viernes, 17 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI WIKI YA 7 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 7 YA MWAKA-A

Somo I: Law 19:1-2, 17-18

Zab: 103:1-2, 3-4, 8, 10, 12-13

Somo II: 1Kor 3:16-23

Injili: Mt 5:38-48

Nukuu

“Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu,” Law 19:2

“Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake,” Law 19:17

 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” 1Kor 3:16

“Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18

“Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?” Mt 5:46

 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48

TAFAKARI: “Msishindane na mtu mwovu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Bwana wetu Yesu Kristo anatushauri kwa msisitizo tusishindane na mtu mwovu. Ukweli ni kwamba kitokacho kwa Mungu ni chema na kama kilivyo kina umilele kwa sababu Mungu wetu ni Mtakatifu, Mkamilifu, na Wamilele. Ni kwa mantiki hii kwamba “hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu,” Lk 6:43-44. Wito wa Yesu kwetu tusishindane na mtu mwovu unalenga katika dhana nzima ya uovu, yaani, uovu kama ulivyo hauna umilele. “Msishindane na Mtu mwovu,” badala yake ni kuliweka tumaini lote kwa Bwana ambaye kwake ndiko kwenye chanzo halisi cha wema na jema, haki, na kweli. Hivyo, “usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake,” Law 19:17. Ni kumcha Bwana na kuuchukia uovu. Hivyo kumcha Bwana ni kuchukia uovu; Kiburi na majivuno, na njia mbovu, Na kinywa cha ukaidi pia nakichukia,” Mit 8:13.

Ndugu yangu, uovu kwa wingi wake hauna ‘umilele.’ Kama umilele ni maisha ya Utukufu wa Mungu wetu, uovu ambao kutokuwa na uzuri/mafaa, ni dhahiri kwenye umilele huo (Utukufu wa Mungu) hakuna uovu. “Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu,” Law 19:2. Uovu ni swala la muda tu. Kwa maana nyingine haki lazima itawale kuona kwetu, kufanya kwetu, na kuhukumu kwetu. Kwani Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti,” Mit 10:2. Wapo wengi kati yetu huishi kwa dhuluma au kuwezeshwa kwa dhuluma, au vyote viwili kwa wakati mmoja. Ndugu yangu, tenda haki kwa kila mmoja apitaye katika mikono yako nawe utalipwa mema. Uovu ni andaki la dhambi, na aliye zama katika andaki hili la dhambi ni vigumu kuubaini uovu wake kwa sababu hakuna nuru tena. “Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema,” Mit 13:21. Ni wazi lazima kuuchukia uovu, na kutenda haki.

Kwa nini basi Yesu anatuambia tusishindane na mtu mwovu? Kujua ukweli huu yatupasa kuutafakari wasifu wa mtu mwovu. Ushirika na mtu mwovu au ushindani na mtu mwovu mavuno yake ni udhalimu. Njia salama ni kumwepa mtu mwovu kwa kuchukia tabia yake hiyo ili ajirudi. “Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana,” Law 19:18. Na kwa sababu hiyo, usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu,” Kut 23:1b. Tabia hii ya mtu mwovu humtenga na Mungu kama asemavyo, kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu,” Kut 23:7c. Hivyo kama wewe ni kiongozi hapo ulipo, kwa nafasi yako wewe ni msimamizi wa kweli na haki kama Mungu anavyoamuru, “basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake,” 2Nya 6:23. Kiongozi asiyefanya hili, bali elewa wazi wale walio chini yake utawaliwa na hofu na ugumu wa maisha. “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” 1Kor 3:16. Je, kama zipo mamlaka za kuwajenga hofu kwa watu tukae kimya kama makaburi? La hasha!

Kukaa kimya kama kaburi kwa kuogopa kuchukiwa katika vita dhidi ya uovu na mtu mwovu ni kujivika aibu yako mwenyewe. Ila kuishinda hali hii ni kuushinda uovu na mtu mwovu. “Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18. Hivyo “hao wakuchukiao watavikwa aibu; Nayo hema yake mwovu haitakuwako tena,” Ayu 8:22. Kadiri ya historia ya ulimwengu huu na watu wake, hasa watu waovu, mwisho wao hauna mema. Kwa nafasi wanazokuwa nazo na kuzitumia vibaya hasa kukataa kweli na kuikandamiza haki, kilio cha wanyonge huamsha hasira ya Mungu. Hakuna mwenye hati miliki ya ulimwengu huu, na wengine kubaki kama wasindikizaji tu. Na “hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu, Na urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi. Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga; Na wazao wake hawatashiba chakula,” Ayu 27:13-14. Mungu huweza ruhusu kucheleweshwa kwa haki ya watu na yule mwovu kwa nia ya kumpa nafasi mwovu huyo kujirudi na kutenda haki, bali Mungu hawezi kufumbia macho kuchezewa milele upatikanaji wa haki hiyo kwa watu wake. Kila mmoja wetu ndani yake anayo chapa ya Mungu, Mwa 1:27. Je, mtu mwovu hupata wapi kiburi chake?

Tabia ya mtu mwovu huamini utetezi wa nguvu zake na kuiondoa kabisa hofu ya Mungu ndani yake. Ni kuishi kwa kujiamini kuliko pindukia. Huku ni kuiasi ile kweli iliyo ndani yako, yaani, ‘umeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,’ Mwa 1:27. “Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao,” 1Kor 3:19. Na kwa sababu hiyo, “Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake,” Zab 36:1. Pamoja na ujasiri huu usiokuwa na mwelekeo wa mtu mwovu, “Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali,” Mit 10:3. Hakika mwisho wa mtu mwovu hauna heri! “Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika,” Mit 11:18. Katika hali kama hii ni vigumu kumshauri mtu mwovu lile lililo jema kwa sababu hupenda kusikia yale ayapendayo na yaliyoujaza moyo wake. Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu,” Mit 17:11a.

Ni mara ngapi tunakutana na matukio ya kuchomwa watu barabarani nasi kwa kutokujua kilichojiri tunashiriki moja kwa moja katika uovu huo? Je, tunatoa hata muda kidogo kuhoji kwa nini mambo yamekuwa kama yalivyo? Je, ni kweli wanaopatwa na matukio kama hayo wanastahili kufa katika mtindo kama huo? Hata kama kuna sababu, je ni halali kuutoa uhai wa binadamu mwenzako kwa mtindo huo? USIUE! (Kut 20:13, Kumb 5:17, Mt 5:21; 19:18; Mk 10:19; Lk 18:20; Rum 13:9, na Yak 13:9). Msukumwa na uovu hana mshipa wa aibu, bali ufurahia uovu wake.

Wapendwa katika Kristo ni wito kwako na kwangu kwamba tuwe watu wa kusimama katika kweli na haki mara zote. Tuuchukie uovu kwa sababu hufifisha nuru ya Mungu ndani mwetu. “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote,” Rum 12:17. Tutende haki, na tuanze pale tulipo. Tuwe watetezi katika kweli na haki kwa wanyonge na wale wote wanaominywa haki zao. Hivyo “neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia,” Efe 4:29. Huku ndiko kuwa nabii kwa wakati wako.

Ndugu yangu, maisha ya ufufuko ni ushindi dhidi ya uovu. Na upendo ndio kielelezo chake. Naye Yesu katika upendo wa kweli anasema, “wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki,” Mt 5:44-45. Kumbe kupenda siyo tu kwa wale wanaotupenda. Yatupasa kufanya zaidi na kupenda zaidi. Tumwone Kristo kwa kila mmoja bila kujali historia yake iwe nzuri au mbaya. Kristo anatupa nafasi tena na tena ya kuwa wapya. Wakati fulani Mtume Petro alitaka kujua kipimo cha kusamehe, naye Yesu akamjibu, “sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini,” Mt 18:22. Kwa maneno mengine, ‘mpe uliyechukuzwa nawe muda wa kutosha.’

Upendo wa Mkristo anayeishi maisha ya ufufuko hana kipimo cha kuutoa upendo wake zaidi ya kupenda bila kipimo akiitafakari thamani ya kuokolewa kwake kwa sadaka ile ya mwenye haki pale Msalabani, yaani, Yesu Kristo. Na hii ndiyo maana ya maneno haya ya Yesu kwetu;Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?” Mt 5:46. Upendo wa kweli na maisha mapya ya ufufuko hayafungamanishwi na uhasili wetu wa kuzaliwa, bali kila siku ni vita ya kuushinda ubinadamu wetu na kuelekea nuru ile ya milele, yaani maisha ya milele. Na hii ndiyo maana ya maneno haya; “Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:47. Kuushinda ubinadamu wetu ndiyo dira na kuishi maisha ya malengo hapa duniani. Tunaishi kwa malengo, na malengo yetu ni kuufikia uzima ule aliyotuhaidia Yesu Kristo, “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:40. Kusudi la kila mmoja wetu ni kuwa kama aliyetuumba, yaani, kuupata ule ukamilifu.Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Ukamilifu huu, ambao ndio Utakatifu, ndicho kigezo cha kuishi maisha hayo ya umilele na Baba yetu wa Mbinguni huko Mbinguni.

Ndugu yangu, pamoja na yote aliyofundisha Kristo Yesu, na ukaribu wake kwa wote waliomzunguka, yaani, wakoma, wazinzi, watoto, wanawake, na wote waliotengwa na jamii, alitaka kujua hili kutoka kwao: Je, wamwonaje? Jibu la Mtume Petro lilisema yote kuhusu Yesu, yaani, “ndiye Kristo wa Mungu,” Lk 9:20. Je, leo wewe na mimi tuna ujasiri huu wa kuwauliza wale wanaotuzunguka na hasa tuliopewa dhamana na wao ya kuwaongoza? TAFAKARI na chukua HATUA!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima,” 1Kor 3:18

Tusali:-Ee Yesu na yote yangu, nijalie hekima kwa kutambua urefu na kina cha upumbavu wangu. Amina.

Fr. Edgar Tanga Ngowi, OSA.

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario