viernes, 24 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 8 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 8 YA MWAKA-A

Somo I: Isa 49:14-15

Zab: 62:2-3, 6-7, 8-9ab

Somo II: 1Kor 4:1-5

Injili: Mt 6:24-34

Nukuu

“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

“Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1

Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2

Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24

TAFAKARI:Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ahadi ya Mungu kwetu ni kutokutusahau katika hali zote hata kama kibinadamu jambo hilo linawezekana. Mungu hawezi kutusaha. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

Maisha yetu ni mpango wa Mungu na kwa malengo ya Mungu. Mpango huu unarahisishwa kwa uwepo wa Mwanaye Yesu Kristo, ambaye hajifanyii mambo yake pasipo Mungu Baba aliyempeleka. “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka,” Yoh 5:30

Ni kwa mtazamo huo, Yesu katika Injili ya leo anatupa angalizo na kusema, “hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi tu. Je, kwa nini twapaswa kumtumikia bwana mmoja? Sababu ya wazi na ya moja kwa moja ni kuondoa ile roho iliyojigawa vipande vipande. Mfano; kama umepata mialiko miwili ya harusi inayofanyika muda ule ule na siku ile ile, yakupasa kuchagua moja wapo utakayokwenda hata kama zote zina uzuri au zimetofautiana. Kuchagua huku ndiko Yesu anapotushauri kuutafuta kwanza ufalme wa Mbinguni, na kuondoa roho ya kujigawa vipande vipande. Naye Yesu anasema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33. Ndugu yangu, unaloneno zaidi ya ukweli huu wa Bwana wetu Yesu Kristo?

Ni kweli isiyo shaka kwamba ukishaingia katika mfumo huu, na mtazamo huu wa fundisho hili ya Yesu, kuutafuta ufalme wa mbinguni kwanza, huwezi kupata “presa”-shinikizo la damu unapowaona watu wakipigana vibega kwa kumwangaikia mfalme tumbo na utajiri wake. Kristo anapokuwa katikati ya yote, yeye atakupatia kadiri ya mahitaji yako na kwa wakati wake. “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mt 6:34. Hata hivyo hapa Kristo Yesu hamaanishi tujikalie tu bila kujishughulisha na kufanya chochote kuhusu maisha yetu. Ndugu yangu yatupasa kumuishi Kristo leo na sasa katika yale yote yampendezayo. Mungu kamwe habariki utupu. Kumbuka ishara ile ya kwanza alioyofanya Yesu kule Kana, Yoh 2:1-11. Ingawa kesho inasikika akilini mwetu, tuelewe kesho hiyo ipo mikono mwa Mungu katika uhalisia wake.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kama tunajua kwamba hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake, Rum 14:7, maisha yetu bila Kristo yatakuwa na walakini mkubwa. “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1. Kama tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu, maisha yako hapa duniani na kadiri ya wito wako ni dhamana kubwa kwa sababu yeshathaminishwa kwa damu ya Yesu pale Msalabani. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, watambua thamani ya maisha yako kama mfuasi wa Kristo?

Wapendwa wana wa Mungu, thamani ya Ukristo wako itategemea sana na namna unavyo mwakilisha Kristo kama wakili wake katika kweli na uaminifu. Ukristo wako usibaki katika jina tu, bali imani ya kweli ndani yako, na Kristo akiwa ndiye kielelezo chako katika yote. Na “hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2. Ni kuwa mwaminifu katika kuifuata njia yake, yaani, kuubeba msalaba wako kwa uaminifu bila kumsaliti Kristo. Ni kuiishi kweli kadiri ya mafundisho yake Kristo, na zaidi amri ile ya upendo.

Ukipenda kama alivyopenda Kristo utafanya yote yampendezaye Mungu. Na mwisho ni kuuishi uzima wa kweli kwa kushiriki Masakramenti katika hali ya usafi wa moyo, na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hali hii ya usafi wa moyo ndiyo impelekeayo Mtume Paulo kusema kwamba, “Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu,” 1Kor 4:3. Mara zote tuongozwe na dhamiri safi na yenye hofu ya Mungu.Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana,” 1Kor 4:4.

Kuujua wajibu wako na kuutimiza kadiri ya takwa lake na kwa upendo ndiko kutakapo kuhesabia haki. “Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu,” 1Kor 4:5. Ndugu yangu, usichoke kutimiza wajibu wako kwa upendo. Hakuna aliyefilisika kwa kupenda na kutoa kwa upendo.

Bwana na Bibi Baraka Mfaume baada ya kutembea umbali mrefu wakiwa wametoka kuhemea, waliliona genge upande wao wa kushoto palipokuwa wanauza machungwa. Basi Bibi Baraka alinunu machungwa manne, yaani, mawili kwa ajili yake, na mawili  kwa ajili ya mmewe. Kwa kiu na njaa ile walioyokuwa nayo, Baba Baraka Mfaume aliyashambulia machungwa yake mawili bila huruma huku wakiendelea na safari yao kuelekea nyumbani akewe akiwa amebeba mkoba wake na ule wa mmewe.

Mara walipo fika nyumbani walipokelewa kwa furaha na watoto wao John na Maria. Mara Bibi Baraka aliomba aletwewe kisu, na mara akayatoa machungwa yake mawili kwenye mkoba wake. Akalipasua chungwa moja katikkati akampa kipande Maria, na kingine akampa John. Huku macho yakiwa yanamtoka Baba Baraka kama mjusi aliyebanwa na mlango, Mkewe akapasua chungwa la pili katikati kisha akampa mmewe kipande kimoja, naye akabaki na kipande kilichobaki. Huu ndio upendo wa Mama wenye kujali na kuwajibika aliousema Nabii Isaya katika somo letu la kwanza. Hata hivyo, upendo wa Mungu kwetu ni zaidi ya mfano wa upendo huu wa Mama. Mungu anatupenda upeo upeo, Yoh 12:24. Huyu ni Mungu asiye tusahau kamwe iwe tunapomtegemea au kumsahau katika hali yoyote ile, Isa 49:15. Akina Baba na wale wote wasio na upendo kama mama mpo?

Tumsifu Yesu Kristo!

Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33

Tusali:- Ee Yesu, uwe kitoshelezo chetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario