JUMAMOSI WIKI YA 7 YA
MWAKA-I
Somo:
YbS 17:1-13
Zab:
103:13-14, 15-16, 17-18a
Injili:
Mk 10:13-16
Nukuu:
“Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata
mavumbini akamrudisha,” Ybs 17:1
“Akawapa wanadamu siku kwa idadi, na muhula
ulioamriwa, akawapa amri juu ya vitu vilivyomo,” YbS 17:2
“Akawajaza
maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu,” YbS 17:6
“Ila Yesu alipoona
alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie;
kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14
“Amin,
nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia
kabisa,” Mk 10:15
TAFAKARI:
“Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.”
Wapendwa wana wa Mungu,
kuupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo ni kujiachia pasipo shaka kwa Yesu
Kristo Mwana wa Mungu aliye hai katika hali ya unyenyekevu, Imani, na Upendo.
Ni kuungana na Kristo na kushiriki neema zake kama watoto wadogo kwa wazazi,
walezi, au walimu wao. Ni kuipokea Habari njema ya wokovu na mafumbo yake yote.
Ni kuambatana na Kristo na kumuishi pasipo mizizi ya dhamba kama: kiburi,
chuki, hisi mbaya na kadhalika. Kama watoto, hatupaswi kuwa na mashaka na lile
atufundishalo Kristo wala lile atuelekezalo kulifanya. Hivyo, “Ye yote
asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” Mk 10:15.
Unyenyekevu na upole ndiyo siri ya kuupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo.
Kwa hali hii, watoto
wadogo wanauishi wongofu wa kweli kwa sababu hawana walipojishikilia kama
sehemu ya usalama wao zaidi ya wazazi wao, au walezi wao, au walimu wao. Kwa
maana hiyo Yesu anasema, “Amin, nawaambia,
Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,”
Mt 18:3. Wongofu huu unatutaka mara zote kulenga lililo kamilifu licha ya kwamba
udhaifu upo. Ni kuyatafuta yale yaliyo juu kule Kristo alipo. Ni kuishi maisha
mapya ya ufufuko. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.” Kol 3:1. Ni kuamini
yapo maisha ya milele mara baada ya maisha ya hapa duniani ambayo ni jukumu la
muda mfupi.
Wapendwa katika Kristo,
na huu ndio mwaliko wa wale wote wanaoishi kama watoto wadogo katika hali ya
Unyenyekevu, Upole, Upendo na Imani kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo,
“Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa
ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14. Kuwazuia watoto wadogo kwa weza maanisha
hali ile ya kupandikizwa hofu na kuwa mbali na upendo wa Mungu Baba. Na
inawezekana pia kutokana na mitazamo yetu, mila na desturi zetu zinatufanya
kuwa mbali na upendo huu wa Mungu Baba. Milango ya Neema na Huruma ya kweli
imefunguliwa kwa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. “Kwa kuwa
torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,”
Yoh 1:17. Hakuna sababu ya kuwa na hofu ndani na katika Kristo Yesu. Kwake
Kristo kuna baraka muda wote, Mk 10:16. Ndugu yangu uhitaji baraka kutoka kwa
Kristo Yesu?
Kuzipata baraka na
neema za Mungu ni pale tu wewe na mimi tunapoukubali udogo wetu. Kuukubali
udogo wako hakumaanishi unyonge au udhaifu, bali hali hiyo husema zaidi kile
ulicho, na utayari wa kujipokea katika mafanikio yako, na mapungufu yako. Hivyo
somo letu la kwanza leo linatupeleka katika tafakari hii ya kina kuhusu uhasili
wetu, kwamba, “Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini
akamrudisha,” Ybs 17:1. Ndugu yangu unaye safari nami katika tafakri hii, ni
vyema ukaelewa jambo hili muhimu katika maisha yako, kwamba pamoja na ufahari
alikuwa nao mwanadamu kwa kila hali, nafsi hiyo lazima ionje mauti. Na hii
ndiyo maana ya “kurudi mavumbini.” Ikiwa huu ndio ukweli, salama yako na yangu
ni kuishi na kutenda katika haki kwa maana, “hazina za uovu hazifaidii kitu,
Bali haki huokoa na mauti.” Mit 10:2. Na “mali hazifaidii kitu siku ya
ghadhabu: Bali haki huokoa na mauti,” Mit 11:4.
Ndugu yangu,
ulimwenguni hapa siyo mahali petu pakudumu. Ulimwengu huu pamoja na mazuri na
mabaya yake, ni sehemu tu ya maandalizi ya umilele. Hivyo, Mungu, “akawapa
wanadamu siku kwa idadi, na muhula ulioamriwa, akawapa amri juu ya vitu
vilivyomo,” YbS 17:2. Mali, uwezo, ufahari, nguvu na mamlaka ni swala la wakati
na muda mfupi tu. Kwaya kama yalivyo au ilivyo hakuna umilele. Ukitumika vyema
katika hayo upo uwezekano wa kuurithi ufalme wa Mbinguni, na kinyume chake
ndiyo kilio na kusaga mengo, Mt 13:42.
Hukumu ya mwisho
inamuhusu kila mmoja wetu mwenye pumzi leo na sasa. Nalisema hili kwa sababu
kati yetu hakuna anayeishi kwa nguvu zake mwenyewe zaidi ya huruma na neema ya
Mungu, Rum 14:7. Hivyo katika uumbaji wetu wanadamu na kwa namna ya pekee
kabisa, Mungu “akawavika nguvu kama Yeye mwenyewe, na kuwafanya kwa mfano
wake,” YbS 17:3, (rejea pia Mwa 1:27). Hii ndiyo tofauti katika ya mwanadamu na
malaika. Malaika humzunguka Mungu wakati wote, bali mwanadamu ni kiumbe
shirikishi cha Mungu. Katika kweli hii, Mungu “Akaitia hofu ya binadamu katika
vyote vyenye mwili, ili wawatawale wanyama na ndege,” YbS 17:4-5. Utawala huu
aliowezeshwa mwanadamu juu ya viumbe vingine siyo ruksa ya angamizo, bali dhamana
ya Kimungu ndani yake, na uwezo wa kutenda katika mwono chanya. Kwa maana
nyingine mwanadamu ni mlinzi wa yale yote aliyoyaumba Mungu ili yote kwa umoja
na upekee wake yaufikie ukamilisho ule kusudiwa ndani ya kila alichokiumba
Mungu. Kumbe si vyema mimi na wewe kuukatisha uhai wa kiumbe kama sisimizi.
Ndugu yangu, maarifa
ikiwa ni pamoja na karama na vipaji ulivyojaliwa na Mungu si kwa faida yako
binafsi, bali kwa ajili ya wengine pale ulipo na mazingira yanayokuzunguka. Je,
umesahau kuwa wewe ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu? Rejea, Mt
5:13-13. Hivyo ni katika uumbaji huo kwamba, Mungu “Akawajaza maarifa ya
hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu,” YbS 17:6. Kumbe jukumu la kwanza
kwako na mwako katika ulimwengu huu licha kuwa sehemu ya kujiandaa kwa maisha
ya umilele yatupasa kupafanya kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi.
Ndugu yangu, kila
alichokujalia Mungu katika maisha unayoishi hakipo hapo kwa bahati mbaya. Vyote
alivyokujalia Mungu vikusaidie wewe na wengine kuuona uso wa Mungu. Hapa ndipo
tunapoona muunganika w asomo hili na Injili ya leo. Mlango wa kupita na kuijua
siri ya Mungu ndani yetu ni kuwa kama watoto wadogo, yaani, ni katika udogo
wako Mungu ujifunua kwako na kwa wengine. Na hii ndiyo maana ya maneno haya:
“Akawafanyizia ulimi, na macho, na masikio, akawapa na moyo wa ufahamu; ili
kuwaonyesha adhama ya kazi yake, ili wajisifie katika miujiza yake, na
kujijulisha kicho chake ulimwenguni, na kulihimidi jina lake takatifu,” YbS
17:7-10. Karama na vipaji alivyotujalia Mungu huo mkondo salama pale tu
tunapokuwa tayari kujinyenyekeza. Pasipo unyenyekevu yote aliyotujalia Mungu
husinyaa. Unyenyekevu ni kirutubisho hali na makuzi ya yale yote aliyotuwezesha
Mungu ndani yetu. Hii ndiyo sheria ya maarifa kaika mafanikio, na uzima katika
urithi, YbS 17:11
Ni wanyenyekevu tu
ufanywa wateule wa Mungu, na katika agano lake, YbS 17:12, na msingi wa agano
hilo ni upendo, Yoh 13:35. Na kwa upendo huo, “Kwa macho yao waliiona enzi ya
utukufu wake, na kwa masikio yao waliisikia sauti yake yenye nguvu,” YbS 17:13.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Bwana alimwumba Adamu katika
mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha,” Ybs 17:1
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nikumbushe daima kuwa mimi ni mavumbi tu na mavumbini nitarudi.
Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario