JUMATATU
WIKI YA 8 YA MWAKA-I
Somo:
YbS 17:20-28
Zab:
32:1-2, 5, 6, 7
Injili:
Mk 10:17-27
Nukuu:
“Kwake makosa yao
hayakufichika, na dhambi zao zote zipo mbele zake,” YbS 17:20-21.
“Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao
wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani,” YbS 17:27
“Shukrani hukoma kutoka
kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya
atamhimidi Bwana,” YbS 17:28
“Yesu akamkazia macho,
akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo
vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk
10:21
“Yesu akawakazia macho,
akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana
kwa Mungu,” Mk 10:27
TAFAKARI:
“Akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na
mali nyingi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ikiwa wewe ni Mkristo uliye hai ni vyema ukafahamu thamani ya Ukristo wako,
yaani umekombolewa kwa Damu ya thamani kubwa sana, yaani Mwana-kondoo, Yesu
Kristo. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha
au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa,
yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hivyo maisha yako na yangu hapa duniani
tunapaswa kuyasalimisha yote na kwa asilimia zote kwa Yesu Kristo Mwana wa
Mungu aliye hai. “Kwake makosa yao hayakufichika, na dhambi zao zote zipo mbele
zake,” YbS 17:20-21. Tendo hili la kujisalimisha ndiko kuabudu kwenyewe kuliko
hai na kwenye kumpendeza Mungu.
Kujiita Wakristo bili
Kristo ni kupotea muda kabisa kwa sababu kwa kufanya hivyo maisha hayo hayana
njia, kweli, uzima (tungali hapa duniani) na ufufuo (maisha ya uzima wa
milele), Yoh 14:6. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii,
tungali hapa duniani wakuhimidiwa ni Mungu, na kwa njia ya pekee na ufunuo
uliokamilika kwa Yeye aliyemwilishwa (Neno), Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa Kristo
Yesu kuna Njia, Kweli, Uzima, na Ufufuo wa wafu. Kwake Yesu na kupitia kwake
tunaheshabiwa haki na Mungu kwa wana na warithi wa ufalme wake Mungu. Na kwa
namna hiyo, “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema
zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka
kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio
na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4. Ndugu
yangu, tumaini yenye uzima lipo kwa Kristo Yesu, na siyo kwa kile tulicho au
yale tunayoyamiliki hapa duniani. “Kwake Yeye sadaka za mtu ni kama pete ya
muhuri, naye ataweka akiba ukarimu wa wanadamu kama mboni ya jicho,” YbS 17:22.
Tungali hapa duniani tu waangalizi wa muda mfupi kwa yale tunayoyamiliki. Kwayo
(tunayoyamiliki) kama yalivyo hayana umilele ingawa tuliyakuta na tutayaacha.
Hivyo wapendwa katika
Kristo, yatupasa mimi na wewe kuyashinda majaribu tukiwa na ufahamu kwamba
‘maisha ni jaribu,’ na kulishinda jaribu ndipo kunakotupatia Imani yenye
thamani kupita yote tuwezayo kuwa nayo. Vita vyetu vya kiimani kama
anavyotufundisha ni kulishinda jaribu. Tokeo la kubebwa na ulimwengu wa vitu ni
anguko kubwa la ‘uzuni.’ Furaha ya kweli ipo pale tunapoyasalimisha yote kwa
Kristo Yesu. Kristo awe tegemeo na msukumu wa yote tuyafanyayo, na tumuone kwa
wengine yale yote tuyafanyayo katika jamii tunayoishi. “Hatimaye atatokea na
kuwapa thawabu, naye atawalipa waovu uovu wao juu ya vichwa vyao,” YbS 17:23.
Lengo hapa siyo tu kuzishika au kuzifahamu amri za Mungu kama ndege yule
‘kasuku,’ bali amri hizo za Mungu zimulike uhai uliopo ndani yetu binafsi na
wale wote tuliowekwa dhamana kwao ikiwa ni pamoja na wale wenye uhitaji wa
pekee.
Ndugu yangu bila shaka,
hii ndiyo sababu ya Yesu leo kwenye Injili kumuuliza yule Mtu aliyetaka kujua
afanye nini ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu. Yesu anamuuliza, “Wazijua amri,
Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na
mama yako,” Mk 10:19. Kwa moyo wa ukunyufu na furaha Mtu yule anamjibu Yesu,
“Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu,” Mk 10:20. Jibu hili linamfurahisha
sana Yesu. Ila Bwana wetu Yesu Kristo hakuishia hapa tu. Yesu anakutaka wewe na
mimi tufanye zaidi kwa ya yale ya kawaida (katika kupenda, kutenda, na hata
kukopesha, Lk 6:32-34) kwani hayo hata waovu huyafanya. Hivyo “Yesu
akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda,
ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni;
kisha njoo unifuate,” Mk 10:21. Hapa ndipo penye utata na tatizo kubwa kwangu
na kwako. Wengi wetu ni vigumu sana kujibadua katika ulimwengu wa vitu. Tupo
tayari “kufa na tai shingoni” kuliko kuviachia vitu na kuwa huru: kifikra,
kiutendaji, na kihuduma, ili kuwa huru kufanya tu yale yaliyo ndani yetu kadiri
ya mpango wa Mungu. Ndugu yangu, Mungu wetu, “huwajalia wale watubuo kurudi, na
wao wanaopotewa na saburi huwafariji,” YbS 17:24. Hili hutoweza kulifanya ikiwa
utajiri na mali ndicho kielelezo cha maisha yako. Kwa kufanya hayo na
kujishikilia kwa hayo hakuna fadhila ndani yake. “Bali wapendeni adui zenu,
tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa
nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa
wasiomshukuru, na waovu, na ndani yake hakuna fadhila,” Lk 6:35.
Hitaji hili la pili, yaani,
‘kufanya zaidi’ ili kujipatia fadhila linakuwa anguko na uzuni mkubwa kwa mtu
yule aliyekuwa na hamasa kubwa sana ya kuurithi ufalme wa Mungu. “Walakini yeye
akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali
nyingi,” Mk 10:22. Ndoto na furaha
yake ya kuujua na kuurithi ufalme wa Mungu anakubali iyeyuke kwa sababu ya
ulimwengu wa vitu. Ndugu yangu, leo hata
ungekuwa na utajiri wa aina gani kuna mambo hutoweza kuyapata kwa utajiri wako
huo hata kama bado tungali hapa duniani. Ngoja nikujuze machache; kwa utajiri
na fedha ulizonazo waweza kuwa na marafiki wengi ila siyo wa kweli na
watakatifu. Kwa fedha na mali ulizonazo waweza kujenga nyumba nzuri, ukawa na
kitanda kizuri cha dhahabu (na chenye nakshi zote), ila huwezi kuununua
uzingizi. Kwa fedha na mali ulizonazo leo hapa duniani unaweza kwenda kokote
upendapo ila Mbinguni ni swala la kuhesabiwa haki na mastahili ya Mungu
Mwenyewe.
Ndugu yangu, kwa fedha na mali ulizonazo
leo waweza kununua chakula kizuri na chenye gharama, kinywaji kizuri na chenye
gharama, ila hutoweza kununua hamu ya chakula hicho. Kwa fedha na mali
ulizonazo waweza kuwanunua watu na kuwahonga watu, ili utimize hazma yako ya
kuwa kile utakacho, ila hutoweza kumnunua Mungu wala kumrubuni. Mwisho wa siku
Mungu atakudhihirishia kile kilichokuwa haki yako mbele ya watu wake
uliowarubuni. Ayubu aliyepatwa na majanga makubwa katika maisha yake, na
kupoteza yote aliyokuwa nayo, anatuambia hivi kuhusu mali na utajiri; “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi
tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na
libarikiwe,” Ayu 1:21. Utajiri wake na mali alizokuwa nazo haikuwa sababu ya
kumkufuru Mungu hata pale ilipoondolewa yote pasipo yeye-Ayubu, kwenda kinyume
na matakwa ya Mungu. Maandiko Matakatifu
yanatuambia, “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia
Mungu kwa upumbavu,” Ayu 1:22. Kwa nini basi mimi na wewe twaulinganisha au
kuufananisha uhai wetu na mali tulizonazo na kumkufuru Mungu? Mali tunazoongelea
hapa ni zote ikiwa pia zile zisizoshikika kama vipaji na karama alizokupa
Mungu. Mbona basi twavimba vichwa na kujisahau pale tunapofanikiwa kutokana na
zawadi aliyotupa Mungu ikiwa ni pamoja na ufahamu wa kiwango cha juu? Ndugu
yangu, hayo yote si mali yako. Umekopeshwa au kupewa kwa muda tu, na ukiwa
navyo ni kwa faida ya wengine. Huku ndiko kushirikishana utajiri wa Mungu na
Utukufu wake. Mali yako halali ni dhambi zako. “Basi umrudie
Bwana na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo,”
YbS 17:25. Hii ndiyo njia salama ya kuurudisha uhusiano wenye siha kati yako na
Muumba wako.
Hivyo
ni vigumu sana, tena sana, kuingia katika Ufalme wa Mungu tukishikamana na
kulandana na vitu na katika fursa hiyo kutokumpa Mungu nafasi na stahili zake.
“Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida
wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” Mk 10:23. Kushikamana huko na vitu
hakutupi heri yoyote, na badala yake ni anguko kubwa. Jambo la kufanya ni hili:
“Umgeukie tena Yeye aliye juu, uyageue maovu, uyakirihi yaliyo machukizo,” YbS
17:26. Bila ukiri huu ni kupotea muda ilhali maisha yetu hapa duniani ni jukumu
la muda mfupi tu.
Ndugu yangu, ni wale tu
walio masikini wa roho (wenye nafasi ya Mungu ndani ya mioyo yao, Mt 5:3, na
wasiokata tamaa wanapoudhiwa kwa kutenda haki kwa wote, Mt 5:10, ndio
watakaourithi Ufalme wa Mbinguni. “Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao
wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani,” YbS 17:27. Na kwa sababu
hiyo, kama washikamana na ulimwengu huu wa vitu na kutokumpa Mungu nafasi, “Ni
rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika
ufalme wa Mungu,” Mk 10:25. Fundisho hili lenye kweli yote linakuwa mshangao
mkubwa kwa wanafunzi wa Yesu, yaani, wale Thenashara. “Yesu akawakazia macho,
akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana
kwa Mungu,” Mk 10:27. Hivyo, ukijiachia kwa Mungu bila kujibakiza yote
hufanyika kwako kadiri ya mapenzi yake Mungu na hitaji lako na wale wanaokuzunguka.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Shukrani hukoma kutoka kwa wafu,
kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi
Bwana,” YbS 17:28
Tusali:-Ee
Yesu, kwa Upendo wako tujalie Neema na Hekima ya kufahamu yale tunayohitaji ili
kwa namna hiyo hiyo tuweze kufahamu hitaji au mahitaji ya wengine.
No hay comentarios:
Publicar un comentario