JUMATATU
YA WIKI YA PILI YA KWARESMA
Somo
la kwanza: Dan 9:4-10
Zab:
89:8, 9, 11, 13
Injili:
Lk 6:36-38
Nukuu:
“Rehema
na msamaha ni kwa Bwana wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana,
Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa
cha watumishi wake manabii,” Dan 9:9-10.
“Basi, iweni na huruma,
kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu,
nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.
TAFAKARI:
“Huruma na Msamaha wa Mungu; kwa kuacha dhambi na kuongoka.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo tutafakari juu ya “huruma na msamaha wa Mungu; kwa kuacha dhambi
na kuongoka.” Ndugu yangu, ni ukweli kabisa kwamba hakuna asiye na dhambi. Wate
tuishio katika dunia hii twaitaji neema na huruma ya Mungu kila wakati. Kuishi
katika ukweli huu, yaitaji unyenyekevu mkubwa. Kishawishi kikubwa cha mwanadamu
ni kule kutaka kuwa sawa na Mungu muda wote. Kiburi hiki ni sababu la anguko la
wazazi wetu wa kwanza. Ila kwa neema ya Bwana wetu Yesu Kristu, sote tumepata
uwezekano wa kumrudia Mungu.
Mpendwa, “tukisema
kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo wetu,” 1Yoh 1:8.
Kuna njia moja tu ya kumrudia Mungu. Njia hii ni kukiri makosa yetu bila
kujibakiza. Ndugu yangu, “tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa
haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9.
Jambo hili linawezekana kwa Mungu kwa sababu yeye ni mwaminifu na “rehema na
msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi,” Dan 9:9.
Kiburi chetu na kukosa
unyenyekevu ndicho Nabii Danieli anatupa angalizo. Nyakati za Nabii Danieli,
watu wote walimwasi Mungu. Kiburi hiki kilikuwa kwa wakuu na wafalme mbele ya
uso wa Mungu. Nabii Danieli kwa niaba ya watu wake anasimama na kusema, “Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa
wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi.” Dan
9:8. Wapendwa, mahangaiko ya watu na uovu kuendelea katika jamii yetu leo kwa
kiasi kikubwa yanatokana na dhambi za kila mmoja wetu kadiri azitendavyo, na
dhambi ya kijamii-“social sin,” ambayo kwa kiasi kikubwa hutendwa na watawala
wetu kwa nafasi waliyokuwa nayo. Jambo hili lilitokea pia wakati wa Nabii
Danieli.
Asiposimama mmoja kati
yetu na kuomba huruma hiyo ya Mungu, kamwe tusitegemee huruma na msamaha wa
Mungu. Tazama taifa letu leo mambo yanavyokwenda. Je, ni mara ngapi, na tena
kwa uwazi kabisa viongozi wetu wanapuuza sauti za waliowaweka madarakani?
Tuelewe kabisa kwamba, sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Kwa ukweli wa jambo hili, embu turejee mchakato mzima wa
pendekezo la Katiba mpya kwenye Bunge la katiba. Je, Mungu kupitia sauti ya
watu alisikilizwa na wale tuliowachagua kufanya kazi hiyo? Cha kushangaza bado
tunapambana na Mungu kwa kufanya kila tuwezacho ili mawazo yetu na tamaa zetu
zishinde nguvu ya Mungu. Jambo hili lina hatari kubwa sana kwa maisha yetu ya
usoni.
Nachelea kujiita Nabii,
ila kadiri nionavyo, hatujampa Mungu nafasi ya kutosha hasa kwa jambo hili
muhimu si tu kwa sisi, bali kwa kizazi kijacho. Mungu hata kaa kimya kamwe
kuona Taifa lake linateketea. Watumishi wa Mungu leo hawasikilizwi hata kama
wakikemea uovu huu. Nyakati za Nabii Danieli kadiri ya somo letu la leo
hawakusikilizwa kabisa. Kwa sauti ya unyonge, Nabii Danieli anasema, “tumefanya
dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha
maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii,
ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na
baba zetu, na watu wote wa nchi,” Dan 9:5-6. Hakika tunaitaji mtu, au nguvu ya
kutuvusha hapa tulipo kama Taifa. Lolote tutakalo tenda kwa sasa bila
kusikiliza sauti ya Mungu, hakutakuwa na baraka yoyote.
Injili yaeleza kwa
undani huruma ya Mungu. Yesu anasema, “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu
alivyo na huruma,” Lk 6:36. Huruma anayotutaka Bwana wetu Yesu Kristo tuwe
nayo, ni huruma katika kutenda tukiwa na hofu ya Mungu. Muda tuliokuwa nao sasa
baada ya kutenda dhambi, na wote tukiwa tunaitaji huruma ya Mungu, si muda wa
kulaumiana na kuhukumiana. Yesu anatupa angalizo; “Msihukumu, nanyi
hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk
6:36. Angalizo hili la Yesu halina maana ya kutowajibika au kutowajibishwa kwa
makosa tunayotenda hasa kwa dhambi ya kijamii-“social sin,” la hasha! Wote
wanaohujumu Taifa hili yawapasa kuona ni kosa na kuchukua hatua. Wasipofanya
hivyo, Mungu mwenyewe atatoa hukumu kwa wakati wake kwa sababu tayari anaona
mateso ya watu wake.
Dhambi ya kijamii ni
kupigana na kushindana na Mungu moja kwa moja kwa kile ulicho kama kiongozi. Umekuwa kama ulivyo
kwa tokeo la tendo la Mungu. Ni Mungu aliyekuweka kuwa hivyo kwa niaba yake
uwatumikie watu wake. Kwani, “sauti ya watu ambao wamekuweka madarakani ni
sauti ya Mungu.” Wengi wetu jambo hili hatulijui kiundani, na kama tunalijua tulichukulia
kimzaha mzaha tu bila umakini na umahiri.
Tendo hili la kupigana
na Mungu kwa uwazi huu, na tena bila kujali na kujirudi, ni kumkufuru Roho
Mtakatifu. Dhambi hii hakuna wa kusamehe. “Bali mtu atakayemkufuru Roho
Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,” Mk 3:29.
Sasa tufanye nini ndugu
zangu? Wapendwa, bila
Yesu na kwa msaada wake, hatuwezi kuvuka bonde hili. Tunamwitaji Yesu sasa
zaidi ya kitu kingine unachoweza kufikiri. Kwa sababu, “Mtu huyu Mungu
amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba
na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Hakuna njia yeyote tuwezayo kupita isipokuwa
kwa njia ya Yesu Kristo. Hili amelisema mwenyewe Yesu Kristo na siyo mimi wapendwa.
“Yesu akawaambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia ya mimi.” Yoh 14:6. Ni katika Yesu Kristo, “ambaye katika yeye tuna
ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi,” Kol 1:14
Ndugu yangu uliyefuatana nami katika tafakari hii, ni
kazi yako kama mbatizwa na mfuasi wa kweli na mwakilishi wa kristo pale ulipo,
tunaposhika na kufuata ushauri huu wa Mtume Paulo, "uwafubue macho yao, na
kuwagueza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na
kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao
waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.” Mdo 26:18. Hii ndiyo
maana ya kuimarishwa katika sakramenti ya Kipaimara.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi, iweni na huruma, kama Baba
yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi
hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa,” Lk 6:36-37.
Ee Yesu, tujalie ujasiri wa kuiishi
Imani yetu na kusimama katika kweli yako siku zote za maisha yetu.
No hay comentarios:
Publicar un comentario