JUMAMOSI WIKI YA 5 YA MWAKA-I
Somo:
Mwa 3:9-24
Zab:
90:2, 3-4, 5-6, 12-13
Injili:
Mk 8:1-10
Nukuu:
“Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami
ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12
“Bwana
Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko
wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na
mavumbi utakula siku zote za maisha yako,” Mwa 3:14
“Kwa
maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini
utarudi," 3:19b
“Nawahurumia mkutano
kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula," Mk
8:2
TAFAKARI:
“Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.”
Wapendwa tutafakari pamoja masomo ya leo
kadiri ya mpango wa mama Kanisa. Masomo haya yanatupa fundisho la "Adhabu
kwa kosa la mwanadamu, na Huruma ya Mungu." Tafsiri ya tendo hili ni
kwamba, “Neema na Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.”
Adhabu anayotoa Mungu kwa kuwafukuza
wazazi wetu wa kwanza kama tuliovyoona katika tafakari yetu ya jana, ni kosa la
kutokukubali ubinadamu wao na kutaka kufanana na Mungu. Ni dhambi ya majivuno!
Ni dhambi ya kutojipokea na kukubali mipaka yako. Ni dhambi ya kuvaa taswira
isiyo yako. Hii ndiyo dhambi ile ya tamaa,
ambayo hutujengea hali ya kutojipokea na kutoridhika kwa kile tulicho. Shetani
kwa umbo la nyoka anatumia mwanya huu kumshawishi Eva. Dhambi hii
inashirikishwa kwa wote wawili, yaani, Hawa an Adamu. Matokeo yake ni anguko
kubwa la wazazi wetu wa kwanza. Mungu anapotaka kujua kilichojiri kila mmoja
anamtupia lawama mwenzake. Mwanamke anamlaumu nyoka, na Adamu anamlaumu mkewe.
“Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda
ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12.
Tukio hili linamfanya
Mungu kutoa adhabu kwa yule mwovu-nyoka na kuvunja agano kati yake na Adamu na
Hawa. “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa
wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo
utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako,” Mwa 3:14. Kuanzia
sasa na milele tungali duniani yote hayatapatikana kwa urahisi. Hata baada ya
kukosa, wazazi wetu wa kwanza hawapo tayari kukiri kosa zaidi ya kujitetea na
kusukuma lawama kwa kitu kingine, (Mwa 3:12-13). Na mwisho wa siku tutarudi
kule tulipopakata, yaani mavumbini (Mwa 3:19b). Tangu
hapa Hawa anakuwa Mama wa wote walio hai. “Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa;
kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai,” Mwa 3:20. Na tangu nyakati
hizo la anguko hili la wazee wetu wa kwanza, kifo hakikuepukika tena hadi leo.
Yaliyo tokea kwa wazazi wetu na leo
yanatokea kila siku kwenye jamii yetu. Ni wangapi kati yetu tusiotaka kujipokea
na kuwa na mioyo migumu kukiri kosa? Neno "samahani," kwa wengi wetu
laonekana ni neno gumu kupita yote. Mtu yupo tayari kutoa machozi kuliko kusema
"samahani." Hiki ni kiburi kilichopindukia.
Wengi wetu pia neno samahani limepoteza
maana yake. Neno samahani lamaanisha kwa wengi, "funika kombe mwana haramu
apite." Neno hili kwa wengi lamaanisha pia, "kukubaliana kwa
kutokubaliana." Inakuaje asubuhi tu naomba msamaha na jioni narudia kosa
lile lile kwa kujua na dhamira safi kwa mtu yule yule? Tufanye tafiti moyo na
nafsi. Hili si jambo la kawaida!
Kwa vile dhamiri ya Mungu ni kumkomboa
mwanadamu, Mungu hajabadili mpango kazi wake. Yesu Kristo anatupa HURUMA na
UPENDO huo wa Mungu, na kuthibitisha kuwa huruma na upendo wa Mungu ni mkubwa
kuliko dhambi zetu.
Baada ya umati ule kukaa na Yesu nyikani
kwa siku tatu ukimsikiliza, HURUMA ya Mungu inatawala. Wote kwa namna ya ajabu
wanashibishwa. Jambo hili latufundisha nini?
Kwanza kabisa, Mungu hutupokea kama
tulivyo ilimradi tu tuwe tayari kumsikiliza. Mungu anasema, "huyu ni mwanangu,
mpendwa wangu, msikieni yeye," Mk 9:7
Pili, tunapokuwa tayari kurudi kwake kwa
toba na majuto, Mungu huanza upya yote ndani yetu bila kujali historia yetu
mbaya. Mwana mpotevu anakiri kosa lake na kusema, "Baba, nimekosa juu ya
mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena," Lk 15:21. Haya ni
majuto ya ndani kabisa. Tunaona karamu kubwa aliyoifanya Baba yake kwa kumpata
tena mwanaye. Baba huyu ambaye ni Mungu wetu, hakuhitaji kujua historia mbaya
ya mwanaye na kuanza kumkaripia. Anachotoa ni maagizo tu, "leteni upesi
vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni
ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu
alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza
kushangilia," Lk 15:22-24. Ni upendo na huruma gani hii ya ajabu!
Bila shaka nyie mlio wazazi na familia
zenu, matukio kama haya hutokea. Swali langu ni hili; umeweza kukaa katika
nafasi ya Baba huyu pale;
-Binti yako uliyempenda na kumsomesha
badala ya kukuletea daraja kwa kwanza form IV au VI, akarudi na mimba tena
mwathirika?
-Mtoto wako wa kiume uliyempa kila
atakacho akafikia kipindi hataki kusoma, kauza thamani zako ndani, na anarudi
kuomba msamaha akiwa tayari "Teja" la madawa ya kulevya?
Jambo la tatu kupata huruma na upendo wa
Mungu ni kujiachia kwake. Mapenzi yake ya timie. Mfano mzuri ni Mama Bikira
María na Mtume Petro. Mama Bikira Maria anasema, "mimi ni mjakazi wa
Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema," Lk 1:38. Baada ya Yesu kutoa
fundisho zito kuhusu mwili na damu yake, wengi walifikia kutomfuata. Yesu
aliwauliza kama Mitume kama nao wanataka kuondoka. Mtume Petro anajibu na
kusema, "Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu," Yoh
6:68-69. Huu ni Unyenyekevu wa hali ya juu kufanywa na binadamu wa kawaida!
Ndugu yangu, HURUMA na UPENDO wa Mungu
kwetu ni waajabu. Maajabu haya hutokea tu pale tunapo kuwa tayari; Kumsikiliza
yeye, kufanya toba ya kweli, na kujiachia kwake bila shuruti au shinikizo.
Fanya sasa uone maajabu na kubarikiwa na Bwana.
Tumsifu Yesu Kristu!
“Bwana Mungu akamtoa katika bustani
ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.” Mwa 3:23
Tusali:-Ee
Mungu, Upendo wako ni waajabu sana. Nijalie kupenda bila kipimo. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario