JUMATATU
WIKI YA KWANZA YA KWARESMA
Somo:
Wal 19:1-2, 11-18
Zab:
19:8, 9, 10, 15
Injili:
Mt 25: 31-46
Nukuu:
“Msiibe, wala
msidanganye, wala msiambiane uongo,” Wal 19:11
“Msiape uongo kwa jina
langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana,” Wal 19:12
“Usimdhulumu jirani
yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku
kucha hata asubuhi,” Wal 19:13
“Usimlaani kiziwi,
wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana,”
Wal 19:14
“Msitende yasiyo haki
katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali
utamhukumu jirani yako kwa haki,” Wal 19:15
“Usiende huko na huko
katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya
jirani yako; mimi ndimi Bwana,” Wal 19:16
“Usimchukie ndugu yako
moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili
yake,” Wal 19:17
“Usifanye kisasi, wala
kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi
yako; Mimi ndimi Bwana,” Wal 19.18
“Na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua
kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume,
na mbuzi mkono wake wa kushoto,” Mt 25:32-33
“Kisha
Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba
yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa
chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa
mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia,” Mt 25:34-36
“Ndipo
wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa,
tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena
ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au
kifungoni, tukakujia?" Mt 25:37-39
Na Mfalme
atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao
ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi,” Mt 25:40
“Kisha
atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa,
mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe
chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa
mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na
kifungoni, msije kunitazama,” Mt 25:41-43
“Ndipo
hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una
kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?” Mt
25:44
“Naye
atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao
walio wadogo, hamkunitendea mimi,” Mt 25:45
“Na
hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda
katika uzima wa milele,” Mt 25:46
TAFAKARI:
“Changamoto katika Imani ya kweli na Matendo halisi, na yenye uhusiano wa wazi
na Hukumu ya Mwisho.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, masomo yetu ya leo yanatualika kutafakari kwa kina katika kuhusisha
Imani ya kweli na matendo halisi. Kwa maana nyingine kuhusisha nadharia ya
jambo na tendo halisi. Hii ndiyo “Changamoto katika Imani ya kweli na Matendo
halisi, na yenye uhusiano wa wazi na Hukumu ya Mwisho.” Kama wewe na mimi ni
wakristo na wafuasi waaminifu wa Kristo, tutakuwa si wa kweli kama tutasema
hatujui nadharia ya Ukristo wetu. Bila shaka tunazijua vyema Amri za Mungu, na
za Kanisa kwa upana wake. Ni kweli kwamba mara nyingi huzirudia amri hizi kama
ndege Kasuku bila tafakari ya tosha na kupoteza maana yake.
Kuna tofauti kubwa sana
kati ya kukijua kitu kinadharia, na kuchukua nadharia ile katika matendo. Somo
la kwanza linaongelea Amri za Mungu na Utakatifu wake katika maana pana, yaani,
nadharia. Na Mungu analiweka jambo hili ili tumtambue kuwa yeye ndiye Bwana
(Wal 19: 14b, 16b, na 18b). Injili ya leo inatutoa kwenye nadhari ya jambo na
kutupeleka kwenye uhalisia wa jambo, yaani tendo halisi linalo akisi nadharia
yenyewe. Ni katika mantiki hii, Yesu anazifupisha Amri hizi za Mungu katika
mambo makuu mawili; Kumpenda Mungu na Jirani. Yesu anasema, “nawe
mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili
zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na
ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine
iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:30-31. Injili ya leo (Mt 25:31-46)
inatudai kuziweka amri hizo kwenye matendo. Na swali kubwa na la wazi la
kujiuliza ni hili; nimefanya nini kumjali mwenye njaa, mgonjwa, aliye uchi,
mfungwa, nk. Haya ndiyo mazingira wewe na mimi tunayoishi kila siku na yakawaida
kabisa.
Wapendwa wana wa Mungu
katika ukweli huu hakuna cha kujitetea na wala kujihesabia haki. Mimi na wewe
tutapigwa mshangao mkubwa siku hiyo ya mwisho. Mara nyingi na walio wengi kati
yetu huonekana wakiwa karibu sana ya wahitaji na hata kuwapigia upwatu wa
nguvu. Bila shaka ukaribu wao kwa wahitaji si kwa lengo la kuumizwa na kutaka
watoka katika hali zao, bali ni njia moja wapo ya kujiinua nafsi zao na
kutafuta kuhurumiwa na jamii kwa matendo yao hayo yasiyokuwa na chembe yoyote
ya huruma ya Mungu. Hawa ndio Yesu anaosema wanayafanya hayo yote ili
wajihesabie haki pasipo haki. “Ndipo wenye haki
watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au
una kiu tukakunywesha? Tena ni
lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au
kifungoni, tukakujia?” Mt 25:37-39. Je, ni kweli kabisa kwamba vituo vyote
vyenye kutoa huduma na kuwalea mayatima vinafanya hivyo kwa dhamiri iliyo safi?
Ndugu yangu, tusisahau maneno haya ya Mfalme siku ya hukumu, “Amin, nawaambia,
kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea
mimi,” Mt 25:40. Je, nifanye nini basi?
Kila mmoja wetu na
ayatazame mazingira yake, na aanze pale alipo kwa kujiuliza swali maswali haya
mawili; Je, hao wahitaji anaowazungumzia Yesu hawapo hapa nilipo? Kama wapo,
ninampango gani nao kadiri ya uwezo wangu na mazingira yangu? Ni kweli kama
Waswahili wasemavyo, “mbuzi hula urefu wa kama yake.” Hivyo kadiri ya nguvu na
uwezo alionijalia Mungu yanipasa kufanya chochote kwa wahitaji walioainishwa na
Kristo Yesu katika Injili ya leo. Tukumbuke pia kosa la Tajiri yule na Lazaro
masikini (Lk 16:20-31) halikuwa juu ya ubaya wa utajiri wake. Kosa la yule
tajiri lilikuwa hali yake ya kutokujali hitaji la Lazaro na siyo utajiri wake.
Hii ni dhambi ya kutokutimiza wajibu. Utajiri na vipawa tulivyopewa na Mungu
vina maana tu pale tunapofaidiana. Huku ndiko Yesu anaposema siku ya mwisho
kutakuwa na mtengano kati ya Kondoo na Mbuzi, akimaanisha Kondoo ni wale walioenenda
njia ya Bwana kwa kuishi wanayoamini na kuwajibika katika matendo (Mt 25:34-36), na mbuzi ni wale walioenda kinyume kwa kuamini
wasiyoishi kwa matendo (Mt 25:41-43). Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari
hii, wajiandalia uwepo wa kundi gani kati ya Kondoo na Mbuzi?
Hakika hapa wengi tutapigwa mshangao. Ni wazi kabisa
kama bado ningali hapa duniani na kwa hiari yangu nimeamua kuwa kama mbuzi, ni
kwa namna hiyo hiyo nitakavyo jiandalia mahali pangu mara baada ya maisha ya
hapa duniani ambayo ni jukumu la muda mfupi. "Na hao watakwenda zao
kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa
milele," Mt 25:46. Basi ndugu zangu, tuchague haki na
kuishi imani ya kweli katika matendo halisi na ya kweli ili tuishi milele mara
baada ya maisha haya ya hapa duniani.
Tusifu Yesu Kristu!
“Mwenye
haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana
Watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa
matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi,” Zab 92:12-14
No hay comentarios:
Publicar un comentario