JUMANNE WIKI
YA 6 YA MWAKA-I
Somo:
Mwa 6:5-8; 7:1-5, 10
Zab:
29:1a, 2, 3ac-4, 3b, 9c-10
Injili:
Mk 8:14-21
Nukuu:
“Bwana akaona ya
kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza
moyoni mwake ni baya tu sikuzote." Mwa 6:5
“..., Angalieni,
jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode." Mk 8:15
TAFAKARI:
“Utayari wa Mungu wa kuanza upya na wote wamchao.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu leo tuone utayari wa Mungu kuanza upya na wale wanaoshika na kuishi
matakwa yake. Hawa ni wale wamchao na wanaoenenda katika njia yake. "Nuhu
ana wawakilisha wale waishikao kweli ya Bwana kwa kupata neema machoni pa
Bwana," Mwa 6:8
Nuhu anapewa maagizo ya
kutengeneza safina ambapo itambidi kuchukuwa wanyanya saba saba kati ya wote
waliosafi mke na mume, na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mke na mume
(Mwa 7:2). Na ndege wa angani saba saba, mke na mume kuifadhi mbegu juu ya uso
wa nchi yote, (Mwa 7:4).
Wakati wa maandalizi ya
kutengeneza safina, Nuhu alionekana kama mwendawazimu machoni pa wengi. Zoezi
hili lilichukua muda mrefu kiasi kwamba wengi walifikiri Nuhu ni mwigizaji tu.
Ndugu yangu, lolote
litokealo kwa mkono wa Mungu halipiti bure. Kila kitu chenye mkono wa Mungu
kina makusudi yake. Ulimwengu wetu wa leo hauna tofauti na nyakati za Nuhu. Leo
kuna kila aina ya uovu. Wapo wanaokemea wakisukumwa na nguvu za kimaadili za
Mungu, ila wapo pia wanao beza nguvu hizo. Tunaishi kama vile nguvu, uwezo na
mamlaka ni kwetu tu wanadamu. Mungu hana tena nafasi juu yetu. Dhuluma, wizi wa
mali ya umma kwa wachache ni tendo la ushujaa leo. Siku chache zilizopita
tuliona sifa kubwa ya mwajiriwa wa ngazi ya juu serikalini ni UFISADI. Neno
hili lilipoteza ukali wake na jamii imeanza kulipokea taratibu kama mojawapo ya
mitindo ya maisha. Kwenye kashfa hii ya ufisadi walimebanwa wengi, hata
viongozi wa Kanisa walikuwepo! Siku zile sadaka kwa baadhi yao zitolewa kupitia
"account," binafsi ya kiongozi wa dini. Je, hali imebadilika? La
hasha! Leo uovu ule ule unafanyika ila kwa njia ya kuwatia watu hofu. Leo mwenye nguvu yu sahihi- “The might is right” hata
kama afanyacho ni hovyo. Tupo kwenye bonde na uvuli wa mauti.
Leo pia ndoa nyingi zipo ICU, na zinazoishi basi ni
kwa mikataba isiyo rasmi. Tunaishi kwa kukubaliana kwa kutokubaliana. Yaani
ndoa hizi zimeshikiliwa na uwepo wa watoto tu, au mali chumwa pamoja. Maana na
upendo katika ndoa haupo.
Kila umtazamaye leo, au kukutana naye, na kuanza
kubadili mawazo kwa moja au jingine, utagundua yaliyomo moyoni mwake. Wengi
tupo "kidilidili tu," na wengi miongoni mwetu tushakata tamaa ya
maisha. Maisha yamekuwa magumu kupindukia, na mbele hakuna tumaini. Haki za
watu zinakanyangwa mchana kweupe, na hakuna hata mmoja wetu mwenye jeuri ya
kusimama na kusema hapana. Wapo watu wasomi wa taifa hili? Wapo wapi wazee wa
taifa hili? Zipo wapi taasisi za dini, ambazo ndizo “sauti za
wasio na sauti?” Kwa nini kumekuwa na ganzi ya mtindo huu? Je, Mungu hana nguvu
tena? Hofu ya Mungu haipo tena! Ni sawa na mwanamuziki mmoja wa kizazi kipya
aliyeimba hivi; "aliye nunua cheni ya dhahabu kanunua feki, na aliyepokea
fedha ya mauzo ya cheni ya dhahabu kapewa fedha feki." Huu ndio ulimwengu
wetu wa leo na wenye mfanano wa enzi za Nuhu. Safina yetu leo ni nini?
Ndugu yangu, safina
yetu ya leo ni jukumu zima la kujisalimisha. Kujisalimisha huku ni moja ya
kujitakasa; yaani kuacha uovu na kukumbatia mema. Ni kuwa na MOYO SAFI kwa yote
tufanyayo, fikiri na kuishi. La sivyo hatutamwona Mungu. Yesu anasema,
"Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu, " Mt 5:8. Ni wakati
wa kubadili mtindo wa maisha kwa kuisalimisha nafsi yako. Kuhusu jambo hili
muhimu Yesu anasema, "Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza;
na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani anafaidiwa nini
mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini
badala ya nafsi yake?" Mt 16:25-26. Ndugu, wakati ndiyo sasa. Badilika!
Katika njili, Yesu anatoa angalizo la kujihadhari na
chachu ya Mafarisayo na chachu ya
Herode. Ubaya wa mafarisayo ulikuwa kutokuishi yale wasemayo. Na chachu ya
Herode ni maisha ya ukatili, kulipa visasi kwa wapinzani wake, na uroho wa
madaraka. Kwa hili kumwaga damu haikuwa jambo la ajabu pale alipoona utawala
wake unatikiswa. Leo Tanzania tumefikia hatua hiyo ya Herode. Wanayoyafanya
hayo ndugu zangu, tunao huku kwenye makanisa yetu. Tunasali nao, na wanatutia
upofu kwa tumchango twao tukubwa. Tuwakemee na hata kutoshiriki damu hiyo.
Tuyaseme kwa uwazi na kuyaishi. Siku hizi watu hawa wanatumia nyumba za ibada
kufikia hatma zao za kupata uongozi, na hata kuhalalisha uovu wao. Tusali daima
Mungu atupatie viongozi na siyo hao wanaijinadi kwa kupitia nyumba za ibada na
makanisa. Yesu analikemea, nasi twapasa kulikemea. Tusipofanya hivyo kama
wafuasi wake, adhabu yake ni kubwa mbele ya kiama. Yesu anasema, "Nami nawaambia,
kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya
malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya
malaika wa Mungu," Lk 8-9. Hii ndiyo Habari siku ya ukumu ya mwisho.
Huwezi kusema unamwogopa Mungu, na hapo hapo unawatendea watu jeuri. Huu ni
unafiki wa hali ya juu, na mbaya zaidi kwa yeyote yule afanyaye maigizo haya
aelewe kwamba anajikaanga na mafuta yake mwenyewe. Mungu kamwe hafanyiwi
dhihaka!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mna macho, hamwoni; mna masikio,
hamsikii? Wala hamkumbuki?” Mk 8:18
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tuumbie moyo safi. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario