UKULU
WA MTAKATIFU PETRO
22/2/2016
Somo:
1Pet 5:1-4
Zab:
23:1-3a, 4, 5, 6
Injili:
Mt 16:13-19
Nukuu:
“lichungeni
kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa
hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo,” I Pet
5:2
“Wala
si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa
lile kundi,” 1Pet 5:3
“Na
Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka,”
1Pet 5:4
“Vivyo
hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu,
mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa
wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5
“Akawaambia,
Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Mt 16:15
“Simoni
Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16
“Yesu
akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu
havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 16:17
“Nami
nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu;
wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18
“Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:19
TAFAKARI:
“Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anafanya kumbumbuku ya Ukulu wa Mtakatifu Petro. Ukulu huu
ndiyo mamlaka na Kiti chake Petro. Ukulu huu wa Mtakatifu Petro hakujitwalia
mwenyewe, bali alihesabiwa haki hiyo na Kristo mwenyewe pale alipotoa ukiri wa
kweli kumuhusu Kristo, yaani aliyetengwa kwa kazi maalumu ya wokovu wetu na
ndiye mwana wa Mungu.
Hivyo, moja ya jukumu
la Kiti hiki ni kuifundisha na kuitetea Imani ya kweli kama kilelezo cha uwepo
wa Kristo katika Kanisa. Petro kama Halifa wake Kristo, na wote waliofuata
baada yake Petro, yaani Mababa watakatifu, wana jukumu hilo kubwa katika
Kanisa. Yesu alitaka kujua kama Mitume wake wanafahamu vyema yeye ni nani na
ujumbe aliokuwa anausimamia. Hivyo aliwauliza wao binafsi wanafikra gani
kumuhusu yeye baada ya kuwauliza watu wanasema nini juu yake. Hivyo Yesu “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Mt 16:15. Jibu la swali hili ndilo linalomwesabia
haki ya Ukulu wa Mtakatifu Petro na wale wote waliofuata baada yake, yaani
Mababa Watakatifu. “Simoni Petro
akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai,” Mt 16:16. Haya ndiyo majibu sahihi ya Mtume Petro yenye
kutoa picha na wajibu wa Kiti hicho-UKULU.
Yesu kwa kuridhika na
jibu la Petro anauthibitisha Ukulu huo kwa kusema, “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu
nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Ni
wazi, uwepo wa Petro kati ya Mitume wenzake na jumuiya ile ya kwanza ya
Wakristo kunampatia nafasi ya pekee katika kutimiza wajibu wake na kutumika
kwake. Ni wazi pia nafasi hii ya pekee kwa Petro siyo tokeo la umahiri wake,
bali ni neema ya Mungu. Naye Yesu anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni
Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye
mbinguni,” Mt 16:17. Mamlaka haya ya Petro kama Halifa wake Kristo ni Neema ya
Mungu mwenyewe. Mbadiliko w ajina Simoni na kuwa Petro, yaani Mwamba,
unathibitisha mtu mpya mwenye jukumu jipya. Hii ndiyo sababu pia ya Mababa
watakatifu kuchagua majina mapya mara baada ya kuhesabiwa haki na Mama Kanisa.
Wapendwa
wana wa Mungu, Ukulu huu wa Mtakatifu Petro unakipa uzito Kiti hicho katika
mamlaka yake kama Yesu mwenyewe asemavyo, “Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani,
litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa
limefunguliwa mbinguni,” Mt 16:19. Haya ndiyo mamlaka ya kiti hiki na hasa kwa
swala hizi la Huruma ya Mungu kwa ondoleo la dhambi. Hii ndiyo sababu pia ya
Baba Mtakatifu kuwa na uwezo na mamlaka ya kuutangaza mwaka huu wa Kanisa kuwa
mwaka wa HURUMA YA MUNGU.
Wapendwa wana wa Mungu,
majukumu na mwonekano wa Ukulu huu ni ule wa kutumika badala ya kutumikiwa. Na
Yesu anasema, “na
mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:27-28.
Kiongozi yeyote yule aliyepewa dhamana na kuhesabiwa haki na Kanisa, yampasa
kutumika na siyo kutumikiwa. Mtume Petro anasema, “lichungeni
kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa
hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo,” I Pet
5:2. Ndugu yangu, wewe na mimi tuliye hesabiwa haki na kupewa dhamana na Mama
Kanisa, hatupo hapo tulipo kwa maslahi yetu binafsi. Mimi na wewe tupo hapo
tulipo kumwakilisha Kristo Yesu aliyetumika badala ya kutumikiwa. “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam,
ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu
huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5. Huduma yo
yote ile isiyokuwa na taswira ya unyenyekevu kamwe haimwakilishi Kristo. Na kwa
namna hiyo hakuna utukufu. Kristo kamwe
hajidhihirishi pasipo unyenyekevu. “Na
Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka,”
1Pet 5:4. Unyenyekevu katika huduma tuzitoazo utawashangaza wengi na hasa wale
ambao mawazo yao hutanguliza nafsi zao.
Tumsifu Yesu Kristo!
Na huku ndiko kutumika. “Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa
yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi,” 1Pet 5:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario