JUMANNE WIKI YA 7 YA MWAKA-I
Somo:
YbS 2:1-13
Zab:
37:3-4, 18-19, 27-28, 39-40
Injili:
Mk 9:29-37
Nukuu:
“Mwanangu, ukija
kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa,” YbS 2:1
“Ujitengeneze moyo
ustahimili, wala usitaharuki siku ya kuteswa,” YbS 2:2
“Uambatane naye wala
usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe,” YbS 2:3
“Kila utakalopelekewa
ulipokee kwa kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako,” YbS 2:4
“Kwa sababu
alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa
katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu
atafufuka,” Mk 9:31
“Akaketi chini,
akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa
mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35
“Mtu akimpokea mtoto
mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi,
humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma,” Mk 9:37
TAFAKARI:
“Umkabidhi Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kufanikiwa katika maisha yanayoongozwa na malengo, ni kuishi maisha
yanayosukumwa au kuongozwa wakati wowote na hofu ya Mungu, sala na maombi.
Maisha yenye mtazamo huu kwa ujumla wake utufikisha kwenye kusudio la maisha ya
kiroho. Kuongozwa au kusukumwa na hofu ya Mungu uturejesha kwenye kusudio la
uumbaji wetu, na hali yetu halisi, yaani, ubinadamu wetu. Hofu hii ya Mungu
umulika na kutukumbusha kila mara kusudi la kuumbwa kwetu, yaani, tumjue Mungu,
Kumb 6:5, tumpende Mungu na majirani zetu, Mt 22:29, kumtumikia Mungu na wale
tuliopewa dhamana juu yao, Gal 5:13, na mwisho tuupate uzima wa milele. Hii ni
hatua ya mwisho kama asemavyo Mtume Paulo katika kuvipiga vita vile vya imani
hapa dunia, yaani, “mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa
watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa
milele,” Rum 2:22. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, hayo ndiyo
maisha yanayoongozwa au kusukumwa na hofu ya Mungu.
Ndugu yangu, hatutaweza
kuifikia hali hiyo kama tutabebwa na wimbi la dunia tunaloishi leo kama
litakavyo. Tunaishi katika ulimwengu wa ushindani, na wakati mwingine pasipo
washindani au washindaniwa. Ni ulimwengu wa vitu, na utafutaji wa vitu kila siku hata kama havina tija leo na
kwa sasa. Mtindo na mtazamo huu wa maisha huaribu na upoteza lengo na sababu ya
kuumbwa kwetu. Hofu ya Mungu hutoweka, na maisha ya sala na maombi hukosa ladha
yake, kama Mtume Yakobo asemavyo, “Mwatamani,
wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na
kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!” Yak 4:2. Maisha yenye msukumo huu
kamwe mbele ya safari hayana ushindi. Ni kushindwa tu! Ni maisha yaliyokosa
malengo. Ni maisha bila hitimisho ambalo kwa
uhakika lipo, yaani, maisha ya umilele.
Ndugu yangu, ni kweli pasipo shaka
kabisa kwamba usipo thamini umilele kama hitimisho la maisha yako, nguvu na
akili zako zote zitajikita kwa haya ya leo na kesho ambayo kwa uhakika kama
yalivyo hayana umilele. Katika kweli hii Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na
wevi huvunja na kuiba; bali
jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi
hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa
hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:19-21. Ndugu yangu,
chunguza kile kinachochukua muda wako mwingi hapa duniani na ujiulize kama kina
uhusiano na umilele wako mara baada ya maisha haya hapa duniani. Ndugu
yangu, tukiwa na uadui na Mungu kuna kushinda kweli vita hiyo? Hakika hakuna
kushinda!
Hivyo pamoja na raha na
anasa zake mwisho wa siku hakuna faida yoyote. Basi kila mmoja na haihoji
dhamiri yake kwa swali hili la Yesu kama anavyotuuliza, “Kwa kuwa itamfaidia
mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?” Mk
8:36-37. Ndugu yangu, pasipo shaka sindano hiyo imekuingia vizuri. Tafakari!
Wapendwa wana wa Mungu,
ili tufikie lengo la maisha ya kiroho twahitaji kuishi na kukumbatia muda wote
fadhila ya unyenyekevu. Unyenyekevu uturudisha katika hali ya ubinadamu wetu
pale tunapotaka kujiumba na kuvaa taswira nyingine kama tokeo la majivuno yetu,
mafanikio yetu kimaisha, na hata ufahamu wetu. Ndugu yangu, chochote kile kitakachojiumba
kama tokeo la kujikuza zaidi na kuipoteza ile hofu ya Mungu ndani yako, mwisho
wake ni kupoteza dira ya hitimisho la maisha yako, yaani, umilele wake.
Ndugu zangu, tusipokuwa
na hofu hii ya Mungu hatutaweza kumtii Mungu na wala kumkaribia kwa sababu
Mungu hatakuwa na nafasi ndani ya moyo wako. “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye
atawakimbia,” Yak 4:7. Hili litawezekana tu pale tutakapokuwa tayari
kujinyenyekesha na kuiishi hofu ya Mungu.
Ndugu zangu, waswahili wana msemo huu:
“Maji ukishayavulia nguo huna budi kuyakoga.” Hivyo wosia kwa ye yote yule
aliye tayari kuliondoa giza, yaani, uovu, na kuuleta mwanga, yaani, wema wa
Mungu na kuishi kama wana Mungu, jambo hili lazima alijue kwa undani, yaani, “ukija
kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa,” YbS 2:1. Hutoweza
kupigana vita dhidi ya uovu kama hujajiandaa vizuri kimwili na kiroho. Elewa
katika vita hiyo unapambana na giza dhidi ya mwanga. Yule mwovu, yaani shetani,
na mwenye kuufurahia ufalme wake, uovu ndiyo heri na furaha kwake. Hivyo
maandalizi ya kimwili na kiroho ni muhimu sana. “Ujitengeneze moyo ustahimili,
wala usitaharuki siku ya kuteswa,” YbS 2:2. Nguvu na silaha yako ni Muumba
wako. “Uambatane naye wala usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe,” YbS 2:3.
Hakuna mtu ye yote aliyemtegemea Mungu akaachwa ukiwa. Itazame historia ya
Kanisa letu Katoliki na ile mbegu iliyopandwa na watakatifu wafiadini. Ukweli
huo wa wafiadini watufundisha kwamba, “kila utakalopelekewa ulipokee kwa
kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako,” YbS 2:4
Wafiadini hawa
walihimarishwa kwa nguvu na neema ya Mungu kwa sababualimtegemea Mungu pasipo
shaka yoyote. Wataalamu wa kufua vyuma, na hasa wale waitengenezayo dhahabu
wanasema hivi, ‘kuijua dhahabu ipo tayari katika kweli yake ni pale utakapoiona
sura yako kwenye dhahabu hiyo.’ Maana yake ni kwamba dhahabu hiyo haina chembe
yoyote ya uchafu. Ni katika kweli hii kwamba jaribu ufananishwa na dhahabu
ipitayo kwenye moto mkali. “Maana dhababu hujaribiwa motoni, na watu wateule kalibuni
mwa unyonge,” YbS 2:5. Jamii yetu ya leo kuitoa hapo ilipo na kuipeleka palipo
pazuri zaidi, hatuna budi kupita kwenye changamoto hii ya dhahabu.
Haya yote yanawezekana
pale tu imani hai katika ufahamu wake na uamaana wake kuwa nguzo imara katika
kuishi na kutenda. Hivyo “basi umwamini Yeye, naye atakusaidia; ukazinyoshe
njia zako, na kulikaza taraja lako katika Yeye,” YbS 2:6. Mahangaiko na
sintofahamu zake katika maisha ni swala la muda tu. Jambo la muhimu katika
safari hii ya ‘mwanga dhidi ya giza,’ ‘wema dhidi ya uovu’ ni kutopoteza
tumaini kwa sababu uovu katika asili yake hauna umilele. Hivyo wito ni kwamba,
“enyi mnaomcha Bwana, zingojeeni rehema zake, msigeuke upande msije mkaanguka.
Enyi mnaomcha Bwana, mwaaminini Yeye sana, thawabu yenu haitawapotea,” YbS
2:7-8
Ufahamu na umaana huu
katika imani utupa furaha ya kweli hata katika mateso. “Enyi mnaomcha Bwana
sasa tarajieni mema na furaha ya daima na rehema,” YbS 2:9. Mateso ukupa maana
endapo wajua sababu ya teso hilo, ukilinganisha na furaha ile ya kweli ambayo
hakuna wa kutuondolea. “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali
ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa
furaha. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo
yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:20, 22.
Historia ya maisha yetu
wanadamu, na hasa mang’amuzi katika maisha, ni mwalimu mzuri sana. Wewe na mimi
yatupasa kwenda kwa adabu tukijali utu wa watu kwa kusimama katika kweli na
haki. Hapa ndipo ilipo pona yetu kwa wale wote tuliopewa dhamana ya uongozi na
umma wa watu. “Angalieni vizazi vya kale mkaone: nani aliyemtumaini Bwana
akaaibika Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita
akadharauliwa?” YbS 2:10.
Tunapodondoka katika
kufikiri kwetu, kuamua kwetu, na kutenda kwetu, tusione haya kukiri mapungufu
hayo kwa sababu huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Ni vyema
mara zote nikajipatanisha mimi na Mungu, mimi na jirani, na mimi na mazingira
yangu. Mafiga haya matatu ni muhimu sana katika ustawi wa upendo, kweli, haki,
na amani katika jamii yoyote ile ya watu. Ndugu yangu, “Bwana yu mwenye huruma na rehema, husamehe dhambi
na kuokoa wakati wa shida,” YbS 2:11.
Kuna anguko kubwa sana pale
ninaposhindwa kujipokea, yaani, kutambua kuwa mimi ni binadamu tu na ndivyo
ilivyompendeza Mungu kuniiumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Mungu
hakufanya makosa wala kukosea kuniumba kama nilivyo. Na agizo la Mungu la mimi niwe
pale alipo Yeye ni hili: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa
mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Bila ukamilifu huu, na utakaatifi huu
siwezi kamwe kuwa pale alipo Mungu. Nisipo kiri hali hii na kuchukua hatua
stahiki huko mbele ya safari ni giza tupu. Angalizo ni hili: “Ole wao wenye
mioyo ya woga, wenye mikono iliyolegea, wakosaji waendao njia mbili. Ole wake
aliye dhaifu wa moyo kwa maana amekosa imani, kwa hiyo hatahifadhiwa,” YbS
2:12-13. Unyenyekevu ndicho kivuko sahihi katika kiunzi hiki cha moyo wa woga,
na mikono legelege (utoaji huduma kwa upendeleo).
Nguvu ya ufahamu,
madaraka, karama, na vipaji tulivyojaliwa na Mungu nivitumie kwa Sifa na
Utukufu wa Mungu. Mungu kwa kupitia hayo aliyonikirimia bila kipimo yamfanye
aonekane kwa watu wote pale nilipo bila kujali itikadi zao kisiasa na kiimani,
na hata historia zao nzuri au mbaya.
Wapendwa katika Kristo,
maisha ya unyenyekevu na hofu ya Mungu hayatupeleki tu karibu na Mungu, bali
utufanya kuwa tayari kutahabikiana katika hali zote za maisha na mahangaiko
yake. Pasipo kujishusha ni vigumu kuyaona
mahangaiko ya wengine na kuyabeba kama moja ya changamoto na misalaba yenye
nuru ya Utukufu.
Yesu anataka tulione jambo hili vizuri
ikiwa yeye ndiye kielelezo chetu. Hivyo ni “kwa
sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda
kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku
tatu atafufuka,” Mk 9:31. Hata hivyo Mwinjili Marko anatuambia hawakulifahamu
neno lile kwa sababu walijawa na uoga na hivyo walishindwa kumuuliza Yesu, Mk
9:32
Ndugu yangu,
kutokujishusha hakutakuandaa na kuwa tayari kutumika kwa ajili ya wengine. Je,
kila mmoja wetu akiupenda ukubwa bila kutumika tutaepuka machafuko? Wanafunzi
wa Yesu, yaani wale Thenashara, wanapatwa na ushindani huu wakiwa njiani
wakipita katikati ya Galilaya na Yesu, Mk 9:34. Yesu anawaambia kiini cha
ukubwa huo wanaoutamani. “Akaketi
chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa
wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote,” Mk 9:35.
Ukubwa ni utumishi, na
kutumika kweli kwa ajili ya wote pasipo kuweka mbele faida au maslahi binafsi.
Huu ndio ule utumishi usio na faida kama anavyotuambia Yesu; “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote
mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa
kufanya,” Lk 17:10. Hakika sote leo tuliopewa dhamana ya uongozi katika nyanja
mbalimbali katika Taifa letu- Tanzania, tungaliishi hofu hii ya Mungu na kweli
katika hali ya kutumika, Kristo angeonekana kwa kila mtu.
Tusifu
Yesu Kristo!
“Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna
hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi,
bali yeye aliyenituma,” Mk 9:37
Tusali:
Ee Yesu Mwema, tujalie fadhila ya unyenyekevu, na utayari wa kutumika kwa ajili
ya wengine. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario