sábado, 11 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 6 YA MWAKA-I


JUMATATU WIKI YA 6 YA MWAKA-I

Somo: Mwa 4:1-15, 25

Zab: 50:1, 8, 16bc-17, 20-21

Injili: Mk 8:11-13

Nukuu:

"Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde." Mwa 4:7

 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani] Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua,” Mwa 4:8

“Wakatokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana naye; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu." Mk 8:11

“Akawaacha, akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng'ambo,” Mk 8:13

TAFAKARI: “Ubaya wa kutokuona mema kwa wenzetu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, masomo yetu ya leo yanatualika kutafakari juu ya ubaya wa kutokuona mazuri kwa wenzetu. Kwa maneno mengine twaalikwa kushinda hisia na wivu hasi kwa yale mazuri kutoka kwa wenzetu.

Katika somo la kwanza bila shaka wote tunajua simulizi la Habili/Abeli na Kaini. Hawa ni ndugu wa damu kabisa. Habili alijulikana kwa shughuli za ufugaji kondoo, na nduguye kama mkulima.

Wivu wa Kaini unatokana na kutokupata kibali mbele ya uso wa Mungu kwa shukrani ya mazao yake kama sadaka. Ilimpasa kujifunza kutoka kwa nduguye namna ya kufanya ili naye sadaka yake ipate kibali (Mwa 4:7). Badala yake anaamua kuitoa roho nduguye ili asipate upinzani.

Dhambi hii wengi miongoni mwetu twaifanya sana; kwa kujua au kutokujua. Haijalishi umetoa roho ya mtu au la! Ukiwa na wivu wowote ule usio wa kujenga, huna tofauti na kosa la Kaini.

Kwa nini Ndugu yangu wajisikia vibaya mwenzako akifanya vizuri? Kwa nini unakosa raha mwenzako akiendelea? Hali hii haijalishi mahali ulipo, wito ulio nao, au ofisi uliyo kabidhiwa na umma au jumuiya yoyote ile. Kwa nini unashindwa kumshukuru Mungu kupitia mazuri ya ndugu yako kifamilia, mtawa mwenzako, mfanyakazi mwenzako, mfanyabiashara mwenzako?

Tatizo kubwa tulilo nalo wengi ni kutaka kufanana na mwingine tukisahau kwamba kila mmoja wetu kaumbwa pekee na tofauti ikiwa ndiyo taswira halisi ya uzuri na utukufu wa Mungu. Kwa nini unapoteza asili yako na kutaka kuwa kivuli cha mwenzako? Ndugu yangu, hayo siyo malengo ya Mungu ya uumbaji wako.

Unachotakiwa kufanya ndugu yangu ni kugundua vipaji na uwezo wako. Utaweza tu kufikia hatua hii ikiwa; kwanza, kwa kujipokea ulivyo. Pili, kwa kutambua mapungufu yako. Tatu, weka bidii kwa kile Mungu alichokupa cha pekee (vipaji vyako). Kupoteza muda kwa kubeza kazi na mazuri ya wengine hakuta kusaidia kamwe. Utaishia tu katika mfadhaiko wa moyo na kuwa na shinikizo la damu la kupanda na kushuka kila mara, na pasipo tiba. Kushinda na kupoteza muda na fedha kwa waganga hakutakusaidia. Eti unaenda kusafisha nyota!  Hakika wajinga ndiyo waliwao!

Katika injili, Yesu anakutana na kundi hilohilo lenye wivu. Mafarisayo hawaoni wala kuamini yote ayatendayo Yesu. Bado wanadai ishara zaidi.

Ndugu yangu, ukiukubali wivu hasi/usio wa kujenga, hakika hautakuwa tofauti na kipofu, tena kipofu wa macho na roho. Jipokee ndugu yangu na fanya mabadiliko ya kweli utaona yaliyojificha ndani yako. Wengi tunaishi na hata kufikia kufa bila kutumia vipaji alivyotupa Mungu. Sababu kubwa tunatumia muda mwingi kujishughulisha na mambo yasiyo yetu na wafanyayo wenzetu. Na tunayafanya hayo aidha kwa kuyaharibu au kuyabeza. Wivu ni hatari sana. Wivu ufifisha akili na roho zetu.

Bwama wetu Yesu Kristo hapendi kupoteza muda na yule anayebeza kazi zake. Kwa busara, "akawaacha, akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng'ambo," Mk 8:13. Yesu anatufundisha kutokupoteza muda kushindana na mwenye wivu. Mwache tu kwani mwisho wa wivu na ubaya ni AIBU! Ufufuko wa Yesu ulikuwa zaidi ya ishara waliyotaka na imekuwa AIBU yao milele. Je, na wewe unataka kuingia mkumbo huo?

Ndugu yangu, jiulize kwa nini unakosa raha kwa mazuri ya mwenzako? Elewa dhambi hii ya wivu ikikua uzaa mauti!(Mwa 4:8)

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga,” Ayu 5:2

Tusali:-Ee Yesu, nipe nguvu na neema ya kutenda mema nyakati zote za uhai wangu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario