lunes, 6 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 5 YA MWAKA-I


JUMATANO WIKI YA 5 YA MWAKA-I

Somo: Mwa 2:4b-9, 15-17

Zab: 104:1-2a, 27-28, 29bc-30

Injili: Mk 7:14-23

Nukuu:

"Bwana akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa wema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika," Mwa 2:16-17

 “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu,” Mk 7:15

“kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote,” Mk 7:19

“Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi,” Mk 7:20

“Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu,” Mk 7:21

“Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi,” Mk 7:23

TAFAKARI: “Yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.”

Mungu ni Upendo na kwake yote huyafanya kwa sababu ya upendo. Wazazi wetu wa mwanzo wanapewa upendeleo ukiambana na utaratibu wa kuishi kwenye hii bustani. Bustani ina mambo makuu matatu; a) Aina zote za miti ya matunda, b) Matunda ya mti wa uzima, na c) Matunda ya mti wa  ujuzi wa wema na mabaya.

Pamoja na kupewa ruksa ya kula matunda yote, waliwe pia angalizo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa wema na mabaya, Mwa 2:17. Tendo la kwenda kinyume na agizo hili ni KIFO. Cha kujifunza leo ni kwamba tangu mwanza kifo hakikuwa katika mpango wa Mungu. Mungu anatutakia uzima wa milele.

Madhara ya kutokufuata maangalizo na utaratibu fulani iwe ni kazi au aina yeyote ya stadi za maisha yapo mengi. Tazama milipuko ya magonjwa mengi sugu na yasiyoponyeka! Yote yametokana na kutumia utashi wetu vibaya. Mara nyingi binadamu twapenda kujua kwa bidii sana kile kilicho jificha nyuma ya "pazia." Je, haitoshi kuyajua haya yaliyomahitaji yetu na yale tu yenye uzima ndani yake? Ni vizuri tukatumia udadisi wetu kumjua Mungu, kuboresha maisha yetu kuelekea utakatifu, na kuifanya dunia hii kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi licha ya kwamba ni sehemu ya kujiandaa kwa maisha ya umilele.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, ni vyema tukazama ndani kidogo kwenye fumbo hili la mtu kama alivyo, ili tuweze kujua ujumbe wa Injili ya leo. Mtu kamili anakuwa katika sehemu kuu tatu:-Nafsi, Roho, na Mwili. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi Nafsi zenu na Roho zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23

Katika hili Roho na Nafsi huwa pamoja na ndizo wewe mwenyewe. Mwili ni nyumba ya roho na nafsi. Katika uumbaji Mungu aliumba mwili kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani ambayo ni roho yake ndipo mtu huyo akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7. Miili tuliyonayo ni nyumba ya Nafsi na Roho. Kwa hali hii sisi binadamu ni wawili. Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi na Roho, na mtu wa nje ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi kuwatenganisha wala kumwona kwa macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo.

Kwa mantiki hii ya fumbo hili la uumbaji wetu na utu wetu, ni muhimu sana mtu atawale hisia zake. Nafsi ikiegemea rohoni huleta matunda mzuri. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Gal. 5:22-23. Kwa maana nyingine, “hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, Mk 7:15a.

Ila nafsi inapoingia katika Mwili mambo huwa mabaya kwani ufanya matendo ya mwili kama tusomavyo katika maandiko matakatifu, “basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal.5:19-21. Kwa maneno mengine ni kwamba, “ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu,” Mk 7:21. Na haya kadiri ya Injili yetu ya leo ndiyo yamtiayo mtu najisi. “Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi,” Mk 7:20.

Ni vizuri kujua nafsi yako imeegemea wapi. Ikiegemea rohoni utaenda Mbinguni. Ikiegemea mwilini utaenda motoni. Na “haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi,” Mk 7:23. Hali na mazingira haya ndiyo mauti yetu ya pili tuilazimishayo kwa uhuru na utashi wetu, licha ya sadaka kubwa aliyoitoa Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani kwa ajili ya dhambi zako na zangu.

Tumasifu Yesu Kristo!

“Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu,” Mk 7:15

Tusali:-Ee Yesu na Mwalimu wangu, nifundishe, niamshe kila mara, na niimarishe ili nafsi yangu iegemee roho. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario