miércoles, 15 de febrero de 2017

TAFAKARI: IJUMAA WIKII YA 9 YA MWAKA-I


IJUMAA WIKI YA 6 YA MWAKA-I

Somo: Mwa 11:1-9

Zab: 33:10-11, 12-13, 14-15

Injili: Mk 8:34-9:1

Nukuu:

“Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja,” Mwa 11:1

“Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote,” Mwa 11:4

“Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya,” Mwa 11:6

“Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote,” Mwa 11:9

“Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate,” Mk 8:34b

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha,” Mk 8:35

TAFAKARI: “Msalaba Mtakatifu ni Utukufu, na Baraka.”

Wapendwa wana wa Mungu, mitikiso katika maisha na hasa nyakati zile ambazo tulizozoea utulivu, mitikiso hiyo ulenga katika ukamilifu wa kile kilichokusudiwa ingawa si rahisi kuelewa kweli hiyo katika mazingira na nyakati hizo za misukosuko. Nyakati hizo za utulivu ni kama zinavyoelezewa kutoka somo letu la kwanza, yaani, “Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja,” Mwa 11:1. Hizi ndizo zile nyakati ambazo mimi na wewe ujiwekea mipango mingi na kuwa na hamu ya kufanya hiki na kile. Na hivi ndivyo ilivyokuwa, “Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote,” Mwa 11:4. Haya yote na katika uzuri wake ni mawazo ya kibinadamu tu, ila Mungu anampango wa kila mmoja wetu na kila alichokiumba, “maanamawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana,” Isa 55:8.

Hivyo, “Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu,” Mwa 11:5. Hapa ndipo tunapoona mpango wa Mungu unavyojidhirisha na kwenda kinyume kabisa na mpango wa mwanadamu na matamanio yake. “Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya,” Mwa 11:6. Ila alitendalo Mungu au kuliamuru ulenga katika ukamilifu licha ya kwamba linaweza kupita katika mateso na sintofahumu nyingi. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho,” Yer 29:11.

Hili ndilo lililokuwa lengo la Mungu katika sintofahamu hii ya babeli, yaani, “Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote,” Mwa 11:9. Embu tazama uzuri wa tendo lile la mvurugano wa lugha hapo Babeli, na hivi leo ulimwengu umeshehena wingi wa lugha mbalimbali. Tendo hili licha ya kuwa teso na msalaba kwa mwanadamu kutokufikia lengo lake la kuujenga mnara ule wa Babeli linaufunua uzuru, furaha, na utukufu wa Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya Msalaba kuwa kitambulisho, kielelezo na uthibitisho wetu Wakristo, kwa wengi ni makwazo na aibu. Kwa kifupi hao ni adui wa Msalaba. "Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo." Flp 3:18. Ndugu yangu, licha kwa mwono wa kibinadamu Msalaba una taswira ya mateso, ndiyo njia pekee, halisi na uhai wa Mkristo kama mfuasi wa Yesu Kristo. "Mtu yeyote asiyechukua Msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu," Lk 14:27.

Je, yatosha tu kuuchukua Msalaba na kumfuata Kristo? La hasha! Kuuchukua Msalaba kwa maanisha mambo makuu yafuatayo; Kujikana nafsi, Kujitwika/kuhiari kwa ukunjufu, na kumfuata Yesu kama kielelezo sahihi cha Msalaba. "Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate," Mk 8:34. Maana yake ni nini? Ndugu yangu, kujikana kuna lenga haswa nafsi na matamanio yake. Siyo yote nafsi ipendayo yana njia, kielelezo na uhai wetu kwa maisha ya umilele. Yesu anatutakia maisha ya umilele. Hapa duniani tupo tu kwa muda mfupi na tunajiandaa tu kwa maisha halisi ya umilele.

Yesu anagusia jambo hilo kwa kusema, "Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?" Mt 16:26. Tunapoizuia nafsi kupata kila kitu kiipendacho ni kuiokoa nafsi hiyo kwa ajili ya umilele, "kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona," Mt 16:24. Je, upo tayari kuachilia fahari kwa uliyoshikamana nayo?

Jambo hili wakati mwingine litakuitaji uyafumua maisha yako yote na kuanza kuyasuka tena. Huku ni kuzaliwa upya katika roho! Yesu analiongelea jambo hili kwa Nikodemo, na kusema, "Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu," Yoh 3:4. Kwa maana, "kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa roho ni roho," Yoh 3:6. Kuikana nafsi ni kuanza mfumo mpya na Kristo. Tatizo kubwa la wengi nikufikiri bado muda upo na kwa hiyo hakuna haraka.

Kujitwika Msalaba kwa maanisha mambo mawili. Kwanza ni jambo la hiari na huru. Hatupaswi kuona aibu hasa pale tunapotaka kujenga mahusiano na Kristo. Yawezekana wakati fulani katika maisha yako uliheshimika sana kutokana na nafasi uliyokuwa nayo na huduma uliyokuwa unatoa; iwe kwenye familia, kuajiriwa au utawani. Leo huna nafasi hiyo na hujulikani tena. Kujenga mahusiano na Kristo katika kujitwika msalaba ni kuanza upya pale ulipo. Tatizo letu hupenda kuishi kindotondoto na kihistoriahiria. Huko haupo tena. Kama gitaa lako limebakia na nyuzi nne badala ya sita, zipige hizo hizo hadi mwisho. Ni kuubeba Msalaba hadi mwisho na kuwabwa juu yake. "Akatoka, hali akichukua Msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la kichwa, au kwa kiebrania, Golgotha. Wakamsulubisha huko, na wengine wawili pamoja naye, huku na mmoja huku, na Yesu katikati" Yoh 19:17-18. Wengi huwa tunafika Golgotha, ila ikifikia kuwabwa tunatoweka. Ndugu yangu, licha ya Yesu kusaidiwa na Simoni Mkirene, hatimaye alikubali kuwabwa. Hapa ndipo kwenye taji la ushindi. Hapa ndipo kwenye FURAHA ya kweli katika mateso. Je, huamini nisemayo?

Haya hapa maneno ya Yesu mwenyewe, "Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu," Mt 5:11-12.

Jambo la pili, kujitwika huku kunaweza kukawa si jambo la hiari yako, bali mshangao unaolenga baraka na ushirikishwaji wa utukufu wa Mungu na kuwa sehemu ya utukufu huo. Jambo hili linamtokea Simoni Mkirene. "Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika Msalaba, auchukue nyuma yake Yesu." Lk 23:36. Ndugu yangu, yaliyotokea kwa Mkirene huyu yawezekana kabisa yametokea kwako au yakatokea kwako. Kuna nyakati nyingine hatujua sababu haswa ya kuingizwa katika mateso ya wengine. Tunawajibika kubeba lawama za wengine hata pale ukweli unapojulikana kwamba hatuhusiki.

Umefikia hata kutengwa na ndugu kwa sababu usizozifahamu. Ndugu yangu, lichukulie jambo hilo kama Mkirene. Ni mshangao wenye neema na utukufu ndani yake. Kwenye Msalaba pana mateso, na penye mateso pana baraka na Utukufu. Kwa mantiki hii, hakuna utukufu pasibo Msalaba; na hakuna Msalaba usio na utukufu tunapoubeba na Kristo aliyeshinda mateso ya Msalaba. Acha kulalamika! Mtazame Yesu. Mpendwa, Msalaba ni fahari kwetu wakristo hasa tunatafakari maneno haya ya siku ya ijumaa kuu kabla ya kutoa heshima kwa Msalaba Mtakatifu. Maneno hayo Padre au Shemasi huyasema akiwa anaufunua Msalaba uliofunikwa kitambaa, na kusema, "Huu ndiyo Mti wa Msalaba, ambao wakovu wetu umetundikwa juu yake. Njoni njoni tuuabudu." Msalaba ni FAHARI kwetu kwa sababu wokovu wetu umetundwa juu yake. Mtume Paulo analiongelea jambo hili kwa kusema, "lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu," Gal 6:14.

Msalaba ni UNYENYEKEVU. Msalaba wa Kristo watufunza unyenyekevu halisi. Msalaba unaturudisha kwenye uhasili wetu kama wanadamu. Tunakumbushwa katika mateso na mahangaiko yetu kuwa na kubaki kama mwanadamu. Tunapojaribu kujikweza na kuwa kama Mungu au kitu kingine, tunabakia kuwa shetani ambaye alitamani hivyo. Mtume Paulo anasema, "tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu,  alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba," Flp 2:8. Unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Unyenyekevu utufunza. Ni darasa la maisha muda wote hadi kufa. Yesu analithibitisha hilo kwa kifo chake. Kwenye ulimwengu huu wa ushindani ni vigumu kunielewa. Ila ukitaka kupata maarifa ya kimungu jinyenyekeze kwa kujua umaana wake, "kwa sababu neno la Msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu," 1Kor 1:18. Ndugu yangu, ni nini zaidi ya nguvu ya Mungu katika maisha yako? Je, ni sifa, kufahamika, pesa, umaarufu, cheo, ufahamu (akili), unavyoving'ang'ania kwa nguvu zote? Je, tunaitaji hayo kufuzu maisha ya umilele? Ndugu yangu unayesoma habari hii jipange sawa sawa!

Msalaba ni UPATANISHO. Tumepatanishwa na Mungu kwa mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo pale msalaba. "Akawapatanisha wote wawili katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba, " Efe 2:16. Kwanza kabisa kwa kuupokea msalaba katika maisha yako ya kila siku unapata nafasi ya kujikusanya na kuzama zaidi katika makusudio ya mahangaiko na mateso yako, na siyo jibu lake. Mahangaiko na mateso mengine katika maisha hubakia kuwa fumbo, na kama ni fumbo halina jibu kwa sababu si tatizo. Matatizo yana majibu, fumbo halina jibu. Tunalielewa tu kwa kujikusanya na kuzama katika tafakari, ikilenga katika umaana wa fumbo hilo (mateso na mahangaiko).

Mfano: mmeishi miaka zaidi 10 bila kupata mtoto. Mnampata mnajawa FURAHA. Mnamsomesha na anapata kazi nzuri. Mnafurahi. Anampata mchumba mwema na mwaminifu. Mnafurahi. Siku moja kabla ya ndoa yao, mtoto wenu huyo anapata ajali anafariki. Mkitazama umri wenu umefikia saa 12 jioni. Nyumbani kwenu mlitegemea mjukuu mnajikuta mpo na paka na mbwa tu. Ni majonzi makubwa. Ila mtazame Mungu. Yesu Kristo ni Mtoto pekee wa Mungu. Lakini Mungu kamtoa sadaka kwa ajili ya wokovu wetu. Katika hili watazame Ibrahimu na Mama María. "Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene," Yoh 19:25. Hapa tunaonja uchungu na Faraja. Ni uchungu kwa namna ya kifo hicho na matazamo wetu kibinadamu. Ni Faraja kwa sababu yametimia makusudio ya Mungu kwa upendo wake  kwetu  sisi wanadamu. "Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake," Yoh 19:30.

Ndugu yangu, hakuna UTUKUFU kwa yeyote ajiitaye mkristo pasipo MSALABA. Msalaba ni Bendera yetu na twapasa kuipeperusha hadi mwisho wa safarí. Ni kweli njiani tunakutana na tufani zito la upepo na vimbunga vya hapa na pale. Shikilia vyema mlingoti huo uliobeba BENDERA. Hapo tutapata NEEMA, BARAKA na UTUKUFU. Ni hapo tu twaweza kulichagua na kukaa mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Basi ndugu yangu, "ukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu, " Ebr 12:2.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate,” Mk 8:34b

Tusali:-Ee Yesu uliye shujaa na mshindi wa mateso, kifo na msalaba, tujalie kila mmoja wetu kuona fahari juu ya Msalaba na changamoto za maisha ya kila siku, kadiri ya wito ulotujalia na huduma tuitoayo. Kamwe tusiupige kisogo msalaba wako Mtakatifu. Tutakatifuze na Msalaba wako wenye ushindi na Utukufu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario