JUMATANO WIKI YA 6 YA MWAKA-I
Somo: Mwa 8:6-13, 20-22
Zab: 116:12-13, 14-15, 18-19
Injili: Mk 8:22-26
Nukuu:
“Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua
dirisha la safina, alilolifanya,” Mwa 8:6
“Akangoja na siku saba
tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe,” Mwa 8:12
“Nuhu akamjengea Bwana
madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye
safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu,” Mwa 8:20
“Bwana akasikia harufu
ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa
sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana
wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya,” Mwa
8:21
“Wakafika Bethsaida,
wakamletea kipofu, wakamsihi amguse,” Mk 8:22
“Ndipo akaweka tena
mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote
waziwazi,” Mk 8:25
TAFAKARI:
“Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya
wanadamu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ukiitazama historia ya uumbaji na wokovu wa mwanadamu katika ujumla wake
utagundua kwamba Mungu ana mpango mpana sana na viumbe vyake, binadamu akiwa
ana nafasi kubwa katika uumbaji huo. “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema
hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya
imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala
hapana mwingine,” Isa 45:18. Hata pamoja na kweli hii, Mungu aliyemuumba
binadamu huyu kwa sura na mfano wake, hakumuumba katika maana au hali ya
kutenda mazuri tu bila kumpa uwezekano wa kutenda mabaya pia.
Mungu alimuumba
mwanadamu huyu huru kweli kweli, katika mizania ya kwenda hata kinyume kabisa
na mpango wake Mungu. Isingelikuwa hivyo basi mwanadamu huyu asingeliwajibika
kwa makosa yake mwenyewe. Hapa ndipo linapokuja swala zima la nguvu ya
kimaadili. Binadamu huru ni yule aliye huru kimaadili, yaani, ‘yupo huru
kufanya baya, na anao uhuru pia wa kutolifanya baya hilo.’ Hivyo kwa uhuru wa
kimaadili aliokuwa nao mwanadamu aweza kumwasi Muumba wake, na kwa uhuru huo
huo aweza kumrudia Muumba wake.
Somo letu la kwanza
laonyesha namna hiyo ya uhuru tuliojaliwa katika muono mpana wa uumbaji, na
somo la Injili linatupa picha kuhusu historia nzima ya wokovu wetu. Taswira
zote hizi mbili zinathibitishwa na maneno haya ya Mungu baada ya Nuhu kumtolea
Mungu sadaka ya kutekekezwa kama tendo la shukrani. “Bwana akasikia harufu ya
kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa
sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana
wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya,” Mwa
8:21.
Ndugu yangu, hii ndiyo
sababu kubwa licha ya nyakati nyingine twapigwa butwaa na kukatishwa tamaa
kuona ‘kwenda sambamba baina ya Mungu (mwenye Nguvu, Uwezo, Ajuaye yote, na
Mtakatifu) na uwepo wa uovu.’ Sehemu hii ya pili ya kwenda sambamba huku baina
ya uwepo wa Mungu na uovu ni tendo hili la uponyaji wa mtu yule aliye kipofu
katika Injili ya leo, Mk 8:22. “Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho
yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi,” Mk 8:25. Ndani
na katika uwepo wa Mungu mwanadamu aweza kutoka na kuingia kwa sababu uhuru huo
anao kimaadili. Hivyo wewe na mimi hatuwezi kukwepa wajibu wala kuwajibika kwa
makosa yetu wenyewe. Uovyo wa yeyote yule, na mbaya zaidi kwa yule aliyepewa
dhamana na umma wa watu ni pale anapokosa nguvu ya kimaadili. Ni sawa na maneno
haya ya Yesu, kwamba, “ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa
imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na
kukanyagwa na watu,” Mt 5:13.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu
akalifungua dirisha la safina, alilolifanya,” Mwa 8:6
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, mara zote tukumbushe wajibu wetu, na tutende kimaadili. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario