IJUMAA WIKI YA 4 YA MWAKA-I
Somo:
Ebr 13:1-8
Zab:
27:1, 3, 5, 8b-9abc
Injili:
Mk 6:14-29
Nukuu:
“Upendano wa ndugu na udumu.
Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika
pasipo kujua,” Ebr 13:1-2.
“Wakumbukeni hao
waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile
ninyi nanyi mlivyo katika mwili,” Ebr 13:3
“Maana Herode
alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na
alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa
furaha,” Mk 6:20
“Mara
akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi
katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji,” Mk 6:25.
“Mfalme akafanya
huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi
karamuni, hakutaka kumkatalia,” Mk 6:26.
TAFAKARI:
“Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
sifa na kutaka umaarufu umewaponza wengi. Ni jambo la busara kujua uwezo na
mipaka yako hasa pale unapotakiwa kutoa maamuzi kwa nafasi uliyo nayo. Ni mara
ngapi kwenye vikao mbalimbali vya maandalizi ya matukio mbalimbali kama vile;
harusi, jenzi mbalimbali, unatoa ahadi ambazo kwa kiasi fulani zipo nje ya
uwezo wako. Waswahili wanasema hivi, “mbuzi hula umbali wa kamba yake.” Leo
tunaona katika Injili tukio la ajabu sana. Mfalme Herode anajiweka kitanzi
mwenyewe kwa kutaka sifa na umaarufu.
Ikiwa ni siku ya
kuzaliwa kwake, Herodi anatoa ahadi kwa Binti yake ambaye aliufurahisha ukumbi
kwa kucheza vizuri. Wakati mwingine yakupasa kuwa na hakiba ya maneno hata kama
hali ya kusema chochote inakuruhusu. Naye Herode akamwapia binti yake, “Lo lote
utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu,” Mk 6:23. Maneno haya
yalikuwa mazito sana kwa binti huyu. Hivyo kwa hali ile alihitaji ushauri wa
haraka. “Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha
Yohana Mbatizaji,” Mk 6:24. Na hii
ndiyo iliyokuwa nafasi ya Herodia ya kumwangamiza Yohane Mbatizaji ambaye
alionekana kero na wingu kwa mahusiano yake na Herode. Tuelewe kwamba Herodia
alikuwa mke wa Filipo ndugu yake Herode. Yohane Mbatizaji alikemea uovu huu kwa
nguvu zake zote kwa Herode kumuoa mke wa ndugu yake. Na sasa Yohane Mbatizaji
anakuwa mbuzi wa kafara.
Wapendwa wana wa Mungu,
wapo wengi katika jamii yetu wanakutwa na umauti kama Yohane Mbatizaji kwa vile
tu wanasimamia kweli na wapo tayari kwa ajili ya kweli. Maisha ya Yohane
Mbatizaji hayana ndoa lolote katika jamii. Ukweli huu hata Mfalme Herode
anaufahamu. “Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki,
mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa
akimsikiliza kwa furaha,” Mk 6:20. Yule binti ya Herode bila kufahamu
kilichokuwa nyuma ya pazia anapeleka ujumbe kadiri alivyoambiwa na Mama yake.
Binti huyu pia anapenda kwa nafasi hii na umati huu wa watu wengi kumfurahisha
Mama yake. Nani kama mama jamani? “Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme,
akaomba akisema, “nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana
Mbatizaji,” Mk 6:25.
Habari hii
inamuhuzunisha sana Mfalme Herode, ila kwa vile aliipenda sifa na umaarufu
anashindwa kuizuia nafsi yake iliyoegemea mwili kwa sasa. “Mfalme akafanya
huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi
karamuni, hakutaka kumkatalia,” Mk 6:26. Hapa
ndipo tunapoona matumizi mabaya ya madaraka tuliyonayo na kulevywa nayo kwa
ajili ya kujenga majina yetu na kusahau haki na unyenyekevu kama viongozi.
Uongozi ni dhamana. Uongozi ni kuwajibika kuliko haki na usawa. Uongozi ni
mizania ya haki kwa wote.
Mfalme Herode
anaisikiliza nafsi yake ambayo kwa sasa inasukumwa na mwili. “Basi matendo ya
mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui,
ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo
nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo
ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Maamuzi yoyote
uyafanyayo katika hali hii hayana baraka ndani yake. Hivyo, “Mara mfalme
akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle
gerezani,” Mk 6:27
Kifo cha ukatili dhidi
ya Yohane Mbatizaji mtu mwenye haki kinakuwa furaha ya muda mfupi kwa Herodia. Naye yule askari mwaminifu “akakileta kichwa
chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye,” Mk
6:28. Hata leo watumishi wetu waaminifu, askari polisi na jeshi, huwa wanapewa
maagizo na viongozi wetu wenye kutaka sifa na kuyajenga majina yao kwa kumwaga
damu za wenye haki kwa kile kisemwacho kama maagizo kutoka juu. Ni mara ngapi
tunashuhudia vitendo vya aibu na uvunjifu wa haki za binadamu kwa “maagizo
kutoka juu.” Ndugu yangu, aliye juu ni Mungu tu. Wengine wote wanaojiona wapo
juu ni kutaka kuchukua nafasi ya Mungu, ambayo hata ibilisi alipenda kufanya
hivyo na mwisho wa siku alilaaniwa milele. Je, nawe wapenda laana hiyo?
Ndugu yangu, ni vyema
ukajua uongozi ni dhamana na mwisho wa siku itakupasa kutoa hesabu yake. Basi
pale tunapokosea kutokana na ubinadamu wetu, tuwe wepesi wa kujirudi na
kujirekebisa. Leo viongozi wetu walio wengi wamefikia hali ya kuhalalisha maovu
yao kwa kile wanachojiita ‘wazalendo na wenye mawazo mapana kwa manufaa ya
nchi’ ilhali ni kwa manufaa yao binafsi na familia zao na vyama vya siasa wanavyoviwakilisha, ambavyo
vinaonekana kushika hatamu ya umilele.
Wapendwa wana wa Mungu,
bila kujinyenyekeza kuliko kweli na haki kutoka mioyoni mwetu pale tunapopewa
dhamana na umma, hata yale mazuri tunayoyafanya hayana thamani yoyote mbele ya
Mungu. Mfalme Daudi kwa unyenyekevu wake na kujua nafasi aliyokuwa nayo kama
kiongozi wa kutenda haki kwa wote bila kujali maslahi binafsi na marafiki zake,
Ufalme wake unabarikiwa hata kwa mrithi wake. Hivyo, “na kwa ajili yake
akainuliwa mwanawe, mtu wa ufahamu aliyekaa salama. Sulemani alimiliki katika
siku za kufanikiwa, naye Mungu akampa raha kumzunguka pande zote, ili alijengee
jina lake nyumba, na kumwekea tayari patakatifu pa milele,” YbS 47:12-13.
Jambo la kushangaza leo
ni hili; kwa asilimia kubwa viongozi tulionao katika jamii yetu leo ni watoto
au familia za viongozi waliokuwapo hapo awali katika uongozi. Kwa jicho la
kawaida kabisa waweza kuona mtoto huyu siyo njia yake, bali ni mazoea ya
kufaidika na mfumo ambao hauna uwajibikaji. Uongozi umekuwa kama ajira ya
kawaida na wala siyo huduma katika maana ya kutumika. Yesu anatuambia, “na mtu
ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt
20:27-28. Ni wazi kwa mfumo huu wa kutokuwajibika na kutumika ndio unao
tugharimu sana katika Taifa letu leo.
Pamoja na kasoro hizo
kijamii salama yetu twaipata kutoka waraka kwa Waebrania kama tulivyosoma na
kusikia. Mosi, yatupasa kudumisha undugu kati yetu bila kujali hali na
mazingira yatu. “Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana
kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua,” Ebr 13:1-2. Palipo
na umimi kila kitu ubaki katika giza. Umimi unapokufa jamii hufurahia uhuru,
amani, umoja, mshikamano, na upendo wa kweli.
Pili, yatupasa kusimama
katika kweli na haki. Tukubali kusikiliza na kukosolewa pale tunaposhindwa
kutoa kwa jamii kile tulichotakiwa kutoa kadiri ya hali na nafasi zetu.Ni
nafasi pia ya kuwa sauti ya wasio na sauti katika jamii inayotuzunguka. Hivyo,
“Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao
wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili,” Ebr 13:3. Hakuna
sababu ya kufurahi uovu au kuhalalisha uovu hata kama umetendwa na nani. Vyombo
vyetu haki, visimamie haki ipaswavyo.
Tatu, na kadiri ya
Injili yetu ya leo, kila mmoja wetu na heshimu maagano yake katika maisha. Na
moja ya maagano hayo ni Ndoa Takatifu. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na
malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu,”
Ebr 13:4. Wahenga wetu wanatuasa hivi; ‘kisicho haki hakiliki.’
Nne, kila mmoja wetu
aridhike na kile apatacho, na kutoka hapo halipo afanye bidii katika kweli na
haki kuongeza kile alichonacho ili kukidhi mahitaji yake ya binafsi na ziada.
Hivyo, “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa
kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa,” Ebr
13:5. Lengo letu likiwa kupata zaidi bila kutoka jasho katika kweli na haki, ni
maumivu kwa wengine hasa wanyonge wasio na pakukimbilia.
Tano, twapaswa kuwa na
moyo wa fadhila na shukrani kwa kila mmoja wetu, na hasa wale waliokuwa sababu
ya sisi kuwa kile tulicho leo na sasa. Hivyo ndugu yangu, “wakumbukeni wale
waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana
mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao,” Ebr 13:7. Moyo usio na shukrani
ukausha mema yote. “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele,” Ebr
13:8. Mkono wa Bwana si mfupi, wala sikio lake si zito kusikia.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kalibu
ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake,” Mit
27:21
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
tujalie neema yako tudumu katika uaminifu wa kweli.Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario