jueves, 2 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 4 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 4 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 13:15-17, 20-21

Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6

Injili: Mk 6:30-34

Nukuu:

“Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake,” Ebr 13:15

“Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu,” Ebr 13:16

 Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha,” Mk 6:30 

Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,” Mk 6:31

TAFAKARI:Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, haki huenda wa wajibu. Kumbe utimizapo wajibu wako vyema una haki ya kupata kadiri ya wajibu uliutimiza. Jambo la ajabu wapo kati yetu wengi hupenda kutendewa haki ilhali ni wachengaji wazuri sana katika kutimiza wajibu wao. Mungu hufurahishwa sana pale unapotimiza wajibu wako vyema na kwa uaminifu kadiri ya nafasi na wito wako. Na yote hayo tuyafanye kwa moyo na upendo. Pamoja na changamoto tutakazokutana nazo, neno la Mungu linatuambia kwamba, “Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu,” Ebr 13:16. Huu ndio wajibu wa kwanza, na sababu ya msingi ya kuumbwa kwetu.

Wajibu huu muhimu hautegemea uzuri wa kile ufanyacho au aina ya kazi ufanyayo, bali ubora katika kufanya na ukamilifu wake. Mtakatifu Theresa wa Yesu, anasema kila mmoja wetu aweza kuwa mtakatifu hasa kwa matendo yale madogo madogo tuyafanyapo kwa ukamilifu wake na uaminifu. Kufikia kiwango cha utendaji katika ukamilifu na uaminifu wake, kitakuhitaji kuwa na nidhamu. Bila nidhamu katika utendaji, ni vigumu kulifikia lengo kusudiwa. Na nidhamu ya utendaji ni pamoja na kuwatii “wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi,” Ebr 13:17. Hata hivyo hapa lazima tuwe makini kwa sababu wapo baadhi ya viongozi wetu leo wanao jifananisha na Mungu, na kupoteza dhana nzima ya uongozi na unyenyekevu. Bila unyenyekevu hakuna utakatifu, wala sala ya utakatifu.

Wapendwa wana wa Mungu, sala ya utakatifu kwanza kabisa ni kuwa na imani ya kwamba kile uombacho ushakipata bila kuwa na shaka yoyote juu Mungu. Pili, sala ya utakatifu ni sala ile isiyobeba ubinafsi wako. Ni sala au maombi yanayojali wengine na kwa nafasi ya pekee wale ambao wapo chini yako au unao wajibika kwao moja kwa moja. Na kielelezo cha sala zetu, na namna ya kusali ni Kristo mwenyewe. Kwake tuna shule ya kweli kujifunza unyenyekevu na kunyenyekea. “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina,” Ebr 13:20-21. Ndugu yangu tunayesafiri pamoja katika tafakari hii, yachunguze maombi yako na sala zako mbele ya Mungu.

Mtume Yakobo anatupa angalizo juu ya sala na maombi yetu na kusema, “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3. Kumbe sala ya utakatifu ni kuepuka pia tamaa zako kwa kile uombacho. Ndugu yangu, Mungu anayafahamu mahitaji yako yote na atakupatia kadiri ya mahitaji hayo. Kumbe unapoishinda nafsi yako katika ubinafsi wake kwa maombi na sala zako, Mungu hukupatia hata yale ambayo hukuyaomba kwa sababu anajua unayahitaji katika kweli na haki. Mungu anayajua mahitaji yako yote. Jambo la muhimu ni hili, ‘timiza wajibu wako kwa uaminifu.’

Wanafunzi wa Yesu wanatimiza wajibu wao kwa uaminifu na wanatoa taarifu ya kile walichokifanya mbele ya Yesu. “Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha,” Mk 6:30. Tendo hili la uaminifu kwa yale waliyoyafanya mitume linamfurahisha Yesu, naye anawaonea huruma.Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula,” Mk 6:31. Ni furaha iliyoje tunapohesabiwa haki kwa yale tuyafanyayo kwa uaminifu na yule mwenye Mamlaka na Haki? Ni furaha ya kweli kweli!

Ndugu yangu, kile ufanyacho kwa uaminifu na kuwajibika kuliko tukuka hubarikiwa na wale ulio wahudumia hubarikiwa pia. Na ndivyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wale wa Yesu. “Naye (Yesu) aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi,” Mk 6:34. Hivyo ni vyema kuuthamini wajibu wako na kufanya kwa uaminifu wote. Leo kama tungewajibika kwa asilimia 50 tu kila mmoja wetu kwa nafasi yake na wito wake, ulimwengu huu, na kwa namna ya pekee nchi yetu ingekuwa mahali pazuri zaidi pa kuishi. Basi nikusihi ndugu yangu anza kuwajibika hapo ulipo katika uaminifu wote. Acha mazoea katika utendaji wako wa kila siku. Ila “kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake,” Ebr 13:15.

Tumsifu Yesu Kristo!

"Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki,” Mit 15:29.

Tusali:-Ee Yesu, tufundishe kweli katika unyenyekevu na kusali. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario