JUMAPILI YA 5 YA
MWAKA-A
Somo I: Isa 58:7-10
Zab: 112: 4-5, 6-7, 8-9
Somo II: 1Kor 2:1-5
Injili: Mt 5:13-16
Nukuu
"Je, Siyo
kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani
kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?" Isa 58:7
“Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya
yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata
nyuma ukulinde,” Isa 58:8
“Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu,
sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima,” 1Kor
2:1.
“Na neno langu na
kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu,
bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili
imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu,” 1Kor
2:4-5.
“Ninyi
ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu,” Mt 5:13.
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate
kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16
TAFAKARI: “Tu
chumvi ya dunia, na nuru ya ulimwengu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya ‘5’ ya mwaka ‘A’ wa
Kanisa. Kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa anatukumbusha kiini cha maisha yetu
hata dunia kama wafuasi hai wa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani, ‘tu chumvi ya
dunia, na nuru ya ulimwengu.’ Kwa mantiki hiyo, Habari Njema ya leo, yaani, Injili, inatupa mifano miwili ya kuwa vielelezo vya Mungu
aliye hai, na wakati huo huo kutoa ushuhuda wa kweli wa maisha yetu ya kila
siku. Vielelezo hivyo ni kuwa chumvi na nuru. “Ninyi
ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee?
Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu,” Mt 5:13.
Chumvi
kwa matumizi ya kawaida mbali na kuwa kikolezo cha kuleta ladha nzuri ya
chakula, ilitumika kuvihifadhi vyakula ili vitumike kwa muda mrefu. Ili kidumu
kwa muda mrefu, chakula kama nyama, samaki, na vinginevyo, vilisowekwa chumvi,
na hivyo havikuweza kuharibika. Chumvi katika mantiki hii na hasa katika somo
hili la Injili imetumika kama mfano halisi katika maisha ya kijamii. Mimi na
wewe ili tuwe kikolezo katika kujenga ushawishi wa maisha yenye malengo,
yatupasa kuchanganyika na watu. Tunaweza tu kuyajua maisha ya watu pale
tunapochanganyika nao na kuwa sehemu ya maisha yao, kwa lengo la kuwasaidia
kutoka katika hali zao duni na huzuni zao. Lengo hili lisipofikiwa chumvi kama
chumvi haina faida yoyote, zaidi ya kutupwa nje na kukanyagwa na watu, Mt
5:13b. Chumvi ni alama ya upendo hai, na upendo hai ni hali ile ya kuwa na
ufahamu wa kutosha wa uhalisia wa mambo, vitu, na watu wanao kuzunguka. Upendo
bila ufahamu ni upofu. Na hali hii ya upendo ni sawa na chumvi kupoteza ladha
yake.
Kielelezo
cha pili katika kutoa ushuhuda wa kweli wa maisha yetu ya kila siku ni kuwa
nuru ya ulimwengu. “Ninyi
ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:14.
Kimaadili yatupasa kuwa nuru. Nguvu ya kimaadili ni ushawishi mkubwa sana wa
watu kutii na kufuata yale tunayowaongoza wayafanye au wayafuate. Nuru ni
ushindi katika giza. Na nuru ni kinyume cha giza. Maendeleo ya watu kwa namna
yoyote ile ni tokeo la ustaarabu wao. Haya ndiyo maadili ya watu katika kuona,
kufikiri, kuamua, na kutenda. Pasipo ustaarabu, maadili pia huwa hovyo. Kwa
maana nyingine, palipo na utaratibu hapana akili. Nuru ambayo ndiyo maadili,
ustaarabu, na kielelezo cha ufahamu wa watu, yaani, akili, ni kitu cha kupewa
kipaumbele. “Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya
kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani,” Mt 5:15.
Watu
wengi hupatwa na mshangaa pale kunapokuwepo na msuguano kati ya kile akisemacho
mtu, na ustaarabu wake yaani, maadili aliyokuwa nayo. Mwenye maadili mazuri,
husukumwa na kutawala namna ya sema yake. Mtu wa mtindo huu uchagua maneno la
kusema kadiri ya hadhira yake, na somo kusudiwa kwa watu husika. Kwa maana
nyingine, mtu huwa na uchaguzi wa maneno ya kusema. Ni kwa maana hiyo kwamba,
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu
mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Nuru ya mtu ni nguvu ya
maadili ya mtu, ambayo ni kama nijamu. Ni vigumu kummiliki farasi katika mwendo
kama hauna nijamu. Nijamu kwa maneno mengine ndiyo nidhamu imuongozaye mtu
kufikia lengo lile kusudiwa. Nijamu ndiyo saumu ile afanyayo mtu siyo tu kwa
kuupa mwili wake nidhamu, bali pia kuuweka upendo katika matendo kwa ajili ya
wahitaji wanao mzunguka.
Hivyo,
saumu
ya kweli ni pamoja na kupatazama pale ulipokosea kutokana na uovu wako, na
kupigania haki za watu ikiwa ni pamoja na wale walioonewa kijamii kutokana na
mifumo miovu ambayo nawe ni sehemu ya mfumo huo. Haya ndiyo matendo ya huruma
yanayopaswa kuendana na Saumu ya kweli. Na hapa ni kuwa chumvi ya dunia, na
mwanga wa ulimwengu.
Matendo hayo ya huruma
ndiyo anayoyahoji Nabii Isaya; "Je, Siyo kuwagawia wenye njaa chakula
chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye
uchi, umvike nguo; wala usijifiche na
mtu mwenye damu moja nawe?" Isa 58:7. Kama najinyima kwa lengo la kufunga,
kile ninachojinyima kiwalenge wahitaji. Kundi hili la wahitaji tunao pande zote
na siku zote. Anza hapo ulipo! Naye Yesu anatuambia ukweli huu kama
alivyowaambia wale waliomnung’unikia juu ya Marhamu ambayo alimwagiwa kichwani
na Mwanamke yule mkosefu, ingeuzwa ili fedha ile wapewe maskini. Naye akawajibu
na kusadifu tendo lile la mwanamke yule kwa kusema, “maana
sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema;
lakini mimi hamnami sikuzote,” Mk 14:7
Wapendwa katika Kristo,
tunapofanya matendo haya ya huruma tunakutana na Yesu katika sura na maumbo
tofauti tofauti. Ni kwa namna hii somo la kwanza kutoka nabii Isaya linalandana
kabisa na ayasemayo Yesu katika Injili ya Mathayo 25:31-46. Hapa tunakutana na
Yesu aliye mwenye njaa, mgonjwa, mfungwa, aliye uchi, mwenye kiu, aliye
kifungoni nk. Huku ni kukutana naye
katika maisha yetu ya kawaida na ya kila siku. Mwisho wa siku Yesu anasema,
"Amin nawaambia, kadiri msivyomtendea mmoja wapo wa hao walio wadogo,
hamkunitendea mimi," Mt 25:45.
Ndugu yangu, hapa ndipo
ilipolala hukumu yetu ya mwisho. Wenye haki watakwenda kwenye uzima wa milele,
na wasio haki wataingia katika adhabu ya milele, (Mt 25:46). Bwana harusi
hatunaye tena. Huu ndio wakati muhafaka wa kufunga na kufanya toba. Zoezi hili
kwa Mkristo na kwa yeyote yule mwenye hofu ya Mungu ni zoezi na tendo endelevu
maisha yake yote. Yesu kesha tufundisha mengi tulipokuwa naye katika makuzi
yetu ya maisha ya kiroho, na sasa yatupasa kuyaishi. "Lakini siku zitakuja
watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga," Mt 9:15b. Kuyafanya
haya kwa uhakika, uaminifu, na ukamilifu wake ndiyo baraka na neema kwetu. “Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya
yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata
nyuma ukulinde, Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi
hapa,” Isa 58:8-9. Amina!
Hivyo ndugu yangu
ninaye safiri nawe katika tafakari hii, usisahau kamwe kundi la wahitaji katika
mfungo wako na maisha yako ya kila siku. Daima uwe mtu wa kutenda haki na
kuitetea pia pale inapokosekana au kukandamizwa kadiri ya nafasi yako na wito
wako.
Somo la kwanza la
tuonyesha, na kutufundisha namna ya kufanya toba ya kweli. Baada ya kutubu na
kuondolewa dhambi, malipizi au toba yetu ya kweli ni kujifunua na kujiweka
karibu na wale wote wanao itaji uwepo wetu, na kuwasaidia kadiri ya uwezo na
nafasi aliyotupa Mungu. Tunapolifanya tendo hilo kuwa letu kwa moyo mkunyufu,
kiwi yetu na Mungu inafanywa kama adhuhuri. "Na kama ukimkunjulia mtu
mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako
itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri," Isa 58:10. Huu ni wito pia wa kuwa chumvi ya dunia, na mwanga wa
ulimwengu.
Ndugu yangu, unapoishi
hapa duniani kuna mambo mawili yanaweza kukufika. Ukiishi vizuri unakuwa
muhenga. Yaani mtu aliyeishi vyema na ameacha kitu cha kuigwa na kusimuliwa kwa
vizazi vyote. Usipokuwa muhenga basi uwezekano wa kuwa mzimu ni mkubwa. Mzimu
ni roho ovu/mbaya. Hapa hakuna cha kuigwa wala kusimuliwa. Mtu anakosa na
kupoteza historia yake. Kuishi vyema na watu kwaitaji unyenyekevu kama msingi
wa fadhila zote. Unyenyekevu huu ni furaha ya Mungu. "Kumcha Bwana ni
maonyo ya hekima; na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu," Mit 15:33
Ni unyenyekevu huu
unaotusukuma tena na tena kupenda kuishi na kila mmoja wetu. Ni unyenyekevu huu
unatufanya kushuka chini kabisa kwa waihitaji. "Afadhali kuwa na roho ya
unyenyekevu pamoja na masikini, kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye
kiburi." Mit 16:19. Kristo ndiye kielelezo cha unyenyekevu wa kweli.
Hakika huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.
Tunachopaswa kuishi si
maisha ya ushindani wa hoja katika majukwaa, bali zaidi ni kuishi na kutoa
ushuhuda wa ukimya wa maisha ya kweli ya Ukristo wetu. Jambo hili ni muhimu
sana, kwani katika utulivu Mungu yupo na kuonekana. “Na baada ya tetemeko la
nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto
sauti ndogo, ya utulivu,” 1Fal 19:12. Huu ni wakati wa mitetemo ya Imani. Nasi
tusienende kadiri ya mitetemo hiyo. Tuitafsiri hiyo mitetemo nako tutakutana na
Mungu katika utulivu.
Ni
wazi katika kutenda lililo la Mungu, yaani, lenye kuongozwa na upendo wa kweli,
tujiandae kupata upinzani. Yule mwovu shetani hafurahii yaliyo mazuri na mema
yenye kuufunua Utukufu wa Mungu. Yesu Kristo mwenyewe alipata upinzani nyumbani
mwake mwenyewe. Katika hili Yesu anasema, “Amin, nawaambia ya
kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24. Je, kama hatukubaliki nyumbani kwetu na watu
wanaotufahamu iwe sababu ya kutokutenda mema? Jibu ni HAPANA! Tuendelee kutenda
wema na upendo kwa wote, kwa sababu asili ya upendo ni Mungu, uwepo wa upendo
ni Mungu, na Upendo ni Mungu. Kuyaona haya ya Mungu ndani yetu kwahitaji
unyenyekevu na kuepuka kujiinua kusiko na sifa wala siha. Hali hiyo ndani yetu
itatuwezesha kusema toka moyoni maneno haya ya Mtume Paulo; “Basi, ndugu
zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa
maneno, wala kwa hekima,” 1Kor 2:1.
Je, mazingira yetu leo
kama Taifa huru yanatuwezesha kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu?
Ndugu yangu, utakubaliana nami kwamba leo hekima imewekwa mfukoni, na silaha
kubwa ya utendaji wetu na hasa wale waliopewa dhamana hiyo na umma, ni ile ya
vitisho na kujengeana hofu. Hapana shaka kabisa baada ya miaka kumi ijayo
tutakuwa taifa ya ajabu kutokea katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.
Na sababu kubwa ni kutokuwa chumvi na mwanga. Tunajisikia salama zaidi kuishi
katika giza, na kufanya vitu kwa usiri.
Mfumo huu wa maisha ni
mfumo wa kutokujiamini ambako kumetokana na kutojitosheleza kwa kile
tulichojiaminisha kuwa tunaweza. Ni vyema kuzisoma alama na nyakati, na
kuzitafsiri kadiri la hitaji la wakati. Mang’amuzi ya maisha, yaani, historia
ya kule tulikotoka na changamoto zake, yataendelea kuwa mwalimu wetu mzuri.
Kujifanya vipofu kwa kukusudia, na kuwa viziwi kwa kuyaziba masikio kwa pamba
ikiwa ni kuogopa kukosolewa, ni dalili tosha za kupoteza ladha kama chumvi, na
wakati huo huo kulikumbatia giza. Anguko lake ni kubwa. Usalama wa leo na sasa
kama tokeo la kuminya haki za watu na hasa kuziba midomo yao, ni janga kubwa na
lenye kishindo kikubwa kesho ambayo sote tunaitamani.
Maisha ya binadamu
pamoja na changamoto zake, yamejawa tumaini la kwamba ‘kesho yaweza kuwa nzuri
zaidi.’ Hata mfumo wa gari una gia nne hadi tano za kusonga mbele, na moja tu
ndiyo ya kurudi nyuma, tena kwa utaratibu. Kuligeuza gari kwa kuangalia
ulikotoka na kupachika gia ya kurudi nyuma ukijifariji kuwa waenda mbele,
litokeapo jambo mbele ya safari ni vigumu sana kustahimili kishindo chake.
Ndiyo maana mara zote tunapigwa na butwaa kwa kutojianda na kutokujua chochote.
Hii yote ni kumbatio la hofu tusioijua. Hofu ni ugonjwa mbaya sana. Hofu
udumaza akili na ufahamu. Kwenye hofu huwezi fikiri sawa sawa. Kwenye hofu
huwezi kupanga sawa sawa. Na palipo na hofu hapana ubunifu na upekee wa vitu au
mambo.
Mungu ndiye anaye
wezesha yote ndani yetu. “Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno
ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya
wanadamu, bali katika nguvu za Mungu,” 1Kor 2:4-5. Sifa na Utukufu ni kwa Mungu wetu. Amina
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Vivyo hivyo
nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze
Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tujalie ujasiri wa kuwa chumvi na mwanga pale tulipo, na kuvishinda vitisho
vyenye kuijenga hofu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario