JUMAPILI
YA 5 YA MWAKA-C
7/2/2016
Somo I: Isa 6:1-2a, 3-8
Zab: 138:1-2, 2-3, 4-5, 7-8
Somo II: 1Kor 15:1-11
Injili: Lk 5:1-11
Nukuu:
“Ndipo
niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye
midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu
yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi,” Isa 6:5
“Kisha
mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto
mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo,
akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na
dhambi yako imefunikwa,” Isa 6:6-7
“Kisha
nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda
kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi,” Isa 6:8
“Maana mimi ni mdogo
katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la
Mungu,” 1Kor 15:9
“Lakini kwa neema ya
Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali
nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya
Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10
“Basi, kama ni mimi,
kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini,” 1Kor 15:11
“Hata
alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu
zenu mvue samaki,” Lk 5:4
“Simoni
akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha,
tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5
“Basi,
walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia
mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja,
wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama,” Lk 5:6-7
“Simoni
Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa
kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8
“Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk
5:10b
TAFAKARI: “Tweka
mpaka kilindini.”
Wapendwa wana Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika
ya ‘5’ ya mwaka ‘C’ wa Kanisa. Wazo kuu la masomo yetu yote matatu linatoka
katika Injili ya leo kwa maneno haya ya Yesu aliyomwambia Simoni, “Tweka mpaka kilindini.” Maneno haya ya Yesu yanaamsha hari
mpya ndani ya tumaini lile ambalo lishapotea kutokana na kukata tamaa, na
wakati mwingine kutojipokea kutokana na historia zetu na mazingira yetu ya
ukuaji yaliyo mabaya. Mara zote tunapopata nafasi ya kukutana na Mungu
anatualika kuanza upya naye, Mungu wetu aliye UPENDO, HURUMA, MSAMAHA, HAKI, na
UPOLE.
Wito
wa Nabii Isaya unaonyesha mtazamo wa Mungu na jinsi tunavyojitazama kama watu
tusiostahili kwa yale Mungu anayotufikiria. Hakika upendo, huruma, msamaha,
haki, na upole wa Mungu hatuwezi kuufananisha na kitu chochote. Mungu atabaki
kuwa Mungu kwa milele yote! Isaya anapotazama mwaliko wa Mungu na kile alicho
anaona ni vitu viwili tofauti. Naye anasema, “Ole
wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami
ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme,
Bwana wa majeshi,” Isa 6:5. Pamoja na historia zetu zilizombaya, kushindwa
kwetu katika maisha, na kudharauliwa kwetu, bado Mungu anasema, “tweka mpaka
kilindini.” Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, ‘kutweka mpaka
kilindini’ kuna maanisha hivi; pamoja na shindwa yako bado una kitu cha kufanya
na kubadili historia yako mbaya. Hivyo kitumie kitu hicho katika ukamilifu wake
na hadi mwisho wake, na yote yatakuwa mapya.” Huu ndiyo ujumbe mahususi.
Mpendwa
katika Kristo, unapojiachia kwa Mungu bila kujibakiza katika maana ya kuyatweka
yote mpaka kilindini, ndipo utakaso unapokujilia na kufanywa upya mbele ya Mungu,
na kuhesabiwa haki kwa mastahili ya Mungu mwenyewe. Isaya anayaendea mabadiliko
haya katika maisha yake kwa sababu Mungu kesha pendezwa naye. “Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka
akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa
amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa
kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na
uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa,” Isa 6:6-7. Ni mara ngapi
tunajiona watu tusiofaa mbele za watu na kujipoteza kabisa? Ndugu yangu, hata
kama ulimwengu wote utakuchukia, Mungu hubaki na upendo wake kwako wa ajabu.
Embu itazame mikono ya Yesu pale msalabani. Yesu anakuambia, ‘tazama
nimeyakubali haya yote na hata kufa kifo cha aibu msalabani kwa sababu nakupenda
kupita vyote.’ Hakika Mungu anatupenda
upeo!
Wapendwa wana wa Mungu,
utaisikia sauti ya Mungu ndani yako unapo utafakari upendo huu wa Mungu ulio wa
ajabu. Isaya anaisikia sauti ya Mungu ndani yake, na kusema, “Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye
ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume
mimi,” Isa 6:8. Isaya anazaliwa upya mwili na roho na sasa yupo tayari
kuyafanya mapenzi ya Mungu. Huwezi kukutana na Mungu katika maisha yako naye
akakuacha kama ulivyokuwa mwanzo.
Kwa
uzoefu aliokuwa nao Simoni kama mvuvi wa samaki, isingekuwa rahisi kuuchukua
ushauri wa Yesu wa kurudi tena ndani ya maji na kuvua samaki. Elewa kwamba
usiku kucha Simoni na wenzake walikesha wakivua bila kupata chochote. Usiku ndio
muda muhafaka wa kuvua samaki. Leo kwa namna ya kushangaza Yesu anamwambia
Simoni azitupe nyavu zake ndani ya maji, na kwenda kinyume kabisa na utaratibu
wa uvuvi. “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka
kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki,” Lk 5:4. Simoni akitambua
alichokifanya usiku kucha bila kupata chochote, “akajibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate
kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” Lk 5:5. Maneno haya ya Simoni
“lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu,” yanaonyesha kujisalimisha kwa Simoni
pasipo shaka mbele ya Yesu. Maneno hayo ya Simoni yenye kuonyesha kujisalimisha
kwake, ndiyo roho na uzima. Katika hili Yesu anasema, “Roho
ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena
ni uzima,” Yoh 6:63. Na neno lile Yesu alilomwambia Simoni “tweka mpaka
kilindini,” ndiyo uzima na ponya yake Simoni.
Na tazama huu ndio
uzima juu ya neno lile la Yesu na kujisalimisha kule kwa Simoni: “Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno,
nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo
cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata
vikataka kuzama,” Lk 5:6-7. Ndugu yangu, yawezekana umekata tamaa katika maisha
yako kutokana na jambo fulani ambalo kwa uelewa wako na uzoefu wako hakuna pa
kutokea. Leo Yesu anakuambia neno hili, “‘tweka mpaka kilindili,’ yaani jaribu tena kile
kilichobaki katika ukamilifu wake, na hadi mwisho wake kabisa, nawe utaona
uwezo wangu.”
Matokeo ya
nguvu na uwezo wa Yesu katika muujiza huu, kinamfanya Simoni kuyaona maisha yake ya ndani. “Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu,
akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana,” Lk 5:8. Ndugu yangu, hutoweza kujiona ulivyo kama
hutojiachia ndani na katika Kristo Yesu. Kuiona vizuri chunusi iliyoko kwenye
paji la uso wako, yakupasa kusimama mbele ya kioo. Kumbe kujiachia mbele ya
kioo kunakuwezesha kujiona vizuri. Yesu ni kioo kwetu, na ndivyo Simoni
alivyojigundua kuwa yu mdhambi. Pamoja na udhaifu ule aliokuwa nao Simoni bado
Mungu anampango na maisha yake. Tena mpangu mahususi kabisa. Naye “Yesu
akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu,” Lk 5:10b. Yesu anaifanya njia katika maisha ya Simoni. Huyu
ndiye baadaye aliyejulikana kama Simoni Petro, na juu yake ndipo lilipo jengwa
Kanisa. Mtume Paulo anatuambia, “Jaribu
halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni
mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile
jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13
Wapendwa wana wa Mungu,
ukiyatazama maisha yako na jinsi Mungu alivyoendelea kuwa upendo na huruma kwako,
hakika yote ndani yetu ni kwa neema ya Mungu. Hakika, “Bwana, kama Wewe
ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3. Hivyo ni pamoja na
historia mbaya aliyokuwa naya Sauli wa Tarso, leo kwa neema ya Mungu
anajulikana kama Mtume Paulo. Paulo anatoa ushuhuda wa maisha yake na kusema, “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa
mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu,” 1Kor 15:9. Hata pamoja na
ukweli huo, huruma na neema ya Mungu ni kubwa zaidi ya uovu wako kama
utajisalimisha kwake. “Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema
yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao
wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami,” 1Kor 15:10. Mungu yupo tayari kuanza upya nawe endapo
tu kama upo tayari. Hizi ni neema za Mungu zinazotuzunguka kila wakati. Na kwa
namna ya pekee mwaka huu wa Kanisa wa huruama ya Mungu ni wakati wa kutumia
fursa hiyo vizuri. Ndugu yangu, tweka mpaka kilindini!
Ngesha
Biloko alijulikana sana kwa upigaji wa gitaa la nyuzi sita. Hakuna aliyeweza
kushindana naye katika ujuzi huu wa uchezaji gitaa. Hivyo liliandaliwa tamasha
kubwa sana, na walialikwa wachezaji maarufu wa gitaa ulimwengu mzima.
Siku moja
kabla ya shindano lile, Ngesha Biloko aliwasili katika jiji lile yalipokuwa
yameandaliwa mashindano yale akiwa na gitaa lake. Biloko alipokelewa vizuri na
kuonyeshwa chumba chake. Kesho yake kama kawaida alifanya mazoezi chumbani
mwake na kujiridhisha.
Jioni
ilifika mashindano yalianza. Biloko alikwa mtu wa kumi katika orodha ile ya
wacheza gitaa 15 maarufu duniani. Ilipofika wakati wake alipokelewa kwa
mbwembwe jukwani kwa sababu wengi waliyajua makali yake. Akiwa jukwani, na watu wote kwenye ukumbi ule
wakisubiri kusikia uchezaji wake, Biloko alipikwa na butwaa alipoona gitaa lake
likiwa na nyuzi tatu tu. Hakujua kilichotokea kuhusu gitaa lake.
Hata hivyo hakuwa na njia
nyingine zaidi ya kuzicheza nyuzi zile tatu zilizobaki. Alijitia ujasiri na
kulicharaza gitaa lile. Baada ya kumaliza dakika zake tano kama ilivyokuwa
imepangwa, ukumbi mzima ulirindima kwa kelele za shangwe na vifijo. Msema
chochote-MC, katika ukumbi ule alisema hivi, “tumekuwa tukisikia uchezaji wako
wa gitaa kwa kuda mrefu sasa, ila leo umekuja na kitu kipya kabisa ambacho
hakijawahi kusikika masikioni mwetu. Viva Biloko, Viva!!”
Ndugu yangu, Biloko
alitweka mpaka kilindini.
Tumsifu Yesu Kristo.
“Lakini tuna hazina
hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si
kutoka kwetu,” 2Kor 4:7
No hay comentarios:
Publicar un comentario