lunes, 8 de febrero de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 5 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 5 YA MWAKA-C
Somo: 1Fal 8:1-7, 9-13
Zab: 132:6-7, 8-10
Injili: Mk 6:53-56
Nukuu:
Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri,” 1Fal 8:9 

Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana,” 1Fal 8:10-11

Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene,” 1Fal 8:12

Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele,” 1Fal 8:13

wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo,” Mk 6:55

Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona,” Mk 6:56

TAFAKARI: “Nyakati za uwepo wa Mungu na Utukufu wake.”

Wapendwa wana wa Mungu, vyote vinavyooneka na visivyoonekana vya udhihirisha uwepo wa Mungu na utukufu wake. Ila kwa namna ya pekee uwepo wako na wangu licha ya kuudhihirisha uwepo na Utukufu wa Mungu, kwa kulitambua jambo hili na KUMRUDISHIA Utukufu huo Mungu, ni furaha kubwa kwa Mungu na baraka wetu. Hatua ya kwanza, yaani, “kutambua” wajibu huu muhimu [“KURUDISHA”] ni kufahamu kuwa uwepo wako leo kwa namna yoyote ile si kwa sababu yako na wasi si kwa nguvu zako na uwezo wako. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum 14:7. Hivyo chochote ufanyacho kwa nia njema na katika ukamilifu wake ni kurudisha sifa na utukufu wa Mungu, na kwa wakati huo huo unaudhihirisha uwepo wa Mungu na utukufu wake.

Ufahamu huu wa kuona haya ya kawaida katiaka maana isiyo ya kawaida katika mtazamo wa Kimungu ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati ya mwenye kujua nyakati za  uwepo wa Mungu na Utukufu wake [kinadharia], na  yule mwenye kuamini na kuishi uwepo huo wa Mungu na Utukufu wake. Ndugu yangu, katika mtazamo na ufahamu huu wa Kimungu kamwe haijalishi ni aina gani ya kazi halali kwa malipo mahali unayoifanya. Vile vile haijalishi ni kiwango gani cha elimu ulicho nacho, na dhamana gani uliyopewa na umma. Ukweli ni kwamba, sababu kubwa ya ukifanyacho husukumwa na HOFU YA MUNGU. Ni kwa wale tu waliofikia hatua hii ya maisha ya kiroho na uweza pamoja na Mtume Paulo, Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8. Utendaji na mtazamo wa mtu wa ngazi hii kiroho na kimaisha ni tofauti kabisa. Uwepo wa mtu huyu popote pale alipo hudhihirisha uwepo wa Mungu na utukufu wake.

Hatua ya pili baada ya kutambua sababu ya uwepo wako hapa duniani ambayo ni kuudhihirisha huo utukufu na uwepo wa Mungu, ni kutimiza  ahadi yako kwa wakati na kwa uaminifu mkubwa uliyomwekea Mungu. Kumbuka ahadi hiyo uliyoweka kwa Mungu ilikuwa ni tokea la kutendewa kwa namna ya pekee na ajabu na Mungu kusikokuwa na mastahili yako wewe kama wewe. Hapa ni wewe na Mungu wako. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” 1Kor 2:11. Mfalme  Sulemani katika hili anatimiza ahadi yake ya kumjengea Mungu nyumba, na kuliweka saduku lile la Agano kulipo salama zaidi. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri,” 1Fal 8:9. Hata hivyo, ni kwa namna hii na mtindo huu uwepo wa Mungu kati ya watu wake ulijidhihirisha. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele,” 1Fal 8:13. Tendo hili ni furaha kwa Mungu na baraka kwa Mfalme Sulemani.

Wapendwa wana wa Mungu, alichokifanya Mfalme Sulemani kinadhihirisha pia uwepo wa Mungu na utukufu wake. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana,” 1Fal 8:10-11. Kile ufanyacho kwa uaminifu katika kweli na haki umwakilisha na kumtambulisha Mungu pale ulipo.

Hatua ya kwanza na hii ya pili, yaani katika kutambua na kutimiza ahadi mbele ya Mungu uwezekana tu pale hayo yanaposukumwa na Imani pasipo shaka. Ndugu yangu, utaweza kuyafanya yote bila shaka kwa vile unaamini kile ufanyacho na kwa sababu gani unakifanya. Hili ndilo tunaloliona katika Injili ya leo. Wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo, [Yesu]” Mk 6:55. Kristo Yesu ndiye kielezo halisi cha Imani, Matumaini, na Mapendo. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu [Kristo Yesu] amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Moja ya Ishara zilizonenewa, Isa 61:1, na kuwa mpango kazi wa Yesu, Lk 4:17-19, ni hili lilitokea leo, yaani,  Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona,” Mk 6:56. Mungu anajidhihirisha kwa watu wake na waja wake wenye hofu naye, na kwa wakati huo huo anaufunua Utukufu wake kwa wale wote wanao mwamini.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, Na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; Umemvika taji ya utukufu na heshima; Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake,” Zab 8:4-6


No hay comentarios:

Publicar un comentario