JUMANNE WIKI
YA 5 YA MWAKA-I
Somo: Mwa 1:20-2:4a
Zab:
8:4-5, 6-7, 8-9
Injili:
Mk 7:1-13
Nukuu:
“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu;
wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote
pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26
“Mungu
akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba,” Mwa 1:27
“Mungu
akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na
kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe
chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28
“Kwa
maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali,
wakishika mapokeo ya wazee wao; tena
wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea
kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba,” Mk 7:3-4
“Akawaambia, Isaya
alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa
huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho
Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi
mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:6-8
“Bali
ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu
changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo
kumtendea neno babaye au mamaye; huku
mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo
mengi yaliyo sawasawa na hayo,” Mk 7:11-13
TAFAKARI:
“Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Ndugu, tufuate
mpango wa Mungu, na Kristo ndiye kielelezo chetu”
Wapendwa wana Mungu,
kwa namna tunavyoishi leo wewe na mimi ni matokea ya mila na tamaduni fulani.
Hivyo binadamu kajengeka kitabia kutokana na historia yake. Mila, tamaduni, na desturi
za mahali hubeba pia falsafa yake, ikiwa ni pamoja na namna ya kuyaona mambo
katika uhasili wake na ukweli wake. Hata hivyo mionekano hiyo wakati mwingine
hubeba dhana potofu pale inapokuwa na mwelekeo wa kuhalalisha kila kitu bila
kujali uhalisia wa kitu husika na kweli yake.
Uwepo wa Mungu ni
dhahiri kwetu kwa njia ya UFUNUO wake. Hivyo kadiri ya historia ya wokovu wetu,
Mungu ndiye aliyechukua nafasi ya kwanza kujifunua kwa mwanadamu, hii ikiwa ni
pamoja na uumbaji wa ulimwengu huu tunaoishi leo pamoja na vitu vilivyomo, Mwa
1:1-31. Hitimisho hili la uumbaji wa leo umekazia mambo makuu matatu; yote yakimlenga
binadamu kwa faida yake: a) Uumbaji wa kila kitu hai kwa jinsi yake (wanyama
pori na wakufungwa), b) Uumbaji wa mtu (kwa mfano wake) mwanamke na mwanamume;
na kuwapa mamlaka ya kutawala vitu vyote, c) Uumbaji wa vyakula (mbegu,
matunda, majani, wanyama). Huu ni mpango mahususi na malengo ya Mungu kwetu. Binadamu
yampasa kutambua ukweli huo na kuuishi, na tena kutoubadilisha katika maana ya
kuugeuza au kubadili tafsiri yake kwa manufaa binafsi.
Mwanadamu anachukua
nafasi ya pekee katika uumbaji huu, yaani, kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,
Mwa 1:27. Ikiwa uwepo wa Mungu ni dhahiri kwa njia ya ufunuo, mwitikio wa
mwanadamu kwa ufunuo huu wa Mungu ndiyo njia ya kumfahamu Mungu na uwepo wake.
Haya yote yanawezekana kwa neema za Mungu na Roho Mtakatifu. “Maana unabii
haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka
kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu,” 2Pet 1:21. Hivyo kwa hasili
mwanadamu anashahuku hii ya kumtafuta na kumjua Mungu. Ndugu yangu tunaye
safiri sote katika tafakari hii, embu tuzame kidogo ndani kwenye somo hili letu
la kwanza.
Wapendwa
wana wa Mungu, masomo yote ya agano la Kale, na hasa yale yaliyochaguliwa
kusomwa siku ya vigilia ya Pasaka, usiku ule Mtakatifu, yanatupatia historia
nzima ya wokovu wetu. Kwa maana hiyo, uwepo wetu hapa duniani si wa bahati
mbaya, wala wewe kuwa katika ulimwengu huu si kwa bahati mbaya. Ulimwengu
umeumwa kwa Upendo wa Mungu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine ulimwengu
huu kama ulivyo umemlenga mwanadamu na kwa lengo la kumweka huru, Isa 45:18.
Msingi
wa haya yote, na sababu yake, tunauona kwenye kitabu cha mwanzo. Wakati
ulipotimia na kufaa, Mungu aliumba ulimwengu kwa neno, na ukawa kama ulivyo. Ni
siku ya sita alipoona inafaa na kumpendeza akamwumba mwanadamu kwa sura na
mfano wake. “Mungu akasema, Na
tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na
ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa
kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Kwa vile ulimwengu ulimlenga mwanadamu, ni
binadamu huyu tu, anayepewa mamlaka ya kuvitawala vile alivyoviumba Mungu.
Utawala huu siyo wa kujifanyia tunavyotaka, ila kuvimiliki katika maana ya
kuvitunza ili viongezeka na kudumu. Tunapewa wajibu huu mkubwa kabisa ambao
hata malaika hawakupewa.
Binadamu
huyu kwa upendo wa Mungu, ameumbwa katika usawa. Hakuna mtumwa na mtwana, au
bwana na mjakazi. Wote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu tukiwa na mastahili
sawa kati ya mwanaume na mwanamke. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano
wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba,” Mwa 1:27. Mastahili haya
yanaendana na wajibu wetu, kila mmoja kadiri ya jinsia yake. Kwa upande
mwingine, haikumaanisha kwamba jinsia moja kuitawala nyingine kwa vigezo vya
utamaduni wetu, mila zetu, makabila yetu, wala utaifa wetu. Mbele za Muumba
wetu sote tu sawa.
Na ni
kwa sababu hii, kunakuwa na uwezekano wa kuzaa na kuongezeka kadiri ya mpango
wa Mungu. Ni kwa sababu hii binadamu anabarikiwa, anawezeshwa na anashirikishwa
uumbaji wa pamoja akishirikishwa na Mungu. Binadamu anakua “Co-creator of God.”
“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia,
Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini,
na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa
1:28. Ndugu yangu, pamoja na uhuru tuliopewa, Mungu hakutupa mamlaka ya
kubadili mpango wake ndani yetu.
Leo
kutokana na ufahamu wa binadamu kuongezeka katika kuyafahamu yanayomzunguka,
amefikia hatua ya kumkosoa Mungu, na kufanya kinyume cha kile alichokinuia. Leo
wapo baadhi yetu wangependa na wanapigania kwa nguvu zao zote kujigeuza jinsia
zao na kuwa vingine. Hili ni kosa ndugu yangu. Kuwa kile alichokufanya; yaani
sura na mfano wake. Tuelewe kwamba ufahamu wa binadamu wote na wenye
kustaajabiwa, ni ujinga wa Mungu. Yatupasa kufuata mapenzi na matakwa ya Mungu.
Hivyo, “Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima;
Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu,” Mit 9:10
Wapendwa wana wa Mungu,
katika Injili ya leo Yesu anawakemea Mafarisayo na baadhi ya Waandishi kutokana
na unafiki wao juu ya kweli ilivyo kadiri ya uwepo wa Mungu na ufunuo wake kwa mwanadamu.
Wanafunzi wa Yesu wanakuwa gumzo kwa vile tu hawakufuata desturi za wazee na
mapokeo yake. “Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi
wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono
najisi?” Mk 7:5. Mapokeo na desturi hizi za Kiyahudi zilibumbwa sana kutoka
torati na kwa kiasi kikubwa walifuata TALMUD, ambayo ni ukweli wa Mungu
uliopotoshwa.
Jambo muhimu sana la
kujua ni kwamba kipindi cha Yesu Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi
hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na
matendo yake kupitia masimulizi) iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud
ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na
MISHNAH (marudio/waliyorudi au mafundisho).
Kwa mantiki hiyo hapo
juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa
350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed)
katika mabado (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi
kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili
la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, na kama nilivyokwisha sema
huu ni ukweli wa Mungu uliopotoshwa.
Talmud hii, yaani, tafsiri
ya Torati iliubeba ubinadamu na kuacha maagizo ya Mungu kama yaliyokuwa katika
Torati. Na kadiri ya Injili ya leo, mapokea ya wazee ni pamoja na haya: “Kwa
maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali,
wakishika mapokeo ya wazee wao; tena
wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea
kuyashika, kama kuosha vikombe, na midumu, na vyombo vya shaba,” Mk 7:3-4. Yesu
analikemea jambo hili kwa lengo la kuwarudisha kwenye kweli kwa kuwaambia, “Isaya
alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa
huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, Wakifundisha
mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu, Ninyi
mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:6-8. Hii ndiyo
sababu ya maneno haya ya Yesu, “Msidhani ya kuwa
nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na
nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka, hata
yote yatimie,” Mt 5:17-18.
Ukweli huu wa Torati
kama mafundisho na maagizo ya kweli ya Mungu waweza kuusoma pia katika sehemu
nyingine za injili kama ifuatavyo; (Mt 7:12; 12:5; 22:40; Lk 2:22; 10:26; 16:16;
24:44;Yoh 1:17; 1:45; 7:19; 7:49). Yesu ni ukweli na amekuja kusimamia kweli ya
Mungu akitambua ukweli huo utatuweka huru. "Basi Yesu akawaambia wale
Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu
kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru," Yoh
8:31-32.
Wapendwa hiyo ndiyo sababu
kubwa ya ugomvi kati ya Yesu na Mafarisayo na Waandishi. Kitendo cha wanafunzi
wa Yesu kutokunawa hadi kiwiko imekuwa shiiida! Jamani haitoshi kunawa kiganja
tu na kuukamata ugali au wali vizuri tu? Yesu anahoji pia, kwa tendo au matendo
wanayoyashikilia yanawafanya wamjue Mungu na makusudio yake katika uumbaji?
Badala yake, mapokeo hayo yaliwafanya watumwa na siyo huru tena. Embu tazama
idadi ya mavitabu yaliyotokana na kurasa 350 tu za Torati. TALMUD ilikuwa na
tafwira ya kiimla (totalitarianism).
Ndugu yangu, hata kwetu
leo ni changamoto kubwa sana. Ni mara ngapi tupo tayari kusimamia ukweli na
badala yake twafumba macho au hata kutoa ushahidi wa uongo na kudhulumu haki za
wanyonge? Yanipasa kuelewa pia, mimi leo kama mbatizwa nasimama badala ya Yesu
kama kuhani, nabii na mfalme. Je, natambua wajibu wangu wa kikuhani
(kutakatifuza malimwengu), kinabii (kutumwa na kusimamia ujumbe sahihi wa
kishuhuda), kifalme (mfalme wa upendo, unyenyekevu, amani na haki)? Ndugu,
tufuate mpango wa Mungu na si wanadamu. Kielelezo chetu ni Kristo!
Kwa kuwaonyesha
kigeugeu chao katika sheria ya Mungu, yaani torati, Yesu anaawambia, “Bali
ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye, Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu
changu cho chote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea
neno babaye au mamaye; huku
mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo
mengi yaliyo sawasawa na hayo,” Mk 7:11-13. Hakika kile wakisemacho sicho
wakiishicho! Hawa ndio wale Yesu aliowasema kuwa ni viongozi vipofu. “Viongozi
vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24. Alisemalo Yesu leo
analisema kwetu pia na jamii yetu ya Tanzania. Si ajabu leo kuona mwizi wa kuku
kafungwa gerezani wakati huo huo wezi wa mabilioni ya fedha za umma ‘wakila
bata,’ mtaani kama ulivyo msema wa jamii yetu leo. DOUBLE STANDARD! Hili Yesu hapendi!
Wapendwa wana wa Mungu, hatuwezi kubeza uwepo wa Mungu
katika maisha yetu. Leo wapo watu huko Kenya wanaotaka kujisajili kama jumuiya
isiyotambua uwepo wa Mungu. Je, unaweza kuwaza kile ambacho hakipo? Ukweli ni
kwamba kadiri unavyokataa uwepo wa Mungu, ndivyo hivyo hivyo unavyo ukubali.
Kumbe ni vyema kuukiri uwepo wake hata kama huelewi sawasawa. Ni
kwa njia hiyo ya kuukubali uwepo wa Mungu, na Mungu hujifua kwako taratibu.
Mfalme Sulemani ni mfano mzuri na wakuigwa kama kiongozi kwenye hofu ya Mungu. “Akasema Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama
wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi
wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote,” 1Fal 8:23. Bila hofu ya Mungu
katika utendaji wetu, ni rahisi sana kufanya kazi ya shetani.
Wapendwa
wana wa Mungu, utampata na kumfikia Mungu kadiri unavyomtafuta. Ndugu yangu, maisha yako yanasukumwa na nini?
Maisha bila Mungu, ni sawa na boti baharini bila usukani. Safari ya mtindo huo
ni majanga tu huko uendapo. Kumbe yatupasa kukiri uwepo wa Mungu na kuomba hivi
kama alivyofanya Mfalme Sulemani, “Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya
watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko
mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe,” 1Fal 8:30. Amina!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Bwana asipoijenga
nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha
bure,” Zab 127:1
Tusali:-Yesu
Mwema, tujalie neema zako tuishi kadiri ya mpango wa Mungu na si kwa kufuata
mipango yetu isiyo na mwelekeo wa umilele.
No hay comentarios:
Publicar un comentario