domingo, 26 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-I

Somo: YbS 35:1-15

Zab: 50:5-6, 7-8, 14, 23.

Injili: Mk 10:28-31

Nukuu:

“Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani,” YbS 35:1

“Amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora, naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabibu ya kushukuru,” YbS 35:2

“Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30.

Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31. 

TAFAKARI: “Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha huongozwa na mfumo au utaratibu fulani kubaliwa pamoja ulio rasmi, au pokeo rasmi kadiri ya mila na desturi fulani za watu. Taifa teule la wana wa Mungu-wana wa Israeli-hawakuwa nje ya ukweli huu. Na “Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani,” YbS 35:1. Maisha ya wetu huakisi tunu za maisha hayo, ambayo hutupa jibu la “kwa nini wanafanya kama wanavyofanya.” Mambo haya kwa tafsiri nyingine ndiyo mang’amuzi ya maisha. Na hili ni wazi kwamba, “amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora, naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabibu ya kushukuru,” YbS 35:2.

Mang’amuzi ya maisha ndiyo msingi wa hekima n abusara za watu katika utofauti wao, na jamii katika upekee wake. Na hitimisho la hayo yote ni mtazamo ule wa pamoja wenye hafiki moja na mwono chanya, yaani, “kuuacha uovu kwampendeza Bwana, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho,” YbS 35:3. Mtazamo pamoja huu hujenga mwelekeo wenye tafsiri pamoja. Hapa ndipo tunapoona umuhimu na swala zima la utaratibu katika kutenda, kutathimini, kuwajibika, na utoaji wa haki pale inapo mwinywa. Mwelekeo huu wa maisha una tahadhari zake pia. Hivyo wewe na mimi wenye hofu ya Mungu ni jambo jema na lenye busara kutojitokeleza “mbele za Bwana mikono mitupu, maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri. Na toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu tamu yake yafika mbele zake Aliye juu,” YbS 35:4-5.

Maisha ya mwanadamu huongozwa kwa lengo au malengo fulani kwa sababu hakuna yeyote aliye katika ulimwengu huu pasipo lengo. Kila chenye pumzi na kisicho na pumzi ni mpango wa Mungu hapo kilipo. Ni Mungu tu mwenye hatma ya kitu hicho, na mwenye mamlaka ya kukihesabia haki chochote kile, chenye pumzi na kisicho na pumzi. Hivyo kama tendo la shukrani kwa Muumba wako wewe ulijaliwa pumzi, “dhabihu ya mwenye haki yakubalikana, wala kumbukumbu lake halisahauliki. Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili,” YbS 35:6-7. Yote yale tuyatoayo mbele ya Mungu hayaongezi wala kupunguza ukuu wa Mungu kwa sababu, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1.

Kumbe tufanyacho wewe na mimi ni tunapotoa shukrani kwa Mungu ni kusadifu uwepo wake, na muungano wake nasi. Ni kusema, “bila wewe Mungu yote ndani yaangu hayana maana.” Hivyo, “kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko,” YbS 35:8. Na kwa mantiki hiyo yatupasa wewe na mimi kumpa “Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” YbS 35:9.

Ndugu yangu, ikiwa hakuna yeyote kati yetu katika ulimwengu huu yupo kwa bahati mbaya, na kila kilichopo cha ufunua utukufu wa Mungu na furaha yake, masikini tuwaonao katika mizania ya kibinadamu nao wana mwakilisha Mungu kama wafanyavyo matajiri na wenye uwezo mbalimbali katika kipimo hicho hicho cha kibinadamu. Hivyo, “amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” YbS 35:10. Utofauti kimaisha, yaani, kati ya aliye nacho na asye nacho, siyo mizania ya Muumba wetu, na wala Yeye hatuoni katika utofauti huo. Ni jukumu lako na langu kuondoa tofauti hiyo kwa sababu hali hiyo ipo ndani ya uwezo wetu, na hakuna aliye tajiri katika ulimwengu huu ambao amekuja nao. Hivyo hakuna njia ya ufupisho katika hili. Na hapa hakuna rushwa. “Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu,” YbS 35:11-12.

Ndugu yangu, elewa kwamba unapofanya jambo hili, yaani, kurejesha usawa na utu kati ya jamii ile unayoishi, warejesha utukufu na furaha ile ilikuwa sababu na kusudi la kuumbwa kwetu, Mwa 1:27. Hivyo Mungu, “hatamkubali yeyote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa. Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake,” YbS 35:13-14. Mungu wetu ni mtetezi mkubwa wa wanyonge na wanaodhulumiwa haki zao kwa sababu, ulimwengu huu haukuumbwa ukiwa, bali uliumbwa ili ukaliwe na watu, Isa 45:18. Na tunapoona maovu haya na hasa kwa wajane yakitokea katika jamii yetu leo swali ni hili: “Je, machozi ya majane hayachuruziki mashavuni mwake? Naye aziugulia taabu zake zilizoyatokeza,” YbS 35:15.

Wapendwa katika Kristo, Bwana wetu Yesu Kristo anakutaka wewe na mimi tusifanye marejesho, au malinganisho, na wala manung’uniko utoapo sadaka ya maisha yako kwake na kwa Injili, yaani, Habari Njema ya Wokovu wetu kwa watu wate. “Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Yesu Kristo kama alivyomwondolea mashaka Petro ndivyo hivyo hivyo anavyokuondolea mashaka wewe na mimi tutoapo sadaka ya maisha yetu kwa ajili yake na Injili. Hivyo licha ya kuyapata haya ya leo na sasa kadiri ya hitaji letu,  tuna hakika ya uzima wa milele ndani na katika Kristo.

Ndugu yangu, kujitoa sadaka ya maisha yako kwa ajili ya Kristo na Injili kwahitaji fadhila ya unyenyekevu. Hapa ndipo kwenye kushushwa na Kristo pale unapojipandisha mwenyewe na pasipo haki, na kupandishwa na Kristo pale unapojishusha kwa kumpa nafasi Kristo ndani ya maisha yako. Kwa maana hiyo, “wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31. Hii ndiyo changamoto kubwa katika maisha yetu ya kiroho.

Ukimruhusu Yesu Kristo ndani ya maisha yako uwe tayari kuyapokea yote kama alivyoyapokea Kristo hadi kuwambwa pale Msalabani. Utatemewa mate, utachekwa, watakushangaa, utakejeliwa, utazushiwa, utashangiliwa, utaonewa huruma, na mwisho utawambwa kama utimilifu wa sadaka ya maisha yako kwa Kristo na Injili. Haya ndiyo maisha ya utauwa. “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa,” 2Tim 3:12. Kwa maana nyingine hii ndiyo heri ile ya kuishi umasikini wa roho, Mt 5:3, kwa kumpa Yesu Kristo nafasi ndani ya maisha yako, na mwisho wa siku kuupata Ufalme wa Mbinguni. Ni kama asemavyo Mtume Paulo kwamba, “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote,” 1Kor 15:19. Ni umasikini kwa kupungua ili Kristo Yesu apate nafasi ndani ya maisha yako, nawe uwe na furaha isiyo na kipimo. “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Wapendwa nani kama Yesu Kristo? Hakuna!

TumsifuYesu Kristo!

“Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31.

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nifundishe njia yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario