sábado, 13 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU

JUMAMOSI BAADA YA JUMATANO YA MAJIVU

Somo: Isa 58:9b-14
Zab: 86:1-6
Injili: Lk 5:27-32
Nukuu:
"Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri," Isa 58:10

Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Lk 5:30

Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi,” Lk 5:31

"Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu," Lk 5:32

TAFAKARI: “Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kipindi hiki cha kwaresma ninatutafakarisha na kutusogeza karibu zaidi na neema na huruma ya Mungu. Kwa upande mwingine ni kuiona "furaha ya Mungu ninapojirudi na kumrudia, pale ninapofanya toba ya kweli kama kieleleza cha kuujenga tena uhusiano wangu na Mungu ulioathiriwa na dhambi zangu." Pamoja na mapungufu yetu na ubinadamu wetu, bado Mungu hajakata tamaa kutupokea kama tulivyo. Furaha yake ni kutupata hasa tunapofanya toba ya kweli. Huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.

Somo la kwanza la tuonyesha namna ya kufanya toba hiyo. Baada ya kutubu na kuondolewa dhambi, malipizi au toba yetu ya kweli ni kujifunua na kujiweka karibu na wale wote wanao itaji uwepo wetu, na kuwasaidia kadiri ya uwezo na nafasi aliyotupa Mungu. Tunapolifanya tendo hilo kuwa letu kwa moyo mkunyufu, kiwi yetu na Mungu inafanywa kama adhuhuri. "Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri," Isa 58:10

Ndugu yangu, unapoishi hapa duniani kuna mambo mawili yanaweza kukifika. Ukiishi vizuri unakuwa muhenga. Yaani mtu aliyeishi vyema na ameacha kitu cha kuigwa na kusimuliwa kwa vizazi vyote. Usipokuwa muhenga basi uwezekano wa kuwa mzimu ni mkubwa. Mzimu ni roho ovu/mbaya. Hapa hakuna cha kuigwa wala kusimuliwa. Mtu anakosa na kupoteza historia yake. Kuishi vyema na watu kwaitaji unyenyekevu kama msingi wa fadhila zote.  Unyenyekevu huu ni furaha ya Mungu. "Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu," Mit 15:33

Ni unyenyekevu huu unaotusukuma tena na tena kupenda kuishi na kila mmoja wetu. Ni unyenyekevu huu unatufanya  kushuka chini kabisa kwa waihitaji. "Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na masikini, kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi." Mit 16:19. Kristo ndiye kielelezo cha unyenyekevu wa kweli. Hakika huruma na neema ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tendo la Yesu la unyenyekevu na huruma linakuwa kero kwa Mafarisayo ambao kwa kiasi fulani katika utendaji wao nasi tumo. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung'unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Lk 5:30. Ni mara ngapi wewe na mimi huendelea kuwanyooshea vidole wale waliodondoka katika dhambi na uovu, na kutokuona tena neema na huruma ya Mungu kwa watu hao wanapojirudi?

Injili yetu ya leo inatupa furaha hiyo ya Mungu na toba ya mwanadamu kupitia mwanaye Yesu Kristo, anaposema uwepo wake si kwa wenye haki, bali kwa wenye dhambi. Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu," Lk 5:31-32. Mapaswa yetu wanadamu ni kutambua tulipojikwaa na kumrudia Mungu. Mlango wa neema na huruma ya Mungu upo wazi muda wote kupitia Sakramenti ya Upatanisho.

Wapendwa katika Kristo, Maandiko Matakatifu yanatupa masimulizi mbalimbali kuonyesha furaha hii ya Mungu-[neema na huruma yake] mja wake anapofanya toba ya kweli. Tazama furaha ya Baba kwa mwana mpotevu, (Lk 15:11-32). Mfano wa mwanakondoo aliyepotea na shilingi moja iliyopotea. Vinapopatikana hivi vilivyopote ni furaha kubwa sana mbinguni. "Nawaambia, vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,"Lk 15:7.

Ndugu yangu, ni upendo mkubwa sana kwetu kupata fursa hii na ukaribu huu na Mungu. Ni wakati mzuri wa kupatanishwa naye. Tusisite kuijongea sakramenti ya upatanisho.  Wakati ufahao ndiyo sasa.

Tumsifu Yesu Kristo!

Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda,

 hakika ataishi, hatakufa,” Eze 18:27-28

No hay comentarios:

Publicar un comentario