viernes, 29 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 6 YA MWAKA-C

JUMAPILI YA 6 YA PASAKA YA MWAKA-C

Somo I: Mdo 15:1-2, 22-29
Zab: 67:1-5, 7 (K) 3
Somo II: Ufu 21:10-14, 22-23
Injili: Yoh 14:23-29
Nukuu:
Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka,” Mdo 15:1

 “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28

Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake,” Ufu 21:22 

Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo,” Ufu 21:23 

 “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26

Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,” Yoh 14:27

 “Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini,” Yoh 14:29 

TAFAKARI: “Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.”

Wapendwa wana wa Mungu, Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya sita ya mwaka “C” wa Kanisa. Tafakari yetu ya leo inalenga kwa kiasi kikubwa tukio lile la Pentekoste, na hasa ahadi ile aliyotuhaidia Bwana wetu Yesu Kristo kwamba, ‘huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.’ Leo anatukumbusha ahadi hiyo tunapotafakari neno hili: “Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini,” Yoh 14:29. Roho huyu Mtakatifu ndiye aliyeliongoza “Kanisa la mwanzo” kwenye changamoto mbalimbali, na hasa swala zima la kupokelewa na kushiriki huduma za kikanisa kwa wale ambao hawakuwa Wayahudi. Ni Roho huyu pia aliyewawezesha Mitume kufanikisha Mtaguso ule wa Yerusalemu. Na Roho huyu Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kupanuka na kuenea kila kona ya dunia hadi leo. Hata hivyo kwa kupanuka huku na kuenea kila kona kwa Kanisa hili la mwanzo, lilikumbwa na kasumba ya ubaguzi uliolenga mila na desturi za Kiyahudi. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tendo la kutahiriwa kwa wayahudi lilibeba tafsiri mbalimbali kwa kadiri walivyoishi na kufanya maagano yao na Mungu.

Kama tulivyoona katika tafakari ya masomo kwa wiki nzima hii iliyokwisha, kwa mara ya kwanza katika historia yao-Wayahudi, tendo hili la kutahiriwa lilibeba maana ya usafi na kwa yule aliyetaka kuoa lilichukua maana ya “Bwana harusi wa damu.” Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri” Kut 4:25-26.  Kutahiri kulimaanisha pia agano kati yao na Mungu hasa kwa tendo la Mungu kuwatoa utumwani Misri, na hapa wanatairiwa kwa mara ya pili. “Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri,” Yos 5:2-4. Kutahiriwa pia kulimaanisha kushika torati kikamilifu. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa?  Rum 2:26. Pamoja na sababu nyingine zote tulizokwisha kuziona, hii ya mwisho ndiyo iliyotumika kama kigezo cha alisiye Myahudi kupokelewa katika jumuiya hii ya Wakristo wa kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa walikuwa Wayahudi. Hapa tunaambiwa, Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka,” Mdo 15:1

Mambo haya ya nje hayakupaswa na hayapaswi kuwa sababu ya kutokuishi upendo wa Kristo katika Kanisa. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3:11. Maandiko Matakatifu, hasa Habari Njema ya Bwana wetu Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohana inasema ukweli huu wa Kristo, kwamba,  Uzima wetu, na uhai wetu kiroho ni katika Kristo Yesu aliye mzabibu nasi matawi yake. Kuishi katika ukweli huu ni kuzaa matunda, yaani kuwa watu wa  upendo, haki na amani kama Kristo mwenyewe. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa,” Yoh 15:2.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, “sisi sote tuna mastahili sawa mbele ya Kristo, yeye ndiye aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda ya kudumu.” Yakiwa haya ndiyo majumuisho ya Mtaguso wa Yerusalemu, Kristo anatupenda kama tulivyo na kutuhesabia haki mbele zake na mbele ya Mungu Baba bila kujali familia tulizozaliwa, koo tulizotoka, kabila tulizotoka, na hata mataifa tuliyotoka. Hakika, ingekuwa haya niliyoyataja kuwa kigezo cha kuwa Mkristo na hata kuwa Mtumishi katika Kanisa lake KRISTO, bila shaka ingekuwa ndoto leo mimi au wewe kuwa kama nilivyo ndani na katika KRISTO. Ni katika msingi huu nilioutaja (Kristo ametuchagua bila ya mastahili yetu), Mtaguso wa Yerusalema wanaafikiana vyema kuhusu swala la watu wa mataifa waliolipokea neno na kuunda ujumuiya ya Kikristo. Ukristo wetu hautokani na hayo matabaka niliyoyasema hapo juu. Ukristo wetu unatokana na kuhesabiwa haki na Kristo mwenyewe, kulikotokana na kutupenda upeo, Yoh 13:1. Hivyo Mtaguso wa Yerusalemu unatoa tamko lifuatalo, sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25. Mtume Paulo na Barnaba wanachaguliwa kwa vigezo vya maisha yao kupeleka ujume huu kwa wale waliolipokea neno. Ni watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo 15:26.

Hata hivyo Yuda na Sila ndio watakaosema kwa vinywa vyao juu ya ujembe huo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao,” Mdo 15:27. Yuda na Sila bila shaka ni watu waliokuwa karibu sana na jumuiya hiyo mpya ya Antiokia. Uwakilishi huu ni njia mojawapo ya kuboresha ukaribu wao na jumuiya ya Yerusalemu, na kuanza kuishirikisha jumuiya hii mpya ya Antiokia yale yote yamuhusuyo Kristo. Ukaribu na umoja huu si wakubebeshana mizigo, bali ni fursa ya kuyatafakari makuu ya Mungu na upendo wake kwa kila mmoja aliyeridhia upendo na umoja huo wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye mleta umoja huo. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28.
Hivyo basi, ili kuendelea na umoja huu na upendo huu ndani na katika Kristo, iliwapasa kujitenga na yale ambayo hayakuwa na mwelekeo wa Kimungu. Ni ukweli kwamba kama tunataka kuishi katika Kristo, yatupasa kujikana wenyewe na kumfuata. Yatupasa kuacha yale ya zamani na kuyachuchumilia yale yampendezayo Kristo. Hivyo basi, jumuiya hii mpya ya Antiokia, inapaswa kufanya haya yafuatayo; yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Tunapoachana na makandokando haya ya maisha ndipo tunapokuwa karibu na upendo wa Kristo na kutimiza mapenzi yake. Huu ndio upendo anaotutaka Kristo tuuishi kama familia yenye hofu ya Mungu na kuwajibika. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Ndugu yangu, jambo hili si rahisi! Mimi na wewe leo tupo hiki tulicho kama tokeo la historia yetu tangu kuzaliwa, makuzi yetu ambayo yameathiriwa na mila na desturi zetu, ufahamu wetu ambao umeathiriwa pia na mfumo mzima wa elimu tuliokuwa nao. Katika mazingira hayo ya makuzi, lengo ni kuuona ukweli kama ulivyo, na siyo kuuona ukweli kama tulivyo. Hapa ndipo penye tofauti kubwa ya kusoma na kuelimika. Wote walioelimika wamesoma, ila siyo wote waliosoma wameelimika. Hapa kusoma simaanishi kwenda darasani kama ilivyo ada, bali kuyaelewa vizuri mazingira yanayokuzunguka, ambayo kwa kiasi kukubwa si lazima kwenda darasani kadiri ya mfumo unavyotutaka. Hivyo kwa mazingira ya Kanisa la mwanzo, na changamoto iliyowakabili, Mtaguso ule uliwalazimu kuyaona yote katika upendo wa Kristo na hatma ya upendo huo ambao ni kifo kile cha Msalaba.

Ndugu yangu, kuukubali ubinadamu wetu ni pamoja na kujitambua na kuzishika amri za Mungu kwani twataka kuongozwa na Mungu na kuwa watoto wa Mungu. Hivyo Yesu anasema, Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Nani asiyependa kutambuliwa na Mungu? Embu fikiri yote uyafanyayo leo kadiri ya wito wako mwisho wa siku yanakosa kibali mbele ya Mungu. Kumpenda Mungu ni kushika amri zake. Kristo kesha tuambia ni amri ipi iliyo kubwa kuliko zote. Je, neno UPENDO ni geni kwako? Yesu anasema, Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24. Hata Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani hakujifanyia mambo yake kadiri atakavyo. Alikuwa makini sana kutimiza mapenzi ya yule alimpeleka yaani Mungu Baba. Swali la kujiuliza mara zote ni hili, je, hapa nilipo na kadiri ya agano au maagano yangu kimaisha ninayafanya mapenzi ya Mungu? Kama jibu ni hapana, Je, nimejiandaaje kujibu swali hili siku ya mwisho?

 Ndugu yangu, mpango wa Mungu kwetu na hasa swala zima la maisha ya umilele limeratibishwa vizuri sana. Nafasi uliyokuwa nayo leo na “mawezekano yake kimaisha,” hayapo kwa bahati mbaya kwako au kwa upendeleo. Yote haya yanasababu kubwa kuhusu maisha yako ya sasa na wale wanaokuzunguka, na hatma  yake, yaani, umilele. Hata hivyo, kwa kutusaidia, Yesu Kristo anatukumbusha jambo muhimu sana ndugu zangu. Naye anasema, Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26. Hivi kama tumefundishwa yote na kukumbushwa yote tunayosababu ya kushindwa mtihani ulio mbele yetu? Ni katika maana hii Yesu anatuambia mwisho wa kiama jambo hili litatokea kwa hakika. “Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje,” Lk 13:28. Neno hili “kusaga meno” limesemwa mara sita katika Habari Njema ya Bwana wetu Yesu Kristo kama iliyoandikwa na Mwinjili Matayo, mara moja kama ilivyoaandikwa na Mwinjili Marko na mara moja kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka. Maana yake ni kwamba hakutakuwa na nafasi ya kujitetea kwani nafasi ya kufanya vema ni leo na sasa. Kristo Yesu angali hapa duniani aliweka yote sawa na kusema bila kupindisha neno, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Yesu Kristo ni njia kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia aliyoichagua Yesu ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukuliana kindugu katika misalaba ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu, tunakutana naye Kristo katika hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii tunakutana nayo katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi wa neno.

Na Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake,  Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa ndani yetu. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.

Kuliishi kiaminifu fundisho hili zito la Kristo, Yoh 14:6, kunatusaidia kuzama ndani ya ule ufunuo wa Yohana na kuona uzuri wa maisha ya umilele kadiri ya somo letu la pili leo. Naye anasema, Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake,” Ufu 21:22. Maana yake ni nini?

Basi mpendwa katika Kristo kwa kuelewa zaidi juu ya neno hilo la Ufunuo 21:22, nikuache na mfano huu:-Bila shaka wengi wetu tuna mawazo ya “kuwa TENA kile tulicho leo na sasa baada ya maisha haya hapa duniani.” Mathalani, kama mimi leo Mama Kanisa kanihesabia haki ya kuwa mtumishi wake na muhudumu kama ‘Baba Paroko au Askofu,’ kwenye maisha baada ya kifo-umilele, hakutakuwa tena na wajibu huo kama Paroko au Askofu kwa sababu huko hakutakuwa na “mwonekano,” “muundo,” “mfumo” tena wa kiparokia au kijimbo. Nawe ndugu yangu unayeishi leo Sakramenti yako ya ndoa ni kukumbushe maneno haya ya Yesu; Naye anasema Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:34-36. Je, maneno haya ya Yesu na yale ya ufunuo wa Yohana 21:22, yanasema chochote katika maisha yako leo? 

Wapendwa wana wa Mungu, bila kujali mtindo wa maisha tunaoishi leo kila mmoja kadiri ya wito wake, sote katika maisha ya umilele tutajulikana kwa cheo chetu tu, yaani, utakatifu wako. Na mahali pa kuutafuta utakatifu huo ni hapa hapa duniani kwa muda huu mfupi tuliokuwa nao. Hivyo, haijalishi mimi ni nani leo, ila kila siku yanipasa niyaone maisha yangu katika mtazamo wa Kimungu, yaani: Maisha ya duniani ni jaribu, Maisha ya duniani ni dhamana, na Maisha ni jukumu la muda mfupi. Utukufu wa Mungu ambao ni UTAKATIFU WAKE ni mwanga na nuru ya kutosha katika maisha hayo ya umilele. Utakatifu wa kila mmoja wetu ambacho ndicho cheo chetu, ni ile hali halisi tutakayokuwa nayo wakati tulipoumbwa, yaani, ‘sura na mfano wake Mungu,’ Mwa 1:27. Hivyo, “wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo,” 1Yoh 3:2. Kumwona Mwana-Kondoo huyu, Yesu Kristo kama alivyo kwawezekana tu katika hali ya utakatifu wako. Kwa sababu,  Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo,” Ufu 21:23. Je, bado taa yangu inawaka, yaani, UTAKATIFU wangu? Je, ile sura na mfano wa Mungu ndani yangu bado inang’aa, au ishafifishwa na mali yangu halali, yaani, dhambi zangu? Tafakari!

Tumsifu Yesu Kristo! 

Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia,” Yoh 14:26


Tusali:-Ee Yesu, uliye Mwana-Kondoo na taa halisi ya Mungu, niwezeshe kila siku kutoififisha ile sura na mfano wa Mungu ndani yangu. Amina

jueves, 28 de abril de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 5 YA PASAKA

JUMAMOSI WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 16:1-10
Zab: 100:1b-2, 3, 5
Injili: Yoh 15:18-21
Nukuu:
 “Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1 

Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani,” Mdo 16:3

Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo 16:4

Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5

Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18

Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19

Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21

TAFAKARI: “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo kwa namna ya pekee tutafakari changamoto za uinjilishaji za Kanisa la mwanzo na changamoto tunazokumbana nazo leo katika utume wetu kama wabatizwa na wahudumu katika Kanisa. Bila shaka wiki nzima hii tumekuwa tukitafakari changamoto hizi na hatua waliyochukuwa Mitume kukabiliana nazo, hasa kwa kuitisha Mtaguso wa Yerusalemu.

Matokea ya Mtaguso huu ulikuwa: Wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Hata hivyo Kanisa bado linakumbana na changamoto za mila na desturi za Kiyahudi. Hivyo ili Timotheo afuatane na Mtume Paulo, inampasa kutahiriwa. Basi akafika Derbe na Listra, na hapo palikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, mwana wa mwanamke Myahudi aliyeamini; lakini babaye alikuwa Myunani,” Mdo 16:1. Je kwa tendo hili Paulo atakuwa ameenda kinyume na maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu? Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii, ni vyema tuelewe jambo hili. Licha ya kwamba Kanisa ni la kiulimwengu, na hili limethibitishwa katika mitaguso mbalimbali, maamuzi ya mitaguso hiyo hayaondoi upekee wa changamoto ya Kanisa mahalia, mfano Kanisa la Tanzania. Hapa ndipo tunapozungumzia busara za kichungaji kuenenda na mazingira husika bila kuwakwaza watu. Hivyo, tukio hili la kutahiriwa kwa Timotheo linaendana na mazingira maalumu bila kuwakwaza watu, ili kuweza kupenyeza ujumbe ule waliokuwa wameubeba au kusudiwa, na hapa ikiwa ni maamuzi ya Mtaguso wa Yerusalemu.

Mtume Paulo anatupa sababu ya kufanya hivyo ikiwa ndiyo busara ya kichungaji. Paulo akamtaka huyo afuatane naye, akamtwaa akamtahiri kwa ajili ya Wayahudi waliokuwako pande zile; kwa maana wote walijua ya kuwa babaye ni Myunani,” Mdo 16:3. Je, Paulo alilifanya jambo hili kutowakwaza Wayahudi? Bila shaka Paulo analifanya jambo hili kwa malengo hayo, kama anavyosema Kristo, Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa,” Lk 17:1-2. Ni vizuri kutowakwaza wale tunaotaka waufahamu ukweli wa Mungu. Kwa upande wa kichunguaji, ni rahisi sana kumhubiri Kristo kwa kwale wasiomjua bado, kuliko kuwarudisha wale waliokatishwa tamaa hasa pale tunapowakwaza.

Kwa mambo yale ambayo hayaendi kinyume na imani yetu, yanapotokea bila kujua au kujiandaa, ni vyema tukayapa muda ili tuyaelewe na kutumia mbinu ya kuwaelimisha wale wayafanyayo, hasa tukilenga katika kutaka kujua ‘kwa nini wanafanya kama wanavyofanya.’ Hivyo kwa kulitambua jambo hilo, inakuwa rahisi kufikisha ujumbe ule uliokusudiwa. Basi walipokuwa wakipita kati ya miji ile, wakawapa zile amri zilizoamriwa na mitume na wazee walioko Yerusalemu, ili wazishike,” Mdo 16:4. Mambo haya huwa tunakutana nayo mara nyingi hasa pale tunapoanza utume mpya katika mazingira mageni kinyume na mila na desturi zetu tulizokulia na kuzizoea. Jambo la msingi ni kushikilia mafundisho sahihi ya Kanisa (katika kuyafundisha kwa lugha nyepesi na mifano hai ili yaeleweke kwa waamini) na yenye mwelekeo wa wokovu, na maisha ya umilele.

Ni dhahiri kwa Kanisa la mwanzo mengi yalifundishwa na yenye kuleta umoja kindugu na Kikanisa kwa ujula wake, ila haya manne yapo wazi, ususani tendo la kutahiriwa kuonekana kama kigezo cha kuchangamana pamoja; Kwanza, mafundisho yalisisitiza kuzishika amri za Mungu. “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu,” 1Kor 7:19.

Pili, kuishi maisha ya Ufufuko ndani na Katika Kristo Yesu, na hapa yakilenga haswa mila na desturi zetu zilizopotofu na zisizo na mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Msalaba wa Kristo ndiyo kielelezo cha huo Utukufu wenyewe. Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya,” Gal 6:14-15. Hapa tunakumbushwa pia hakuna Utukufu pasipo Msalaba kwa ye yote yule aliye mfusi mwaminifu wa Yesu Kristo.

Tatu, mafundisho ya Kanisa la mwanzo yalijikita kwenye kweli ya kuwa yote katika yote na Kristo Yesu. Kujitoa bila kujibakiza katika hali ya kusahau tofauti zetu zisizo na mwelekeo wa wokovu na maisha ya umilele. Hivyo hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote,” Kol 3.11.

Nne, yote yapo kama yalivyo kwa neema ya Mungu. Hakuna kati yetu mwenye kujihesabia haki mwenyewe. Zipo sehemu nyingi katika Maandiko Matakatifu, na hasa Agano Jipya zinazoonyesha kweli hii. Hivyo ndugu yangu, kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi,” 2Kor 1.12

Hivyo wapendwa wana wa Mungu, wewe na mimi yatupasa kujua kweli hii, kwamba, utamaduni wa mahali fulani ni sehemu ya Maisha yao, na hivyo ni Utakatifu wao. Kwa maana hiyo, tuwapo katika mazingira hayo ni kufanya kama alivyoambiwa Musa na Mungu, “Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu,” Kut 3:4-5. Yatupasa kuvivua viatu vyetu, ili kujua utakatifu wa mahali pale. Yatupana kuwa tayari kuona upya na watu wa mahali pale ili kujua ukweli halisi ya maisha yao. Uinjilishaji wetu na umisionari kwa ujumla wake unapokosa dhana hii ya kuona upya yale tunayokutana nayo, ukiambatana na  upole wa kujifunza, mwisho wa siku tunaishia kutokuwaelewa watu husika na kuwa na sintofahamu kubwa. Mtihani huu Mtume Paulo anaufaulu vizuri, na matokea yake ni kwamba, Makanisa yakatiwa nguvu katika ile Imani, hesabu yao ikaongezeka kila siku,” Mdo 16:5. Ukiona kila unayekutana naye anakukimbia ujue kunatatizo kubwa katika mahusiano yako na wale unaokutana nao. Kabla ya kumtafuta mchawi, zama kwanza ndani yako na jipekue vizuri namna yako ya kufanya mambo, na namna ya kufikisha kwao kile ulichotarajia-ujumbe.

Wakati mwingine yawezekana kabisa ukakumbana na pingamizi kubwa kutokana na mazoea yao ambayo yamekuwa sehemu ya tabia yao. Unapotenda jambo jema kwa watu na mapokeo yao yakawa mabaya, wala usikate tamaa. Tumia njia njingine ili ujumbe ule ule uwafike vyema. Na zaidi ya hayo Yesu anatuimarisha kwa kutupa moyo na kusema, Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi,” Yoh 15:18. Kama ulimwengu huo ulishamchukia yule kwa wakati huu unayemtumikia, hakika huyo huyo ndiye atakaye kupa njia na namna ya kufanya pale ukutanapo na mkwamo. Yesu anasema hivi kuhusu hali hii mara inapotoka: Na watakapowachukua ninyi, na kuwasaliti, msitafakari kwanza mtakayosema, lakini lo lote mtakalopewa saa ile, lisemeni; kwa maana si ninyi msemao, bali ni Roho Mtakatifu,” Mk 13:11. Kwa vile ujumbe uusemao na kuusimamia si wetu binafsi, kwa wakati huo Roho Mtakatifu atatusaidia kuyasema yale yatupasaya kuyasema kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Ukweli ni kwamba yeyote anayekuwa ndani na katika Kristo, ujitenga na mwelekeo na mtazama wa yale tunayoyaishi na kukutana nayo kila siku. Mtu huyu huyaona mambo yote katika mtazamo mwingine. Unapokuwa na maisha yenye malengo, na hasa maisha katika ufuasi wa Kristo, utayaona yote katika umilele. Kukiona kitu katika umilele wake, ukweli huu hupingana na dhana ya leo na sasa. Tupo katika ulimwengu wa ‘ponda mali kifo chaja.’ Hivyo Yesu Kristo anatuambia kuhusu ukweli huu, kwamba,  “Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia,” Yoh 15:19. Hufanyapo kila kitu na kupigiwa makofu, jaribu kuchunguza makofi hayo. Wakati mwingine makofi hayo huashiria kejeri.

Mwisho tuwe tayari kutendwa vibaya kama Kristo alivyotendwa kwa sababu watesi hawa hawamjua yule aliyempeleka Kristo. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21. Tusisahau pia matatizo na magumu katika utume wetu, yanatufanya kukua na kukomaa kiroho.

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka,” Yoh 15:21


Tusali:-Ee Yesu, uliyeshinda uovu kwa wema, tujalie uvumilivu. Amina

miércoles, 27 de abril de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 5 YA PASAKA

IJUMAA WIKI YA 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 15:22-31
Zab: 57:8-9, 10, 12
Injili: Yoh 15:12-17
Nukuu:
sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25

watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo 15:26

Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao,” Mdo 15:27 

Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28

yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29

Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12

Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki,” Yoh 15:13

Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Mdo 15:16

TAFAKARI: Maamuzi na wakaraka wa Mtaguso wa Yerusalemu: “Sisi sote tuna mastahili sawa mbele ya Kristo, yeye ndiye aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda ya kudumu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, “sisi sote tuna mastahili sawa mbele ya Kristo, yeye ndiye aliyetuchagua bila mastahili yetu ili tuzae matunda ya kudumu.” Yakiwa haya ndiyo majumuisho ya Mtaguso wa Yerusalemu, Kristo anatupenda kama tulivyo na kutuhesabia haki mbele zake na mbele ya Mungu Baba bila kujali familia tulizozaliwa, koo tulizotoka, kabila tulizotoka, na hata mataifa tuliyotoka. Hakika, ingekuwa haya niliyoyataja kuwa gizezo cha kuwa Mkristo na hata kuwa Mtumishi katika Kanisa lake KRISTO, bila shaka ingekuwa ndoto leo mimi kuwa kama nilivyo. Ni katika msingi huu nilioutaja (Kristo ametuchagua bila ya mastahili yetu), Mtaguso wa Yerusalema wanaafikiana vyema kuhusu swala la watu wa mataifa waliolipokea neno na kuunda ujumuiya ya Kikristo. Ukristo wetu hautokani na hayo matabaka niliyoyasema hapo juu. Ukristo wetu unatokana na kuhesabiwa haki na Kristo mwenyewe, kulikotokana na kutupenda upeo. Hivyo Mtaguso wa Yerusalemu unatoka tamko lifuatalo, sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,” Mdo 15:25. Mtume Paulo na Barnaba wanachaguliwa kwa vigezo vya maisha yao kupeleka ujume huu kwa wale waliolipokea neno. Ni watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo,” Mdo 15:26.

Hata hivyo Yuda na Sila ndio watakaosema kwa vinywa vyao juu ya ujembe huo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao,” Mdo 15:27. Yuda na Sila bila shaka ni watu waliokuwa karibu sana na jumuiya hiyo mpya ya Antiokia. Uwakilishi huu ni njia mojawapo ya kuboresha ukaribu wao na jumuiya ya Yerusalemu, na kuanza kuishirikisha jumuiya hii mpya ya Antiokia yale yote yamuhusuyo Kristo. Ukaribu na umoja huu si wakubebeshana mizigo, bali ni fursa ya kuyatafakari makuu ya Mungu na upendo wake kwa kila mmoja aliyeridhia upendo na umoja huo wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye mleta umoja huo. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,” Mdo 15:28.

Hivyo basi, ili kuendelea na umoja huu na upendo huu ndani na katika Kristo, iliwapasa kujitengana na yale ambayo hayakuwa na mwelekeo wa Kimungu. Ni ukweli kwamba kama tunataka kuishi katika Kristo, yatupasa kujikana wenyewe na kumfuata. Yatupasa kuacha yale ya zamani na kuyachuchumilia yale yampendezayo Kristo. Hivyo basi, jumuiya hii mpya ya Antiokia, inapaswa kufanya haya yafuatayo; yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu,” Mdo 15:29. Tunapoachana na makandokando haya ya maisha ndipo tunapokuwa karibu na upendo wa Kristo na kutimiza mapenzi yake. Huu ndio upendo anaotutaka Kristo tuuishi kama familia yenye hofu ya Mungu na kuwajibika. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Ndugu yangu, jambo hili si rahisi! Mimi na wewe leo tupo hiki tulicho kama tokeo la historia yetu tangu kuzaliwa, makuzi yetu ambayo yameathiriwa na mila na desturi zetu, ufahamu wetu ambao umeathiriwa pia na mfumo mzima wa elimu tuliokuwa nao. Katika mazingira hayo ya makuzi, lengo ni kuuona ukweli kama ulivyo, na siyo kuuona ukweli kama tulivyo. Hapa ndipo penye tofauti kubwa ya kusoma na kuelimika. Wote walioelimika wamesoma, ila siyo wote waliosoma wameelimika. Hapa kusoma simaanishi kwenda darasani kama ilivyo ada, bali kuyaelewa vizuri mazingira yanayokuzunguka, ambayo kwa kiasi kukubwa si lazima kwenda darasani kadiri ya mfumo unavyotutaka. Hivyo kwa mazingira ya Kanisa la mwanzo, na changamoto iliyowakabili, Mtaguso ule uliwalazimu kuyaona yote katika upendo wa Kristo na hatma ya upendo huo ambao ni kifo kile cha Msalaba.

Upendo huu miongoni mwetu wenye taswira ya Kristo mwenyewe, ni upendo unaoitaji kujitoa sadaka kwa wengine. Kupenda kama Kristo alivyotupenda kunatudai kujitoa sadaka kwa wale tunaoishi nao kila siku. Upendo usiojitoa sadaka bado hujafikia ukomavu wake. Yanipasa kujisikia furaha tena na tena ninapojitoa sadaka kwenye familia yangu, jumuiya yangu ya kitawa, jumuiya yangu ndogo ndogo ya Kikristo, na hata Kanisa langu ninaposali na kumsifu Mungu. Yesu anatuambia, Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki,” Yoh 15:13. Hili Yesu kalifanya kwa vitendo. Hatua hii ya upendo ni ukomavu katika maisha ya Kiroho. Mimi na wewe iwe changamoto yetu ya kudumu.

Ndugu yangu, tunayafanya haya yote si kwa vile sisi ni mashujaa wa kufanya hivyo. La hasha! Tunafanya hayo yote kwa sababu  yupo ambaye kabla ya sisi kuyafanya hayo kesha yafanya na anaendela kuyafanya ndani mwetu kwa  nguvu na neema zake. Mtu huyu ni Kristo mwenyewe. Unapoona unatenda jambo jema na watu wakaliitikia kwa moyo wa upendo, elewa jambo hilo linamkono wa Kristo ndani yake. Wewe na mimi katika tendo hili tutakuwa tumetumika vizuri kama watumishi waliofanya vyema yale waliopaswa kuyafanya. Hivyo katika kweli hii, Yesu natuambia, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Mdo 15:16. Hakika matunda yanayotokana na kutumika vyema kwa nguvu na neema za Mungu, hudumu daima hata kama kwa wakati ule sisi hatutakuwepo kushuhudia ukweli huo. Hivyo mara zote tujione hivi: Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10 

Ndugu yangu usiache kutenda mema hata kama kwa hali ya ubinadamu wako unakatishwa tamaa kufanya hivyo. Uhalisi wa wema huo ni Mungu mwenyewe.

Tumsifu Yesu Kristo.

Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Mdo 15:16


Tusali:- Ee Yesu wangu na yote kwangu, nitumie vyema kama chombo chako kisicho na faida. Amina

martes, 26 de abril de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 5 YA PASAKA

ALHAMISI WIKI 5 YA PASAKA
Somo: Mdo 15:7-21
Zab: 96:1-2a, 2b-3, 10
Injili: Yoh 15:9-11
Nukuu:
Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini,” Mdo 15:7

Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao,” Mdo 15:11

Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu,” Mdo 15:19-20

Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10

TAFAKARI:Tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ni siku nyingine tena kwa neema ya Mungu tunapata fursa ya kulitafakari neno lake. Leo kwa namna ya pekee tulitafakari hili neno, “Tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu.” Hakika kile tulicho mbele ya Mungu si kile tunachokipigania sana na kutupotezea muda mwingi hapa duniani, ikiwa kitu hicho kinalenga tu ubinafsi wetu. Njia ya Mungu ni ya ajabu sana. Ni ukweli usiotia shaka kwamba leo katika mazingira yetu bila ya kufahamika hutambuliki. Kufahamika huku hakujalishi tu kujuana na mtu. La hasha! Naposema kufahamika ni pamoja na utaratibu tuliojiwekea katika jamii tunayoishi. Mfano: Viwango vya kufaulu kwa wale waliopata bahati ya kusoma. Bila kupita viwango na masharti hayo, maisha yako huko mbeleni ni utata mtupu. Viwango vya kimadaraja kutokana na kufaulu kwako na kukufanya kuwa pale ulipo leo, navyo ututofautisha na wengine na wakati mwingine hutufanya kujisahau na kujiona huo ndio mwisho wa yote.

Maisha ya hapa duniani yanakikomo chake. Na tena ni kwa muda mfupi tu. Maisha anayotutaka Mungu tuishi ni ya umilele. Hivyo kuwa kwetu salama na kupata mastahili mbele ya Mungu ni kwa njia ya NEEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO. Je, hii inamaana kwamba tusijishughulishe na haya tunayoyaishi leo na utaratibu wake? La hasha! Ukweli ni kwamba Mungu anatupenda kama tulivyo na atatuokoa kama tulivyo, ili hali tu, yale tunayoyaishi yaakisi Umungu wake. Niwe tajiri au masikini, mwenye elimu ya pekee au kawaida, mwenye cheo au kabwela, kwa maisha yangu niishiyo kama hayaakisi Umungu wake ni kama moshi unaotoweka mara.

Mtazamo huu wa Kimungu ndiyo msingi wa Mtaguso wa Yerusalemu kuhusu uhalali wetu mbele ya Mungu na wokovu wetu. Uhalali huu si mastahili yetu, bali ni wema na upendo wa Mungu aliyekuwa wa kwanza kutupenda. Je, kuna sababu ya kujichukia? Huna sababu yoyote ya kujichukia. Yupo anayekupenda zaidi ya vyote vyenye thamani katika dunia hii. Mtu huyu akupendi tu, bali anakutakia maisha ya umilele. Huyu ndiye Yesu Kristo aliyekufa kwa ajili yako na kila siku anakufa kwa ajili yako unapomwelekea, ili mwisho wa siku uurithi ufalme wa Baba  na kuishi naye milele yote.

Ufahamu huu ndiyo unaomfanya Mtume Petro kusimama na kuuambia mkusanyiko ule wa Mitume juu ya wale waliolikubali neno la Mungu na kuokolewa nalo. Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini,” Mdo 15:7. Mtume Petro anavunja ukimya. Mara nyingi katika maisha yetu tunashindwa kuuona ukweli kama ulivyo tunaposafiri na kuishi katika nukuu za mila na desturi zetu ambazo nyingi zina mapungufu makubwa.

Ni kweli kwamba tupo kile tulicho kutokana na matokea ya historia yetu. Ni ukweli pia, tusipotoka katika mfuko huu kifikra ni vigumu kuuona ukweli kama ulivyo, na badala yake kuuona ukweli huo kama tulivyo. Wayahudi waliithamini na kuilinda sana historia yao, bila kujua kwamba Mungu hakuacha kujifunua kwao na wale waliowazunguka. Kama ilivyo kweli kwamba hakuna binadamu yeyote aliye hai kwa sababu yake mwenyewe bila Mungu, ni kwa namna hiyo uwepo wetu hauwezi kuwa na maana bila Mungu mwenyewe. Hivyo kwa namna ya pekee na mpango wa Mungu kama ulivyo, twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao,” Mdo 15:11. Mungu huyu hana ubaguzi kwa kile alichokiumba kwa sura na mfano wake. Kufanya hivyo ni kujibagua Yeye mwenyewe, na hivyo kuufifisha Umungu wake kwa vile alivyoviumba.

Wapendwa wana wa Mungu, ni ukweli huu unaomfanya Mtume Yakobo aliyekuwa Askofu wa Yerusalemu wakati ule wa Mtaguso huu kusimama na kutoa neno la mwisho kuhusu tatizo lile juu ya watu wa Mataifa waliomgeukia Mungu na wokovu wake. Naye anasema, Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu,” Mdo 15:19-20. Matendo haya ya kipagani hayana nafasi mbele ya Mungu aliye yote katika yote. Mungu ufurahi pale tunapozishika amri zake kwa uaminifu na haki. Na sheria yake ni UPENDO. Tujipende kama tulivyo na kuumbwa kwetu, na tuwapende wenzetu kama walivyoumbwa kwani wanaufunua uzuri wa Mungu, na tumpende Mungu kwani ndiye uzima wetu na yetu yote, umilele wote.

Ndugu yangu, neno UPENDO si geni kwako, na wala kwangu. Hii ndiyo amri anayotusisitiza Bwana wetu  Yesu Kristo anaposema, Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Ni furaha kubwa sana kuishi bila hatia. Kuishi bila hatia ni kuishi katika upendo wa Kristo. Kristo ni mwalimu wetu na mfano wetu halisi wa Upendo. Kama hujui fani ya Kristo katika somo la upendo, “utazame msalaba wake.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10


Tusali:-Ee Yesu Mwema, usituache. Amina