miércoles, 15 de febrero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 6 YA MWAKA-I


ALHAMISI WIKI YA 6 YA MWAKA-I

Somo: Mwa 9:1-13

Zab: 102:16-18, 19-21, 22-23

Injili: Mk 8:27-33

Nukuu:

“Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi,” Mwa 9:1

 “Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi," Mwa 9:13

“Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo,” Mk 8:29

“Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate,” Mk 8:34

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha,” Mk 8:25

TAFAKARI: “Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli isiyo shaka kwamba nafsi husalimika kwa kulipenda na kuliegemea tunda la roho, Gal 5:22-23, na pale tu unapokuwa tayari kumfuata Kristo, kujikana nafsi, na kujitwika msalaba wako kwa hiari bila shuruti. Yesu “akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate,” Mk 8:34. Tukijua aliye mkamilifu ni Mungu tu, basi kila mwanadamu ili aufikie ukamilifu na kumwona Mungu kama alivyo itampasa kujisafisha kwa kile ambacho kwa tafsiri ya ndani ni ‘msalaba wa kila mmoja wetu.’

Msalaba katika tafsiri hii twaweza kusema ni mapungufu aliyokuwa nayo kila mmoja wetu karidi ya maisha na wito wake. Madhaifu na mapungufu yetu huponywa pale tu tunapoyapokea ndani na katika Kristo. Hivyo, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:2-3

Ukweli wa maisha na tafsiri ya ‘Msalaba,’ katika mwono wa Injili ya leo unatupeleka ndani zaidi kuijua Imani yetu na yule tunayemwamini na kumfuata. Kumjua ni nani tunayemfuata, Yesu anauliza swali la uchokozi kwa wanafunzi wake, na Petro anatoa jibu, tena jibu lililo sahihi kabisa. “Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo,” Mk 8:29. Kristo yaani, aliyewekwa kwa sababu hiyo, yaani, wokovu wa mwanadamu. Huyu ndiye Masiha kwa ajili ya wokovu wetu.

Imani ya kweli huwezi itofautisha na matendo ya kweli yanayoambatana na kile mtu anachoamini. Na wakati mwingine matendo (ya upendo na huruma) husema zaidi ya kila kilicho ndani ya mtu yaani, Imani (yanayoonekana na yasiyoonekana). “Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu,” Yak 2:18. Nabii Isaya yupo tayari kupokea kadhia zote kwa sababu anayo Imani na Mungu anayemwamini kuwa ndiye msaada na kweli katika yote. “Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:6. Nabii Isaya yupo tayari kupokea fedheha zote akijua mwisho wa siku mateso yake si bure kwani anaye mtetezi wa kweli yaani, Mungu. “Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya,” Isa 50:7.

Je, mateso uliyonayo yanakupa mwanga zaidi kuhusu Imani yako? Tunapozungukwa na mateso na hali ya kukata tamaa tujifunze kutoka kwa Mtume Paulo na kusema, Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Mwenye Msalaba kuna upya wa mambo, nuru, uhai, na furaha ya kweli. Naye Mtume Paulo anasema, “Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu,” 2Kor 12:10. Ikiwa tafsiri ya udhaifu na mahangaiko yetu ni “Msalaba,” basi hatuna sababu ya kukata tamaa kwa sababu, kwenye angaiko na udhaifu huo kuna upya wa mambo, nuru, uhai, na furaha ya kweli. Je, nifanye nini?

Katika hali na mazingira hayo napaswa kuwa na muono chanya, yaani, nikubali na kupokea kuwa hilo ni tatizo, na kutoka hapo nichukue hatua kuelekea upya huo, nuru hiyo, uhai huo, na furaha hiyo ya kweli. Je, kabla ya kutumia dawa kwa ajili ya uponyaji, haitupasi kwanza kujua una sumbuliwa na ugonjwa gani? Kama hili twalifanya, ni hivyo hivyo hata kwa maisha ya kihoro na afya yake.

Hivyo hatuna sababu ya kujidhuru au kuendelea kuutia uhai matatani. Utajiri wako mkubwa siyo mali na vitu ulivyonavyo vya kushikika, bali ni afya yako, uhai wako. Bila afya na uhai ulionao, yote ulionayo ya kushikika upoteza maana yake. Na hili ndilo angalizo, na agizo la Mungu kwetu, kwamba, “Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu,” Mwa 9:6. Uhai ni mali ya Mungu, na zawadi ya Mungu kwetu. Niliye hai leo yanipasa kuulinda uhai wangu, na wa mwenzangu hadi hapo Mungu mwenyewe atakapoutwa.

Baada ya gharika ile, Mungu anaurudisha uhai na ukaribu wake kwa viumbe vyake. “Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi,” Mwa 9:1. Kuzaa, kuongezeka, na kuijaza nchi, kwa funua furaha na utukufu wa Mungu. Hakuna chochote kilicho na kama kilivyo kisichoifunua furaha na utukufu wa Mungu. Ndugu yangu, “hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum 14:7. Mungu huwasiliana na mwanadamu kila siku na kwa njia mbalimbali. Mawasiliano haya hayakinzani na uelewa wa mwanadamu kwa nyakati zote, licha ya maendeleo aliyo nayo. Hivyo si sahihi kusema kwamba, “maendeleo ya sanyansi na technologia yamemfanya mwanadamu kuwa mbali na Muumba wake.” Kinyume chake ni kwamba, mwanadamu huyu yupo mbali na maendeleo hayo kwa kukikimbia kivuli chake. Hapa ndipo tunapoona vizuri ile falsafa ya mbuni, yaani, “kukificha kichwa chake kwenye mbawa zake, ilhali mwili sehemu yote ya mwili ikiwa wazi na kuonekana.”

Hatuwezi kumkimbia Mungu kwa vigezo vya maendeleo na upya wa ufahamu wetu. Maendeleo hayo ya kisayansi na kiteknologia yalishawekwa na Mungu mwenyewe, naye hachoki kuyaratibisha. Naye anasema, “Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi," Mwa 9:13. Je, katika kweli hii, wavumbua kilicho chako katika upya na upekee wake, au wakitambulisha kile ambacho kilikuwa bado kutambulika kwa wengine? Tafakari!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha,” Mk 8:25

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie neema ya kuishi fumbo zima la Msalaba kwa sababu katika huo kuna Utukufu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario