IJUMAA WIKI YA 5 YA MWAKA-I
Somo:
Mwa 3:1-8
Zab:
32:1-2, 5, 6, 7
Injili:
Mk 7:31-37
Nukuu:
“Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya
bustanini twaweza kula;lakini m atunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu
amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa,” Mwa 3:2-3
“Nyoka
akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku
mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu,
mkijua mema na mabaya,” Mwa 3:4-5
“Mwanamke
alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa
kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na
mumewe, naye akala,” Mwa 3:6
“Wakafumbuliwa
macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini,
wakajifanyia nguo,” Mwa 3:7
“akatazama
juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka,” Mk 7:34
“Mara masikio yake
yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri,” Mk 7:35
“Akawaonya wasimwambie
mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza
habari,” Mk 7:36
“wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena,
Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme,” Mk 7:37
TAFAKARI:
“Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.”
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na ukweli kwamba zipo sababu nyingi ambazo zaweza mfanya yeyote yule
kutokuwa na furaha ya kweli ndani yake, hii ni dhahiri kwa mwanadamu yeyote
yule, yaani, “kutokujipokea kama ulivyo.” Hili linapochukuwa nafasi ya kwanza
katika maisha yako mambo mawili yaweza kutokea:- moja, kuishi maisha linganishi
mara zote. Pili, kuishi uvuli wa mambo na siyo uhalisia wake. Embu tuzame
kidogo katika mamba haya mawili.
Kuishi maisha
linganishi msingi wake ni ule ule yaani, kutokujipokea kama ulivyo, na kupoteza
mwelekeo mzima wa maisha yanayoongozwa na malengo. Chombo chochote kile cha
usafiri kinapokosa mwelekeo ukubwa na chochote kile kingali safarini. Ajali kwa
chombo kama hiki kisicho na mwelekeo ni kitu cha kufikia tu. Wapo wengi
miongoni mwetu kama asemavyo Mtume Paulo, “maana twasikia kwamba wako watu
kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini
wanajishughulisha na mambo ya wengine,” 2The 3:11. Huku ni kuishi maisha
yasiyokuwa na malengo, na chanzo chake ni kutojijua na kujipokea. Kwa hali hii
hakuna mabadiliko hata angekuja kwa mara nyingine Bwana wetu Yesu Kristo.
Mtindo huu wa maisha na
mazingira yake kamwe hayawezi kukupa furaha. Unapoteza muda mwingi kujitafuta
nje ilhali kile ulicho ki ndani yako. Usipogusa kweli hii ndani yako hutoweza
kuwa na furaha.
Ndugu yangu, hakuna
filamu nzuri na ya pekee kama filamu ya kwako mwenyewe. Hata hivyo filamu hii
yahitaji ujasiri mkubwa sana kuitazama kwa sababu inatisha sana. Je, ujasiri
huo unao? Anza leo kujipekuwa. Mkalishe kwenye kiti huyo wa ndani, nawe kaa
mbele yake, mtazame, na mhoji. Zoezi hili litafunua kile ulicho ambacho sicho
ujitambulishacho popote pale ulipo.
Kuishi uvuli wa vingine
kwa maanisha maana ile ile ya kupotea katika msingi ule ule wa kutojipokea kama
ulivyo. Wewe na mimi tu binadamu katika maana ya kwamba tumeumbwa kwa sura na
mfano wa Mungu, Mwa 1:27. Hivi ndivyo ilivyompendeza Mungu aliye MTAKATIFU NA
MKAMILIFU. Uumbaji huu ni tokeo la upendo wa Mungu huyu MTAKATIFU NA MKAMILIFU.
Hivyo ikiwa uumbaji huu waufunua Utukufu wa Mungu na Furaha yake, basi hicho
kilichoumbwa kwa sura na mfano wake, yaani, Mwanadamu, kiini chake ni huo
utukufu na furaha hiyo ya Mungu. Na hivi kwa kiasi fulani twaweza yatafsiri
maneno haya, “maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo
ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer
29:11. Je, katika kweli hii unayo sababu yoyote ya kuishi kivuli cha mwingine?
Je, Mungu alikosea kukuumba kama ulivyo, na tena katika upekee ulio nao? Je,
wafikiri Mungu hana mpango wa pekee juu yako?
Ndugu yangu, pamoja na
malengo mengi tuliyonayo kwa kutafuta fahamu mbalimbali (elimu) tuzipatazo toka
kwenye familia zetu, shule, vyuo, hadi hapo ulipo, moja na la msingi ni
kukusaidia kujijua katika maana ya uwezo wako (capacity), karama zako, na
mazingira yako ili mwisho wa siku uipate furaha ile ya kweli ndani yako.
Ukichepuka katika kweli hii huwezi epuka kuwa kivuli cha kitu kingine. Hicho
kivuli hakitoweza kukupa furaha. Ni sawa na kuvaa kinyago na kuificha sura yako
halisi.
Kutojipokea
ambapo kunapelekea kuishi maisha linganishi na uvuli wa vitu ndicho kisemwacho
katika masomo yetu yote mawili ya leo. Mungu alipomuumba mwanadamu, wazazi wetu
wa mwanzo Adam na Hawa, aliwapa pia sehemu nzuri ya kuishi. Na panapokuwa zaidi
ya mmoja kuna kuwa na utaratibu wake wa kuishi, na hiyo ndiyo akili. Penye
akili kuna utaratibu, na pasipo na utaratibu hapana akili. Kweli hii anaikiri
mwanamke yule (Hawa) kwa nyoka yule anayemrubuni ‘kula matunda yote ya bustani’
katika bustani ile Mungu aliyoiandaa yao na kusema, “Matunda ya miti ya
bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu
amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa,” Mwa 3:2-3. Nyoka kwa kujua
udhaifu wao, yaani, wa kutojipokea kama walivyo, anawapa hakikisho la hofu yao,
yaani, kifo, na kuwaambia, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba
siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama
Mungu, mkijua mema na mabaya,” Mwa 3:4-5. Kutokujua uwezo wako ndani yako, ni
rahisi sana kurubuniwa kwa sababu nafasi ya kutokuwa na utoshelevu ni kubwa
sana ndani yako. Na matokeo yake, “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa
chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa
katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala,” Mwa 3:6. Tendo hili
la kwenda kinyume cha utaratibu (kutokutii) ni kujipatia utoshelevu ambao ni
tokeo la kutojipokea kama walivyo.
Je,
ni mara ngapi tunaona vituko mtaani mwetu watu wanavyojipodoa na mwisho wa siku
wanabadilika na kuwa vinyago vya kutisha? Leo binadamu amefika mbali zaidi hata
anamkosoa Mungu kwa kubadili maumbile yake. Siku ya ufufuo wa wazima na wafu
hakika vitashuhudiwa vituko vingi!!! Tokeo la moja kwa moja kwa kile
walichokitaka wazazi wetu wa mwanzo kwa kuuvunja utaratibu ule ni hili la kuwa
na soni. “Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona
majani ya mtini, wakajifanyia nguo,” Mwa 3:7. Sijui siku hiyo ya ufufuo wa
wazima na wafu kama kutakuwa na majani ya mtini kuifunika soni itakayojitokeza.
Ndugu
yangu, kujipokea kama ulivyo ni chanzo cha furaha yako ya ndani. Tendo hilo
kwako ni mwisho wa aibu na kinyago ulicho nacho, na mwanzo wa maisha mapya.
Hili ndilo linalojitokeza leo katika somo letu la Injili. Kiziwi yule alikubali
kuivua aibu na kinyago chake na kuanza maisha mapya. Yesu akaitoa aibu na
kinyago chake “akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake,
Funguka,” Mk 7:34. Mara baada ya tendo hili, safari mpya na yenye furaha ya
kweli ilianza. “Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake
kikalegea, akasema vizuri,” Mk 7:35. Huu si kiziwi na bubu tena, bali ni mtu
mpya na mwenye furaha ya kweli.
Furaha
ni kama kikohozi. Huwezi kuzuia. Yesu “Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri
ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari,” Mk 7:36. Ni nani
kati yetu aweza kukaa kimya kwa kuondolewa aibu na kinyago alicho nacho?
Hakika, “wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema;
viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme,” Mk 7:37. Huyu ndiye Mungu mwenye
kutuwazia mema wakati wowote, Yer 29:11. Huyu ndiye Mungu atuongozaye kila siku
ya maisha yetu kuelekea ukamilifu ule anautaka kwako na kwangu tuufikie, Mt
5:48. Huyu ndiye Mungu anayependa wewe na mimi pamoja na udhaifu wetu tuishi
milele kwa sababu ndani yetu ipo chapa yake, yaani, katuumba kwa sura na mfano
wake. Mungu asingependa chapa hiyo ipotee. Kumbe yanipasa kutafakari juu ya
aibu na kinyago changu. Kristo ndiye Daktari wetu. Amina.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini kadiri ya alivyozidi
kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari,” Mk 7:36.
Tusali:-
Ee Yesu na Mwokozi wangu, niondolee aibu na kinyago changu ili niipata furaha
ya kweli ndani yangu. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario