UKULU WA MTAKATIFU
PETRO
Somo:
1Pet 5:1-4
Zab:
23:1-3a, 4, 5, 6
Injili:
Mt 16:13-19
Nukuu:
“lichungeni kundi la
Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama
Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo,” I Pet 5:2
“Wala si kama
wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile
kundi,” 1Pet 5:3
“Na Mchungaji mkuu
atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka,” 1Pet 5:4
“Vivyo hivyo
ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate
kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5
“Akawaambia,
Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Mt 16:15
“Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa
Mungu aliye hai,” Mt 16:16
“Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa
mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17
“Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18
“Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote
utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote
utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:19
TAFAKARI:
“Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anafanya kumbumbuku ya Ukulu wa Mtakatifu Petro. Ukulu huu
ndiyo mamlaka na Kiti chake Petro. Ukulu huu wa Mtakatifu Petro hakujitwalia
mwenyewe, bali alihesabiwa haki hiyo na Kristo mwenyewe pale alipotoa ukiri wa
kweli kumuhusu Kristo, yaani, aliyetengwa kwa kazi maalumu ya wokovu wetu na
ndiye mwana wa Mungu.
Hivyo, moja ya jukumu
la Kiti hiki ni kuifundisha na kuitetea Imani ya kweli kama kilelezo cha uwepo
wa Kristo katika Kanisa. Petro kama Halifa wake Kristo, na wote waliofuata
baada yake Petro, yaani, Mababa watakatifu, wana jukumu hilo kubwa katika
Kanisa. Yesu alitaka kujua kama Mitume wake wanafahamu vyema yeye ni nani na
ujumbe aliokuwa anausimamia. Hivyo aliwauliza wao binafsi wanafikra gani
kumuhusu yeye baada ya kuwauliza watu wanasema nini juu yake. Hivyo Yesu “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Mt 16:15. Jibu la swali hili ndilo linalomwesabia
haki ya Ukulu wa Mtakatifu Petro na wale wote waliofuata baada yake, yaani
Mababa Watakatifu. “Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo,
Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Haya
ndiyo majibu sahihi ya Mtume Petro yenye kutoa picha na wajibu wa Kiti
hicho-UKULU.
Yesu kwa kuridhika na
jibu la Petro anauthibitisha Ukulu huo kwa kusema, “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Ni
wazi, uwepo wa Petro kati ya Mitume wenzake na jumuiya ile ya kwanza ya
Wakristo kunampatia nafasi ya pekee katika kutimiza wajibu wake na kutumika
kwake. Ni wazi pia nafasi hii ya pekee kwa Petro siyo tokeo la umahiri wake,
bali ni neema ya Mungu. Naye Yesu anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “Heri
wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba
yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17. Mamlaka haya ya Petro kama Halifa wake Kristo
ni Neema ya Mungu mwenyewe. Badiliko la jina Simoni na kuwa Petro, yaani
Mwamba, unathibitisha mtu mpya mwenye jukumu jipya. Hii ndiyo sababu pia ya
Mababa watakatifu kuchagua majina mapya mara baada ya kuhesabiwa haki na Mama
Kanisa.
Wapendwa
wana wa Mungu, Ukulu huu wa Mtakatifu Petro unakipa uzito Kiti hicho katika
mamlaka yake kama Yesu mwenyewe asemavyo, “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme
wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni;
na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:19.
Haya ndiyo mamlaka ya kiti hiki na hasa kwa swala zima la Huruma ya Mungu kwa
ondoleo la dhambi. Hii ndiyo sababu pia ya Baba Mtakatifu kuwa na uwezo na mamlaka
ya kuutangaza mwaka wa Kanisa wa HURUMA YA MUNGU.
Wapendwa wana wa Mungu,
majukumu na mwonekano wa Ukulu huu ni ule wa kutumika badala ya kutumikiwa. Na
Yesu anasema, “na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza
kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile
Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe
fidia ya wengi,” Mt 20:27-28.
Kiongozi yeyote yule
aliyepewa dhamana na umma wa watu, ama kuhesabiwa haki na Mama Kanisa, yampasa
kutumika na siyo kutumikiwa. Mtume Petro anasema, “lichungeni kundi la Mungu
lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu
atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo,” I Pet 5:2. Ndugu yangu,
wewe na mimi tuliye hesabiwa haki na kupewa dhamana na Mama Kanisa, ama umma wa
watu kwa mujibu wa sheria na taratibu zake, hatupo hapo tulipo kwa maslahi yetu
binafsi. Mimi na wewe tulio hesabiwa haki hiyo na Mma Kanisa tupo hapo tulipo
kumwakilisha Kristo Yesu aliyetumika badala ya kutumikiwa.
Nawe uliyepewa dhamana
hiyo na umma wa watu kwa mujibu wa sheria na taratibu zake upo hapo ulipo kwa
ajili ya umma huo wa watu waliokuweka hapo kwa kazi hiyo maalum, na siyo
kuutafuta utukufu binafsi, na mwisho wa siku kujeuka na kuwa mungu mtu. Nafasi
zote tuzipatazo kwa ajili ya huduma kwa jamii, yatupasa kutumikia kwa
unyenyekevu, heshima, na kujali utu wa watu. “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini
wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu
Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5.
Ndugu yangu, huduma yo
yote ile isiyokuwa na taswira ya unyenyekevu kamwe haimwakilishi Kristo, wala
umma wa watu tunaowatumikia. Na kwa namna hiyo na katika huduma hiyo hakuna
utukufu wala sifa kwa Mwenyezi Mungu. Kristo
kamwe hajidhihirishi popote pale pasipo na unyenyekevu. “Na Mchungaji
mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka,” 1Pet 5:4.
Unyenyekevu katika huduma tuzitoazo utawashangaza wengi na hasa wale ambao mawazo yao hutanguliza nafsi zao.
Tumsifu Yesu Kristo!
Na huku ndiko kutumika: “Wala si
kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile
kundi,” 1Pet 5:3
Tusali:-Ee
Yesu na Mwalimu wetu, tujalie fadhila ya unyenyekevu, ili kutumika kwetu kwa ajili
ya wengine kudhihirishe uwepo wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario