viernes, 10 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 6 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 6 YA MWAKA-A

Somo I: YbS 15:15-20

Zab: 119: 1-2, 4-5, 17-18, 33-34

Somo II: 1Kor 2:6-10

Injili: Mt 5:17-37

Nukuu

“Ukipenda, utazishika amri zake, na kutenda amini ni shauri lako,” Ybs 15:15

“Mbele ya mwanadamu upo uzima na mauti, naye atapewa apendavyo,” YbS 15:17

“Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika,” 1Kor 2:6

“Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao,” 1Kor 2:9

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17

Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi,” Mt 5:36

TAFAKARI: “Ukipenda, utazishika amri zake, na kutenda amini ni shauri lako.”

Wapendwa wana wa Mungu, Sheria ya Bwana ni utaratibu wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu, na kuwa na mahusiano mazuri naye kwani Yeye ndiye uhai na uzima wetu. “Ameweka mbele yako moto na maji; utanyosha mkono wako uchaguavyo,” YbS 15:16 Wana wa Israeli walipewa sheria kama mwongozo wa kutenda na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. “Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe,” Kut 24:12. Sheria hizi zilipaswa kufuatwa kiaminifu, upendo kwa jirani, na bila kuzichakachua. “Ukipenda, utazishika amri zake, na kutenda amini ni shauri lako,” Ybs 15:15

Ukamilifu na uaminifu wa mtu ulipatikana katika kuzishika sheria za Bwana. Kwa sababu, “sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima.” Zab 19:7. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuzishika sheria za Bwana. Na hilo ndilo lililokuwa kusudi la sheria. Jambo la kushangaza wakati wa Yesu, Wayahudi hawakuwa wanafuata Torati kama iliyokuwa mwanzo, yaani, nyakati za Musa. Wayahudi walikuwa wanafuata tafsiri ya Torati ambayo iliendana na matamanio yao na siyo ya Mungu. Huu ndio ugomvi uliokuwepo kati ya Yesu na Waandishi na Mafarisayo.

Matamanio haya ya Mafarisayo na Waandishi katika ubinadamu wao ambayo yalienda kinyume na tamanio la  Mungu juu ya sheria nyakati zile za Yesu, ndiyo hayo yaliyojitokeza pia nyakati zile za Nabii Eliya na wale wafuasi wa miungu ya Baali. Kuwarudisha kwenye mstari wa kweli na haki, ikiwa ni kumfuata na Mungu wa kweli na wakuabudiwa, Nabii Eliya anawaasi na kusema, “Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno,” 1Fal 18:21.

Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kwa hiki kilichotokea, Wayahudi hawakupaswa kukengeuka katika imani yao. Ila kadiri tusomapo historia ya Taifa hili la Israeli na kutafakari, tunaona mambo hayakuwa kama yalivyopaswa kuwa. Hali ya uvuguvugu wa imani ya kweli ilikuwa hivyo hata nyakati za Yesu hata pamoja na kupewa torati kama mwongozo wa kufuata na kuwa karibu na mapenzi ya Mungu.

Jambo muhimu sana la kujua ni kwamba kipindi cha Yesu, Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na matendo yake kupitia masimulizi), iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)

Kwa mantiki hiyo hapo juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa 350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed) katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, (Mt 15:2-3, 6; Mk 7:3, 5, 8, 9, 13). Naye Yesu anawaambia, “Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:8. Kwa maneno mengine ni sawa na kuchagua mauti na kuacha uhai. “Mbele ya mwanadamu upo uzima na mauti, naye atapewa apendavyo,” YbS 15:17

Mapokea haya ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Mtume Paulo baada ya kuongoka na kuujua ukweli kuhusu sheria ya Bwana anawaambia Wakolosai, “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Ukweli ni kwamba, Mtume Paulo kama Mfarisayo kabla ya kuongoka kwake aliyafuata mapokeo haya ya wazee ambayo yalikuwa ni ‘ukweli wa Mungu uliopotoshwa.’ Paulo anakiri jambo hili na kusema, Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal 1:14.

Kwenye jambo hili, yaani kweli ya Sheria ya Bwana, Yesu anawakemea Mafarisayo na Waandishi na kusema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17. Hapa Yesu akubaliani nao kwa swala la kuichakachua Torati kama walivyokwisha kufanya. Yesu anarudisha mpango mzima wa Mungu katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Yesu anatoa zaidi maana ya sheria na ushikaji wa sheria hiyo. Yesu anawakosoa Mafarisayo kwa unafiki wao katika sheria na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache,” Mt 23:23

Utimilifu wa sheria kadiri ya mpango mzima na mtazamo wa Yesu umebebwa katika upendo. Hii ndiyo amri mpya. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Mtakatifu Agustino anatuambia kwamba, “ukipenda utafanya yote.” Ni katika mantiki hii kwamba, “mkipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Je, leo hatushangai kuona baadhi ya viongozi wakiichakachua Katiba ya nchi zao kwa ajili ya matamanio yao na uchu wao wa madaraka? Jambo hili limekuwa chanzo kikubwa cha machafuko mengi duniani na hasa kwenye bara letu la Afrika. Ni ukweli usiopingika kwamba, vikundi vingi vya kigaidi vimejitokeza pale sauti ya wengi katika mkondo sahihi, yaani, demokrasia ilipokanyagwa, kuporwa, kubezwa, na hata kubakwa kwa manufaa wa watu wachache tu katika kundi zima la walio wengi. Tanzania yetu leo haipo mbali na ukweli huu. “Hekima ya Bwana yatosha, mkuu mwenye uweza hutazama vyote,” YbS 15:18. Ni vyema tukasoma alama za nyakati. Nguvu ya madaraka aliyopewa kiongozi na umma wa watu, siyo fimbo ya kuwachapa, bali kuwaongoza katika kweli na haki.

Leo jamii yetu imeingiwa na hofu na ubaridi wa ajabu kwa sababu, ‘mwenye nguvu apaswa kupishwa.’ Wengi waanza kujisiri kuwa kuzuizini ilhali wapo huru. Hapa hakuna tena hekima ya Mungu. Leo tunatumia nguvu nyingi sana kujenga mnara wa hekima ya kibinadamu, na mwisho wa siku ni kama yale yaliyotokea kule Babeli, Mwa 11:3-9. “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika,” 1Kor 2:6. Leo baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya uongozi na umma wanasahau kuwa wao ni binadamu, tena wenye mifupa na nyama, na kinyume chake wanajifananisha na Mungu. Katika mazingira haya hakuna “hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu,” 1Kor 2:7. Na mtego wa wengi, hasa upofu wa madaraka hawaijui hekima hii “hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu,” 1Kor 2:8. Unapotumia madaraka yako vibaya na kuwaumiza watu, kuwanyong’onyesha watu, na hata kuwatia hofu watu, ujue waendelea kumsulubisha Kristo aliyekufa kwa ajili yako na hao usiowatendea haki na kweli. Kristo alikuwa kwa ajili yako na yangu ili sote tuwe huru mwili na roho. Ndugu yangu pasipo na unyenyekevu hapana uwepo wa Mungu. Hivyo hivyo pasipo upendo, kweli, na haki twaukataa uwepo wa Mungu. Hivyo, “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao,” 1Kor 2:9. Na hayo ndiyo yafanywayo na wanyenyekevu wa Mungu, yaani, wenye hofu ya Mungu.

Wapendwa katika Kristo, Injili yetu ya leo yatutaka tuyapime matendo yetu vyema hasa katika mizania ya kusamehe na kusamehewa. Yesu katika hili anatoa angalizo kubwa na kusema, "haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni," Mt 5:20. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki kuwa ni watu wema, na ndiyo kipimo cha kweli. Ndugu yangu, Mungu pekee ndiye hutuhesabia haki, tena si kwa matakwa yetu, bali kwa matakwa yake kwa sababu Yeye tu ndiye HAKI. Sisi binadamu tunashiriki tu ukamilifu wa Mungu kwa kuwezeshwa naye. Kwa mantiki hiyo, Mungu “hakumwamuru mtu yeyote awe asi, wala kumruhusu atende dhambi,” YbS 15:20. Ila kila mmoja wetu kawezeshwa kuwa mkamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu, Mt 5:48. Hata hivyo katika kweli hii kila mmoja yupo huru kuchagua uzima au umauti, YbS 15:17.

Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki na kuwa miungu watu. Huu ni upofu uliopitiliza. Kuwajua vizuri Mafarisayo na Waandishi nakualika usome sura yote ya 23 ya mwinjili Mathayo. Ni kwa sababu hiyo Yesu anatoa angalizo kwanza kama kweli tunataka uponyaji, lazima kusamehe kama hatua muhimu na mizania ya  kusamehewa.

Kusamehe ni amri kama kweli na sisi tunataka kusamehewa. Sala ya ‘Baba yetu’ imeliweka jambo hili wazi kama sharti la upatanisho na Mungu. Cha ajabu sala hii tunaisali wengine kila siku na kila mara kwa siku, ila bado kusamehe ni shiiida! Je, utaponywaje kama tatizo lako ni kuvunjika mguu, ila "P.O.P" umefunga shingoni? Mbona kila siku unatibu ugonjwa usioumwa kwa dawa tofauti? Kwa nini inakuwiya vigumu kusamehe na kupatana na ndugu yako? Je, wewe ni mkamilifu sana? Unatofauti gani na mafarisayo na waandishi wanachukuwa nafasi ya Mungu kwa kujihesabia haki?

Wapendwa wana wa Mungu, ukitaka sala yako, na maombi yako yapate kibali mbele ya Mungu, jipatanishe wewe mwenyewe, wewe na uliyekosana naye, na pia wewe na Mungu. Hivyo “basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23. Wengi na hasa wale tuliokosewa hupenda kuyarefusha mambo sana, na wakati mwingine tungependa tunyunyuziwe ubani kwa cheteso cha dhahabu ili tuwe tayari kwa kuyaongelea yale yaliyotutatiza.

Ila baraka na neema hutujia pale tunapokuwa na uhusiano mzuri na wenzetu, mazingira, na Mungu Muumba wetu. Furaha ya Mungu kwetu ni kuuishi upendo wa kweli na kuwa na mahusiano mazuri kati yetu na viumbe vyake vingine. Mahusiano haya mazuri huufunua utukufu wake Mungu. Maisha kama safari, yatupasa kuulinda uhusiano huo na ndugu zetu, mazingira na Mungu kadiri tunavyosafiri hadi mwisho wa safari yetu hapa duniani. Haya ni maisha yanayoongozwa na Roho wa Mungu ambaye utupa hofu hiyo ya Mungu ndani yetu. “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu,” 1Kor 2:10

Ni kwa mantiki hiyo agizo la Yesu lakutaka wewe na mimi, "patana na ndugu yako uwapo naye njiani," Mt 5:25. Maana yake ni nini? Kupatana na ndugu yako mngali njiani ni kufanya juu chini kupatana na ndugu yako angali yu hai. Msivute muda pasipo sababu. Kengele ikishagongwa hakuna tena pa kujitetea. Maapizo na laana hazikusaidii chochote. Unazidi jizibia riziki zako bure na baraka kutoka kwake mwenyezi Mungu. Unaposamehe unajiponya na kumponya mwenzako pia. "Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi," Yoh 13:35.

Wapendwa wana wa Mungu, ibada na sadaka zetu kwa Mungu huwa safi na za kumpendeza Mungu pale tunapokuwa na amani ya kweli ndani mwetu, na ndugu zetu, mazingira yetu, na Muumba wetu. “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako,” Mt 5:23-24. Amani hii ni pale unapokuwa tayari kupatana na kusamehe bila kipimo.

Wengi tumeshuhudia watu hawapendi kupatana na kuishia kuapizana pasipo sababu. Wapo wengine hata baada ya kuzidiwa wakiwa kitandani karibu ya kufa wanapoomba upatanisho na ndugu yake kunakuwa na mkwamo bila mwitikio wowote na mwisho mtu huyo hufariki katika hali ya  majonzi makubwa. Hivi unajisikiaje ndugu yako kufa akikuomba upatane naye nawe kwa kiburi chako hukusikia na hatimaye ndugu yako anafariki? Ndugu yangu, “Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani,” Mt 5:25. Je, kwa kutokupatana na ndugu yako angali hai, utajibu nini mbele ya Kadhi-Mungu mwisho wa siku?

Wapendwa wana wa Mungu, hapa ndipo tunapoweza kuona udogo wa kitu unavyokuwa na kufikia ukubwa wake ambao unatuwia vigumu kujinasua. Huu ndio mtazamo wa dhambi kadiri ya Injili ya leo. Kumbe kadiri ya Injili ya leo dhambi haihesabiki tu kwa kufanya tendo halisi, bali hata kwa kuwaza na kuvutwa kwa hisia ya kufanya dhambi hiyo. Mizania ya dhambi ipo sawa kwa kufanya au kutokufanya ili hali tu tamaa ile ya kufanya jambo hilo ipo ndani yako. Kilichokosekana hapo ni mazingira halisi ya kulitenda jambo hilo, ila uzito wa dhambi ni ule ule. Tafsiri hii ya dhambi inatupeleka mbali zaidi na kututoa katika mtazamo wa kizamani ya kusema kuna dhambi ndogo na kubwa. Yesu anatupa angalizo katika jambo hili: “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake,” Mt 5:27-28. Je, si yale yamtokayo mtu moyoni mwake ndiyo yamtiayo unajisi? Je, si ndani ya moyo wa mtu ndipo kwenye vyanzo vya yale yote yamjazayo mtu na kumfanya kile alicho? Pasipo utulivu wa ndani viongoza matamanio yako ya nje (jicho, au mkono, Mt 5:29-30) hukosa mwelekeo. Nuru ile ya ndani inapofifishwa yote ya nje huenda mrama.

Wapendwa wana wa Mungu, “Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi,” Mt 15:17-18. Utulivu wa ndani ndiyo taswira halisi ya mtu.

Wapendwa wana wa Mungu, ‘ujumbe mchanganyo’ ni maoteo ya kilicho kiovu. ‘Nataka sitaki’ imewaponza wengi sana katika maamuzi yao na mwisho walijikuta katika janga ambalo hawakutarajia. Mfano: Kesi nyingi za ‘kubakwa’ na hata kufanyiwa vitendo vibaya nje ya ridhaa ya mtu, vimetokea kwa sababu ya ujumbe mchanganyo. Kujiepusha na hali na mazingira hayo maovu, Yesu anatuambia, “maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu,” Mt 5:37. Maneno yako yapaswa kunyooka kama kiapo chako. Kwa upande mwingine kiapo chochote kile kinachochukuliwa au ‘kuliwa’ bila hitaji la ‘kiapo’ kama kiapo, na kuchukuliwa kama maongezi tu ya kawaida, kiapo hicho kama kilivyo ujeuka kuwa kufuru. Amri ya pili ya Mungu inakataza jambo hilo kama isemavyo, “usilitaje bure jina la Mungu wako,” Misale ya Waamini, Toleo la 1993, uk. 1077.

Mkristo wa kweli na mwenye kuishi vyema Ukristo wake, haitaji viapo kumfanya aamini au kuwaaminisha wengine ukweli wa kitu. Na ndiyo maana Yesu anasema, “lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu,” Mt 5:34-35. Mara nyingi anaye apa kwa vitu ni kielelezo cha wazi kwamba kile akisemacho hakina ukweli. Je, tunapokula viapo mbalimbali twafanya makosa? La hasha! Hatufanyi makosa katika maana ya kujengeana uaminifu na utayari wetu wa kutimiza kile tulichokubaliana kwa sifa na utukufu wake Mungu, hasa pale linapojitokeza swala ya huduma kwa watu au umma. Hatufanyi jambo hili kama maongezi yetu ya kawaida, bali kwa wakati na kusudi maalum.

Wapendwa wana wa Mungu, yatupasa pia kutofautisha kitu kimoja hapa na cha muhimu sana. Kiapo akifanyacho mtu kama nilivyokwisha kusema hapo juu, hakibebwi katika ishara zile na alama zile tuzifanyazo kwa sababu hata uwepo wa ishara na alama hizo tuzitumiazo hatujui uhasili wake katika maana ya ‘kwa nini zipo kama zilivyo.’ Tofauti hii Yesu anaisema kwa mfano huu, kwamba, Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi,” Mt 5:36. Kwa maelezo haya twajifunza mambo mawili. Kwanza, ‘kiapo’ siyo kitu cha kawaida katika maana ya kucheza nacho. Pili, kiapo siyo hitimisho la kila kitu kama tunakichukulia ‘kiapo’ katika maongezi ya kawaida. Kwa kufanya hivyo twayapalilia maoteo ya uovu na yule mwovu-shetani.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu,” 1Kor 2:10

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie hekima, unyenyevu, na moyo wa msamaha. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario