IJUMAA WIKI YA 7 YA
MWAKA-I
Somo:
YbS:6:5-17
Zab:
119:12, 16, 18, 27, 34, 35
Injili: Mk 10:1-12
Nukuu:
“Ukitaka kujipatia
urafiki, umpate kwa kumjaribu, wala usiwe na haraka katika kumwamini; yaani,
kuna rafiki wakati wa kufaa, ambaye yeye hatadumu wakti wa msiba wako,” YbS
6:7-8
“Mcha Mungu hunyosha urafiki wake, kwa maana
alivyo yeye mwenyewe ndivyo alivyo na jirani yake,” YbS 6:17.
“Lakini tangu mwanzo wa
kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke,” Mk 10:6
“Kwa sababu hiyo mtu
atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata
wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja,” Mk 10:7-8
“Basi alichokiunganisha
Mungu, mwanadamu asikitenganishe,” Mk 10:9
“Akawaambia, Kila
mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu
mwingine, azini,” Mk 10:11-12
TAFAKARI:
“Tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.”
Wapendwa wana wa Mungu,
hakuna hata mmoja kati yetu ambaye yupo katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya.
Ni kwa maana hiyo hiyo kwamba hakuna kati yetu aliyejipangia kuwa kama alivyo;
kijinsia, kuchagua azaliwe na wazazi wa aina gani, kabila gani, au taifa gani.
Tupo kama tulivyo kwa makusudi yake Mungu kwa sababu anampango mzuri na kila
mmoja wetu. Je, una sababu yoyote ya kumlaumu Mungu au kumkosoa Mungu kwa kile
ulicho? Angalizo: “Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni,
mwamuzi amesimama mbele ya milango,” Yak 5:9. Leo kutokana na matumizi mabaya
ya neno ‘uhuru,’ tumefikia hatua ya kukosoa
kila kitu ambacho kimsingi ni kwenda kinyume kabisa na kusudi la uumbaji wetu.
Kwa mfano swala la jinsia Maandiko
Matakatifu yanatufundisha kwamba, “tangu mwanzo wa kuumbwa
ulimwengu, aliwafanya mume na mke,” Mk 10:6.
Leo walio wanaume wanataka kuwa wanawake na walio wanawake wanataka kuwa
wanaume kwa kisingizio cha kutumia uhuru wao. Baadhi ya nchi za ulaya wazazi
hawana tena mamlaka ya kuamua juu ya watoto wao. Mtoto akifikia umri ufaao
kisheria ujiamulia jinsia aipendayo. Je, tunaenda kinyume na mpango wa Mungu?
Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Mungu
akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba,” Mwa 1:27. Hii ghiliba na kasumba ya kujibadili na kuwa kitu kingine
inatoka wapi? Kwa nini tunashindwa kujipokea?
Kumkosoa
Mungu katika suala la uumbaji wake ni sawa na kuhasi na kuikataa ile ‘ndiyo’
iliyomo ndani mwetu. Ukosoaji huu utupelekea kuishi maisha yasiyo na malengo na
mwisho wa siku tunageuka kuwa vituko.
Je, unayekwenda kinyume na matakwa ya Mungu ndiyo
yako ipo wapi?
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa upendo wake juu yetu, Mungu hakuishia tu kumuumba Adamu, bali aliona inafaa
Adamu akawa na mwenza wake na kuifanya familia kama shina na msingi wa maisha
kumwelekea Yeye mwenyewe kama ulivyo ule Utatu Mtakatifu wa umoja
usiogawanyika, yaani, Mungu Mmoja na nafsi tatu; Baba, Mwana, na Roho
Mtakatifu. Tukirudi kwenye kusudi na hitaji la uwepo wa familia, ni kwa “sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye,
ataambatana na mkewe; na hao wawili
watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja,” Mk
10:7-8. Familia itatoka wapi kama tutafuata matamanio yetu na tamaa zetu kwa
kisingizio cha uhuru usio na mipaka?
Ndugu zangu,
“alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe,” Mk 10:9. Leo mwanadamu
amejitwalia mamlaka yasiyo yake na kujaribu kuuvaa umungu ambao pamoja na
umungu huo wa kijivika, kifo hakijaacha kumwaibisha mwanadamu huyo. Hata hivyo
kwa kiburi chake mwanadamu huyu hapendi kujirudi na kuwa kile kilicho kusudi la
Mungu juu yake. Kusudi la Mungu la kumfanya mtu mme na mtu mke kuwa kitu kimoja
ni kuufunua upendo wake kwetu, mshikamano wake, na ukaribu wake kwetu usiokoma.
Ni jukumu na wajibu
wetu kuudhihirisha upendo huo wa kweli kati yetu. Hilo “pendo na lisiwe na
unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa
ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu,” Rum 12:9-10. Tunapokosa upendo huu
na umoja huu na hasa katika funganishi la Sakramenti ya Ndoa na
kujishikamanisha na mwingine nje ya ndoa husika, muonekano huo hauna jina
lingine zaidi ya ‘uzinifu.’ Hivyo, “kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine
azini juu yake; na mke, akimwacha
mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini,” Mk 10:11-12.
Ndugu yangu, ukubali
mpango wa Mungu ndani yako. Mungu anasababu kubwa ya kukuumba kama ulivyo. Hata hivyo, pamoja na Sakaramenti hii ya ndoa
kushambuliwa na maadui wengi, somo latu la kwanza kutoka kile kitabu cha Yoshua
Bin Sira, anatutaka kutafakari kwa kina juu ya rafiki na urafiki wa kweli, na
Injili kwa kiasi kikubwa adui wa ndoa ni wanandoa wenyewe. Ndoa nyingi leo
zimekosa mwelekeo kwa sababu tu ya kuendekeza na kula amini ya usafiki usio na
tija wala siha, na kukosa msimamo kati ya wanandoa wenyewe
1.
MARAFIKI NA URAFIKI:
Marafiki hawapo nyuma
kuharibu ndoa, hasa pale wanandoa wanaposahau fumbo la kuwa mwili mmoja.
“Ukitaka kujipatia urafiki, umpate kwa kumjaribu, wala usiwe na haraka katika
kumwamini; yaani, kuna rafiki wakati wa kufaa, ambaye yeye hatadumu wakti wa
msiba wako,” YbS 6:7-8. Ndugu yangu, ukishafunga ndoa hakuna rafiki yeyote
aliye muhimu na mkuu zaidi ya mwenzi wako. Ule mtindo wa kukaa na marafiki hadi
manane ya usiku haupo tena. Huku ni kuugawa mwili wako mchana peupe pee!
Wakati mwingine mambo
makubwa na ya siri kifamili tunawaamini marafiki tuliokutana nao kwenye bar na
vilabu vya pombe na muziki, kuliko mwenzi wako wa Ndoa. Ndugu yangu uliye
kwenye Sakramenti hii Takatifu ya Ndoa elewa ukweli huu: “Maneno matamu
yatamzidishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea wamsalimuo,” YbS
6:5. Kuwa makini sana na marafiki wale wakuzungukao kama paka, na
wakubembelezao kama mmbu kipindi cha masika.
Mfano; mikataba
mbalimbali ya biashara, miradi mbalimbali tunahifadhi kwa marafiki. Kisingizio,
‘eti mwanamke hapaswi kujua kila kitu.’ Wakati fulani mama mmoja alimwuliza
mume wake, tena kwa upole, "Baba Eddy, mbona lile duka la umoja famili
wanasema ni lako wakati mimi sijui licha ya kuonyeshwa vielelezo vyote?"
"Hivi kwa nini unapenda kunifuatilia na kufuatilia mambo yangu? Huna kitu
cha kufanya? Au umekosa nini huku ndani! Kula, kuvaa, na gari nimekupa. Bado
havikutoshi? Au unataka hii roho yangu? Chukua!" Mumewe alifoka na
kumtolea mimacho kama kenge wa jangwa la rahara. We baba wewe, ukifa ghafla
hiyo mali itakuwa ya nani? Ona ulivyo na familia kubwa na tegemezi bado.
Mara nyingi mali za
familia hizi upotea kwa uficho huo huo. Kutokuambiana ukweli ni saratani mbaya
sana katika Ndoa nyingi leo. Elewa, mkeo sio thamani za ndani kama sofa na
vinginevyo. Huyo ni nyama na mfupa wako. Ndugu yangu, “Hakuna badala ya rafiki
amini, wala uzuri wake hauna bei. Rafiki amini ni kifungu uzima; naye amchaye
Mungu atampata,” YbS 6:15-16. Je, Mke wako siyo zaidi ya rafiki? Tafakari na
chukua hatua.
Akina mama nao
huwaamini mashoga zao kuliko hata ndugu wa familia ya mumewe. Angalizo kwenu
akina Mama kwenye ndoa zenu: “Mcha Mungu hunyosha urafiki wake, kwa maana
alivyo yeye mwenyewe ndivyo alivyo na jirani yake,” YbS 6:17. Kwenye kundi hili
la akina Mama wenye mtindo huu wa maisha, wapo wenye miradi ya siri ambayo
mwisho wake ni kifo tu. Mnashangaa nyumba inapigwa mnada wakati mmoja wa
mwanandoa hajui. Inasikitisha sana. Hii ni saratani. Marafiki wamekuwa karibu
na tumewakaribisha hadi chumbani. Maandiko Matakatifu leo yanatuambia hivi juu
ya marafiki hawa hatarishi: “Pia kuna rafiki tena, ambaye anakula mezani pako,
bali siku ya mabaya haonekani; wakati wa kufanikiwa kwako atakuwa sawa nawe, na
kupiga domo juu ya watumishi wako; lakini ukipatwa na masaibu atakugeua, na
kujificha mbali nawe na uso wako,” YbS 6:10-12. Ni vyema kujua mipaka ya
urafiki na uhusiano wako juu ya agano lako la hiyo ndoa takatifu.
Hatuwezi kukaishi kama
kisiwa, yaani, kuwaogopa jirani zetu na kutokuwa na uhusiano nao. Jambo la
msingi ni kuwa na mahusiano yenye afya na yale yenye mwelekeo wa kutaabikiana
katika hali zote za maisha. Hivyo, kipimo ni hiki: “Basi ujitenge na adui zako;
tena ujihadhari na rafiki zako. Walakini rafiki aliye amini ndiye ngome; naye
aliyempata amepata tunu,” YbS 6:13-14. Urafiki wa kuzungukana, na ule usio wa
wivu wa maendeleo ni saratani hatarishi katika afya ya maisha yetu kama
wanandoa, na hata maisha yoyote yale.
2.
WANANDOA WENYEWE:
Ndoa inakuwa na uhai
haya yakizingatiwa kadiri ya mtazamo wa Mtume Petro. "Neno la mwisho ni
hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikivu,
wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye
kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka," 1Pt 3:8-9.
Ndugu yangu, maneno
hayo ni mazito sana kwa wanandoa. Kwa upande wa kina mama, wapo wanaoishi
kwenye ndoa bado hawana utambuzi au tofauti na usichana wao. Mama kwenye ndoa
tambua kwamba kila siku yakupasa "kupungua" kwa ajili ya familia yako
"iongezeke." Familia, yaani, Baba na watoto wenu waongezeke; upendo,
furaha, afya, akili na mambo mengine mengi tu. Je, utapunguaje? Mtume Petro
anatuambia, "kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka
nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni
usioonekana, katika mapambo yasiyo haribika; yaani, roho ya upole na utulivu,
iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu," 1Pt 3:3-4. Mtume Petro hapa hapingi
mama usiende “salón” au kutokuvaa vizuri; bali uelewe kwamba hayo siyo vipauwa
mbele katika familia.
Wengi leo katika ndoa
wanatumia muda mwigi nje badala ya ndani. Vikao kila siku visivyoisha. Sema za
kiroho januari hadi disemba, mikutano ya injili hadi manane ya usiku, nk. Je,
saa ngapi utaijenga nyumba na ndoa yako? Huku ni kukosa busara kama
tunavyoaswa, "Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, kadhalika
mwanamke mzuri asiye na akili," Mit 11:22. Kwa maana hiyo, "kila
mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa
mikono yake mwenyewe," Mit 14:1. Wakati mwingine unamtafuta mchawi ilhali
mchawi mwenyewe ndiwe wewe.
Wanawake wengi ni wawivu kupindukia. Jua
likichomoza tu utakuta mkeka upo nje. Nikujigalagaza kwenye mkeka kama dagaa wa
kigoma na samaki wale “kayabo” wa kanda ya ziwa. Masikini wa Mungu labda mumewe
alivutiwa na umbo lake la kushikika, baada ya nusu mwaka afadhali ya mkuyu wa
handeni. Licha ndoa ni zaidi ya haya ya nje, ila nayo huleta matamanio ya
kutazama kwingine kama tulipo kuna pazia na kiza. Elewa mumeo kama ameajiriwa
au kujiajiri mwenyewe, awapo huko naye ameolewa na hiyo kazi yake. Awapo
nyumbani anaitaji amani na utulivu.
Wanawake wengi hawana
muda wa kuyasoma mapigo ya mioyo ya waume zao. Mmewe akifika nyumbani tu
anadakwa mlangoni na risala ya mahitaji; utasikia yafuatayo: unajua hakuna
sukari, chumvi, unga, nk. Mpe mmeo kwanza nafasi ya kupumzika. Muulize habari
za huko alikotoka. Muulize angependa kupata nini kabla ya kile ulichomwandalia.
Wakati mwingine kuandaa meza anafanya mfanyakazi wa ndani. Au akifanya yeye,
yaani, Mama mwenye nyumba utashangaa. Ugali kaupika saa sita mchana wakati
mumewe ufika nyumbani saa kumi jioni. Ugali unatoka jasho tu. Kwa nini usiandae
mboga tu na wakati mumeo anapata chai ukawa unasonga ukali?
Angalia! Huko alikotoka
mumeo kila mahali kuna bar na nyama choma. Na nyumba nyingi pembezoni mwa
barabara kuna vibao vimeandikwa "vyumba bado vipo." Ni kwa namna hii
sebule ujeuka kuwa Bar au kilabu cha pombe. Hutomwona mumeo nyumbani. Akiwa
kwenye Bar au kilabuni ambapo sasa ndiyo sebule yake, hapo anahudumiwa vizuri
na kwa umahiri. Huuliwa, "uncle tukusaidie nini? Anajibu, "bia,
kilimanjaro." "Ya baridi "au ya moto? Mhudumu anasisitiza. Kwa
vile nyumbani weshagombana na mkewe, anajibu, "ya baridi." Tazama
binti huyu, hakai mbali na mteja wake. Wewe ulipomwandalia chakula mmeo ulirudi
kwenye mkeka wako. Binti huyu hukaa nyuzi 45 hivi. Baba huyu akimeza fundo moja
la bia ananyanyua macho anakutana na tabasam la nguvu. Kama Baba huyu alikuwa
na mpango wa kunywa bia moja huongeza zadi na kufika hadi bia 5. Hapa
kwishakuwa sebuleni pake. Nani wa kulaumiwa? Pamoja na udhaifu huu, wanawake
wengi huwasema vibaya sana waume zao. Wengine ufikia hatua ya kuwaita waume zao
"vyuma chakavu." Wapendwa katika ndoa na familia, onyaneni kindugu tena
mkiwa chumbani.
Baadhi ya wanaume nao
ni balaa! Kumtukana hata kumpiga mkewe mbele za watu au marafiki zake na watoto
wake ni ufahari. Ona matusi hayo anavyoyafyatua kama bomu la skadi.
"Mwanamke gani wewe nimekuokota bar? Bado sijaoa!" Unayasema maneno
haya mbele ya watoto wako. Hata kama ni kweli hubakia maumivu makubwa kwa
watoto. Mtume Petro anasema, "ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili;
na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja wa
neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe." 1Pt 3:7.
Mke wako haitaji
umnunulie ndege ili awe na furaha. Ni wewe tu kusadifu kila kitu kidogo
anachokifanya nyumbani. Mmefikia hatua ya kuwaita wake zenu "magoli
kipa." Mkimaanisha wao ni kudaka tu! Jambo hili halipendezi mbele ya
Mungu. Nyote wawili yawapasa kusomana tabia na kupongezana kwa kila kitu
mfanyacho kizuri. Mmeo akikununulia kitu kabla ya kukikosoa mpongeze na
kumwambia siku nyingine ukitaka kuninunulia kitu itapendeza tukienda sote
wawili. Ukweli ni kwamba, wanaume hawana uhalisi wa kuchambua uzuri kama uzuri,
tupo zaidi katika idadi ya kitu au vitu. Leo niwaacha na maadui hao wawili wa
ndoa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi
alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe,” Mk 10:9
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tufungamanishe siku zote na kusudi la lako katika maisha yetu.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario