ALHAMISI WIKI YA 7 YA
MWAKA-I
Somo: YbS 5:1-10
Zab: 1:1-2, 3, 4, 6
Injili: Mk 9:40-49
Nukuu:
“Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako,”
YbS 5:
“Usichelewe kumrudia Bwana, wala usikawie siku ya siku; kwa maana
ghadhabu ya Bwana itatokea kwa ghafula, nawe utaangamia wakati wa kisasi,” YbS
5:7
“Wala usizitegemee mali za udhalimu, kwa kuwa hazitakufaidia lolote siku
ile ya hasira,” YbS 5:8
“Usipepete kwa kila upepo, wala usiipitie kila njia. Uwe mtu thabiti wa
akili, na liwe moja neno lako,” YbS 5:9-10
“Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa
ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41
“Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa
wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na
kutupwa baharini,” Mk 9:42
“Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto,”
Mk 9:49
TAFAKARI: “Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa
za moyo wako,”
Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli pasipo shaka kwamba maisha yetu hapa
duniani ni jukumu la muda mfupi. Masomo yetu ya leo yanatutaka tuyaone maisha
kama dhamana. Maisha ni dhamana tukijua tunaowajibu wa kufanya kwa muda na siku
tutakazokuwa hapa duniani. Ulimwengu huu ukiwa kama kiganja cha mkono, nasi
wanadamu kama vidole vya mkono huo, kwa pamoja na hasa tukijali umoja katika
utofauti wetu, tunao wajibu wa kupafanya mahali hapa-dunia, kuwa sehemu nzuri
ya kuishi kwa kila moja, huku tukiutamani ule umilele. Hivyo, “Usifuate roho
yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako,” Pamoja na ukweli kwamba
hakuna masikini asiyekuwa na kitu cha kutoa, na hakuna tajiri asiyekuwa
muhitaji, hakuna tokeo chanya iwapo tamaa za moyo ndiyo msukumo wa maisha yako.
Ukiruhusu hali hiyo itawale maisha yako ni rahisi sana kuzikanyaka haki za
wanyonge ili ukidhi hitaji la moyo wako. Ndugu yangu, tonge la ugali upata umbo
lake zuri la mviringo kwa sababu vidole vyote vitano vya mkono vimeshiriki
katika uumbaji huo vikijali umoja katika utofauti wao.
Jamii isiyojali umoja katika utofauti ili wote kwa pamoja walifikie lile
lengo na haki ya kuishi bila kubughudhiwa, hakika jamii hiyo kudongoka katika
machafuko ni swala la kufikia tu. Maisha ya mtindo huo hayawezi kamwe yakaepuka
hofu, yaani, kwa matajiri kwa utajiri wao, na masikini kwa umasikini wao. Ila
ukweli ni kwamba, “Mwanadamu hawezi kudumu katika fahari yake bila Mungu.”
Hali ya unyonyaji na kutokuwa na fursa sawa kwa wote, ni tatizo kuwa
sana leo katika jamii yetu. Mazingira na hali kama hii ndiyo anayoikemea Yakobo
Mtume na kusema, “Haya basi, enyi matajiri!
Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia,” Yak 5:1. Ni wazi kwa mashaka haya
wenyenazo-matajiri-huanza kwanza kujenga wigo katika eneo la ujenzi kabla
ujenzi wenyewe. Na hata baada ya ujenzi kukamilika, wigo huo uzungushiwa nyaya
za umeme na makaripio mengi. Hii yote ni hofu na dalili za kutokuwa na usawa na
fursa kwa wote katika jamii tunayoishi leo. “Usizitumainie mali zako,
wala usiseme, “Zanitosha basi.” YbS 5:1. Mwisho
wa siku Mtume Yakobo anaonya juu ya tabaka hili lisilojali kwa kujilimbikizia
mali. Naye anasema, “Mali zenu
zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo,” Yak 1:2.
Leo
kati yetu wapo watu wanaosali kila kukicha Mungu awape maisha marefu ili
waendelee kuvitumbua na kuvitafuna walivyojikusanyia hata kwa njia zisizo
halali. Ndugu yangu, “usiwe
mjasiri wa kutenda dhambi juu ya dhambi; wala usiseme, “Huruma zake zi nyingi,
ataniachilia dhambi zangu zijapokuwa zi nyingi,” kwa sababu rehema na ghadhabu
zatoka kwake, na hasira yake itawakalia wakosaji,” YbS 5:5-6. Vile vile kati yetu wapo, tena walio wengi
wanaosali kila siku Mungu awapunguzie ugumu wa maisha. Hawa ni wale wasio na
uhakika wa mlo wa asubuhi na mchana, na jioni pale tu wakibahatika.
Wapendwa
wana wa Mungu, aliyenacho tena cha ziada na kuona jirani yake akitaabika bila
kumnyooshea mkono wa heri, ajue anajikolezea jehenam angali hapa hapa duniani. Wito kwako na kwangu ni huu: “Usichelewe
kumrudia Bwana, wala usikawie siku ya siku; kwa maana ghadhabu ya Bwana
itatokea kwa ghafula, nawe utaangamia wakati wa kisasi,” YbS 5:7. Hakika, “dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na
kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba
katika siku za mwisho,” Yak 1:3. Pasipo shaka, siku ya mwisho ya tabaka hili ni
mateso yasiyo kifani. Kuepuka kadhaa na mateso hayo, Yesu anatuasa, “Kwa kuwa
ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa
Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41.
Wapendwa
katika Kristo, embu
tazama maisha ya wakulima yalivyo ya taabu na gharama kubwa katika uzalishaji!
Embu tazama wanavyonyongwa katika bei za mazoa yao! Tazama kelele za wakulima
hao zinavyopotea hewani bila kusikilizwa! Ndugu zangu na wote wale msiowasikia
kelele za wakulima hawa, na ninyi wenye mamlaka, “angalieni, ujira wa wakulima
waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio
vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi,” Yak 5:4. Ni Mungu
huyu aliyetajiri kwa kumwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14, sote katika utofauti
wetu kwa vile ndivyo inavyompendeza kutuumba, Mwa 1:27, na kuufunua utukufu
wake, katufanya sote matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo,
jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba
ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Je mimi niliye Mkristo
na tajiri-katika mali, najua ukweli huu na kuwajibika kadiri na uwezo na
utajiri aliyonipatia Mungu?
Leo kuishi maisha ya anasa ndiyo fahari na kujulikana na wengi toka
Misikitini, Makanisani, na Serikalini. Ndugu yangu, “wala usizitegemee mali za
udhalimu, kwa kuwa hazitakufaidia lolote siku ile ya hasira,” YbS 5:8. Saratani
hii imeingia hata katika siasa zetu na hatma ya uongozi. Uongozi umekuwa wa
kuhudumiwa na siyo kuhudumu. Kila mmoja anataka kuwa mkubwa na kuogopwa. Hali
na mtazamo huu kijamii ubinya kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki kwa wote,
na mbaya zaidi kwa wale wasionacho. Hii ni kwa sababu kama asemavyo Yakobo
Mtume, “mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha
mioyo yenu kama siku ya machinjo,” Yak 5:5. Kwa mtindo huu, duara la umasikini
linaendelea kutanuka na kuwa kubwa zaidi, huku watu wachache wakijineemesha
jasho la walio wengi. Mnyonge hana pa kushika kwa sababu kote kuna kaa la moto.
Wale wachache wanaojitokeza na kukemea unyonyaji huu uliokithiri wanachukuliwa
kama waalifu wa kivita na kufichwa kusikojulikana na hata kupoteza uhai wao.
“Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi,” Yak 5:6.
Ndugu yangu, kama tujuavyo maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda
mfupi, na kwa upande mwingine kuwa ni dhamana, basi tujue hata mahangaiko haya ya wengi wanyonge
ni ya muda tu. Jambo la muhimu la kuondokana na hali hii ni kila mmoja kujali
na kuwajibika kwa nafasi yake, na kuuchukia uovu kwa nguvu zake zote. Wosia ni
huu: “Usipepete kwa kila upepo, wala usiipitie kila njia. Uwe mtu
thabiti wa akili, na liwe moja neno lako,” YbS 5:9-10, yaani, jema libaki kuwa
jema, na ovu lichukiwe kama lilivyo ovu.
Wapendwa
wana wa Mungu, tutende haki kwa usawa tukimwogopa Mungu. La sivyo tuwe tayari
kwa haya ayasemayo Kristo Yesu juu ya wadogo na wanyonge katika jamii. “Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa
wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na
kutupwa baharini,” Mk 9:42. Kufungwa jiwe na kutupwa baharini kulimaanisha
kupotea kabisa na kutokuonekana machoni mwa watu. Tunajua mwili ulio zama
kwenye maji baada ya muda huelea. Hivyo kwa kufungiwa jiwe na kutupwa baharini
hakuna tena uwezekana wa kuelea juu. Basi ni vyema tukavichambua kwa makini
viashiria (vilema) vyote vile vinavyotuweka mbali na upendo wa Mungu na watu
wake. Naye Yesu katika hili anatushauri kwamba, “Na mkono wako ukikukosesha,
ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili,
na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; ambamo humo funza wao hafi, wala moto
hauzimiki,” Mk 9:43-44. Baadhi yetu tumekuwa watu wa kujilimbikizia mali tu
kila kukicha hata kama hatuzihitaji. Basi ni vyema ukautazama vizuri mkono wako
na kupunguza kasi hiyo ya kujilimbikizia mali na nyingi zikiwa za dhuluma.
Wapo pia kati yetu kazi yao ni kuvuruga utarajibu wa kweli na haki
uliopo ili wengi wakose na wachache akiwemo na yeye wafaidike na kuneemeka.
Hivyo mienendo hiyo siyo sahihi na wala haimpendezi Mungu. Hii ni kama miguu.
“Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete,
kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo
humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki,” Mk
9:46. Basi tutazame mienendo yetu na kujali zaidi faida ya wengi. Jicho likiwa
mfano wa ufahamu wetu katika kuona, kuchambua (mema na mabaya), na kufanya kwa
weledi, ufahamu huu wapaswa kujali uzalendo wa kweli katika vita dhidi ya uovu
kwenye jamii yetu leo. Hivyo, Yesu anatushauri pia, “Na jicho lako
likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu,
una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto
hauzimiki,” Mk 9:47-48. Ni jambo la kusikitisha sana tunapoona mtu msomi na
aliyejaliwa ufahamu wa kutosha wa mambo mengi anakuwa ndiye kichokoo cha kwanza
cha maovu katika jamii. Ndugu yangu, elewa umepewa dhamana kubwa sana mbele ya
watu wa Mungu na Taifa yako.
Wapendwa wana wa Mungu, Nabii Isaya anasema maneno haya mazito kwa kila mmoja
wetu, “wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika
wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu
sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?” Isa 33:14. Mungu mwenye haki na
mwenye kutuhesabia haki atampa kila mmoja kadiri ya matendo yake pale
tunapotimiza wajibu na sababu ya kuumbwa kwetu. Hii ndiyo ‘chumvi ya moto’
anayoisema Yesu, akiimaanisha kwamba tusipo vishinda vilema vyetu vyenye
kutupeleka katika kutenda dhambi, basi tuwe na uhakika wa mateso yasiyo na
mwisho. “Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto,” Mk 9:49. Ndugu yangu, maisha ni dhamana.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi
ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake,” Mk 9:41
Tusali:-Ee Yesu Mwema, niumbie moyo safi ndani yangu, ile niweze
kila kuvishinda vilema vyangu, na niwe tayari kuyafanya mapenzi yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario