jueves, 16 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 6 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 6 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 11:1-7

Zab: 145:2-3, 4-5

Injili: Mk 9:1-13

Nukuu:

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1

“Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri,” Ebr 11:3

 Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu,” Mk 9:4

“Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye,” Mk 9:7

TAFAKARI: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuzikabili sintofahamu za maisha kadiri ya wito na mazingira yako wangu, yanipasa kuwa na uelewa sahihi wa imani ya kweli. Waraka huu kwa Waebrania unaelezea “imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1. Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni ‘kutokuwa na shaka yoyote ilhali ukiwa umeyakabidhi yote mikono mwa Mungu katika maana ya ufahamu wa kweli wa kile ukiaminicho, na wakati huo huo umaana wake (rationality and significativity).’ Imani tu bila kubeba ufahamu wake na umaana wake ni kishawishi kikubwa cha kuanguka kwenye ujinga na upumbavu. Ni kwa mantiki hii ‘imani siyo ushuhuda tu uliobebwa katika miujiza na alama nyingine kama hizo.’ Imani ni zaidi ya hayo licha kwamba kama yapo katika kweli uimarisha imani changa. Imani ni zaidi ya ishara tuzionazo kwa sababu, Imani “ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1b.

Imani katika ufahamu na umaana ujidhihirisha katika haya yafuatayo kadiri ya somo letu hili la leo. Kwanza kabisa Imani huongeza na kuimarisha ufahamu wetu. Ni kwa mantiki hiyo “kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri,” Ebr 11:3. Ni kama afundishavyo Mtakatifu Agustino kwamba, ‘imani utupeleka katika kuelewa, na kuelewa huimarisha imani.”

Pili, imani katika kuyaishi na kuyatenda kiadili huwezesha mtu kuhesabiwa haki. Ila jambo la kutofautisha hapa ni hili; utakatifu wa mtu siyo tokeo la mafanikio yake kutokana na ‘weza yake’ ya kibinadamu, bali ni neema ya Mungu ifanyayo kazi ndani ya mtu. Ni kwa maana hiyo, “kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena,” Ebr 11:4.

Tatu, imani utuvusha kwa yasiyowezekana kibinadamu. Ni “kwa imani Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alimhamisha; maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu,” Ebr 11:5. Kweli hii inathibitishwa pia na Yesu, na kusema, “kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe habarini, nao ungewatii,” Lk 17:6.

Nne, Imani utuweka karibu na Mungu, na umpendeza Mungu. Hivyo, “pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao,” Ebr 11:6. Leo kati yetu bila kuona, na kuwa na ushahidi shikika, hakuna sababu kimantiki kuamini uwepo wa Mungu. Ila yapo mengi tu ya kimantiki ambayo hayahitaji vigezo vya kushikika wala kuonekana ili kuamini. Mfano, huwezi kuwa mrefu zaidi yako mwenyewe.

Tano, Imani huwezesha lisilo kimantiki kadiri ya mang’amuzi ya mwanadamu. “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani,” Ebr 11:7. Leo wewe na mimi tu warithi wa ufalme wa Mungu kwa sadaka ile aliyoitoa Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani.

Hivyo kwa kubadilika kwake sura Yesu Kristo kuliko ambatana na kutokewa kwa Eliya na Musa, kunathibitisha ufunuo kamili wa Mungu kupitia mwanaye Mpenzi Yesu Kristo, na kukamilika kwa unabii wote, yaani, Eliya, na sheria na mamlaka yote yaani, Musa. “Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu,” Mk 9:4. Hivyo hapana tena ufunuo ulio wa wazi na kamili zaidi ya ufunuo huu wa Mungu kupitia mwanaye Mpenzi. Tendo hili linathibitishwa na sauti ya Mungu mwenyewe kwa viumbe vyote: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye,” Mk 9:7. Ndugu yangu, Je, unafuata sauti gani katika maisha yako?

Sauti hii kutoka mbinguni inampata Yesu Kristo heshima, mamlaka, na utukufu. “Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,” 2Pet 1:17. Nasi tunapoisikia sauti hiyo na kuishi ukweli huo, tunajazwa nguvu, heshima na utukufu kwa kuishi ndani na katika Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, zipo sauti nyingi katika maisha yetu. Je, sauti hizo zinatupeleka karibu na Yesu au zinatutenganisha na ukweli wake? Kusikia sauti hii ni kuyafanya mapenzi yake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1

Tusali:-Ee Yesu na Mchungaji wetu, kamwe usitutenge na sauti yako. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario