JUMATATU
WIKI YA 5 YA MWAKA-I
Somo:
Mwa 1:1-19
Zab:
104:1-2a, 5-6, 10, 12, 24, 35c.
Injili:
Mk 6:53-56
Nukuu:
“Mungu
akaona ya kuwa ni vyema,” Mwa 1:18b.
“wakaenda
mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi,
kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo,” Mk 6:55.
“Na kila alikokwenda,
akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni,
wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona,” Mk
6:56
TAFAKARI:
“Mungu aliyaumba yote akaona ya kuwa ni vyema.
Na Kristo Yesu ndiye Uzima.”
Wapendwa taifa la Mungu
karibuni kwa tafakari fupi ya masomo yetu ya leo kadiri ya mpango wa Mama
Kanisa. Somo la kwanza linatupa kazi nzuri ya uumbaji wa ulimwengu. Uumbaji huu
ni mpango mzima wa maandalizi ya viumbe vya Mungu, binadamu likiwa ndilo
kusudio lake kubwa. “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni
Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba
ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa
45:18. Ndugu yangu ni upendo wa ajabu kwetu sisi binadamu. Embu tazama mito,
bahari, jua, mwanga na misitu. Vyote vya ufunua uzuri wa Mungu na upendo wake
kwetu. Vyote vya sema, "nipo kwa sababu yako wewe mwanadamu.
Vyote vinavyooneka na
visivyoonekana vya udhihirisha uwepo wa Mungu na Utukufu wake. Ila kwa namna ya
pekee uwepo wako na wangu licha ya kuudhihirisha uwepo na Utukufu wa Mungu, kwa
kulitambua jambo hili na KUMRUDISHIA Utukufu huo Mungu, ni furaha kubwa kwa
Mungu na baraka wetu. Hatua ya kwanza, yaani, “kutambua” wajibu huu muhimu
[“KURUDISHA”] ni kufahamu kuwa uwepo wako leo kwa namna yoyote ile si kwa
sababu yako na wasi si kwa nguvu zako na uwezo wako. “Kwa sababu hakuna mtu
miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum
14:7. Hivyo chochote ufanyacho kwa nia njema na katika ukamilifu wake ni
kurudisha sifa na utukufu wa Mungu, na kwa wakati huo huo unaudhihirisha uwepo
wa Mungu na utukufu wake.
Ufahamu huu wa kuona
haya ya kawaida katika maana isiyo ya kawaida katika mtazamo wa Kimungu ndiyo
tofauti kubwa iliyopo kati ya mwenye kujua nyakati za uwepo wa Mungu na Utukufu
wake [kinadharia], na yule mwenye kuamini na
kuishi uwepo huo wa Mungu na Utukufu wake. Ndugu yangu, katika mtazamo na ufahamu
huu wa Kimungu kamwe haijalishi ni aina gani ya kazi halali kwa malipo mahali
unayoifanya. Vile vile haijalishi ni kiwango gani cha elimu ulicho nacho, na
dhamana gani uliyopewa na umma. Ukweli ni kwamba, sababu kubwa ya ukifanyacho
husukumwa na HOFU YA MUNGU. Ni kwa wale tu waliofikia hatua hii ya maisha ya
kiroho na uweza pamoja na Mtume Paulo, “Kwa maana kama tukiishi, twaishi
kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa,
tu mali ya Bwana,” Rum 14:8. Utendaji na mtazamo wa mtu wa ngazi hii kiroho na
kimaisha ni tofauti kabisa. Uwepo wa mtu huyu popote pale alipo hudhihirisha
uwepo wa Mungu na utukufu wake.
Hatua ya pili baada ya
kutambua sababu ya uwepo wako hapa duniani ambayo ni kuudhihirisha huo utukufu
na uwepo wa Mungu, ni kutimiza ahadi
yako kwa wakati na kwa uaminifu mkubwa uliyomwekea Mungu. Kumbuka ahadi hiyo uliyoweka kwa Mungu ilikuwa ni
tokea la kutendewa kwa namna ya pekee na ajabu na Mungu kusikokuwa na mastahili
yako wewe kama wewe. Hapa ni wewe na Mungu wako. “Maana ni nani katika
binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake?
Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” 1Kor 2:11.
Kile ufanyacho kwa uaminifu katika kweli na haki
umwakilisha na kumtambulisha Mungu pale ulipo. Na alipoyafanya yote akaona ya
kuwa ni vyema, Mwa 1:18b.
Hatua
ya kwanza na hii ya pili, yaani katika kutambua na kutimiza ahadi mbele ya
Mungu uwezekana tu pale hayo yanaposukumwa na Imani pasipo shaka. Ndugu yangu,
utaweza kuyafanya yote bila shaka kwa vile unaamini kile ufanyacho na kwa
sababu gani unakifanya. Hili ndilo tunaloliona katika Injili ya leo. “Wakaenda
mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi,
kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo, [Yesu]” Mk 6:55. Kristo Yesu ndiye
kielezo halisi cha Imani, Matumaini, na Mapendo. “Simeoni
akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu [Kristo Yesu] amewekwa
kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,”
Lk 2:34. Moja ya Ishara zilizonenewa, Isa 61:1, na kuwa mpango kazi wa Yesu, Lk
4:17-19, ni hili lilitokea leo, yaani, “Na kila alikokwenda, akiingia
vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi
waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona,” Mk 6:56. Mungu
anajidhihirisha kwa watu wake na waja wake wenye hofu naye, na kwa wakati huo
huo anaufunua Utukufu wake kwa wale wote wanao mwamini.
Somo hili la Injili la zidi
onyesha upendo wa Mungu Baba kwa mwanaye Yesu Kristo kwa njia ya uponyaji. Yesu
anatenda moja kati ya yale matatu: Njia, Ukweli na Uzima. "Yesu
akamwambia, mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa
njia ya mimi," Yoh 14:6. Yesu ni UZIMA. Watu kwa makundi wanafurika kupata
uzima. Ndugu yangu, mbona unasita kupata uzima huu? Kwa nini washindwa hata
kushika pindo la vazi lake? Leo tunashika pindo la vazi la Yesu na kujazwa
uzima tunaposhiriki vyema masakramenti yake. Ukiishi vyema sakramenti yako ya
ndoa, wajazwa uzima na Baraka. Tukiwa na utapia Roho twalishwa na kupata uzima
kwa sakramenti ya Ekaristi Takatifu. "Basi Yesu akawaambia, Amini, amini,
nawaambia, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima
wa milele ndani yake," Yoh 6:53. Tukiwa wagonjwa kwa uzito wa dhambi zetu,
twaponyeshwa kwa sakramenti ya kitubio/upatanisho. "Wo wote
mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa." Yoh 20:23. Ndugu yangu, mbona sakramenti hizo kwako ni kama
kituo cha polisi? Kwa nini wasubiri mpaka sasa? Vunja hivyo vizuizi upate Uzima
wa Milele.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mtu
ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza
juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake,” Zab 8:4-6
Tusali:-Ee Yesu,
nipe fursa ya kulishika pindo la vazi lako kila mara. Niondolee aibu ya
kutoshiriki Sakramenti zako Takatifu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario