JUMAPILI
YA 2 YA KWARESMA YA MWAKA-C
Somo
I: Mwa 15:5-12, 17-18
Zab:
27:1, 7-8, 8-9, 13-14
Somo
II. Flp 3:17-4:1
Injili:
Lk 9:28b-36
Nukuu:
“Akamleta
nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu.
Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini
Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki,” Mwa 15:5-6
“Akamwambia,
Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa
miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.” Mwa 15:9
“Ikawa,
jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka
ulipita kati ya vile vipande vya nyama,” Mwa 15:17
“Maana
wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia
hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo,” Flp 3:18
“mwisho
wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao
mambo ya duniani,” Flp 3:19
“Kwa
maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi,
Bwana Yesu Kristo,” Flp 3:20
“atakayeubadili
mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule
ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake,” Flp 3:21
“Basi,
ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu,
hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu,” Flp 4:1
“Ikawa
katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe,
yakimeta-meta,” Lk 9:29
“Na
tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu,
wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu,” Lk 9:30-31
“Petro
na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini
walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja
naye,” Lk 9:32
“Ikawa
hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri
sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha
Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo,” Lk 9:33
“Sauti
ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,”
Lk 9:35
TAFAKARI:
“Na hili ndilo agano letu la milele, ‘Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni
yeye.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Mama Kanisa leo anaadhimisha Dominika ya pili ya kwaresma ya mwaka “C” wa
Kanisa. Masomo yetu yote matatu ya leo yanatuelekeza ni wapi lilipo agano letu
la milele, na mapaswa yake kama kweli twataka kulifikia agano hilo, yaani,
maisha hayo ya umilele.
Ndugu yangu
tunayesafiri wote katika tafakari hii, elewa kwamba uwepo wako katika ulimwengu
huu, na haya yote katika ulimwengu huu yanaufunua uwepo wa Mungu, ikiwa ni
pamoja na fumbo zima la wokovu wetu. Hivyo uwepo wako si bahati mbaya hata
kidogo! Wewe ni kusudi la pekee la Mungu ambalo mwisho wake ni umilele wa
maisha yako. Ukweli huu unajidhihirisha katika historia ya wokovu wa mwanadamu.
Huu ni mpango mahususi wa Mungu ambao tunaweza kuuona katika maeneo makuu
manne; Uumbaji wa ulimwengu, Uumbaji wa mwanadamu, Maagano ya Mungu na watu
wake, na mwisho tendo la kumwilishwa.
Uumbaji wa ulimwengu
unathibitisha na kujionyesha kama sababu ya maandalizi ya uumbaji wa mwanadamu.
Mwanadamu anaandaliwa sehemu ya kuishi ili amjue Muumba wake, ampende,
amtumikie, na mwisho arudi kwake alipoandaliwa, yaani uzima wa milele. Hivyo, “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi,” Mwa 1:1.
Mbingu na nchi hizi hazikuumbwa tu bila malengo. “Maana
Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na
kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na
watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18. Huu ndio mpango wa Mungu
juu ya mwanadamu. Hakika ni mpango wa pekee sana. Uwepo wako leo si bahati
mbaya.
Na
alivyoyaona yote yanafaa na kupendeza, ndipo ilipompendeza Mungu kumuumba
mwanadamu kwa sura na mfano wake. “Mungu
akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke
aliwaumba,” Mwa 1:27. Na kwa sababu hii mwanadamu anaowajibu huu mbele ya
Mungu; kumjue, kumpenda, kumtumia, na kurudi kwake alipomwandalia, yaani, uzima
wa milele. Hata pamoja na wajibu huu msingi, uwepo wako na wangu katika
ulimwengu huu lazima uwe wa kuzaa matunda mena kila tunapopata fursa ya kuvuta
pumzi aliyotupa Mungu. Naye Yesu anatuambia hivi, “Si
ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka
mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote
mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Kristo ndiye aliyetuchangua
sisi kwa sababu pasipo yeye hakikufanyika cho chote lilichofanyika. “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo
alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika
cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Ndugu yangu ona ulivyo tokeo na mpango
maalumu wa Mungu!
Pamoja na uumbaji huu
wa pekee wa mwanadamu, Mungu hakumwaacha ajiendee peke yake. Kwa nyakati
mbalimbali Mungu amefanya maagano na watu wake ili kuwa nao karibu na wao
walifikie lengo la kuumbwa kwao, yaani maisha ya milele. Somo letu la kwanza
linazungumzia mpango na ukaribu huu wa Mungu kwa watu wake. Naye Mungu akamleta
nje Abramu “akasema, Tazama sasa mbinguni,
kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao
wako. Akamwamini Bwana, naye
akamhesabia jambo hili kuwa haki,” Mwa 15:5-6. Mungu anamuhesabia haki Abramu
kwa sababu ya hofu ya Mungu iliyokuwa ndani mwake.
Hata
pamoja na hakikisho hilo la haki, Abramu anataka kujua ukweli na uhakika wa
jambo hilo. Naye Mungu anajidhihirisha hivi katika agano lile, “Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na
mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana
njiwa.” Mwa 15:9. Kielelezo hiki tambulishi cha Mungu kinaendana na kipimo cha
utii wa Abramu. Abramu anafanya kama Mungu alivyomwamuru na haya ndiyo matokeo
yake. “Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza,
tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya
nyama,” Mwa 15:17. Mungu anajidhihirisha
katika hali ya tanuru ya moshi na mwenge unaowaka. Licha ya maagano kama haya
kati ya Mungu na watu wake, Mungu huyu ameendelea kuwa karibu na watu wake
kupitia Manabii na Waamuzi.
Wapendwa wana wa Mungu,
kwa upendo usio na kipimo, wakati ulipotimia, (Ebr 1:1-2), katika historia hii
ya wokovu, Mungu mwenyewe amejimwilisha na kukaa nasi. “Naye
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama
wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14. Hivyo
wapendwa katika Kristo, lnjili ya leo inauweka sawa ukweli huu kwa mambo makuu
matatu; Dira yetu ya kufuata kama Wakristo, Utumilifu wa nyakati, na Hatma yetu
iliyojengeka katika agano la umilele. Haya yote yanafanyika katika tukio hili
la kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya simulizi la Injili ya leo.
Kwanza, Dira yetu ya
kufuata kama Wakristo. Heshima na cheo chako kama Mkristo ni utakatifu wako.
Hivyo maisha yetu kama Wakristo kuelekea umilele yatafikika na kuwezekana kama
ni tokeo la utakatifu wetu kwa kuyaona maisha kama ni jukumu la muda fupi hapa
duniani na kama pia sehemu pekee ya maandalizi. Udhihirisho wa utakatifu huu
kama dira yetu ya maisha ni tendo lile la kubadilika sura Kristo Yesu. “Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake
ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta,” Lk 9:29. Kristo anavikwa Utukufu wake ambao ataunyakua
rasmi mara baada ya mateso, kifo na ufufuko huko Yerusalemu. Hivyo Utukufu wa
Kristo hautenganishwa na msalaba/mateso. Kwa maana nyingine hakuna Utukufu
pasipo msalaba. Kama Kristo ndiye njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, nasi wafuasi
wake itatupasa kupita njia hiyo hii ya msalaba, ukweli huu anaotufundisha, ili
tuufikie uzima ule, yaani maisha ya milele.
Pili, ukamilifu wa nyakati. Katika tendo
hili la kugeuka sura, tunaelezwa tokeo la watu wawili, yaani Musa na Eliya
katika mazungumzano na Yesu. “Na
tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu,
wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu,” Lk 9:30-31. Katika
tendo hili, Musa anawakilisha Torati, na Eliya Unabii. Hivyo leo Yesu
anaikamilisha Torati. Naye Yesu anatuambia, “Msidhani
ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali
kutimiliza. Kwa
maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala
nukta moja ya torati haitaoondoka, hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Torati inatimilizwa kwa amri ya upendo kwa Mungu
na jirani. “Basi yo yote
myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo
torati na manabii,” Mt 7:12. Ni ndani na
katika Kristo tu tunapata neema na kweli kwa mkono wake. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli
zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Na huku ndiko kutimilika kwa
sheria na kutamalaki kwa upendo, kweli, na neema.
Leo pia unabii wote
ulionenwa juu ya Kristo na historia nzima ya wokovu wetu unakamilika. Unabii
huu unafika ukomo wake kwa uwepo wa Kristo ambaye ni UPENDO WA MUNGU kwetu.
Mtume Paulo anasema, “Upendo haupungui neno
wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma;
yakiwapo maarifa, yatabatilika,” 1Kor 13:8. Huyu ndiye Kristo Yesu!
Tatu, hatma yetu
iliyojengeka katika agano la milele. Kristo ndiye kielelezo chetu na wokovu
wetu. Leo Mungu Baba anauweka ukweli huu hadharani na kusema, “Huyu ni
Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,” Lk 9:35. Hili ndilo agano la milele
kati yetu na Mungu, na Kristo akiwa ndiye daraja na mlango halisi wa sisi
kupitia kwani ni kwake tu tutakuwa salama kama njia, ni kwa Kristo tu
tunalishwa kweli katika kweli, na Kristo tu ndiye uzima halisi.
Wapendwa wana wa Mungu,
pasipo shaka yoyote tutaelewa sasa vizuri somo letu la pili hasa pale Mtume
Paulo anaposema sisi wenyeji wetu upo mbinguni. Tumeumbwa ili tuishi milele. “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka
huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo,” Flp 3:20. Hivyo ndugu yangu
lazima utambue kwamba maisha yako hapa duniani ni jukumu la muda mfupi. Kuishi
maisha yanayoongozwa na malengo kunatusukuma kuelewa ukweli huu, yaani uzima wa
milele. Hivyo wale wote wanaoishi bila lengo hili la umilele “mwisho
wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao
mambo ya duniani,” Flp 3:19. Duniani hapa ni sehemu ya maandalizi ya umilele,
na kupita tu. Haya siyo makazi yetu ya kudumu. Mungu hajakusudia jambo katika
uumbaji wako. Na unapolazimisha jambo hili, yaani kushikamana na ulimwengu huu
basi unakuwa adui wa msalaba wa Kristo, na sadaka yake pale msalaba haisemi
chochote kuhusu ukombozi wako, Flp 3:18. Hivyo
ndugu yangu, ni Kristo tu “atakayeubadili
mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule
ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake,” Flp 3:21. Kwa
maana nyingine, kwa nguvu zako bila Kristo ni bure. Utajiri wako bila Kristo ni
bure, na vipaji na karama zako bila Kristo ni bure pia. Na katika ukweli huu
wapendwa katika Kristo, “ninaowaonea
shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi
wangu,” Flp 4:1. Kwa Kristo kuna furaha ya kweli. Amina
Mzee Mbute Mabiti alifahamika sana
kwa utajiri wake usihesabika. Alijali sana shughuli zake na hivyo kuchangamana
kidogo sana wa watu. Alipenda sana kusafiri mwenyewe safari fupi na za mbali.
Ilikuwa ni marufuku kumpakiza mtu kwenye gari yake ‘Toyota Landcruzer V 8.’
Umuombapo ‘lift’ na ikiwa amekuonea huruma usimamisha gari yake na kukupa nauli
ya uko uendako na kusema, “komaa uwe na lako,” huku akikutolea macho kama mjusi
aliyebanwa kwenye mlango. Hakika alikuwa Mzee Mabiti kama jina lake.
Siku moja akiwa anasafiri na kupita
katikati ya mbuga moja ya wanyama alikutana na wamasai wawili, mume na mke.
Baba huyu Mmasai aliomba ‘lift’ kwani hali ya mke wake haikuwa nzuri kwa sababu
alikuwa karibu na kujifungua. Mzee Mabiti alisimamaisha gari yake kama kawaida.
“Kulikoni? Mnashida gani, na niwasaidie nini?” aliwauliza Bwana na Bibi wale
Wamasai kwa jeuri. “Baba lai, tunaomba lifuti,” Bwana yule mmasai alimjibu kwa
unyonge. “Siwezi kuwapa ‘lift’ kwenye gari yangu, na sijawahi fanya hivyo kwa
yeyote yule. Chukueni elfu kumi hii itawasaidia,” Mzee Mabiti alijibu kwa
hasira. “Asante Baba lai, ila baki na hela yako kwa maana hapa mbugani
haitatusaidia zaidi ya msaada wa lift,” yule Bwana alimshukuru Mzee Mabiti.
Basi, Mzee Mabiti alipandisha kioo cha
gari yake, na kuondoka mwendo wa mashindano ya magari. Akiwa umbali wa kama
kilometa mbili hivi, Mzee Mabiti alipata mpasuko wa tairi moja ya nyuma, upende
wa kushoto wa gari yake na kuserereka pembeni ya njia. Haja kaa sawa, akaliona
kundi la simba wanne wanakuja kulielekea gari lake. Mzee Mabiti hakuweza kutoka
nje ya gari yake kwa lengo la kuvisha tairi nyingine aendelee na safari yake.
Baada ya nusu saa hivi wale Wamasai mtu
na mke wake wakawa wamefika katika eneo la tukio huku simba wakiwa
wananing’inia kwenye vioo wa gari ile. Wale Wamasai wakawafukuza simba wale
kiasi cha kilomita moja hivi, na kurudi kumjulia hali Mzee Mabiti. Mzee Mabiti
hakuwa na biti tena. Alijawa na upole wa
aibu kubwa. Alitoka ndani ya gari yake na kuomba msamaha ile familia. Bwana
yule Mmasai akamsaidia kubadili lile tairi, na bila kusema neno Mzee Mabiti
akawafungulia mlango mwenyewe na kuanza safari. “Leo nimejifunza mambo mengi
kutoka kwenu ndugu zangu. Na hiki ndicho nilichojifunza: mali, ufahari, fedha
siyo kitu kama hauna upendo wa kweli na kuwajali watu wengine. Nisameheni bure
kwa kile kitendo kisicho cha utu nilichokifanya kwetu. Mzee Mabiti aliyasema
maneno yale huku machozi yakimtoka. “Sisi Baba lai ameshakusamehe yooote.
Asante sana kwa msaada yako,” Walimjibu kwa moyo wa shukrani.
Tumsifu Yesu Kristo.
“Kwa
maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi,
Bwana Yesu Kristo,” Flp 3:20
Ee
Yesu, nijalie jicho la upendo wa kweli ili niweze kukuona kwa kila
nitakayekutana naye katika maisha yangu na huduma nitakayokuwa naitoa kwa ajili
ya watu wako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario