ALHAMISI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU MWAKA-C
Somo:
Kumb 30:15-20
Zab:
1:1-4, 6
Injili:
Lk 9:22-25
Nukuu:
“Angalia,
nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda
Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri
zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate
kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki,” Kumb 30:15-16
“Nazishuhudiza
mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti,
baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19
“kumpenda
Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo
uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia
baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20
“akisema,
Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa
makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka,” Lk 9:22
“Akawaambia
wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake
kila siku, anifuate,” Lk 9:23
“Kwa
kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza
nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24
“Kwa
kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza
mwenyewe?” Lk 9:25
TAFAKARI:
“Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila
siku, anifuate.”
Wapendwa wana wa Mungu,
maelekezo ya Mungu juu ya maagizo yake iwe amri au sheria, hayana lengo la
kuukandamiza uhuru wetu, bali endapo tutakuwa ndani ya mwongozo huo hapo ndipo
ulipo uhai na umilele wetu. Kwa maana nyingine, Mungu wetu siyo mfano wa Jitu
katili ambalo lengo na kiini cha utendaji wake ni kwa ajili ya ubinafsi wake.
Mungu alipenda na kupendezwa kumuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake si kwa
kujifaidia mwenyewe, bali kwa sifa na utukufu wake. Uwepo wetu haumpunguzi wala
kumwongezea Mungu chochote na hasa katika utukufu wake. Ila kuishi kadiri ya
maagizo ya Mungu kuna faida kwetu ikiwa ni kuishi katika Amani ya kweli, na
mwisho wa maisha haya hapa duniani tuwe na maisha ya umilele pamoja naye.
Hata pamoja na nia
njema hii ya Mungu, hatushurutishi kumtii ili tufaidike na utukufu wake, ila
kwa kumfuata kwa hiari bila kuburuzwa ni njia mojawapo ya kufunuliwa utukufu
wake. Hivyo leo ni hiari yetu kuchagua uzima au umauti. “Angalia,
nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda
Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri
zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate
kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki,” Kumb 30:15-16. Ndugu yangu, Mungu tu ndiye apaswa kuabudiwa
kuliko kweli na haki. Kinyume cha hapo ni balaa tupu, Kumb 30:18. Ni
katika ukweli huu kwamba “kujisalimisha” kwa Mungu ndiyo njia pekee na sahihi
ya kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kurudi kwake mbinguni. Kujisalimisha
huku kwa hiari ndiko Yesu anakosema “kuikana nafsi.” “Kwa
kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza
nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha,” Lk 9:24. Kumbe licha ya uhai na umauti kuwa sehemu
ya ubinadamu wetu, ipo nafasi kubwa ya umilele kama tutaamua vyema hatima ya
maisha yetu kwa kujisalimisha kuliko kwa hiari. Naye Mungu anasema, “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo,
kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima,
ili uwe hai, wewe na uzao wako,” Kumb 30:19.
Wapendwa wana wa Mungu, uzima wetu upo
pale tunapozishika amri za Mungu siyo kwa woga mbali kwa kuzipenda kwani mwisho
wake ni umilele. “Kumpenda
Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo
uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia
baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa,” Kumb 30:20. Kumbe
tafsiri ya sheria ya Bwana siyo teso bali ni njia ya kuyajua mapenzi yake
kwako. “Heri walio kamili njia zao, Waendao
katika sheria ya Bwana,” Zab 119:1
Kwa maana hiyo, ni lazima nichague kumtii Mungu katika Imani.
Kila wakati unapoamini hekima ya Mungu na kufanya kila analosema, hata pale
unapokuwa huelewi, unakuza urafiki wako na Mungu. Mara nyingi hatufikiri utii
kama sifa ya urafiki; huo ni kwa ajili ya uhusiano na mzazi, mkubwa wa kazi,
siyo kwa rafiki. Lakini Yesu aliweka wazi kwamba utii ni kigezo cha uhusiano na
Mungu. “Ninyi
mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo,” Yoh 15:14. Sisi ni marafiki na
Mungu, lakini siyo sawa na Yeye. Yeye ni kiongozi wetu atupendaye, na
tunamfuata. Tunamtii Mungu, si kama wajibu au kwa hofu au kwa kushurutishwa,
lakini kwa sababu tunampenda na tunaamini kwamba anajua kile kilicho bora
kwetu. Tunataka kumfuata Kristo kwa shukrani kwa yote aliyotufanyia, na
tunapomfuata kwa karibu, ndipo urafiki wtu naye unakuwa wa kina zaidi.
Wasioamini mara nyingi
hudhani kwamba Wakristo hutii kwa sababu ni wajibu, au kuogopa lawama, au
kuogopa hukumu, lakini ukweli ni kinyume cha hayo. Kwa sababu tumesamehewa na
kuwekwa huru, tunatii kwa upendo, na utii wetu hutuletea furaha kubwa! Yesu
anasema, “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda
ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika
amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za
Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo
nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe,” Yoh
15:9-11.
Angalia
jinsi ambavyo Yesu anatutazamia kufanya yale tu aliyotenda kwa Baba yake.
Uhusiano wake na Baba yake ni kielelezo kwa uhusiano wetu naye. Yesu alifanya
chochote Baba alichomwagiza kufanya, kwa upendo. Urafiki wa kweli si wa kukaa
tu ni wa vitendo. Yesu anapotuagiza kuwapenda wengine, kusaidia wahitaji,
kuwagawia wengine mali zetu, kuwa na maisha safi, kusamehe, na kuwaleta wengine
kwake, upendo hutuchochea kutii mara moja. Mara nyingi tunapewa changamoto ya
kumfanyia Mungu “mambo makubwa.” Ni dhahiri kwamba Mungu anafurahishwa zaidi
tunapotenda mambo madogo madogo kwa ajili yake kutokana na utii wa upendo.
Yawezekana huwa hayaonekani kwa wengine, lakini Mungu anayaona na kuyahesabu
kuwa matendo ya kuabudu.
Nafasi
kubwa inaweza kutokea mara moja katika maisha, lakini nafasi ndogo ndogo
zinatuzunguka kila siku. Hata katika matendo madogo kama vile kusema kweli,
kuonyesha wema, kuwatia moyo wengine, tunaleta tabasamu katika uso wa Mungu.
Mungu anathamini matendo rahisi tu ya utii kuliko sala zetu, sifa na sadaka. “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za
kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni
bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu,” 1Sam 15:22
Yesu
alianza huduma yake ya hadharani katika umri wa miaka thelathini kwa kubatizwa
na Yohane. Katika tukio hilo Mungu alizungumza kuto mbinguni; “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye,” Mt 3:17. Je, Yesu alikuwa anafanya nini kwa miaka
thelathini ambacho kilimfurahisha Mungu? Maandiko Matakatifu hayasema kitu
kuhusu miaka hiyo iliyojificha, isipokuwa kwa maneno machache kutoka Mwinjili
Luka, “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii;
na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake,” Lk 2:51. Miaka thelathini ya
kumpendeza Mungu ilijumlishwa katika maneno: “naye alikuwa akiwatii.”
Hivyo wapendwa katika
Kristo, kama tuonaavyo masomo yetu ya leo yanatuelekeza kufanya maamuzi ya
kweli kuhusu maisha yetu na kumfuata Kristo. Je, Yesu anasema nini juu ya AMRI?
Yesu yupo wazi kabisa kuhusu amri na mahusiano yake na umilele. Amri ni ‘Upendo’
ambao kwa kupitia Yeye, yaani Kristo, upendo wa Mungu Baba ni dhahiri kwetu. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda
ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Hivyo kumpenda Kristo na Mungu
Baba ni kuishika amri hii ya Mapendo. “Mkinipenda,
mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Hivyo mara zote yanipasa mimi na wewe
nimwone Kristo kwa yeyote yule nitakaye kutana naye bila kujali itikadi zetu za
maisha, familia zetu, koo zetu, makabila yetu na utaifa wetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, kumtambua Kristo katika maana ya kuwa na amri zake Kristo na
kuzishika ni kumpenda Kristo na huko ndiko kupendwa na Mungu Baba. Hili ndilo
dhihirisho la Kristo kwetu, yaani kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Naye Yesu
anasema, “Yeye aliye na amri zangu, na
kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami
nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Ndugu yangu, wewe na mimi tu
wafuasi wa Kristo kwa kuzishika amri zake na huko ndiko kukaa katika pendo la
Kristo.
“Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo
langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo
lake,” Yoh 15:10. Licha kwamba hapa Yesu katumia wiki kuelezea amri, ukweli ni
huu anaousema kuhusu amri; “Amri yangu
ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi,” Yoh 15:12. Sadaka ya Yesu pale
msalabani yanipasa ihakisi na isadifiwe na kutukuzwa daima kwa kupendana sisi
kwa sisi. Tusipofanya hivyo, ni kwamba tunaendelea kumsulubisha Yesu pale
msalabani.
Kati ya mtihani mgumu
wa maisha ni kuamua kuacha jambo fulani ulilozoea na kuanza njia nyingine. Hapa
ndipo wengi hushindwa. Mara nyingi tunajawa hofu ya sintofahamu ya mambo
yajayo. Ila kama kweli tunataka kuwa karibu na Mungu, na kuokoa nafsi zetu
yatupasa kufanya maamuzi. Maamuzi ye yote yale katika maisha yana gharama zake.
Na uamuzi utakaochukua lazima utapimwa. Wengi watakushangaa na hata kukucheka.
Wala usihofu kwani duniani hapa ni mahali tu pa kujiandaa kwa ajili ya umilele.
Somo la kwanza kwa
mantiki hiyo, linatupa angalisho; kuchagua kati ya kifo au uhai. Uzuri na utamu
wa maisha haya ya leo na sasa unatutia upofu wa kuona uzuri wa maisha ya
umilele. Jambo hilo Yesu analiongelea katika mfumo wa msalaba. Tusipokuwa
tayari kujikana, kuchukua misalaba yetu, na kumfuata, hatufai kuwa wanafunzi wake.
“Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila
siku, anifuate,” Lk 9:23
Jambo
hili la maanisha nini?
Kuikana nafsi ni tendo
la kuvua mwelekeo na mvuto wa yale uyapendayo na yasiyo na tija ukilinganisha
na maisha ya umilele. Na maisha yasiyo na tija ni pamoja na "ponda mali kifo chaja." Ni
maisha ya kutokuwa na hofu ya Mungu. Ni maisha ya kujipenda kupita kiasi na
kujihurumia. Ni maisha ya kuukataa ubinadamu wako na mipaka yake na kujiona
mungu mtu. Huku ni kutoikana nafsi.
Kuubeba msalaba ni
kukubali kuongozwa. Ni kukubali mapungufu yako kama binadamu ili iwe changamoto
kwako kuelekea ukamilifu. Ni kujipokea. Ni hali ya uitaji wa neema ya Mungu. Ni
hatua muhimu ya awali kuanza kukua kiroho. Ni kukubali kujiachia mikoni mwa
Mungu na kumtegemea yeye tu. Ni kuwa na imani juu ya Mungu ingawa mapungufu
yako kama binadamu.
Kumfuata Yesu, ni
kumfanya Yesu kuwa njia, na ukweli, na ulizi, Yoh 14:6. Yesu ni njia kuelekea
uzima wa milele. Hakuna njia nyingine ndugu yangu. Na njia aliyochagua Yesu ni
msalaba. Nasi kama wafuasi wake, msalaba haukwepeki. Yesu ni ukweli. Ukweli huu
ndio utakao tuweka huru, Yoh 8:32. Yesu Kristo ndiyo uzima wetu. Mwili na damu
yake Yesu ni uzima na uhai kwetu, Yoh 6:54.
Ndugu yangu, wakati wa
kukata shauri ni sasa na kumrudia Mungu. Kishawishi kikubwa ni kudhani kuwa
muda bado upo. Linalowezekana leo, lisingoje kesho.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa
maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata
kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:4, 10
No hay comentarios:
Publicar un comentario