viernes, 31 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 5 YA KWARESMA-A


JUMAPILI YA 5 YA KWARESMA-A

Somo I: Eze 37:12-14

Zab: 130:1-2, 3-4, 5-6, 7-8

Somo II: Rom 8:8-11

Injili: Yoh 11:1-45

Nukuu:

Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12

“Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4

“Lakini Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa,” Yoh 11:13-14

“Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26

“Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27

“Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa,” Yoh 11:32

“Yesu akalia machozi,” Yoh 11:35

“Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8

“Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake,” Rum 8:9

“Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki,” Rum 8:10

“Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11

TAFAKARI: “Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi.”

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na maendeleo aliyoyafikia mwanadamu leo, ikiwa ni pamoja na kuishi kwa kujiwekea vilinda uhai wake, “life securities,” hata hivyo uhakika huo bila Mungu ni sawa na kutwanga maji katika kinu. “Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Ndugu yangu, pamoja na mipango yako ya muda mfupi na mrefu uliyojiwekea, kati yetu hakuna ajuaye ni kitu gani kitakachomtokea sekunde chachetu tu zijazo. Je, tusifanye chochote kwa kuwa huu ndio ukweli? Hapana! Tuyafanye na kuyapanga yote katika usahihi wake, na tufanye hivyo kwa kumshirikisha Mungu kwa kila jambo.

Mara nyingi penye mafanikio-‘kibinadamu,’ wengi wetu hitaji na uwepo wa Mungu huwa hitaji la nyongeza. Tunaamini yote huenda sawa bila Yeye (Mungu) kuwepo. Hiki ndicho kiburi kikubwa sana cha mwanadamu asiye na hofu ya Mungu ndani yake. Hali na mazingira haya yanawakuta wana wa Israeli nyakati zile za Nabii Ezekieli. Mungu anawafananisha waasi hawa wa imani kama mifupa isiyokuwa na nyama. Na hivi ndivyo wana hawa wa Israeli walivyofananishwa na Mungu (mifupa isiyo na nyama wala uhai) katika swala zima la imani. “Mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa,” Eze 37:11. Bila mkono wa Mungu tuyafanyayo hata kama yatavuma sana hayatakuwa na mwisho mzuri. Na hivi ndivyo Nabii Ezekieli alivyozamishwa na Mungu katika tafakari nzito na chukuliwa nje katika roho ya Bwana.

Hata katika hali hii ya uasi na kukosa dira katika imani, Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee. Mungu ndiye uhai na uzima kwa kila kipumuacho, na Yeye huweza kubadili tabia na mienendo ya vyote alivyoviumba. “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7. Mungu akiwa ndiye yote na katika yote, kwa upendo na huruma wake, “humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” 1Sam 2:8. Tunapomrudia Mungu katika toba na majuto ya kweli, Mungu huyabadili maisha yetu na kutufanya wapya mbele za macho yake. Na hivi ndivyo alivyoitoa ahadi yake kwa wana wa Israeli na kusema, “Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12. Naye Mungu asema hivi juu ya mifupa ile ikiwa ni pamoja na hali nzima ya udhaifu wako na wangu kwamba, “Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi,” Eze 37:5. Hakuna jambo la kumshinda Mungu kwa sababu namna tulivyo, na vyote tulivyonavyo vyaonyesha Furaha ya Mungu, na kuufunua Utukufu wake.

Wapendwa katika Kristo, ukweli huu kwamba hakuna jambo la kumshinda Mungu, na kweli kwamba namna tulivyo na vyote ulivyonavyo vyaufunua utukufu na furaha ya Mungu, vinajidhihirisha katika Injili ya leo kwa Lazaro kurudishiwa uhai wake. “Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4. Pamoja na kweli kwamba Wayahudi walimwinda Yesu ili wa mwangamize, Yesu hakuwa na hofu ya kurudi kwao na kuyafanya mapenzi ya Baba yake. Naye “…akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena,” Yoh 11:7. Wanafunzi wa Yesu kwa hofu iliyomwisha jengeka kwa kukoswa koswa Yesu kuuawa, wanapokea habari hii kwa mashaka. “Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?” Yoh 11:8.

Ndugu yangu, mpango ‘ovu wa mwanadamu’ kamwe hauwezi kufanikiwa kwa lile jema alilokwisha likusudia Mungu kulifanya, ingawa Mungu aweza ruhusu ovu ili kulipata jema katika ukamilifu wake. Yesu akiwa analijua hilo aliwaondolea hofu wanafunzi wake na kuwajibu, “Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu,” Yoh 11:9. Kwa maneno mengine Yesu anataka kukuambia wewe na mimi hivi: -‘palipo dhamiri njema na safi katika kulifanya jambo jema na lenye kumpendeza Mungu hapana sababu ya kuwa na hofu licha ya kweli kwamba mazingira ya kulifanya jambo hilo yameghubikwa na utata.’ Leo mambo mengi yanakwenda ndivyo sivyo kwa sababu tu kati yetu na tulio wengi tumejawa hofu pasipo hofu, kuifunga midomo yetu tunapotakiwa kusema, na mwisho wa siku kwa kujua twashirika moja kwa moja katika ‘ovu hilo’ licha ya kwamba twajiweka mbali na kweli hiyo. Na hapa ndipo penye anguko kubwa kwa sababu mmoja kati yetu “…“akienda usiku hujikwaa; kwa sababu nuru haimo ndani yake,” Yoh 11:10.

Ndugu yangu, kile alichokisema Yesu, yaani, “…mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:32, ndicho anachotaka kukithibitisha mbele ya wanafunzi wake. Na zaidi ya hayo Yesu anakutaka wewe na mimi leo kuamini pasipo shaka yoyote kwamba Yeye ndiye njia, na kweli, na uzima; na mtu haji kwa Baba, ila kwa njia yake, Yoh 14:6. Ni katika mantiki hii Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba, “…Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha,” Yoh 11:11. Hata hivyo wanafunzi wake hawakufahamu alichomaanisha Yesu kwa maneno hayo. Tafsiri ya alichokisema Yesu ni hiki: “…alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa,” Yoh 11:13-14.

Ukweli ni kwamba hata baada ya Yesu kuiweka habari ile ya Rafiki yake wazi, yaani, Lazaro kuwa amekufa, Tomaso aitwaye Pacha-mwanafunzi wake Yesu, anabeba habari ile kwa wepesi mkubwa bila kufikiri na kuzama ndani kwa kile alichokisema Yesu. Na hivi ndivyo ilivyokuwa: “Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye,” Yoh 11:16. Hapa Tomaso anaonekana mtu asiye na hofu wala shaka, ila wakati utathibitisha kile alicho Tomaso. Ni Tomaso huyu huyu baada ya ufufuko wa Yesu aliyekuwa mtu mwenye mashaka mengi juu ya ufufuko wa Kristo.

Swali la kujiuliza ni hili:-ikiwa Yesu alijua fika habari ya kuumwa kwake Lazaro hadi kupatwa na mauti, kwa nini basi alijichelewesha kufika na kumponya ugonjwa wake kabla ya kufikwa na mauti hiyo? Ndugu yangu mpendwa, sehemu ya kwanza la swali hili Yesu mwenyewe kesha ijibu. Na jibu ni hili: -“Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4. Na sehemu ya pili ya jibu la swali hili inathibitisha kile alicho Kristo Yesu, yaani, ndani na katika Yeye ipo njia, kweli na uzima, Yoh 14:6. Na ndiyo maana kwa makusudi kabisa Yesu anafika siku ya nne baada ya kifo cha rafiki yake Lazaro. Siku ya nne ikiwa mwili waanza kuoza hakuna tena uwezekano wa kurudi katika ‘hali hai’ kadiri ya mila na desturi za kiyahudi. Hivyo “…Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne,” Yoh 11:17

Kuchelewa kwa Yesu kunaongeza uzuni na majonzi kwa dada zake Lazaro- Martha na Mariamu. “Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa,” Yoh 11:21-22, 32. Lakini ukweli ni kwamba alipo Kristo halijaharibika jambo kwa sababu, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Yesu anawandolea hofu, mashaka, na uzuni Martha na Mariamu kwa kuthibitisha kile alicho, kwamba, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26. Naye Martha pasipo shaka anamjibu Yesu, “Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27. Huzuni na majonzi haya ya Martha na Mariamu, pamoja na majirani zao, ikiwa ni pamoja na imani ile waliyokuwa nayo juu ya Kristo Yesu, inaunyong’onyeza moyo wa Yesu sana. “Yesu akalia machozi,” Yoh 11:35. Tendo hili linathibitisha pasipo shaka asili wa pili wa Yesu, yaani, ‘ubinadamu wake.’ Hakika Yesu anakupenda wewe na mimi upeo, Yoh 13:1.

Kwenye jambo hili la ‘ubinadamu wake Yesu,’ linakuwa kejeri kwa Wayahudi. “Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?” Yoh 11:36-37. Ndugu yangu, alipo Kristo halijaharibika jambo! “Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake,” Yoh 11:38. Kwa nini basi Kristo ashindwe ikiwa “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika?” Yoh 1:3. Ni swala la wakati tu! Hapa tunakumbushwa kuwa na subira kwa kila jambo hasa pale tunapogubikwa na sintofahamu. Wewe na mimi katika hali hii ya sintofahamu twapaswa kumwachia Kristo Yesu usukani wa maisha yetu. Majigambo na kujikweza hakutatupeleka kokote. Kama wakati fulani ulifanikiwa na ukajiona mafanikio hayo ni kutokana na uwezo wa kiakili zako, utajiri wako, na misimamo yako kijamii na kisiasa, basi jua kwamba safari bado. Dhababu ili iwe thahabu kweli lazima iwe imepita katika moto mkali. Na utajua dhahabu hiyo imefika kiwango cha kuitwa dhahabu pale tu utakapoona sura yako kwenye dhahabu hiyo. Je, waujua udhaifu wako?

Wapendwa wana wa Mungu, ni Kristo peke yake awezaye kutuondolea uzuni na majonzi yetu. Mara  “Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne,” Yoh 11:39. Haijalishi ni kwa kiasi gani tumedhoofishwa na magonjwa yetu, mateso yetu, na sintofahamu zetu. Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba pamoja na hayo yote, ‘ukiamini utaona utukufu wa Mungu, Yoh 11:40. Na ndivyo ilivyo kuwa kwa familia ya Martha na Mariamu. “Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma,” Yoh 11:41-42. Yesu ndiye kimbilio na mteteze wetu mwaminifu. Ni wewe na mimi kujiaminisha na kujisalimisha kwake.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa imani Yesu hututoa katika vifungo vya udhaifu wetu. Kristo kesha ikata minyororo ya kuzimu naye anazo fungu za mauti na za kuzimu, Ufu 1:17-18. Kwa Kristo Yesu uzima upo. Hivyo “Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje,” Yoh 11:43. Lazaro anarudishiwa uhai wake, na kwa tendo hilo Mungu anaufunua utukufu, uzuri, na furaha yake kwa wale wote wenye kumwamini. “Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini,” Yoh 11:45. Amina!

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, ni vema ukafahamu jambo hili la msingi kuhusiana na uumbaji wa Mungu na sababu ya kuishi kwetu. Napenda kuyachukua maneno haya ya Mtume Paulo kwamba, “kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina,” Rum 11:36. Jambo la msingi hapa ni kweli kwamba Mungu hakuhitaji kukuumba wewe, bali alichagua kukuumba kama ulivyo kwa furaha na utukufu wake. Kwa maana hiyo, maisha yetu hapa duniani yapaswa kuufunua, kuuonyesha Utukufu wa Mungu, na furaha yake.

Ndugu zangu katika Kristo, mwanadamu angali akiwa hapa duniani utoa Utukufu wa Mungu na furaha yake kwa kufanya mambo yafuatayo: Mosi, kwa kumwabudu Mungu, yaani maisha yako yote, kwa kuwapenda watu wengine bila kumbagua ye yote. Pili, kwa kuishi na kuwa kama Kristo. Tatu, kwa kutumia vipaji vyako vyote kwa ajili ya wengine, yaani kufaidiana. Na nne, kwa kueneza habari njema za Mungu kila pande za dunia. Hata hivyo licha ya ukweli huu, mwanadamu huyu anaweza kuufunua utukufu wa Mungu na furaha yake kwa kutenda matendo ya roho, Gal 5:22-23, na siyo yale ya mwili yasiyo na uzima ndani yake, Gal 5:19-21. “Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani,” Rum 8:6. Mtu hawezi kumpenda Mungu kama anafuata matendo ya mwili wake tu.

Ni kweli kwamba kiini cha dhambi ni pale mtu anapojipenda yeye zaidi kuliko Mungu. “Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8. Hivyo basi kama tunataka kuishi na kuwa kama Kristo lazima tufuata sheria ya roho, yaani, matendo ya roho, ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria, Gal 5:22-23. Uzima huu tuupatao kwa matendo ya roho upo ndani ya Kristo pale tunapotaka kuishi na kufanana naye. “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti,” Rum 8:2. Hivyo kwa kuishi na kufanana kama Kristo tunaufunua Utukufu wa Mungu na furaha yake ya kutuumba.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kwa upande mwingine, sheria ya dhambi ni matendo yale yasiyo na uzima ndani yake, na kwayo kamwe hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Matendo haya ni haya; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo. Mtume Paulo anasisitiza kwamba, “katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Je, hutaki kuurithi ufalme wa Mungu na maisha ya umilele?

Kuishi na kutenda kwetu ili kuwe kwa sifa na utukufu wake Mungu kwa tulazimu kufikiria mambo ya roho.Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho,” Rum 8:5. Ndugu yangu, utawezaje basi kuishi na kufanana na Kristo kama muda wote wa ufuata mwili na kufikiri mambo ya mwili? Hii ni changamoto kwa kila mmoja wetu. Ni kweli kwamba hatuwezi kuyawaza ya roho kama hatuna mwili. Jambo la msingi na la kufahamu hapa ni kwamba ‘vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele,’ Rum 11:36. Hivyo hakuna kilicho chako katika maana ya umiliki halali zaidi ya dhambi zako. Sasa nifanye nini katika hali hii?

Wapendwa katika Kristo, tunahitaji roho wa Kristo ndani yetu ili tuyafuate matendo ya roho na mwisho tuwe mali ya Kristo. Roho huyu ni zawadi kwetu kutoka kwa Mungu, na hufanya kazi ndani yetu kadiri apendavyo yeye kututumia kadiri ya mpango mzima wa Mungu. Hivyo, “ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11. Hapa ndipo tunapoona Upendo na Huruma ya Mungu kwetu. Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee kwa sababu ya dhambi zake. Mimi na wewe tunapewa kila siku fursa ya kutubu na kumrudia Mungu. Katika mantiki hii yanipasa kuzitazama dhambi zangu, kuzitubu, na mwisho kuwa huru kutoka utumwa huu wa dhambi. Ni kwa namna hiyo hiyo sina haki wala sababu ya msingi kuwanyooshea vidole wengine ilhali mimi mwenyewe nahitaji upendo na huruma ya Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wangu, bila Wewe mimi si lolote wala chochote. Amina

domingo, 26 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMAMOSI WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Yer 11:18-20

Zab: 7:1-2, 8bc-9, 10-11

Injili: Yoh 7:40-53

Nukuu:

“Lakini mimi nalikuwa kama mwanakondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa, wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, “Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.”” Yer 11:19

“Je, torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?” Yoh 7:51
 
TAFAKARI: “Haki ya mnyonge ni haki ya Mungu; dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu, binadamu hawezi kushinda kesi hii.”

Wapendwa wana wa Taifa ya Mungu, leo kadiri ya masomo yetu, yanatualika tutafakari juu ya “haki ya mnyonge ni haki ya Mungu; dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu, binadamu hawezi kushinda kesi hii.” Katika mazingira ya Nabii Yeremia na hata mazingira na nyakati za Yesu Kristo, wanyonge walidhulumiwa na haki zao kuporwa au kukanyagwa. Hawakuwa na watetezi, na hata kwenye ukweli juu ya wanyonge, ulipindishwa kwa visingizio mbalimbali kama tutakavyoona kwa Yeremia na Yesu Kristo. Je, nyakati zetu hali imebadilika na kuwa bora zaidi, licha kwamba Yesu Kristo kuwa mtetezi wa wanyonge na hata kuutoa uhai kwake kwa ajili ya kweli?

Ndugu yangu, Nabii Yeremia anasema ni kwa namna gani mtu mnyonge anavyoonewa kutokana na hali na upole wake. Katika jamii yoyote ile ya watu, licha ya historia yao na utamaduni wao, wale waliojaliwa ufahamu wa kuelewa mambo, hutumika sana katika kutafuta ukweli, usawa, haki, amani, na kuzisimamia. Ni watu hawa hawa kwa kukosa hofu ya Mungu hutumia upole na hali za wanyonge kuwadhulimu haki zao. Katika uovu huu, Nabii Yeremia anasema, “Lakini mimi nalikuwa kama mwanakondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa, wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, “Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.”” Yer 11:19

Mnyonge huyu hanyimwi tu haki zake, bali huondolewa hata haki za kizazi chake kijacho na kufutwa kabisa. Lengo ni kuuharibi mti pamoja na matunda yake. Wapendwa wana wa Mungu, dhuluma kama hii afanyiwayo mnyonge, binadamu mwenye kufanya hayo kamwe hataweza kushinda katika dhuluma hii. Mungu mara zote hulia na wanyonge. “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” I Sam 2:6-8.

Ndugu yangu, dhuluma dhidi ya mnyonge ni dhuluma dhidi ya Mungu mwenyewe. Tenda haki kwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. “Usimnyang’anye maskini; wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni; Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka,” Mit 22:22-23. Kuna heri na baraka kubwa kutoka kwa Mungu unapotenda mema na kuwatetea wanyonge. “Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab 41:1. Tuwe watu wa kutenda mema kwa wote na tuanze pale tulipo. Lifanye jambo hilo kuwa tabia yako nyumbani kwako, kazini kwako na hata kwenye utume wako, iwe jumuiyani na hata Kanisani. Tuwe watetezi wa wanyonge na hasa wale wasiokuwa na sauti na mahali pa kupeleka malalamiko na vilio vyao.

Watendao maovu na hasa kuwanyanyasa wanyonge kwa kunyonga haki zao, kamwe hawataishi kwa amani. Ninapolitazama taifa letu leo, na harakati zake hasa kwa swala zima la Katiba, napata mashaka sana. Wasomi wetu na wale tuliowapa dhamana ya kutetea na kusimamia haki kwa wote na hasa kwa wanyonge, wamekuwa watu wa kwanza kupora haki za wanyonge na kufanya Katiba pendekezwa kuwa na taswira yenye mwelekeo wa kulinda maslahi yao na familiza zao, kulinda utajiri waliokwisha pora kwa wanyonge, kuweka uwezekano wa familia zao na marafiki zao kuwa madarakani daima, na hata kuzuia mnyonge kupata haki yake pale atakapoidai kwa haki.

Katika hili na mazingira kama haya, Mungu anasema, “hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge,” Dan 4:17. Dhuluma yeyote juu ya wanyonge, Bwana ataijibu mara moja. Tuwe na hamu na matumaini ya kutenda mema siku zote, na tuendelee kutenda haki. Kwa kuwa, “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu,” Isa 66:2. Kumdhulumu mnyonge ni kugusa mboni ya jicho la Mungu.

Injili letu ya leo yaonyesha ni kwa namna gani mnyonge anavyodhumiliwa haki zake na hasa swala zima la kutoa hukumu. Yesu Kristo anahukumiwa hata bila kusikilizwa. Wanapanga njama za kuutoa uhai wake kwa vile tu ananena iliyo kweli na kutenda mema. Hata licha ya kusutwa na dhamiri zao, Mafarisayo bado wanasukumwa na dhamiri zao mbaya kutenda uovu. “Je, torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?” Yoh 7:51. Nikodemu, aliyekuwa mfuasi wa siri wa Kristo, na aliyekuwa anamwendea usiku kupata habari za ufalme wa Mungu, anajaribu kutoa ushauri ili kuunusuru uhai wa Yesu. Ushauri huu haukubaliki machoni mwa Mafarisayo kwa sababu binadamu  akishachagua kumtumikia shetani, uwepo wa Mungu unatoweka. Dhamiri iliyo mbovu na ufu, husahau hata yale mazuri tuliyojiwekea kwa ajili ya kutenda haki.

Ndugu yangu, Taifa letu linautaratibu mzuri tu wa kutoa haki licha ya kwamba yapo maeneo fulani yanaitaji marekebisho. Hata hivyo, bado haki za wanyonge zinakanyagwa kiasi kwamba hata aibu hatuna tena. Kujilimbikizia mali za wizi uliotokana na kodi za wanyonge, ni dhambi ambayo ukiifanya itakutafuna wewe na hata kizazi chako hadi kizazi cha nne baada ya wewe. Fedha na mali zisizo halali ni kujiwekea sanamu na kuanza kuziabudu. Tukianza kuambudu mali na vitu, Mungu hana tena nafasi ndani yetu. “Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana wa uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,” Kumb 5:9. Hii ni laana kubwa sana. Ufisadi kwenye Taifa letu la Tanzania,  umekuwa moja ya sifa, na tunaaminishwa kupokea jambo hilo kama la kawaida. Uovu huu dhidi ya masikini na wanyonge binadamu hawezi kushinda kamwe kwani ni uovu dhidi ya Mungu mwenyewe. Leo tupo kwenye mkakati na harakati wa kutumbua ‘majipu.’ Je, tutafikia malengo kweli ikiwa hata watumbuaji wa majibu kikanuni nao wanamajipu hadi mikononi? It is just a play within a play!

Bwana wetu Yesu Kristo ni neno aliyefanyika mwili. Hivyo ni Mungu mwenyewe. Kutokumpatia haki stahili Yesu Kristo, ni kutokumpatia Mungu mastahili yake. Je, vita hii binadamu mwenzangu tutashinda, au ndiyo tunazidi kujichumia laana tu kila kukichwa. Ndugu yangu kilio cha wanyonge katika Taifa letu leo kwa ujumla wake ni kilio cha Mungu.

Mpendwa, mara zote kuwa na hofu ya Mungu na tenda wema kwa wote bila kujali historia ya mtu na hata hali yake kijamii. Sote mbele ya Mungu tunamizania na mastahili sawa. Wayahudi wanatafuta histori ya neno aliyefanyika mwili-Yesu Kristo, kwenye kumbukumbu zao. Wanampa Yesu Kristo nafasi ya Nabii. Yesu Kristo siyo nabii, bali ni nafsi ya Pili ya Mungu. Bado Wayahudi wanawaza kibinadamu. Tusimsaidie mtu au kumsikiliza mtu shida zake kwa kuanza kutazama historia yake. Hili ni kosa kubwa sana kufanya. Tumtazame mtu kadiri ya kile anachohitaji kwetu na tufanye kwa haki na stahili zote.

Tumsifu Yesu Kristo

“Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena,” Yoh 7:46

Tusali:-Ee Yesu, nipe neema ya kukuona mara zote kwa wale ninao wahudumia. Amina

 

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 4 YA KWARESMA


IJUMAA WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Hek 2:1a, 12-22

Zab: 34:16-17, 18-19, 20, 22

Injili: Yoh 7:1-2, 10, 25-30

Nukuu:

“Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia,” Hek 2:21-22

“Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30

TAFAKARI: “Mpango wa Mungu kwa mwanadamu; na njia ovu za mwanadamu”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa namna ya pekee tutafakari neno hili, “Mpango wa Mungu kwa mwanadamu, na njia ovu za mwanadamu.” Mpendwa, somo la leo ikiwa ni pamoja na Injili ya leo, yote kwa ujumla wake yanaongelea Mpango wa Mungu kwa sisi wanadamu, na matendo maovu tuyafanyayo kwa kujua au kutokujua ili mradi tu kwenda kinyume na matakwa yake Mungu. Tunaona jinsi ya mtu wenye haki anavyodhulumiwa na kutendwa vibaya bila hatia yo yote. Tuona katika somo hilo la kwanza binadamu anavyokaa vikao vya kutenda maovu na kushauriana kufanya hivyo kwa utaratibu na kufanikisha jambo hilo.

Mwisho Mungu analiona jambo hilo na analiweka wazi. “Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa, kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu, wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia,” Hek 2:21-22. Jambo lo lote ovu lifanyikalo gizani ipo siku litawekwa hadharani. Mungu kwa uwezo na mamlaka aliyokuwa nayo aweza kuruhusu uovu kwa lengo la kutoa fundisho. Na katika mantiki hii, lililo ovu haliwezi kushinda kamwe! Na kamwe Mungu hawezi kuwa sehemu ya uovu ule kwa sababu Mungu ni Mkamilifu katika ukamifu wote. Kwa hiyo, ye yote yule ajivuniaye kwa uovu anapoteza muda wake bure na mwisho wa siku anajichumia mzingo wa dhambi.

Tunapoitazama jamii yetu leo kama Watanzania, ni wakati wa kulitazama kwa ukaribu Taifa letu na kuliombea sana. Wale wote wafanyao ovu kinyumbe na mpango wa Mungu hasa kwa wale wasiokuwa na sauti, si kwamba hawana chembe ya umungu ndani yao, ila wameamua kufanya hivyo kwa ajili ya nafsi zao na ubinafsi wao. Wamekubali kupatwa na upofu wa kutokuona mema kwa faida ya wengi. Mtu huyu mwenye haki, yaani, mwananchi asiye na sauti, akitegemea wenye hekima na busara wamtete, anajikuta anasalitiwa. Mtu huyu ni Kristo anayeteseka leo na sasa. Wategemewa hawa, wamekuwa vipofu kutumia hekima zao kwa kung’ang’ania madaraka na kusahau cheo chao halisi, yaani, Utakatifu wao. Hakika adhabu yao mbele ya Mungu ni kubwa.

Injili yetu pia yatuonyesha mtu mwenye haki anavyowindwa na hata kufikia hatua ya kuutoa uhai wake. Yesu Kristo usalama wake unaingia matatani kwa vile tu anasimamia kweli, haki, huruma, msamaha na upendo. Hii ndiyo asili ya Kristo, na ndiyo asili ya Mungu. Ndiyo kusema kwamba kweli ya Kristo ni kweli ya Mungu. Kristo akiwa neno aliyefanywa Mwili, Yoh 1:14, ni Mungu yule yule tunayetaka kumwangamiza. Je, ikiwa binadamu kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27, vita hii binadamu ataiweza? “Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado,” Yoh 7:30. Hii ni ishara wazi kwamba nguvu za binadamu katika uovu wake dhidi ya Mungu na hasa kwa wanyonge hazitafanikiwa kamwe!

Mambo yote tuyaonayo leo yaliyo kinyume na mpango wa Mungu yana mwisho wake. Hakuna uovu wowote duniani, au tawala zozote duniani zilizodumu kwa muda wote. Uovu ni kinyume kabisa na uwepo wa Mungu na mpango wake kwa ulimwengu huu. Yote haya tuyaonayo yanasubiri saa yake. Je, tufanye nini katika nyakati hizi za sintofahamu?

Katika nyakati hizi za sintofahamu, kamwe tusipoteze matumaini ndani na katika Kristo. Ni Kristo tu aliyeshinda uovu kwa wema atakayetupitisha katika mkwamo huu. Kristo anateseka sana na wale wanyonge na wasio na hatia katika jamii yetu leo. Kuwa na matumaini ni wito wa kuwa na Imani na Kristo. Imani ya kwamba yote yana mwisho wake, ni swala la Muda tu. Tutaweza kudumu katika matumaini na imani ndani na katika Kristo, kama tuna upendo wa kweli ndani yetu na Kristo. Upendo ni msingi mkubwa wa Matumaini na Imani. Ni katika kupenda twaweza kufanya yote ikiwa ni pamoja na kudumu katika sala hasa kwa kipindi hiki kigumu.

Ndugu yangu, tuwe macho kwa kila kitu tunachokumbana nacho leo, na kukitafakari kwa undani na kumwomba Roho Mtakatifu atusaidie kuona yale yote yaliyojifisha sirini.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi,” Yoh 7:28

Tusali:-Ee Yesu, uliyekubali kuzichukua dhambi zetu pasipo Wewe kutenda dhambi, tufungulie hekima yako hii ili nasi tuwajibike kikamilifu katika kuliondoa giza nene hili la uovu katika jamii yetu leo. Amina

 

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 4 YA KWARESMA


ALHAMISI WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Kut 32:7-14

Zab: 106:19-20, 21-22, 23

Injili: Yoh 5: 31-47

Nukuu:

“Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14

“Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44

TAFAKARI: “Huruma ya Mungu, Uzima, na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, “Huruma ya Mungu, Uzima na Utukufu ndani na katika Yesu Kristo.” Somo la kwanza Mungu anaonyesha huruma kwa watu wake kupitia Mtumishi wake Musa “…alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu,” Kut 31:18, waliobaki chini wakisubiri maelekezo hayo ya Mungu, walijifanyia mambo yao kwa kujichongea sanamu zoa kama utambulisho wa Mungu wao wa kutengeneza. Hili lilikuwa ni chukizo kubwa kwa Mungu. Kwa hasiri hii Mungu anataka kuliangamiza taifa lote la Israeli kwa kutokuwa na subira. Bwana akamwambia Musa, “Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu. Basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize,” Kut 32:9-10.

Musa analiombea taifa lake, kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake alizozitoa na kuzifanya na Ibrahimu, Isaka na Israeli. Kwa huruma yake Mungu, “…akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake,” Kut 32:14. Mungu wetu ni Huruma na mara zote yupo tayari kuturumia na kutusamehe tunapoyakiri makosa yetu na kumrudia. Huruma hii ya Mungu iwe pia ndani yetu hasa pale ninapotakiwa kutoa huruma hiyo bila masharti katika kusamehe. Huu ndiyo mwito wetu pia sisi sote tunaomwamini Mungu, na Mwanaye Yesu Kristo.

Injili yetu ya leo inatupa msingi wa kile tuaminicho na malengo yetu kama wafuasi wake Kristo. Ndugu yangu, uzima wako na utukufu wako hauwezekani pasipo kuwa ndani ya Kristo na katika Kristo. Wayahudi hawaukubali ukweli huu, na badala yake wanamdhihaki Yesu Kristo kwa kutokuamini kwao. Hawatambui pia yale yote yaliyofunuliwa juu ya Kristo katika safari nzima ya historia hii ya wokovu. Yesu anasema mshitaki wao mkuu ni kazi zake, na yale yote yasemwayo kuhusu Yeye katika Maandiko Matakatifu. “Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu,” Yoh 5:45-46.

Uzima na utukufu wetu wapatikana katika Kristo kwani Yeye yupo kwa ajili ya hayo na ameyafia hayo. Yatupasa kuyaamini atufundishayo. Na kama hatuyaamini atufundishayo tuziamini kazi zake. “Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu. Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?” Yoh 5:40-41,44. Utukufu wa kweli ni ule utokao kwa Mungu, ambao kwa namna ya pekee ndiyo Yesu Kristo anatujalia sisi kutipitia mateso, kifo na ufufuko wake. Hakuna utukufu kwa Mkristo bila msalaba. Uzima huu twaupata kwa kula na kunywa damu yake katika mastahili 1Kor 11:27, ikiwa ndiyo njia ya pekee ya kushiriki mateso, kifo, na utukufu wa Kristo. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54.

Ndugu yangu, wakati ndiyo sasa wa kujipanga sawa sawa na kujua uzima na utukufu wako unatoka wapi. Ishi imani yako ipasavyo na “msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.” Ebr 13:9.

Tumsifu Yesu Kristo

Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma,” Yoh 5:36

Tusali:-Ee Yesu Kristo, nakiri na kuamini kwamba Uzima na Utukufu vya toka kwako tu Wewe uliye yote katika yote. Amina

 

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMATANO WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Isa 49:8-15

Zab: 145:8-9, 13cd-14, 17-18

Injili: Yoh 5:17-30

Nukuu:

“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

“Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24

TAFAKARI: Usikivu wa Upendo wa Mungu Baba na Mwana, hu na uzima wa milele ndani yake.

Wapendwa wana wa Mungu, “Usikivu wa Upendo wa Mungu Baba na Mwana, hu na uzima wa milele ndani yake.” Yesu Kristo anaudhihirisha upendo wa Mungu Baba kwetu, na kwa njia yake twaweza kumjua Baba Mungu. Hili ndiyo fumbo kubwa la kumwilishwa kwa neno wa Mungu na kuwa mwanadamu.

Ahadi ya Mungu kwetu ni kutokutusahau katika hali zote hata kama kibinadamu jambo hilo linawezekana. Mungu hawezi kutusaha. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

Maisha yetu ni mpango wa Mungu na kwa malengo ya Mungu. Mpango huu unarahisishwa kwa uwepo wa Mwanaye Yesu Kristo, ambaye hajifanyii mambo yake pasipo Mungu Baba aliyempeleka. “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka,” Yoh 5:30

Wayahudi wanapinga ufundishi na utendaji wa Yesu, hasa kwenye uelewa wa Mungu mmoja tu, na si katika nafsi tatu. Kadiri ya uelewa na mtazamo wa Kiimani wa Kiyahudi, kama ilivyopia kwa dini nyingine kama Waislamu, Mungu hawezi kuwa na mtoto, na Yesu kusema yeye ni Mwana wa Mungu, wakati wanajua yeye binafsi na wazazi wake, ni kufuru kubwa sana. Lakini ukweli ni kwamba, nafsi hizi tatu hujitofautisha katika utendaji. Na katika utendaji huu wa nafsi mojawapo, hauondoi uwepo na ushirikiano wa nafsi nyingine.

Ndugu yangu, yawezekana kupenda bila kujua na wakati mwingine kutokufanya chochote, ila huwezi kujua ukaacha kufanya na kupenda. Mbali zaidi ni kwamba, kupenda na kufanya huku msingi wake ni kuamini yale ayafanyayo Yesu Kristo pamoja na uelewa wetu kibinadamu kutotosheleza kuzama kabisa katika fumbo la Utatu Mtakatifu. Tuanze na kuyaamini haya ayasemayo na kuyafanya Yesu Kristo, na katika safari hiyo tutajua taratibu siri ya fumbo hili la Utatu Mtakatifu na kupenda.

Ahadi ya kuyafanya hayo yote, Yesu Kristo anaweka wazi jambo hili, na kusema, “Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Yoh 5:24. Jambo hili la kusikia neno na kumwamini Yesu Kristo liongoze dira nzima ya maisha yetu ya kiroho. Mpendwa, kuwa na uzima ndani ya Kristo na katika Kristo ni kumfanya Kristo kuwa pumzi ya maisha yako kila siku; katika kufikiri, kutenda, na kuishi.

Tumsifu Yesu Kristo!

Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba,” Yoh 5:22-23

Tusali:-Bwana Yesu, uwe pumzi na uhai wangu. Amina

 

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMANNE WIKI YA 4 YA KWARESMA

Somo: Eze 47:1-9, 12

Zab: 46:1-2, 4-5, 7-8

Injili: Yoh 5:1-3a, 5-16

Nukuu:

“Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko, maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi popote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9

“Akawajibu, “Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, ‘Jitwike, uende,’” Yoh 5:11

TAFAKARI: “Uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, “uzima na uponyaji upo ndani na katika Yesu Kristo.” Maono ya Nabii Ezekieli juu ya mto wa uponyaji ambao chanzo chake ni patakatifu, unatupa maandalizi ya Mungu katika uponyaji ambao umekamilika ndani na katika Yesu Kristo. Ndani ya maji hayo kutakuwa na uzima na kila kiumbe kitapata uhai. “Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu. Na matunda yake yatakuwa ni chakula, na majani yake yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12

Ndugu yangu, neema na baraka kadiri ya maono ya Nabii Ezekieli kulingana na  mto huu zipo ndani ya Kristo, na Kikanisa zinajidhihirisha katika sakaramenti zake. Katika Injili ya leo, uzima na uponyaji wajidhihirisha katika Kristo. Ndani ya Kristo tunapata uhai na uzima tele. Ndani ya Kristo tunapata neema na baraka. Ndani ya Kristo tunatambua njia, kweli, na uzima kuelekea umilele.

Katika uponyaji huu, Yesu anamuuliza huyu asiyejiweza, “Wataka kuwa mzima?” Yoh 5:6. Ingawa jibu la huyu asiyejiweza haliendani na swali (“Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu wingine hushuka mbele yangu,” Yoh 5:7), Yesu anajua mateso na mahangaiko yake, na hivyo analitenda jambo kuu kwa ndugu huyu.

Yawezekana kutokana na mahangaiko na mateso tuliyonayo, iwe ni ugonjwa au kitu kingine, yameshatufanya tupoteze ufahamu na mwelekeo wa matumaini. Lakini tukumbuke kwamba katika hali hiyo Yesu anatuuliza kama twataka kuwa wazima. Yesu anaturudishia hadhi yetu na utu wetu kuufanya upya na kutufanya tuanze maisha mapya. Angalisho kubwa katika maisha haya mapya, ni kutokutenda dhambi. “Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi,” Yoh 5:14.

Ndugu yangu, tunaishi katika neema na baraka zake Mungu tunapokuwa katika hali ya usafi kiroho na kimwili, yaani hali ya kutokutenda dhambi. Kwa kipindi hiki cha kwaresma tunapotafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni kipindi pia cha kujitakasa kwa sala, na kuziungama dhambi zetu. Ndugu yangu, “tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala nena lake halimo mwetu,” I Yoh 1:8-10

Tumsifu Yesu Kristo!

 Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru,” Zab 36:9

Tusali:-Ee Yesu, ndani yako na katika wewe upo uzima na uponyaji. Amina

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 4 YA KWARESMA


JUMATATU YA WIKI 4 YA KWARESMA

Somo: Isa 65:17-21

Zab: 30:1, 3, 4-5, 10-11a, 12b

Injili: Yoh 4:43-54

Nukuu:

“Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni,” Isa 65:17

“Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?””, Yoh 4:44,48.

TAFAKARI: “Mara zote Mungu huanza upya na watu wake; Kristo Yesu ndiye ufunuo halisi wa utimilifu huo wa Mungu”

Wapendwa wana wa Mungu, “Mara zote Mungu huanza upya na watu wake; Kristo Yesu ndiye ufunuo halisi wa utimilifu huo wa Mungu.” Nabii Isaya katika somo letu la leo anaelezea furaha hiyo ya Mungu kuanza upya na watu wake baada ya kuyaona mateso yao. “Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni,” Isa 65:17. Mwanzo huu mpya ni pamoja na kuwapa watu wake maisha marefu, ila watenda dhambi watalaaniwa ingawa watafaidi kwa kuwa na umri mrefu. Kwa namna nyingine, mafanikio yetu pasipo Mungu si kidhibitisho cha kufaulu kwetu. Amani ya kweli upatikana pale tunapomuhusisha Mungu yote tufanyayo.

Utimilifu huu wa kazi ya Mungu ya kuanza upya na watu wake inajidhihisha ndani ya mwanaye, yaani, Yesu Kristo. Ishara za Yesu Kristo zadhihirisha utimilifu wa ahadi ya Mungu kuanza mpya na watu wake. Jambo hili liliwekwa wazi siku ya kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo. “Alipokuwa katika kusema, wingi jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika like wingu, ikasema, Huyu ni Mwangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye,” Mt 17:5. Je, waamini maneno hayo?

Ndugu yangu ule Mkristo, kufanikiwa kwetu kiimani, ikiwa ni kuanza yote upya kuelekea maisha ya umilele, mpango huu unawezekana tu kwa njia ya Yesu na ndani ya Yesu. Kinachoongoza safari hii ya kiimani ni Msimamo wa Imani tuliyonayo juu ya Yesu. Tunapokuwa na imani thabiti, yote hudhihirishwa ndani yetu. Tunapokuwa na imani Mungu hufanya mambo makubwa na kujidhihirisha kwetu. “Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20. Ukristo bila Kristo ni sawa na samaki kutamani kuishi jangwani.

Kwa njia ya Imani hii, leo tunaona uponyaji wa mtoto wa diwani. Kwa kuiona imani hii, Yesu anamwambia, “Enenda; mwanao yu hai.” Yoh 4:50. Ila tunapewa angalizo na changamoto katika swala la Imani. Tusiamini tu kwa sababa ya kuziona Ishara. Imani ya kweli haiitaji Ishara. Ila tunapoamini kweli, Mungu ujidhihirisha ndani ya kile tunachoamini. Kwa jambo hili Yesu anasema, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?” Yoh 4:48. Ishara si kigezo cha Imani. “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1.

Ndugu yangu, tusisahau kwamba, “kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri,” Ebr 11:3. Na ni kwa njia hii ya imani yote yawezekana katika Yesu Kristo Kristo, ambaye yeye twapaswa kumwamini na kumsikiliza kila wakati.

Kwa nini basi ndugu yangu kila siku unahama makanisa na vikundi vya kitume tutafuta ishara?

Tumsifu Yesu Kristo!

…Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki,” Lk 11:29-30

Tusali:-Ee Yesu na Mkombozi wetu, twaamini yote yanawezekana ndani yako na kwa njia yako. Amina.

 

sábado, 25 de marzo de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA-A


JUMAPILI YA 4 YA KWARESMA-A

Somo I: 1 Sam 16:1b, 6-7, 10-13a

Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6

Somo II: Efe 5:8-14

Injili: Yoh 9:1-41

Nukuu:

Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,”

“Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake,” Yoh 9:3

“Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu,” Yoh 9:5

“Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,” Yoh 9:6

“Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona,”Yoh 9:25

“Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yoh 9:35

“Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia,” Yoh 9:38

“Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu,” Yoh 9:39

 “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41

“Enendeni kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c

“kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli,” Efe 5:9

“Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru,” Efe 5:13

TAFAKARI: “Enendeni kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya nne ya Kwaresma ya mwaka “A” wa Kanisa. Mwaliko wa Dominika ya leo watutaka sote tuenende katika nuru na kama watoto wa nuru. Nuru ni alama na uwepo wa Mungu kati yetu, na kwa namna hiyo hiyo ni vita dhidi ya giza, yaani, uovu. Hivyo kuenenda katika nuru ni kuvipiga vita vya giza, yaani, aina zote zile za uovu.

Katika kweli hii, vita dhidi ya uovu vinaushindi katika mpango mathubuti wa Mungu kupitia watu wake aliowachagua na kupendezwa nao. Kunapotokea udhaifu katika vita hivi, Mungu umwinua mwingine katika kundi shindwa lile na kufanikisha hadhma yake.

Ni katika mantiki hiyo kwamba, baada ya Sauli kukosa sifa mbele za macho ya Mungu, Mungu anafanya zaidi kwa manufaa ya watu wake. Hivyo Mungu anawachagulia tena Mfalme wana wa Israeli. Samweli mtumishi wa Mungu anapewa maelekezo na Mungu na anafanya kadiri ya maelekezo hayo. Yese alikuwa na wana wazuri na wenye uwezo. Pamoja na hayo yote, Mungu anamchagua yule amtakaye kwa makusudi yake na watu wake.

Baada ya kukosekana yule amtakaye Mungu, Samweli mtumishi mwaminifu  wa Mungu anamuuliza Yese, “Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku,” 1Sam 16:11.

Mtazamo wa leo na msukumo wa kijamii na kisiasa ni vigumu sana kusikia sauti ya Mungu ndani ya mioyo yetu. Tunaishi sana katika ushabiki na wakati mwingine tunaingiwa upofu na kutokuona vitu sawasawa. Leo si jambo la ajabu kuona mtu asiyependwa na watu ndiye anayetangazwa kuwa mshindi na aliyechakuliwa na watu kwa kishindo. Demokrasia (iliyovikwa kama koti la dharura) kwa nchi zenye mfumo wa kimla ni kwamba wengi usema ila baadhi na wacheche sana ndio wanaoamua. Udhalimu huu hauna nafasi mbele ya Mungu. Kilicho cheupe na kiwe cheupe na kilicho giza na kitambulike kuwa giza. Kwa nini tunatanguliza nafsi zetu mbele zaidi ya kile atakacho Mungu kupitia watu wake?

Mungu wetu hatazami kama sisi tutazamavyo katika hulka na ushabiki wetu. Mungu hufanya kadiri ya ukamilifu wake. Nasi kama wanadamu tunaalikwa kila siku kuwa wakamilifu kama Yeye Mungu alivyo. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mk 5:48. Ni vyema ufahamu uwepo wako hapa duniani. Ndugu yangu unanye safiri nami katika tafakari hii elewa kwamba upo hapa nduniani kupigana kufa na kupona juu ya cheo chako ambacho ni utakatifu wako. Mengine yote na fahari zake ni mbwembe tu. Huwezi kumwona Mungu kama si mtakatifu. Je, unajua hilo? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu hakumaanishi “mbainisho wa hiki kizuri na hiki kibaya, bali kusimama katika kweli na haki pale ulipo, ukitambua dhamana uliyopewa na umma wa watu.” Bila hili kufanyika hayo yote utakayoyaainisha hubaki kuwa mbwembwe tu kama ulivyo upepo wa kisulisuli.

Hivyo, Daudi anapata sifa mbele za Mungu ingawa hakuwa matarajio ya familia ya Yese. “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,” 1Sam 16:7. Mungu utazama moyo ule unaomwelekea na kufanya mapenzi yake. Na katika jambo hili, kutenda lililo jema hakuwezi kugubikwa na mila na desturi zetu, bali katika kweli na haki.

Injili ya leo inachanganua taswira tatu katika vita hivi vya mwanga dhidi ya uovu. Moja; -Kristo Yesu ndiye mwanga halisi, Yoh 1:9, na kielelezo halisi cha upendo, huruma, kweli, na haki ya Mungu, Yoh 13:1. Na kwa kinywa chake Yesu anasema, “Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu,” Yoh 9:5.

Pili; -ni taswira ya wakumbatia uovu kulikotokana na kufa kwa dhamiri zao. Kwa nyakati zile za Yesu kundi hili lilibeba Mafarisayo, Waandishi, Masadukayo, na wale wote kwa namna moja au nyingine waliupinga mwanga ambao ndiye Kristo mwenyewe. Na leo kama ilivyokuwa nyakati zile za Yesu, watu hawa ni wale wote wanaojihesabia haki pasipo haki na kweli yenyewe. Ni wale wote wasiona upendo na huruma ya Mungu, na kutaka kuwa wasemaji wa Mungu kwa kujihesabia urafiki na Mungu. Ni wale wenye uhakika pasipo uhakika kwani hata wao wenyewe hawajijui sawasawa. Na hivi ndivyo wanavyojiinua, na kusema, “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo,” Yoh 9:31. Je, mwenye dhambi hana sura na mfano wake Mungu? Na kwa maana hiyo Mungu hana upendo na huruma tena kwa huyu aliyedondoka katika tope la dhambi? Ndugu yangu, Mungu mwenyewe anakuambia wewe na mimi tulio wadhambi kwamba, “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18.

Tatu; -ni taswira ya uovu wenyewe ikiwa ndilo giza lenyewe. Katika Injili ya leo Ndugu yetu kipofu ndiyo giza lenyewe ambalo Kristo aliye Mwanga analiondoa ingawa wakumbatia uovu hawapenda tendo hilo. Na sababu kubwa ya kutokupenda ni kwamba kile kilicho katika giza hufurahia kuwa katika hali hiyo hiyo isiyo kinzani. Ila kwa Mungu hali hii siyo ya kawaida na isiyovumilika. Naye Yesu anasema, “Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu,” Yoh 9:39. ‘Wanaoona wawe vipofu’ kwa maanisha wale wote wanaojiaminisha kuwa wanajua ilhali hawajui hubaki katika hali hiyo hiyo. Ni ulemavu katika ufahamu.

Maneno haya ya Yesu ‘Wanaoona wawe vipofu’ yanamtofautisha mtu ‘mjinga’ na ‘mpumbavu.’ Mjinga hujifunza kutoka katika hali yake ya kutokujua na kufika katika hali/hatua ya kujua asichokijua. Mpumbavu hana muda wa kujifunza kwa sababu anajiaminisha katika upumbavu wake kwamba anajua ilhali hajui chochote. Na hili ndilo jibu la Yesu kwa Mafarisayo waliotaka kujua kama na wao ni vipofu, Yoh 9:40. “Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41. ‘Kama mngekuwa vipofu msingkuwa na dhambi,’ kwa maneno mengine Yesu anawakumbusha kwamba, ‘kama mngekubali ujinga wenu wa kutokujua isingelikuwa kosa kwa sababu mngeukubali mwanga/kweli nanyi mngekuwa huru, Yoh 8:32.

Tukija kwenye taswira ya tatu, yaani, giza lenyewe ambalo katika Injili ya leo linawakilishwa na Ndugu yetu mwenye upofu halisi, Yesu anaweka wazi uhalisia wa tatizo lenyewe na kusema, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake,” Yoh 9:3. ‘Kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake’ kwa maanisha kwa upande mmoja hakuna lisilowezekana kwa Mungu hata kama kwa upeo na uwezo wetu wanadamu jambo hilo lishafika mwisho wake. Na kwa upande mwingine maneno haya ya Yesu yalibeba ujumbe mzito kwa kile alicho Kristo mwenyewe (Asili, Nguvu, na Mamlaka), yaani, Njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Ndani na katika Kristo Yesu yote hayo matatu (Njia, Kweli, na Uzima) yawezekana pasipo shaka yo yote. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa ndugu yetu yule Kipofu: “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,” Yoh 9:6, naye akapata kuona.

Pamoja na kuzongwa sana na kundi lile la wakumbatia uovu na vipofu wa kujinadi kama alivyo wathibitisha Yesu mwenyewe kuwa ni vipofu wanaoona, Ndugu yetu aliyepata kuona anatoa ushuhuda juu ya Kristo Yesu na kusema, “Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona,”Yoh 9:25. Huu ni ujumbe mzito sana kwa Mafarisayo na kwa wakati mwingine wewe na mimi tunaishi hali hii ya kifarisayo kwa nyakati tofauti tofauti. Je, tunaona sawasawa? Ndugu yetu aliyekuwa kipofu katika uhasili wake sasa anaona. Je, ndugu yangu unaona sawasawa? Yesu aliposikia wanamsonga sana kwa sababu la kile alichomtendea, alitaka kujua msimamo wa Ndugu yetu aliyeponywa kama kweli anaamini tendo lile. Yesu akamuuliza, “Wewe wamwamini Mwana wa Mungu?” Yoh 9:35. Naye akamjibu, “Naamini, Bwana. Akamsujudia,” Yoh 9:38. ‘Bwana akamsujudia,’ ni tendo la heshima kubwa sana mtu kupewa na hasa kutoka kwa Kristo mwenyewe.

Ndugu yangu, unaposimama katika kweli na haki ni tendo la furaha kubwa sana kwa Mungu ingawa katika ulimwengu wa giza yakupasa kulipa gharama yake. Tendo hili ni kuishi kweli ile na chapa ile ya Mungu ndani yako, Mwa 1:27. Ni kuwa kielelezo halisi cha upendo na furaha ya Mungu kama kiumbe chake. Chapa hii ya Mungu na uhasili wake ndani yetu tunaipoteza au kuififisha kwa kutenda dhambi.

Wito kwako na kwangu leo ni kwamba, ili tuwe salama mwili na roho yatupasa kuenenda “kama watoto wa nuru,” Efe 5:8c. Hapa ndipo tunadhihirisha kweli tu wanafunzi wa Kristo katika kweli na haki. Tuepuka bla bla nyingi zenye kumpamba Mungu kwa uzuri wa maneno yetu majukwani ili hali twatembea na upofu ulio tukuka kimwili na kiroho. Ndugu yangu tuliye safiri wote katika tafakari hii, “…tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli,” Efe 5:9. Kwa kuwa “…yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru,” Efe 5:13. Kristo Yesu ndiye Nuru yetu halisi, na kielelezo halisi cha hofu ya Mungu ndani mwetu. Tumwogope Mungu kwa kusimama katika kweli na haki.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa,” Yoh 9:41

Tusali:-Ee Yesu, tuondolee upofu wetu kama tunda la upumbavu wetu. Amina