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 15:7-21
Zab: 96:1-2a, 2b-3, 10
Injili: Yoh 15:9-11
Nukuu:
Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini,” Mdo 15:7

Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao,” Mdo 15:11

Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu,” Mdo 15:19-20

Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10

TAFAKARI:Tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni siku nyingine tena kwa neema ya Mungu tunapata fursa ya kulitafakari neno lake. Leo kwa namna ya pekee tulitafakari hili neno, “Tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu.” Hakika kile tulicho mbele ya Mungu si kile tunachokipigania sana na kutupotezea muda mwingi hapa duniani, ikiwa kitu hicho kinalenga tu ubinafsi wetu. Njia ya Mungu ni ya ajabu sana. Ni ukweli usiotia shaka kwamba leo katika mazingira yetu bila ya kufahamika hutambuliki. Kufahamika huku hakujalishi tu kujuana na mtu. La hasha! Naposema kufahamika ni pamoja na utaratibu tuliojiwekea katika jamii tunayoishi. Mfano: Viwango vya kufaulu kwa wale waliopata bahati ya kusoma. Bila kupita viwango na masharti hayo, maisha yako huko mbeleni ni utata mtupu. Viwango vya kimadaraja kutokana na kufaulu kwako na kukufanya kuwa pale ulipo leo, navyo ututofautisha na wengine na wakati mwingine hutufanya kujisahau na kujiona huo ndio mwisho wa yote.

Maisha ya hapa duniani yanakikomo chake. Na tena ni kwa muda mfupi tu. Maisha anayotutaka Mungu tuishi ni ya umilele. Hivyo kuwa kwetu salama na kupata mastahili mbele ya Mungu ni kwa njia ya NEEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO. Je, hii inamaana kwamba tusijishughulishe na haya tunayoyaishi leo na utaratibu wake? La hasha! Ukweli ni kwamba Mungu anatupenda kama tulivyo na atatuokoa kama tulivyo, ili hali tu, yale tunayoyaishi yaakisi Umungu wake. Niwe tajiri au masikini, mwenye elimu ya pekee au kawaida, mwenye cheo au kabwela, kwa maisha yangu niishiyo kama hayaakisi Umungu wake ni kama moshi unaotoweka mara.

Mtazamo huu wa Kimungu ndiyo msingi wa Mtaguso wa Yerusalemu kuhusu uhalali wetu mbele ya Mungu na wokovu wetu. Uhalali huu si mastahili yetu, bali ni wema na upendo wa Mungu aliyekuwa wa kwanza kutupenda. Je, kuna sababu ya kujichukia? Huna sababu yoyote ya kujichukia. Yupo anayekupenda zaidi ya vyote vyenye thamani katika dunia hii. Mtu huyu akupendi tu, bali anakutakia maisha ya umilele. Huyu ndiye Yesu Kristo aliyekufa kwa ajili yako na kila siku anakufa kwa ajili yako unapomwelekea, ili mwisho wa siku uurithi ufalme wa Baba  na kuishi naye milele yote.

Ufahamu huu ndiyo unaomfanya Mtume Petro kusimama na kuuambia mkusanyiko ule wa Mitume juu ya wale waliolikubali neno la Mungu na kuokolewa nalo. Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini,” Mdo 15:7. Mtume Petro anavunja ukimya. Mara nyingi katika maisha yetu tunashindwa kuuona ukweli kama ulivyo tunaposafiri na kuishi katika nukuu za mila na desturi zetu ambazo nyingi zina mapungufu makubwa.

Ni kweli kwamba tupo kile tulicho kutokana na matokea ya historia yetu. Ni ukweli pia, tusipotoka katika mfuko huu kifikra ni vigumu kuuona ukweli kama ulivyo, na badala yake kuuona ukweli huo kama tulivyo. Wayahudi waliithamini na kuilinda sana historia yao, bila kujua kwamba Mungu hakuacha kujifunua kwao na wale waliowazunguka. Kama ilivyo kweli kwamba hakuna binadamu yeyote aliye hai kwa sababu yake mwenyewe bila Mungu, ni kwa namna hiyo uwepo wetu hauwezi kuwa na maana bila Mungu mwenyewe. Hivyo kwa namna ya pekee na mpango wa Mungu kama ulivyo, twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao,” Mdo 15:11. Mungu huyu hana ubaguzi kwa kile alichokiumba kwa sura na mfano wake. Kufanya hivyo ni kujibagua Yeye mwenyewe, na hivyo kuufifisha Umungu wake kwa vile alivyoviumba.

Wapendwa wana wa Mungu, ni ukweli huu unaomfanya Mtume Yakobo aliyekuwa Askofu wa Yerusalemu wakati ule wa Mtaguso huu kusimama na kutoa neno la mwisho kuhusu tatizo lile juu ya watu wa Mataifa waliomgeukia Mungu na wokovu wake. Naye anasema, Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu,” Mdo 15:19-20. Matendo haya ya kipagani hayana nafasi mbele ya Mungu aliye yote katika yote. Mungu ufurahi pale tunapozishika amri zake kwa uaminifu na haki. Na sheria yake ni UPENDO. Tujipende kama tulivyo na kuumbwa kwetu, na tuwapende wenzetu kama walivyoumbwa kwani wanaufunua uzuri wa Mungu, na tumpende Mungu kwani ndiye uzima wetu na yetu yote, umilele wote.

Ndugu yangu, neno UPENDO si geni kwako, na wala kwangu. Hii ndiyo amri anayotusisitiza Bwana wetu  Yesu Kristo anaposema, Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Ni furaha kubwa sana kuishi bila hatia. Kuishi bila hatia ni kuishi katika upendo wa Kristo. Kristo ni mwalimu wetu na mfano wetu halisi wa Upendo. Kama hujui fani ya Kristo katika somo la upendo, “utazame msalaba wake.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10


Tusali:-Ee Yesu Mwema, usituache. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario