JUMATANO
YA MAJIVU
Soma
I: Yoe 2:12-18
Zab:
50:3-4, 5-6ab, 12-14, 17
Somo
II: 2Kor 5:20-6:2
Injili:
Mt 6:1-6, 16-18
Nukuu:
"Lakini hata sasa,
asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia,
na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie
Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye
mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye
hughairi mabaya." Yoe 2:12-13
"Yeye asiyejua
dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu
katika Yeye," 2Kor 5:20
"Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni," Mt 6:1
TAFAKARI:
“Mwanzo wa safari ya kujitakasa Jangwani.”
Wapendwa wana wa Mungu,
karibuni kwa tafakari hii tunapoanza safari yetu ya kujitakasa huko jangwani.
Leo Mama Kanisa anaanza safari hiyo rasmi na wana wake kwa kujitakatifuza.
Safari hii itatuchukua siku 40-"Quadragesima," ambayo hutambulika
kama "Kwaresma."
Kwa
nini ni siku 40?
Maana ya awali kabisa,
40 huwakilisha muda wa kutosha. Ni muda wa kutosha kwa Mungu, na kwa mwanadamu
akiutumia vizuri ataufikia utakatifu wake. Namba 40 imetumika sana
kuelezea "kutosha" kitu au "kikomo" cha kitu, hasa pale
binadamu anapohusika kwa mwongozo wake Mungu na kumrudia baada ya maasi
yasababishwayo na dhambi.
Taifa la Israel
liliteseka vya kutosha jangwani kwa miaka 40. "Nami miaka arobaini
nimewaongoza jangwani; nguo zenu
hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako,"
Kumb 29:5
Wakati wa Nuhu
"mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku," Mwa
7:12. "Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa
humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku," Kut 24:18. Ndugu
yangu katika agano la kale yapo matukio zaidi 140 yenye uhusiano wa muda wa
kutosha yaani namba hiyo 40.
Ikiwa kielelezo chetu
ni Yesu Kristo, Kwaresma yetu ina mwono wa mfungo wa Yesu mwenyewe jangwani kwa
siku arobaini, mchana na usiku. "Akafunga siku arobaini mchana na usiku,
mwisho akaona njaa," Mt 4:2.
Safari yetu leo inaanza
kwa kupakwa majivu kwenye paji la uso ikiashiria mambo makuu mawili; kwanza
ubinadamu wetu, ikimaanisha kuwa yatupasa kuwa wanyenyekevu. Pili, sisi tu
mavumbi na mavumbini tutarudi. Ni ishara ya toba na majuto. Ni mabadiliko ya
ndani yanayotuweka karibu na Mungu na baraka zake.
Somo letu la kwanza
latupa picha hiyo ya mfungo. Mungu yupo tayari kuanza upya nasi pale tu,
tutakapomjeukia na kuacha njia zetu mbaya. Huruma ya Mungu kwetu inategemea
mabadiliko yetu kumwelekea yeye. Mungu yupo tayari kughairi adhabu yake
tunapomwelekea. "Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo
yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu,
wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana,
Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi
wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya." Yoe 2:12-13. Je,
ndugu yangu upo tayari kuanza na upya na Mungu? Wakati ndiyo sasa.
Ni
mambo gani ya kufanya katika safari hii?
Yapo mambo makuu matatu
ya kufanya kadiri ya injili ya leo. Jambo la kwanza, kwaresma yamaanisha ni
muda wa kusali na kumrudia Mungu. Kusali huku si kwa kupayuka, bali kwa kuzama
zaidi ndani ya nafsi zetu. Kikomo chake isiwe tu pasaka, bali maisha yetu yote.
Na mapenzi ya Mungu kwetu katika Kristo ni haya, “Angalieni
mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni
lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. 16 Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo
ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu,” 1The 5:15-18
Silaha ya mkristo
yeyote ni sala. Kama kweli tunaitaji ulinzi wa Mungu, sala inapaswa kuwa tabia
yetu. Kuwa mtu wa sala. Sala ya kweli na ya watakatifu ni hali ya kuomba ukiwa
na imani kuwa ushapata hata kama bado.
Kusali huku pia kulenge
kung'oa "dhambi Dola." Mfano: Serikali ya Tanzania inaongozwa na dola
ya Chama Cha Mapinduzi-CCM. Chama hiki ndicho kilichounda serikali. CCM ndiyo
dola tawala. Katika mfumo wa maisha ya kiroho, kila mmoja wetu anayo
"dhambi dola," ikimaanisha dhambi tawala. Dhambi hii ni ile ambayo
kila mara unajikuta ushadondoka huko na inakupelekea kuwa kero kwani kila mara
unaiungama. Weka mikakati na Mungu kuiacha kwa msaada wake-"by the Will
Power of God-WPG" Hili ni lengo kubwa na mojawapo ya sala hasa kipindi
hiki cha Kwaresma.
Pili, ni kufunga.
Kufunga hapa kwa maanisha kujinyima kwa ajili ya faida yako na wengine. Jambo
hili ni kwa chochote kile utakacho amua kufanya. Yatupasa pia kulenga katika
mambo yale yanayogusa mfumo wa maisha yetu ya kila siku. Mara nyingi watu wengi
hulenga kujinyima kula. Si mbaya! Ila unalifanya hilo kwa makusudio ya nini?
Faida ya kwanza ni kwa afya yako. Jambo la pili na la maana liwe kwa ajili ya
waitaji. Usianze kuwatafuta kwa kwenda mbali. Anza na familia yako tukijua
kwamba ukarimu huanza nyumbani. Itazame jumuiya yako. Wapo wahitaji wengi sana.
Tazama majirani zako wasio ndani ya jumuiya yako. Na mwisho litazame Kanisa
lako; iwe kigango au parokia. Naye Yesu anatuambia, “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa
ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35
Tatu, Kwaresma yetu
analenga katika swala zima la kutoa sadaka. Hapa yakupasa kujifunza namna ya
kutoa sadaka. Kwanza si kwa kujionyesha bali kwa kutambua wajibu wako na
kumtolea Mungu mastahili yake. Yote ni mali ya Mungu. 1 Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya
Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Na Mungu ndiye msingi wa
vyote. “Mbingu
ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe
uliyeupiga msingi wake,” Zab 89:1. Hivyo ndugu yangu, tunamtolea
Mungu kama shukrani kwa yale anayotukirimia. Sadaka yako iwe kamilifu na yenye
kumpendeza Mungu. “Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi
kwenu,” Lk 11:41. Usimtolee Mungu makapi.
Hapa imaanishe sadaka halali. Ukiangalia sh 50 hadi 200 kwa mfano, hutaona
maandishi haya, "fedha halali kwa malipo ya sh 50, 100, au 200." Ila
kwa upande wa sh 500 hadi 10000 maandishi hayo yapo. Je, wewe unayetoa kila
mara sh. 50 tu kama sadaka yako, ni pesa halali hiyo? TAFAKARI!
Ndugu yangu,
tukiyafanya hayo na kuyaishi, mfungo wetu wa siku 40-Kwaresma, utakuwa na maana
sana. Na pasaka yetu itamaanisha ukombozi wa kweli, wa mwili na Roho. Hiyo
ndiyo maana halisi ya sadaka ya Yesu pale msalabani. Yeye aliyekubali kuchukua
dhambi zetu ingawa hakuwa na dhambi. Yeye aliyekubali kuwa masikini, ili sisi
tuwe matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi
alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi
mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ni upendo wa ajabu wa
Mungu. Safarí imeanza basi tusikubali kubaki nyuma.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ee
Yesu uliye dharauliwa kwa ajili ya dhambi zangu niwezeshe nifanye toba ya
kweli. Amina”
No hay comentarios:
Publicar un comentario