martes, 7 de febrero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 5 YA MWAKA-I


ALHAMISI WIKI YA 5 YA MWAKA-I

Somo: Mwa 2:18-25

Zab: 128:1-2, 3, 4-5

Injili: Mk 7:24-30

Nukuu:

"Bwana Mungu akasema, si vema huyu mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye." Mwa 2:18

“Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye,” Mwa 2:20

“Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu,” Mwa 2:21-22

“Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume,” Mwa 2:23

“Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja,” Mwa 2:24

"Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa," Mt 7:27.

“Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto,” Mk 7:28

“Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako,” Mk 7:29.

TAFAKARI: “Hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.”

Wapendwa taifa la wana wa Mungu, masomo yetu leo yanatualika kutafakari UPENDO na HURUMA ya MUNGU kwetu. Somo la kwanza linazidi kuonyesha upendo huo kwa kumpatia Adam mwenzi wake na kumwondolea huzuni zake kwa kuishi upweke. Pia kwa tendo hilo la kimungu tunafundishwa maisha ya pamoja ni maisha ya kimungu kama ulivyo uhusiano wa UTATU MTAKATIFU; Mungu Baba, Mwana na Roho mtakatifu.Tendo hilo pia la tufundisha kwamba tupo hapa duniani kwa ajili ya wenzetu pia kwa sababu tuna huo mfanano wa sura na mfano wa Mungu.

Kwa upande wa Adamu, msaidizi wake Eva, siyo mjakazi wala mtumwa wake; bali mwenzi wake na ‘msafiri twaliwa’ mwenzake katika uzima na umilele, yaani, utakatifu. Adamu bila Eva hajakamilika, na Eva bila Adamu kadhalika. Hapa kuna tendo la kimungu la UKAMILISHANO. Tendo hili ndilo taswira halisi ya ndoa na umaana wake. Ni agano na siyo mkataba. Katika agano hili kuna kupoteza kwa ajili ya mwingine. Hesabu ya Mungu hapa ni ya pekee. Kwa kawaida 1+1=2. Kwa upende wa hesabu ya Mungu, 1+1=1. Maana ya jibu la Mungu ni hii, "kwa hiyo mwanamke atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili MMOJA," Mwa 2:24.

Adamu anaonyesha furaha ya tendo hili la UPENDO wa Mungu kwa namna hii ya ajabu, akisema, "sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanaume," Mwa 2:23. Hakujawahi tokea dunia mtunzi  aliye onyesha ya moyoni na mguso wa furaha ya kimungu kama Adamu kwa tenzi hii ya pekee, Mwa 2: 23.

Ndugu yangu, mbona wamfanya mwenzi wako wa ndoa kama kigaragosi fulani hivi? Huo sio mpango na upendo wa Mungu. Je, mnaokimbilia kupeana talaka kwa sababu nyepenyepesi mwataka kuvunja mpango wa Mungu? Yesu ananena hivi kuhusu talaka, "Lakini tangu mwanzo wa kuumba ulimwengu, alifanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si mwili tena, bali mwili mmoja," Mk 10:6-8. Hapa tunapewa tena hesabu ya kimungu na Yesu, 1+1=1. Ndugu yangu unayesoma habari hii, "Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu," Ebr 13:4.

Somo la Injili la tuonyesha pia HURUMA na UPENDO wa Mungu. “Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa," Mt 7:27. Nini maana ya maneno haya?  Ni kweli pasipo shaka kabisa kwamba katika mpango mzima wa wokovu wetu wanadamu, ilimpasa Mungu aanze na kundi fulani la watu, na kwa Upendo na upendeleo wake wa kimungu Taifa la wana wa Israeli walipewa upendeleo huo wa kwanza.

Pili, yatupasa kujua vizuri lugha aliyotumia Yesu kumjibu mama huyu asiye Myahudi aliyemwendea kwa shida ya uponyaji wa mwanaye. Ni lugha iliyokwisha zoeleka katika jamii ile wakati ule kati ya Wayahudi na majirani zao. "Watoto" hapa yamaanisha wana wa Israeli, "mbwa" ni wale wasio Waisraeli, ikimaanisha watu wa mataifa. Na "mkate," ikimaanisha huduma ya uinjilishaji wa habari njema ya wokovu. Kwa mantiki hiyo Yesu alitumwa kwanza kwa taifa hili la kiyahudi. "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israelí," Mt 15:24. Hii ndiyo sababu hasa ya Yesu kuyasema hayo yote. Ila kwa jibu lake anaonyesha HURUMA kwetu pia, yaani, nasi tupo katika mpango wa wokovu wa Mungu baada ya wana wa Israeli kushiba. Jibu la mama huyu ni mwelekeo wa sisi sote tunapokuwa mbele ya Mungu tukijua wote ni wadhambi na waitaji pia. Ni tendo la unyenyekevu. Anajibu na kusema, "Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto," Mk 7:28.

Swali ni kwamba, kama Yesu alitumwa kwanza kwa wana wa Israeli, mbona walimkataa? Mtume Paulo anatupa jibu lake, anaposema, "Basi nasema, Je, Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu," Rum 11:11.

Ndugu yangu, tazama maajabu ya Mungu wetu! Mipango yake ni ya ajabu machoni mwetu, UPENDO na HURUMA vya ufunua UKUU wake na UHASILI wake. Yatupasa sote wenye ufahamu na utambuzi huu kujibu UPENDO na HURUMA ya Mungu kwa KUJINYENYEKEZA kwake kama tendo pekee la uhitaji wetu sisi wanadamu. Tendo hili litakuwa FURAHA ya Mungu na kwetu pia.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto,” Mk 7:28

Tusali:-Bwana wewe ndiwe mwenye haki. Utazame udogo wangu, nijalie ufahamu wako, utambuzi wa Upendo, Huruma yako, na daima nijinyenyekeze kwako. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario