sábado, 18 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 7 YA MWAKA-I


JUMATATU WIKI YA 7 YA MWAKA-I

Somo: YbS 1:1-10

Zab: 93:1ab, 1c-2, 5

Injili: Mk 9:13-28

Nukuu:

“Hekima yote yatoka kwa Bwana, nayo yakaa kwake hata milele,” YbS 1:1

“Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote, na ufahamu wa busara tangu milele,” YbS 1:4

 “Yupo Mmoja aliye na hekima, naye yu wa kuogopwa sana,  ameketi katika kiti cha enzi,” YbS 1:8

 “Ina wote wenye mwili kama aitoavyo, na wale wampendao amewapa kwa wingi,” YbS 1:10

Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye,” Mk 9:23

Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu,” Mk 9:24

TAFAKARI: “Hekima yote yatoka kwa Bwana, nayo yakaa kwake hata milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, si jambo la ajabu leo kusikia kila kona kelele za watu wenye hofu ya Mungu kukemea uvunjwaji wa haki za binadamu ulio waziwazi, na wa mchana kweupe. Uvunjwaji wa haki huu unanzia pale ulipo, familia unayoishi, tamaduni ikiwa ni pamoja na mila, desturi, na mazingira unayoyaishi, mfumo wa siasa unaouishi au kurisishwa, uchumi unaotawala maisha yako kila siku, na Imani unayoishi kutokana na yale unayoyaamini. Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, ni vema ukajua kwamba huwezi kuongelea haki bila wajibu.

Haki ni tunda la wajibu wako. Hivyo kama umewajibika vyema unayohaki na mastahili ya kile ulichokiwajibikia. Ni kwa namna na mtazamo huu tunaongelea uvunjifu wa haki pale mmoja wetu licha ya kuwajibika kama impasavyo haki yake inaporwa waziwazi mchana kweupe. Uporaji wa haki hizi mara nyingi hufanywa na wale wenye “NGUVU” katika sehemu husika. Jambo la ajabu ni hili; katika jamii yoyote ile wenye “nguvu” hupewa dhamana hiyo na kundi hili linalohujumiwa na wenye “nguvu” hawa. Kinachosikitisha ni kwamba, badala ya waliodhaminishwa kuwa watetesi, wao wanakuwa wahujumu. Hawa ni wale wasiokuwa na hofu ya Mungu ndani yao, na kipauwa mbele chao ni ubinafsi wao. Katika hali hii, amani kamwe haiwezi ikatawala. Jamii ya mtindo huu huwa na utulivu wa kukubaliana kwa kutokubaliana. Ni hali lenye kujionyesha kwa matumizi makubwa ya mabavu na nguvu.

Ila jambo la kukumbuka ni kwamba palipo na mgandamizo mkubwa wa nguvu pasipo nafasi ya kutokea, tokeo lake ni mpasuko usiokifani. Hivyo tunahitaji amani katika maana ya kutambua utu wa watu na tofauti zao katika kutenda na kufikiri. Tunahitaji amani kwa kuheshimu matakwa ya wengi na yenye mwelekeo chanya wa namna watakavyo kutawaliwa, kuwajibika, na kuuwajibisha utawala ule uliopewa dhamana na umma wao. Ni katika amani hii tunaweza kuona matunda yake, yaani, haki ikitendeka pasipo ghiliba. Hivyo, “tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani,” Yak 3:18. Na wale waitafutao na kuifanya amani ni wale wasiyotanguliza mbele ubinafsi wao, wala falsafa za makundi yao (vyama vya siasi), bali umoja wa wote katika utofauti wao, wakijali uhalisi na Utaifa wao.

Wapendwa katika Kristo, tunapopindisha kweli hii katika jamii, tuwe tayari kwa machafuko ya kila aina. Na mwenye kujisifia katika mambo haya ni mpanda matatizo katika jamii husika na matunda yake ni machafuko yasiyokwisha. Kweli ya kitu chochote kile haiwezwi pindishwa kwa maslahi binafsi au ya kikundi cha walio wachache. Na kama ikiwezekana mafanikio yake ni ya muda mfupi tu. Na hivi ndivyo Yesu asemavyo kuhusu kweli; “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:32. Tunapoipindisha kweli ili tupate kuungwa mkono na wasio na ufahamu juu ya kweli, tutayapata ya dunia hii kwa muda mfupi na kujeuka kuwa mashetani, yaani, wapinga kweli.  “Hekima yote yatoka kwa Bwana, nayo yakaa kwake hata milele,” YbS 1:1

Hekima ishukayo kutoka mbinguni ni kweli ile ya Neno aliyemwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na huyu ndiye Kristo. “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli,” Yoh 8:36. Mgandamizo wowote  ule wa haki za watu hauwezi kamwe kuzika kweli ya kile kilicho haki yao. Hivyo katika hali yoyote ile katika mwono huu, amani haitakuwepo.

Yesu Kristo ndiyo kielelezo cha haki kama tunda la amani. Kristo Yesu hakuja kuyatafuta yalio yake binafsi, bali kutuweka huru katika utumwa wa dhambi. Hii ndiyo hekima itokayo juu. “Nani awezaye kuhesabu mchanga wa bahari na mtone ya mvua na siku za milele?” YbS 1:2. Kumbe safari kuelekea hekima ni kujua uwezo na mapungufu yako. Huu ndio wito wa kila mmoja wetu mwenye hofu ya Mungu ambao mwisho wake ni kuwa wakamilifu kama Baba wa Mbinguni alivyo mkamilifu. Ndugu yangu, “yupo Mmoja aliye na hekima, naye yu wa kuogopwa sana, ameketi katika kiti cha enzi,” YbS 1:8. Yesu anatukumbusha mwito huu na kusema, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.

Ndugu yangu, pale ulipo simama katika kweli, na kuwa mtetezi wa haki za watu wote, na kwa namna ya pekee wanyonge kwa maana, “heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu,” Zab 41:1. Yote haya yanawezekana tu kama tunamwamini Yesu Kristo, na kile alichokijia katika ulimwengu huu. Hii ndiyo hekima ya Mungu ambayo “Bwana ndiye aliyeiumba na kuiona na kuihesabu, na kuimwaga juu ya kazi zake zote,” YbS 1:9. Katika kweli hii, Yesu anawakemea wale wasiokuwa na imani naye hasa katika Injili ya leo tunapoona wanafunzi wake wanashindwa kumtoa pepo kijana yule aliyefikwa na mkasa ule. “Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu,” Mk 9:19. Kumbe palipo na mashaka na pasipo njia, tuyapeleke mahangaiko yote hayo kwa Kristo kwa Imani thabiti na ya kweli.

Katika tendo hili la Imani Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, “Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye,” Mk 9:23. Je, ukiweza nini? Ukiweza katika maana ilivyotumika hapa, inatukumbusha kuwa na ufahamu pasipo shaka juu ya Yeye, yaani, Kristo ni nani kwetu. Naye anasema,Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ndugu yangu, bila Kristo hatuwezi kufanya lolote lile, liwe dogo au kubwa, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5b. Je, wewe na mimi tuna jeuri katika kweli hii? Kwa nini basi kujifanya miungu watu? Elewa jambo hili hili juu ya hekima: “Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote, na ufahamu wa busara tangu milele,” YbS 1:4. Ni vyema wewe na mimi kuiomba hekima hii ili ituongoze kule aliko Mungu, yaani, kwenye uzima na umilele.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa kutambua ukweli huu, “mara babaye yule kijana (aliyekuwa na pepo) akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu,” Mk 9:24. Kumbe tunapopotoka kutokana na hekima hizi za dunia, ubinadamu, na ushetani, si vibaya tukajirudi na kutambua ubinadamu wetu unaohitaji neema na huruma ya Mungu. Ni katika mantiki hii kwamba hekima “ina wote wenye mwili kama aitoavyo, na wale wampendao amewapa kwa wingi,” YbS 1:10. Kristo yupo tayari muda wote kukushika mkono unapotambua mapungufu yako yalioyopelekea anguko lako na hasa ulipoikuza nafsi yako na kutokumpa Mungu nafasi.

Ni kwa neema na huruma hii ya Mungu, Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama,” Mk 9:27. Tendo hili linakuwa fundisho kubwa kwa wanafunzi wake Yesu. “Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa?” Mk 9:28. Kushindwa kwa wanafunzi wa Yesu ni moja ya kuwa na Imani haba ingawa Yesu anawaambia, namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba,” Mk 9:29. Kwa namna nyingine ni kuwa na Imani thabiti yote yawezekana.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yupo Mmoja aliye na hekima, naye yu wa kuogopwa sana,  ameketi katika kiti cha enzi,” YbS 1:8

Tusali:-Ee Yesu na Jemedari wangu, nijalie hekima ya kuona uhalisi wa jambo kama ulivyo, na siyo kuuona uhalisi huo kama nilivyo. Amina

 

 

 

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario