martes, 28 de febrero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU


ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU

Somo: Kumb 30:15-20

Zab: 1:1-4, 6

Injili: Lk 9:22-25

Nukuu:

Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19.

kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20

“Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23

Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24.

Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?” Lk 9:25

TAFAKARI: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.”

Wapendwa wana wa Mungu, maelekezo ya Mungu juu ya maagizo yake iwe amri au sheria, hayana lengo la kuukandamiza uhuru wetu, bali endapo tutakuwa ndani ya mwongozo huo hapo ndipo ulipo uhai na umilele wetu. Kwa maana nyingine, Mungu wetu siyo mfano wa Jitu katili ambalo lengo na kiini cha utendaji wake ni kwa ajili ya ubinafsi wake. Mungu alipenda na kupendezwa kumuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake si kwa kujifaidia mwenyewe, bali kwa sifa na utukufu wake. Uwepo wetu haumpunguzi wala kumwongezea Mungu chochote na hasa katika utukufu wake. Ila kuishi kadiri ya maagizo ya Mungu kuna faida kwetu ikiwa ni kuishi katika Amani ya kweli, na mwisho wa maisha haya hapa duniani tuwe na maisha ya milele pamoja naye.

Hata pamoja na nia njema hii, Mungu hatushurutishi kumtii ili tufaidike na utukufu wake, ila kwa kumfuata kwa hiari bila kuburuzwa ni njia mojawapo ya kufunuliwa utukufu wake. Hivyo leo ni hiari yako na yangu kuchagua uzima au umauti. “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki,” Kumb 30:15-16. Ndugu yangu, Mungu tu ndiye apaswa kuabudiwa kuliko kwa kweli na haki. Kinyume cha hapo ni balaa tupu, Kumb 30:18. Ni katika ukweli huu kwamba “kujisalimisha” kwa Mungu ndiyo njia pekee na sahihi ya kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kurudi kwake mbinguni. Kujisalimisha huku kwa hiari ndiko Yesu anakosema “kuikana nafsi.” “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24. Ingawa uhai na umauti kuwa sehemu ya ubinadamu wetu, ipo nafasi kubwa ya umilele kama wewe na mimi tutaamua vyema hatma ya maisha yetu kwa kujisalimisha huko kuliko kwa hiari. Naye Mungu anasema, “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19.

Wapendwa wana wa Mungu, uzima wetu upo pale tunapozishika amri za Mungu siyo kwa woga mbali kwa kuzipenda kwani mwisho wake ni umilele. “Kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20. Hivyo tafsiri ya sheria ya Bwana siyo teso bali ni njia ya kuyajua mapenzi yake kwako. “Heri walio kamili njia zao, Waendao katika sheria ya Bwana,” Zab 119:1

Kwa maana hiyo, ni lazima nichague kumtii Mungu katika Imani. Kila wakati unapoamini hekima ya Mungu na kufanya kila analosema, hata pale unapokuwa huelewi, unakuza urafiki wako na Mungu. Mara nyingi hatufikiri utii kama sifa ya urafiki na Mungu wa sababu ya mausiano yasiyo ya afya kati yetu na mzazi, mkubwa wa kazi, na hata majirani zetu. Lakini Yesu aliweka wazi kwamba utii ni kigezo cha uhusiano na Mungu. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo,” Yoh 15:14. Sisi ni marafiki na Mungu, lakini siyo sawa na Yeye. Yeye ni kiongozi wetu atupendaye, na tunamfuata. Tunamtii Mungu, si kama wajibu au kwa hofu au kwa kushurutishwa, bali kwa sababu tunampenda na tunaamini kwamba anajua kile kilicho bora kwetu. Tunataka kumfuata Kristo kwa shukrani kwa yote aliyotufanyia, na tunapomfuata kwa karibu, ndipo urafiki wetu naye unakuwa wa kina zaidi.

Wasioamini mara nyingi hudhani kwamba Wakristo hutii kwa sababu ni wajibu, au kuogopa lawama, au kuogopa hukumu, lakini ukweli ni kinyume cha hayo. Kwa sababu tumesamehewa na kuwekwa huru, tunatii kwa upendo, na utii wetu hutuletea furaha kubwa! Yesu anasema, “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe,” Yoh 15:9-11.

Angalia jinsi ambavyo Yesu anatutazamia kufanya yale tu aliyotenda kwa Baba yake. Uhusiano wake na Baba yake ni kielelezo cha uhusiano wetu naye. Yesu alifanya chochote Baba alichomwagiza kufanya, kwa upendo. Urafiki wa kweli si wa kukaa tu, bali ni wa vitendo. Yesu anapotuagiza kuwapenda wengine, kusaidia wahitaji, kuwagawia wengine mali zetu, kuwa na maisha safi, kusamehe, na kuwaleta wengine kwake, upendo hutuchochea kutii mara moja. Mara nyingi tunapewa changamoto ya kumfanyia Mungu “mambo makubwa.” Ni dhahiri kwamba Mungu anafurahishwa zaidi tunapotenda mambo madogo madogo kwa ajili yake kutokana na utii wa upendo. Yawezekana huwa hayaonekani kwa wengine, lakini Mungu anayaona na kuyahesabu kuwa matendo ya kuabudu.

Nafasi kubwa inaweza kutokea mara moja katika maisha, lakini nafasi ndogo ndogo zinatuzunguka kila siku. Hata katika matendo madogo kama vile kusema kweli, kuonyesha wema, kuwatia moyo wengine, tunaleta tabasamu katika uso wa Mungu. Mungu anathamini matendo rahisi tu ya utii kuliko sala zetu, sifa na sadaka. “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu,” 1Sam 15:22.

Yesu alianza huduma yake ya hadharani katika umri wa miaka thelathini kwa kubatizwa na Yohane. Katika tukio hilo Mungu alizungumza kuto mbinguni; “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye,” Mt 3:17. Je, Yesu alikuwa anafanya nini kwa miaka thelathini ambacho kilimfurahisha Mungu? Maandiko Matakatifu hayasemi kitu kuhusu miaka hiyo iliyojificha, isipokuwa kwa maneno machache kutoka Mwinjili Luka, kwamba “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake,” Lk 2:51. Miaka thelathini ya kumpendeza Mungu ilijumlishwa katika maneno: “naye alikuwa akiwatii.” 

Hivyo wapendwa katika Kristo, kama tuonavyo masomo yetu ya leo yanatuelekeza kufanya maamuzi ya kweli kuhusu maisha yetu na kumfuata Kristo. Je, Yesu anasema nini juu ya AMRI? Yesu yupo wazi kabisa kuhusu amri na mahusiano yake na umilele. Amri ni ‘Upendo’ ambao kwa kupitia Yeye, yaani Kristo, upendo wa Mungu Baba ni dhahiri kwetu. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Hivyo kumpenda Kristo na Mungu Baba ni kuishika amri hii ya Mapendo. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Hivyo mara zote yanipasa mimi na wewe nimwone Kristo kwa yeyote yule nitakaye kutana naye bila kujali itikadi zetu za maisha, familia zetu, koo zetu, makabila yetu na utaifa wetu.

Wapendwa wana wa Mungu, kumtambua Kristo katika maana ya kuwa na amri zake Kristo na kuzishika ni kumpenda Kristo na huko ndiko kupendwa na Mungu Baba. Hili ndilo dhihirisho la Kristo kwetu, yaani, kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Naye Yesu anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Ndugu yangu, wewe na mimi tu wafuasi wa Kristo kwa kuzishika amri zake na huko ndiko kukaa katika pendo la Kristo. “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Licha kwamba hapa Yesu katumia muda mwingi kuelezea amri, ukweli ni huu anaousema kuhusu amri; “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Sadaka ya Yesu pale msalabani yanipasa ihakisi na isadifiwe na kutukuzwa daima kwa kupendana sisi kwa sisi. Tusipofanya hivyo, ni kwamba tunaendelea kumsulubisha Yesu pale msalabani.

Kati ya mtihani mgumu wa maisha ni kuamua kuacha jambo fulani ulilolizoea na kuanza njia nyingine. Hapa ndipo wengi hushindwa. Mara nyingi tunajawa hofu ya sintofahamu ya mambo yajayo na tusiyo yajua. Ila kama kweli tunataka kuwa karibu na Mungu, na kuokoa nafsi zetu yatupasa kufanya maamuzi. Maamuzi ye yote yale katika maisha yana gharama zake. Na uamuzi utakaochukua lazima utapimwa. Wengi watakushangaa na hata kukucheka. Wala usihofu kwa sababu duniani hapa ni mahali tu pa kujiandaa kwa ajili ya umilele.

Somo la kwanza kwa mantiki hiyo, linatupa angalisho; kuchagua kati ya kifo au uhai. Uzuri na utamu wa maisha haya ya leo na sasa unatutia upofu wa kuona uzuri wa maisha ya umilele. Jambo hilo Yesu analiongelea katika mfumo wa msalaba. Tusipokuwa tayari kujikana, kuchukua misalaba yetu, na kumfuata, hatufai kuwa wanafunzi wake. “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23.

Jambo hili la maanisha nini?

Kuikana nafsi ni tendo la kuvua mwelekeo na mvuto wa yale uyapendayo na yasiyo na tija ukilinganisha na maisha ya umilele. Na maisha yasiyo na tija ni pamoja  na "ponda mali kifo chaja." Ni maisha ya kutokuwa na hofu ya Mungu. Ni maisha ya kujipenda kupita kiasi na kujihurumia. Ni maisha ya kuukataa ubinadamu wako na mipaka yake na kujiona mungu mtu. Huku ni kutoikana nafsi.

Kuubeba msalaba ni kukubali kuongozwa. Ni kukubali mapungufu yako kama binadamu ili iwe changamoto kwako kuelekea ukamilifu. Ni kujipokea. Ni hali ya uitaji wa neema ya Mungu. Ni hatua muhimu ya awali kuanza kukua kiroho. Ni kukubali kujiachia mikononi mwa Mungu na kumtegemea yeye tu. Ni kuwa na imani juu ya Mungu ingawa mapungufu yapo kama binadamu.

Kumfuata Yesu, ni kumfanya Yesu kuwa njia, na ukweli, na ulizi, Yoh 14:6. Yesu ni njia kuelekea uzima wa milele. Hakuna njia nyingine ndugu yangu. Na njia aliyochagua Yesu ni msalaba. Nasi kama wafuasi wake, msalaba haukwepeki. Yesu ni ukweli. Ukweli huu ndio utakao tuweka huru, Yoh 8:32. Yesu Kristo ndiyo uzima wetu. Mwili na damu yake Yesu ni uzima na uhai kwetu, Yoh 6:54.

Ndugu yangu, wakati wa kukata shauri ni sasa na kumrudia Mungu. Kishawishi kikubwa ni kudhani kuwa muda bado upo. Linalowezekana leo, lisingoje kesho.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:4, 10

Tusali:-Ee Yesu na Ngome yangu, nijalie neema ili niweza kujinasua katika vifungo vyangu vya kimwili na kiroho. Amina

 

lunes, 27 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMATANO YA MAJIVU


JUMATANO YA MAJIVU

MWANZO WA KIPINDI CHA KWARESMA

Soma I: Yoe 2:12-18

Zab: 50:3-4, 5-6ab, 12-14, 17

Somo II: 2Kor 5:20-6:2

Injili: Mt 6:1-6, 16-18

Nukuu:

"Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana,  Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya." Yoe 2:12-13

"Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye," 2Kor 5:20

"Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni," Mt 6:1

TAFAKARI: “Mwanzo wa safari ya kujitakasa Jangwani.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibuni kwa tafakari hii tunapoanza safari yetu ya kujitakasa huko jangwani. Leo Mama Kanisa anaanza safari hiyo rasmi na wana wake kwa kujitakatifuza. Safari hii itatuchukua siku 40-"Quadragesima," ambayo hutambulika kama "Kwaresma."

Kwa nini ni siku 40?

Maana ya awali kabisa, 40 huwakilisha muda wa kutosha. Ni muda wa kutosha kwa Mungu, na kwa mwanadamu akiutumia vizuri ataufikia utakatifu wake.

Namba 40 imetumika sana kuelezea "kutosha" kitu au "kikomo" cha kitu, hasa pale binadamu anapohusika kwa mwongozo wake Mungu na kumrudia baada ya maasi yasababishwayo na dhambi.

Taifa la Israel liliteseka vya kutosha jangwani kwa miaka 40. "Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako," Kumb 29:5

Wakati wa Nuhu "mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku," Mwa 7:12. "Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku," Kut 24:18. Ndugu yangu katika agano la kale yapo matukio zaidi 140 yenye uhusiano wa muda wa kutosha yaani namba hiyo 40.

Ikiwa kielelezo chetu ni Yesu Kristo, Kwaresma yetu ina mwono wa mfungo wa Yesu mwenyewe jangwani kwa siku arobaini, mchana na usiku. "Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa," Mt 4:2.

Safari yetu leo inaanza kwa kupakwa majivu kwenye paji la uso ikiashiria mambo makuu mawili; kwanza ubinadamu wetu, ikimaanisha kuwa yatupasa kuwa wanyenyekevu. Pili, sisi tu mavumbi na mavumbini tutarudi. Ni ishara ya toba na majuto. Ni mabadiliko ya ndani yanayotuweka karibu na Mungu na baraka zake.

Somo letu la kwanza latupa picha hiyo ya mfungo. Mungu yupo tayari kuanza upya nasi pale tu, tutakapomjeukia na kuacha njia zetu mbaya. Huruma ya Mungu kwetu inategemea mabadiliko yetu kumwelekea yeye. Mungu yupo tayari kughairi adhabu yake tunapomwelekea. "Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana,  Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya." Yoe 2:12-13. Je, ndugu yangu upo tayari kuanza upya na Mungu? Wakati ndiyo sasa.

Ni mambo gani ya kufanya katika safari hii?

Yapo mambo makuu matatu ya kufanya kadiri ya injili ya leo. Jambo la kwanza, kwaresma yamaanisha ni muda wa kusali na kumrudia Mungu. Kusali huku si kwa kupayuka payuka, bali kwa kuzama zaidi ndani ya nafsi zetu. Kikomo chake isiwe tu pasaka, bali maisha yetu yote. Na mapenzi ya Mungu kwetu katika Kristo ni haya, “Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu,” 1The 5:15-18 

Silaha ya mkristo yeyote ni sala. Kama kweli tunaitaji ulinzi wa Mungu, sala inapaswa kuwa tabia yetu. Kuwa mtu wa sala. Sala ya kweli na ya watakatifu ni hali ya kuomba ukiwa na imani kuwa ushapata hata kama bado.

Kusali huku pia kulenge kung'oa "dhambi Dola." Mfano: Serikali ya Tanzania inaongozwa na dola ya Chama Cha Mapinduzi-CCM. Chama hiki ndicho kilichounda serikali. CCM ndiyo dola tawala. Katika mfumo wa maisha ya kiroho, kila mmoja wetu anayo "dhambi dola," ikimaanisha dhambi tawala. Dhambi hii ni ile ambayo kila mara unajikuta ushadondoka huko na inakupelekea kuwa kero kwani kila mara unaiungama. Weka mikakati na Mungu kuiacha kwa msaada wake-"by the Will Power of God-WPG" Hili ni lengo kubwa na mojawapo ya sala hasa kipindi hiki cha Kwaresma.

Pili, ni kufunga. Kufunga hapa kwa maanisha kujinyima kwa ajili ya faida yako na wengine. Jambo hili ni kwa chochote kile utakacho amua kufanya. Yatupasa pia kulenga katika mambo yale yanayogusa mfumo wa maisha yako ya kila siku. Mara nyingi watu wengi hulenga kujinyima kula. Si mbaya! Ila unalifanya hilo kwa makusudio ya nini? Faida ya kwanza ni kwa afya yako. Jambo la pili na la maana liwe kwa ajili ya waitaji. Usianze kuwatafuta kwa kwenda mbali. Anza na familia yako tukijua kwamba ukarimu huanza nyumbani. Itazame jumuiya yako. Wapo wahitaji wengi sana. Tazama majirani zako wasio ndani ya jumuiya yako. Na mwisho litazame Kanisa lako; iwe kigango au parokia. Naye Yesu anatuambia, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35.

Tatu, Kwaresma yetu inalenga katika swala zima la kutoa sadaka. Hapa yakupasa kujifunza namna ya kutoa sadaka. Kwanza si kwa kujionyesha bali kwa kutambua wajibu wako na kumtolea Mungu mastahili yake. Yote ni mali ya Mungu. “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Na Mungu ndiye msingi wa vyote. “Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake,” Zab 89:1. Hivyo ndugu yangu, tunamtolea Mungu kama shukrani kwa yale anayotukirimia. Sadaka yako iwe kamilifu na yenye kumpendeza Mungu. “Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu,” Lk 11:41. Usimtolee Mungu makapi. Hapa imaanishe sadaka halali. Ukiangalia sh 50 hadi 200 kwa mfano, hutaona maandishi haya: "fedha halali kwa malipo ya sh 50, 100, au 200." Ila kwa upande wa sh 500 hadi 10000 maandishi hayo yapo. Je, wewe unayetoa kila mara sh. 50 tu kama sadaka yako, ni pesa halali hiyo? TAFAKARI!

Ndugu yangu, tukiyafanya hayo na kuyaishi, mfungo wetu wa siku 40-Kwaresma, utakuwa na maana sana. Na pasaka yetu itamaanisha ukombozi wa kweli, wa mwili na Roho. Hiyo ndiyo maana halisi ya sadaka ya Yesu pale msalabani. Yeye aliyekubali kuchukua dhambi zetu ingawa hakuwa na dhambi. Yeye aliyekubali kuwa masikini, ili wewe na mimi tuwe matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ni upendo wa ajabu wa Mungu. Safarí imeanza basi tusikubali kubaki nyuma.

Tumsifu Yesu Kristo!

"Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye," 2Kor 5:20

Tusali:-Ee Yesu uliye dharauliwa kwa ajili ya dhambi zangu niwezeshe nifanye toba ya kweli. Amina

domingo, 26 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 8 YA MWAKA-I

Somo: YbS 35:1-15

Zab: 50:5-6, 7-8, 14, 23.

Injili: Mk 10:28-31

Nukuu:

“Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani,” YbS 35:1

“Amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora, naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabibu ya kushukuru,” YbS 35:2

“Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30.

Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31. 

TAFAKARI: “Mpe Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha huongozwa na mfumo au utaratibu fulani kubaliwa pamoja ulio rasmi, au pokeo rasmi kadiri ya mila na desturi fulani za watu. Taifa teule la wana wa Mungu-wana wa Israeli-hawakuwa nje ya ukweli huu. Na “Mwenye kuishika torati ndiye azidishaye matoleo; mwenye kuziangalia amri ndiye aitoaye kafara ya amani,” YbS 35:1. Maisha ya wetu huakisi tunu za maisha hayo, ambayo hutupa jibu la “kwa nini wanafanya kama wanavyofanya.” Mambo haya kwa tafsiri nyingine ndiyo mang’amuzi ya maisha. Na hili ni wazi kwamba, “amlipaye mwenzake hisani yake hutoa sadaka ya unga bora, naye atoaye sadaka kwake maskini hutoa dhabibu ya kushukuru,” YbS 35:2.

Mang’amuzi ya maisha ndiyo msingi wa hekima n abusara za watu katika utofauti wao, na jamii katika upekee wake. Na hitimisho la hayo yote ni mtazamo ule wa pamoja wenye hafiki moja na mwono chanya, yaani, “kuuacha uovu kwampendeza Bwana, na kujitenga na udhalimu ni kipatanisho,” YbS 35:3. Mtazamo pamoja huu hujenga mwelekeo wenye tafsiri pamoja. Hapa ndipo tunapoona umuhimu na swala zima la utaratibu katika kutenda, kutathimini, kuwajibika, na utoaji wa haki pale inapo mwinywa. Mwelekeo huu wa maisha una tahadhari zake pia. Hivyo wewe na mimi wenye hofu ya Mungu ni jambo jema na lenye busara kutojitokeleza “mbele za Bwana mikono mitupu, maana sharti hayo yote yatendeke kwa ajili ya amri. Na toleo lake mwenye haki lina kibali madhabahuni, na harufu tamu yake yafika mbele zake Aliye juu,” YbS 35:4-5.

Maisha ya mwanadamu huongozwa kwa lengo au malengo fulani kwa sababu hakuna yeyote aliye katika ulimwengu huu pasipo lengo. Kila chenye pumzi na kisicho na pumzi ni mpango wa Mungu hapo kilipo. Ni Mungu tu mwenye hatma ya kitu hicho, na mwenye mamlaka ya kukihesabia haki chochote kile, chenye pumzi na kisicho na pumzi. Hivyo kama tendo la shukrani kwa Muumba wako wewe ulijaliwa pumzi, “dhabihu ya mwenye haki yakubalikana, wala kumbukumbu lake halisahauliki. Umheshimu Bwana kwa jicho la ukarimu, wala usimtolee malimbuko ya kazi za mikono yako kwa ubahili,” YbS 35:6-7. Yote yale tuyatoayo mbele ya Mungu hayaongezi wala kupunguza ukuu wa Mungu kwa sababu, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1.

Kumbe tufanyacho wewe na mimi ni tunapotoa shukrani kwa Mungu ni kusadifu uwepo wake, na muungano wake nasi. Ni kusema, “bila wewe Mungu yote ndani yaangu hayana maana.” Hivyo, “kwa kila kitolewacho uonyeshe ukunjufu wa uso, hata sehemu ya kumi uiweke wakfu kwa changamko,” YbS 35:8. Na kwa mantiki hiyo yatupasa wewe na mimi kumpa “Mungu kama alivyokupa wewe, na kama mkono wako ulivyopata, utoe kwa ukarimu,” YbS 35:9.

Ndugu yangu, ikiwa hakuna yeyote kati yetu katika ulimwengu huu yupo kwa bahati mbaya, na kila kilichopo cha ufunua utukufu wa Mungu na furaha yake, masikini tuwaonao katika mizania ya kibinadamu nao wana mwakilisha Mungu kama wafanyavyo matajiri na wenye uwezo mbalimbali katika kipimo hicho hicho cha kibinadamu. Hivyo, “amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye ni nani awezaye kulipa isipokuwa ni Yeye; kwa kuwa Bwana hulipa, naye atakulipa wewe mara saba,” YbS 35:10. Utofauti kimaisha, yaani, kati ya aliye nacho na asye nacho, siyo mizania ya Muumba wetu, na wala Yeye hatuoni katika utofauti huo. Ni jukumu lako na langu kuondoa tofauti hiyo kwa sababu hali hiyo ipo ndani ya uwezo wetu, na hakuna aliye tajiri katika ulimwengu huu ambao amekuja nao. Hivyo hakuna njia ya ufupisho katika hili. Na hapa hakuna rushwa. “Usidhanie kuwa unaweza kutoa rushwa, kwa maana Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Yeye hazipokei; wala usiwaze moyoni kutoa dhabihu ya jeuri, kwa kuwa Bwana ndiye mhukumu wala hakijali cheo cha mtu,” YbS 35:11-12.

Ndugu yangu, elewa kwamba unapofanya jambo hili, yaani, kurejesha usawa na utu kati ya jamii ile unayoishi, warejesha utukufu na furaha ile ilikuwa sababu na kusudi la kuumbwa kwetu, Mwa 1:27. Hivyo Mungu, “hatamkubali yeyote juu ya maskini, naye ataisikiliza sala yake aliyedhulumiwa. Hatayadharau kamwe malalamiko ya yatima, wala ya mjane amwelezapo habari zake,” YbS 35:13-14. Mungu wetu ni mtetezi mkubwa wa wanyonge na wanaodhulumiwa haki zao kwa sababu, ulimwengu huu haukuumbwa ukiwa, bali uliumbwa ili ukaliwe na watu, Isa 45:18. Na tunapoona maovu haya na hasa kwa wajane yakitokea katika jamii yetu leo swali ni hili: “Je, machozi ya majane hayachuruziki mashavuni mwake? Naye aziugulia taabu zake zilizoyatokeza,” YbS 35:15.

Wapendwa katika Kristo, Bwana wetu Yesu Kristo anakutaka wewe na mimi tusifanye marejesho, au malinganisho, na wala manung’uniko utoapo sadaka ya maisha yako kwake na kwa Injili, yaani, Habari Njema ya Wokovu wetu kwa watu wate. “Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Yesu Kristo kama alivyomwondolea mashaka Petro ndivyo hivyo hivyo anavyokuondolea mashaka wewe na mimi tutoapo sadaka ya maisha yetu kwa ajili yake na Injili. Hivyo licha ya kuyapata haya ya leo na sasa kadiri ya hitaji letu,  tuna hakika ya uzima wa milele ndani na katika Kristo.

Ndugu yangu, kujitoa sadaka ya maisha yako kwa ajili ya Kristo na Injili kwahitaji fadhila ya unyenyekevu. Hapa ndipo kwenye kushushwa na Kristo pale unapojipandisha mwenyewe na pasipo haki, na kupandishwa na Kristo pale unapojishusha kwa kumpa nafasi Kristo ndani ya maisha yako. Kwa maana hiyo, “wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31. Hii ndiyo changamoto kubwa katika maisha yetu ya kiroho.

Ukimruhusu Yesu Kristo ndani ya maisha yako uwe tayari kuyapokea yote kama alivyoyapokea Kristo hadi kuwambwa pale Msalabani. Utatemewa mate, utachekwa, watakushangaa, utakejeliwa, utazushiwa, utashangiliwa, utaonewa huruma, na mwisho utawambwa kama utimilifu wa sadaka ya maisha yako kwa Kristo na Injili. Haya ndiyo maisha ya utauwa. “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa,” 2Tim 3:12. Kwa maana nyingine hii ndiyo heri ile ya kuishi umasikini wa roho, Mt 5:3, kwa kumpa Yesu Kristo nafasi ndani ya maisha yako, na mwisho wa siku kuupata Ufalme wa Mbinguni. Ni kama asemavyo Mtume Paulo kwamba, “Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote,” 1Kor 15:19. Ni umasikini kwa kupungua ili Kristo Yesu apate nafasi ndani ya maisha yako, nawe uwe na furaha isiyo na kipimo. “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Wapendwa nani kama Yesu Kristo? Hakuna!

TumsifuYesu Kristo!

“Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza,” Mk 10:31.

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nifundishe njia yako. Amina

sábado, 25 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 8 YA MWAKA-I


JUMATATU WIKI YA 8 YA MWAKA-I

Somo: YbS 17:20-28

Zab: 32:1-2, 5, 6, 7

Injili: Mk 10:17-27

Nukuu:

“Kwake makosa yao hayakufichika, na dhambi zao zote zipo mbele zake,” YbS 17:20-21.

 “Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani,” YbS 17:27

“Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi Bwana,” YbS 17:28

“Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21

“Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27 

TAFAKARI: “Akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.”  

Wapendwa wana wa Mungu, ikiwa wewe ni Mkristo uliye hai ni vyema ukafahamu thamani ya Ukristo wako, yaani umekombolewa kwa Damu ya thamani kubwa sana, yaani Mwana-kondoo, Yesu Kristo. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hivyo maisha yako na yangu hapa duniani tunapaswa kuyasalimisha yote na kwa asilimia zote kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai. “Kwake makosa yao hayakufichika, na dhambi zao zote zipo mbele zake,” YbS 17:20-21. Tendo hili la kujisalimisha ndiko kuabudu kwenyewe kuliko hai na kwenye kumpendeza Mungu.

Kujiita Wakristo bili Kristo ni kupotea muda kabisa kwa sababu kwa kufanya hivyo maisha hayo hayana njia, kweli, uzima (tungali hapa duniani) na ufufuo (maisha ya uzima wa milele), Yoh 14:6. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, tungali hapa duniani wakuhimidiwa ni Mungu, na kwa njia ya pekee na ufunuo uliokamilika kwa Yeye aliyemwilishwa (Neno), Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa Kristo Yesu kuna Njia, Kweli, Uzima, na Ufufuo wa wafu. Kwake Yesu na kupitia kwake tunaheshabiwa haki na Mungu kwa wana na warithi wa ufalme wake Mungu. Na kwa namna hiyo, “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4. Ndugu yangu, tumaini yenye uzima lipo kwa Kristo Yesu, na siyo kwa kile tulicho au yale tunayoyamiliki hapa duniani. “Kwake Yeye sadaka za mtu ni kama pete ya muhuri, naye ataweka akiba ukarimu wa wanadamu kama mboni ya jicho,” YbS 17:22. Tungali hapa duniani tu waangalizi wa muda mfupi kwa yale tunayoyamiliki. Kwayo (tunayoyamiliki) kama yalivyo hayana umilele ingawa tuliyakuta na tutayaacha.

Hivyo wapendwa katika Kristo, yatupasa mimi na wewe kuyashinda majaribu tukiwa na ufahamu kwamba ‘maisha ni jaribu,’ na kulishinda jaribu ndipo kunakotupatia Imani yenye thamani kupita yote tuwezayo kuwa nayo. Vita vyetu vya kiimani kama anavyotufundisha ni kulishinda jaribu. Tokeo la kubebwa na ulimwengu wa vitu ni anguko kubwa la ‘uzuni.’ Furaha ya kweli ipo pale tunapoyasalimisha yote kwa Kristo Yesu. Kristo awe tegemeo na msukumu wa yote tuyafanyayo, na tumuone kwa wengine yale yote tuyafanyayo katika jamii tunayoishi. “Hatimaye atatokea na kuwapa thawabu, naye atawalipa waovu uovu wao juu ya vichwa vyao,” YbS 17:23. Lengo hapa siyo tu kuzishika au kuzifahamu amri za Mungu kama ndege yule ‘kasuku,’ bali amri hizo za Mungu zimulike uhai uliopo ndani yetu binafsi na wale wote tuliowekwa dhamana kwao ikiwa ni pamoja na wale wenye uhitaji wa pekee.

Ndugu yangu bila shaka, hii ndiyo sababu ya Yesu leo kwenye Injili kumuuliza yule Mtu aliyetaka kujua afanye nini ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu. Yesu anamuuliza, “Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako,” Mk 10:19. Kwa moyo wa ukunyufu na furaha Mtu yule anamjibu Yesu, “Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu,” Mk 10:20. Jibu hili linamfurahisha sana Yesu. Ila Bwana wetu Yesu Kristo hakuishia hapa tu. Yesu anakutaka wewe na mimi tufanye zaidi kwa ya yale ya kawaida (katika kupenda, kutenda, na hata kukopesha, Lk 6:32-34) kwani hayo hata waovu huyafanya. Hivyo “Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate,” Mk 10:21. Hapa ndipo penye utata na tatizo kubwa kwangu na kwako. Wengi wetu ni vigumu sana kujibadua katika ulimwengu wa vitu. Tupo tayari “kufa na tai shingoni” kuliko kuviachia vitu na kuwa huru: kifikra, kiutendaji, na kihuduma, ili kuwa huru kufanya tu yale yaliyo ndani yetu kadiri ya mpango wa Mungu. Ndugu yangu, Mungu wetu, “huwajalia wale watubuo kurudi, na wao wanaopotewa na saburi huwafariji,” YbS 17:24. Hili hutoweza kulifanya ikiwa utajiri na mali ndicho kielelezo cha maisha yako. Kwa kufanya hayo na kujishikilia kwa hayo hakuna fadhila ndani yake. “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu, na ndani yake hakuna fadhila,” Lk 6:35.

Hitaji hili la pili, yaani, ‘kufanya zaidi’ ili kujipatia fadhila linakuwa anguko na uzuni mkubwa kwa mtu yule aliyekuwa na hamasa kubwa sana ya kuurithi ufalme wa Mungu. “Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi,” Mk 10:22. Ndoto na furaha yake ya kuujua na kuurithi ufalme wa Mungu anakubali iyeyuke kwa sababu ya ulimwengu wa vitu. Ndugu yangu, leo hata ungekuwa na utajiri wa aina gani kuna mambo hutoweza kuyapata kwa utajiri wako huo hata kama bado tungali hapa duniani. Ngoja nikujuze machache; kwa utajiri na fedha ulizonazo waweza kuwa na marafiki wengi ila siyo wa kweli na watakatifu. Kwa fedha na mali ulizonazo waweza kujenga nyumba nzuri, ukawa na kitanda kizuri cha dhahabu (na chenye nakshi zote), ila huwezi kuununua uzingizi. Kwa fedha na mali ulizonazo leo hapa duniani unaweza kwenda kokote upendapo ila Mbinguni ni swala la kuhesabiwa haki na mastahili ya Mungu Mwenyewe.

Ndugu yangu, kwa fedha na mali ulizonazo leo waweza kununua chakula kizuri na chenye gharama, kinywaji kizuri na chenye gharama, ila hutoweza kununua hamu ya chakula hicho. Kwa fedha na mali ulizonazo waweza kuwanunua watu na kuwahonga watu, ili utimize hazma yako ya kuwa kile utakacho, ila hutoweza kumnunua Mungu wala kumrubuni. Mwisho wa siku Mungu atakudhihirishia kile kilichokuwa haki yako mbele ya watu wake uliowarubuni. Ayubu aliyepatwa na majanga makubwa katika maisha yake, na kupoteza yote aliyokuwa nayo, anatuambia hivi kuhusu mali na utajiri; “Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe,” Ayu 1:21. Utajiri wake na mali alizokuwa nazo haikuwa sababu ya kumkufuru Mungu hata pale ilipoondolewa yote pasipo yeye-Ayubu, kwenda kinyume na matakwa ya Mungu.  Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu,” Ayu 1:22. Kwa nini basi mimi na wewe twaulinganisha au kuufananisha uhai wetu na mali tulizonazo na kumkufuru Mungu? Mali tunazoongelea hapa ni zote ikiwa pia zile zisizoshikika kama vipaji na karama alizokupa Mungu. Mbona basi twavimba vichwa na kujisahau pale tunapofanikiwa kutokana na zawadi aliyotupa Mungu ikiwa ni pamoja na ufahamu wa kiwango cha juu? Ndugu yangu, hayo yote si mali yako. Umekopeshwa au kupewa kwa muda tu, na ukiwa navyo ni kwa faida ya wengine. Huku ndiko kushirikishana utajiri wa Mungu na Utukufu wake. Mali yako halali ni dhambi zako. “Basi umrudie Bwana na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo,” YbS 17:25. Hii ndiyo njia salama ya kuurudisha uhusiano wenye siha kati yako na Muumba wako.

Hivyo ni vigumu sana, tena sana, kuingia katika Ufalme wa Mungu tukishikamana na kulandana na vitu na katika fursa hiyo kutokumpa Mungu nafasi na stahili zake. “Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” Mk 10:23. Kushikamana huko na vitu hakutupi heri yoyote, na badala yake ni anguko kubwa. Jambo la kufanya ni hili: “Umgeukie tena Yeye aliye juu, uyageue maovu, uyakirihi yaliyo machukizo,” YbS 17:26. Bila ukiri huu ni kupotea muda ilhali maisha yetu hapa duniani ni jukumu la muda mfupi tu.

Ndugu yangu, ni wale tu walio masikini wa roho (wenye nafasi ya Mungu ndani ya mioyo yao, Mt 5:3, na wasiokata tamaa wanapoudhiwa kwa kutenda haki kwa wote, Mt 5:10, ndio watakaourithi Ufalme wa Mbinguni. “Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? Ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani,” YbS 17:27. Na kwa sababu hiyo, kama washikamana na ulimwengu huu wa vitu na kutokumpa Mungu nafasi, “Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mk 10:25. Fundisho hili lenye kweli yote linakuwa mshangao mkubwa kwa wanafunzi wa Yesu, yaani, wale Thenashara. “Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu,” Mk 10:27. Hivyo, ukijiachia kwa Mungu bila kujibakiza yote hufanyika kwako kadiri ya mapenzi yake Mungu na hitaji lako na wale wanaokuzunguka.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi Bwana,” YbS 17:28

Tusali:-Ee Yesu, kwa Upendo wako tujalie Neema na Hekima ya kufahamu yale tunayohitaji ili kwa namna hiyo hiyo tuweze kufahamu hitaji au mahitaji ya wengine.

viernes, 24 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 8 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 8 YA MWAKA-A

Somo I: Isa 49:14-15

Zab: 62:2-3, 6-7, 8-9ab

Somo II: 1Kor 4:1-5

Injili: Mt 6:24-34

Nukuu

“Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

“Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1

Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2

Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24

TAFAKARI:Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ahadi ya Mungu kwetu ni kutokutusahau katika hali zote hata kama kibinadamu jambo hilo linawezekana. Mungu hawezi kutusaha. “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe,” Isa 49:15

Maisha yetu ni mpango wa Mungu na kwa malengo ya Mungu. Mpango huu unarahisishwa kwa uwepo wa Mwanaye Yesu Kristo, ambaye hajifanyii mambo yake pasipo Mungu Baba aliyempeleka. “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka,” Yoh 5:30

Ni kwa mtazamo huo, Yesu katika Injili ya leo anatupa angalizo na kusema, “hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Hata ukifanikiwa ni kwa muda mfupi tu. Je, kwa nini twapaswa kumtumikia bwana mmoja? Sababu ya wazi na ya moja kwa moja ni kuondoa ile roho iliyojigawa vipande vipande. Mfano; kama umepata mialiko miwili ya harusi inayofanyika muda ule ule na siku ile ile, yakupasa kuchagua moja wapo utakayokwenda hata kama zote zina uzuri au zimetofautiana. Kuchagua huku ndiko Yesu anapotushauri kuutafuta kwanza ufalme wa Mbinguni, na kuondoa roho ya kujigawa vipande vipande. Naye Yesu anasema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33. Ndugu yangu, unaloneno zaidi ya ukweli huu wa Bwana wetu Yesu Kristo?

Ni kweli isiyo shaka kwamba ukishaingia katika mfumo huu, na mtazamo huu wa fundisho hili ya Yesu, kuutafuta ufalme wa mbinguni kwanza, huwezi kupata “presa”-shinikizo la damu unapowaona watu wakipigana vibega kwa kumwangaikia mfalme tumbo na utajiri wake. Kristo anapokuwa katikati ya yote, yeye atakupatia kadiri ya mahitaji yako na kwa wakati wake. “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mt 6:34. Hata hivyo hapa Kristo Yesu hamaanishi tujikalie tu bila kujishughulisha na kufanya chochote kuhusu maisha yetu. Ndugu yangu yatupasa kumuishi Kristo leo na sasa katika yale yote yampendezayo. Mungu kamwe habariki utupu. Kumbuka ishara ile ya kwanza alioyofanya Yesu kule Kana, Yoh 2:1-11. Ingawa kesho inasikika akilini mwetu, tuelewe kesho hiyo ipo mikono mwa Mungu katika uhalisia wake.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, kama tunajua kwamba hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake, Rum 14:7, maisha yetu bila Kristo yatakuwa na walakini mkubwa. “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1. Kama tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu, maisha yako hapa duniani na kadiri ya wito wako ni dhamana kubwa kwa sababu yeshathaminishwa kwa damu ya Yesu pale Msalabani. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, watambua thamani ya maisha yako kama mfuasi wa Kristo?

Wapendwa wana wa Mungu, thamani ya Ukristo wako itategemea sana na namna unavyo mwakilisha Kristo kama wakili wake katika kweli na uaminifu. Ukristo wako usibaki katika jina tu, bali imani ya kweli ndani yako, na Kristo akiwa ndiye kielelezo chako katika yote. Na “hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2. Ni kuwa mwaminifu katika kuifuata njia yake, yaani, kuubeba msalaba wako kwa uaminifu bila kumsaliti Kristo. Ni kuiishi kweli kadiri ya mafundisho yake Kristo, na zaidi amri ile ya upendo.

Ukipenda kama alivyopenda Kristo utafanya yote yampendezaye Mungu. Na mwisho ni kuuishi uzima wa kweli kwa kushiriki Masakramenti katika hali ya usafi wa moyo, na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hali hii ya usafi wa moyo ndiyo impelekeayo Mtume Paulo kusema kwamba, “Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu,” 1Kor 4:3. Mara zote tuongozwe na dhamiri safi na yenye hofu ya Mungu.Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana,” 1Kor 4:4.

Kuujua wajibu wako na kuutimiza kadiri ya takwa lake na kwa upendo ndiko kutakapo kuhesabia haki. “Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu,” 1Kor 4:5. Ndugu yangu, usichoke kutimiza wajibu wako kwa upendo. Hakuna aliyefilisika kwa kupenda na kutoa kwa upendo.

Bwana na Bibi Baraka Mfaume baada ya kutembea umbali mrefu wakiwa wametoka kuhemea, waliliona genge upande wao wa kushoto palipokuwa wanauza machungwa. Basi Bibi Baraka alinunu machungwa manne, yaani, mawili kwa ajili yake, na mawili  kwa ajili ya mmewe. Kwa kiu na njaa ile walioyokuwa nayo, Baba Baraka Mfaume aliyashambulia machungwa yake mawili bila huruma huku wakiendelea na safari yao kuelekea nyumbani akewe akiwa amebeba mkoba wake na ule wa mmewe.

Mara walipo fika nyumbani walipokelewa kwa furaha na watoto wao John na Maria. Mara Bibi Baraka aliomba aletwewe kisu, na mara akayatoa machungwa yake mawili kwenye mkoba wake. Akalipasua chungwa moja katikkati akampa kipande Maria, na kingine akampa John. Huku macho yakiwa yanamtoka Baba Baraka kama mjusi aliyebanwa na mlango, Mkewe akapasua chungwa la pili katikati kisha akampa mmewe kipande kimoja, naye akabaki na kipande kilichobaki. Huu ndio upendo wa Mama wenye kujali na kuwajibika aliousema Nabii Isaya katika somo letu la kwanza. Hata hivyo, upendo wa Mungu kwetu ni zaidi ya mfano wa upendo huu wa Mama. Mungu anatupenda upeo upeo, Yoh 12:24. Huyu ni Mungu asiye tusahau kamwe iwe tunapomtegemea au kumsahau katika hali yoyote ile, Isa 49:15. Akina Baba na wale wote wasio na upendo kama mama mpo?

Tumsifu Yesu Kristo!

Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:33

Tusali:- Ee Yesu, uwe kitoshelezo chetu. Amina

jueves, 23 de febrero de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 7 YA MWAKA-I


JUMAMOSI WIKI YA 7 YA MWAKA-I

Somo: YbS 17:1-13

Zab: 103:13-14, 15-16, 17-18a

Injili: Mk 10:13-16

Nukuu:

“Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha,” Ybs 17:1

“Akawapa wanadamu siku kwa idadi, na muhula ulioamriwa, akawapa amri juu ya vitu vilivyomo,” YbS 17:2

 “Akawajaza maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu,” YbS 17:6

“Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14

Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” Mk 10:15 

TAFAKARI: “Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo ni kujiachia pasipo shaka kwa Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai katika hali ya unyenyekevu, Imani, na Upendo. Ni kuungana na Kristo na kushiriki neema zake kama watoto wadogo kwa wazazi, walezi, au walimu wao. Ni kuipokea Habari njema ya wokovu na mafumbo yake yote. Ni kuambatana na Kristo na kumuishi pasipo mizizi ya dhamba kama: kiburi, chuki, hisi mbaya na kadhalika. Kama watoto, hatupaswi kuwa na mashaka na lile atufundishalo Kristo wala lile atuelekezalo kulifanya. Hivyo, “Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa,” Mk 10:15. Unyenyekevu na upole ndiyo siri ya kuupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo.

Kwa hali hii, watoto wadogo wanauishi wongofu wa kweli kwa sababu hawana walipojishikilia kama sehemu ya usalama wao zaidi ya wazazi wao, au walezi wao, au walimu wao. Kwa maana hiyo Yesu anasema, “Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni,” Mt 18:3. Wongofu huu unatutaka mara zote kulenga lililo kamilifu licha ya kwamba udhaifu upo. Ni kuyatafuta yale yaliyo juu kule Kristo alipo. Ni kuishi maisha mapya ya ufufuko. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.” Kol 3:1. Ni kuamini yapo maisha ya milele mara baada ya maisha ya hapa duniani ambayo ni jukumu la muda mfupi.

Wapendwa katika Kristo, na huu ndio mwaliko wa wale wote wanaoishi kama watoto wadogo katika hali ya Unyenyekevu, Upole, Upendo na Imani kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao,” Mk 10:14. Kuwazuia watoto wadogo kwa weza maanisha hali ile ya kupandikizwa hofu na kuwa mbali na upendo wa Mungu Baba. Na inawezekana pia kutokana na mitazamo yetu, mila na desturi zetu zinatufanya kuwa mbali na upendo huu wa Mungu Baba. Milango ya Neema na Huruma ya kweli imefunguliwa kwa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Hakuna sababu ya kuwa na hofu ndani na katika Kristo Yesu. Kwake Kristo kuna baraka muda wote, Mk 10:16. Ndugu yangu uhitaji baraka kutoka kwa Kristo Yesu?

Kuzipata baraka na neema za Mungu ni pale tu wewe na mimi tunapoukubali udogo wetu. Kuukubali udogo wako hakumaanishi unyonge au udhaifu, bali hali hiyo husema zaidi kile ulicho, na utayari wa kujipokea katika mafanikio yako, na mapungufu yako. Hivyo somo letu la kwanza leo linatupeleka katika tafakari hii ya kina kuhusu uhasili wetu, kwamba, “Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha,” Ybs 17:1. Ndugu yangu unaye safari nami katika tafakri hii, ni vyema ukaelewa jambo hili muhimu katika maisha yako, kwamba pamoja na ufahari alikuwa nao mwanadamu kwa kila hali, nafsi hiyo lazima ionje mauti. Na hii ndiyo maana ya “kurudi mavumbini.” Ikiwa huu ndio ukweli, salama yako na yangu ni kuishi na kutenda katika haki kwa maana, “hazina za uovu hazifaidii kitu, Bali haki huokoa na mauti.” Mit 10:2. Na “mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu: Bali haki huokoa na mauti,” Mit 11:4.

Ndugu yangu, ulimwenguni hapa siyo mahali petu pakudumu. Ulimwengu huu pamoja na mazuri na mabaya yake, ni sehemu tu ya maandalizi ya umilele. Hivyo, Mungu, “akawapa wanadamu siku kwa idadi, na muhula ulioamriwa, akawapa amri juu ya vitu vilivyomo,” YbS 17:2. Mali, uwezo, ufahari, nguvu na mamlaka ni swala la wakati na muda mfupi tu. Kwaya kama yalivyo au ilivyo hakuna umilele. Ukitumika vyema katika hayo upo uwezekano wa kuurithi ufalme wa Mbinguni, na kinyume chake ndiyo kilio na kusaga mengo, Mt 13:42.

Hukumu ya mwisho inamuhusu kila mmoja wetu mwenye pumzi leo na sasa. Nalisema hili kwa sababu kati yetu hakuna anayeishi kwa nguvu zake mwenyewe zaidi ya huruma na neema ya Mungu, Rum 14:7. Hivyo katika uumbaji wetu wanadamu na kwa namna ya pekee kabisa, Mungu “akawavika nguvu kama Yeye mwenyewe, na kuwafanya kwa mfano wake,” YbS 17:3, (rejea pia Mwa 1:27). Hii ndiyo tofauti katika ya mwanadamu na malaika. Malaika humzunguka Mungu wakati wote, bali mwanadamu ni kiumbe shirikishi cha Mungu. Katika kweli hii, Mungu “Akaitia hofu ya binadamu katika vyote vyenye mwili, ili wawatawale wanyama na ndege,” YbS 17:4-5. Utawala huu aliowezeshwa mwanadamu juu ya viumbe vingine siyo ruksa ya angamizo, bali dhamana ya Kimungu ndani yake, na uwezo wa kutenda katika mwono chanya. Kwa maana nyingine mwanadamu ni mlinzi wa yale yote aliyoyaumba Mungu ili yote kwa umoja na upekee wake yaufikie ukamilisho ule kusudiwa ndani ya kila alichokiumba Mungu. Kumbe si vyema mimi na wewe kuukatisha uhai wa kiumbe kama sisimizi.

Ndugu yangu, maarifa ikiwa ni pamoja na karama na vipaji ulivyojaliwa na Mungu si kwa faida yako binafsi, bali kwa ajili ya wengine pale ulipo na mazingira yanayokuzunguka. Je, umesahau kuwa wewe ni chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu? Rejea, Mt 5:13-13. Hivyo ni katika uumbaji huo kwamba, Mungu “Akawajaza maarifa ya hekima, na kuwapa kupambanua wema na uovu,” YbS 17:6. Kumbe jukumu la kwanza kwako na mwako katika ulimwengu huu licha kuwa sehemu ya kujiandaa kwa maisha ya umilele yatupasa kupafanya kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi.

Ndugu yangu, kila alichokujalia Mungu katika maisha unayoishi hakipo hapo kwa bahati mbaya. Vyote alivyokujalia Mungu vikusaidie wewe na wengine kuuona uso wa Mungu. Hapa ndipo tunapoona muunganika w asomo hili na Injili ya leo. Mlango wa kupita na kuijua siri ya Mungu ndani yetu ni kuwa kama watoto wadogo, yaani, ni katika udogo wako Mungu ujifunua kwako na kwa wengine. Na hii ndiyo maana ya maneno haya: “Akawafanyizia ulimi, na macho, na masikio, akawapa na moyo wa ufahamu; ili kuwaonyesha adhama ya kazi yake, ili wajisifie katika miujiza yake, na kujijulisha kicho chake ulimwenguni, na kulihimidi jina lake takatifu,” YbS 17:7-10. Karama na vipaji alivyotujalia Mungu huo mkondo salama pale tu tunapokuwa tayari kujinyenyekeza. Pasipo unyenyekevu yote aliyotujalia Mungu husinyaa. Unyenyekevu ni kirutubisho hali na makuzi ya yale yote aliyotuwezesha Mungu ndani yetu. Hii ndiyo sheria ya maarifa kaika mafanikio, na uzima katika urithi, YbS 17:11

Ni wanyenyekevu tu ufanywa wateule wa Mungu, na katika agano lake, YbS 17:12, na msingi wa agano hilo ni upendo, Yoh 13:35. Na kwa upendo huo, “Kwa macho yao waliiona enzi ya utukufu wake, na kwa masikio yao waliisikia sauti yake yenye nguvu,” YbS 17:13.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bwana alimwumba Adamu katika mavumbi, na hata mavumbini akamrudisha,” Ybs 17:1

Tusali:-Ee Yesu Mwema, nikumbushe daima kuwa mimi ni mavumbi tu na mavumbini nitarudi. Amina.