IJUMAA
WIKI YA 2 YA KWARESMA
Somo: Mwa 37:3-4,
12-13a, 17b-28
Zab:
105:16-17, 18-19, 20-21
Injili:
Mt 21:33-34, 45-46
Nukuu:
“Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko
ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani,” Mwa 37:4
“Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la
mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake,”
Mt 21:41
TAFAKARI: “Wivu na kutokuona mazuri ya wenzetu, na mwisho
kupelekea umauti.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari kwa undani
kuhusu “wivu na chuki ya kutokuona mazuri ya wenzetu, na mwisho wake
kutupelekea katika umauti. Somo letu leo la kwanza ikiwa ni pamoja na Injili
kwa namna moja yanaongelea hathari za wivu, na tokeo lake, yaani umauti.
Bila shaka ndugu yangu unajua vizuri kisa cha Yusufu
na ndugu zake. Yusufu akiwa ni mtoto wa mwisho, alitokea kupendwa sana na baba
yake. Kupendwa kwa mtoto wa mwisho si jambo ya ajabu katika makuzi na hata
katika mila na desturi zetu. Ni kweli iliyo wazi kwamba aliye wa mwisho
hutupiwa jicho na wengi. Kwa wazazi ni wakati wa kujitazama na kujiona kupitia
mtoto wao huyu wa mwisho. Mtoto huyu wa mwisho ujeuka kuwa kama kioo kwa wazazi
wao. Hili si jambo baya. Hali hii pia huwa kivutio kwa ndugu zake, na kupendwa
na wote.
Ila cha kushangaza kwa familia hii ya Israeli, tendo
la kupendwa sana Yusufu na baba yake, linakuwa kero kwa ndugu zake, na hata
kupanga mpango wa kumwua. Hii ni chuki ya hali ya juu.
Kujaribu kumwaga damu ya ndugu yako kwa sababu tu anapendwa, tena na baba yako,
ni jambo la kushangaza sana.
Ndugu yangu, swali la
kujiuliza ni hili, kwa nini unachukia wakati mwenzako anafanikiwa? Kwa nini
ukose usingizi kwa mafanikio ya mwenzako? Sisemi tusiwe na wivi, ila wivu huo
uwe wivu wa maendeleo. Kama mwenzako kajenga nyumba akatumia bati kuezeka, basi
wewe jitahidi uezeke kwa vigae. Huu ni wivu wa maendeleo usiokuwa na madhara
kwa mwingine.
Yanayomtokea Yusufu,
yanamulika pia maisha ya Yesu na hatma ya kifo chake. Ndugu za Yusufu baada ya
kuguswa na dhamiri zao, wanaamua kumuuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande
ishirini tu vya fedha. Yesu pia anauzwa na mwanafunzi wake, Yuda Eskariote kwa
vipande thalathini tu vya fedha. Mbele ya safari, Yusufu anakuwa mwokozi kwa
ndugu na familia yake wakati wa njaa. Yesu pia ni kielelezo chetu na mwokozi
wetu kwa njia ya mateso, kifo, na ufufuko wake.
Wivu usio wa kujenga ni
chanzo cha mateso na hata kifo kwa wengine. Katika Injili, Yesu nafundisha kwa
mfano na kuwakumbusha waandishi na mafarisayo safari nzima ya wokovu na
makusudi ya Mungu katika kumkomboa mwanadamu. Ila kwa mioyo yao migumu iliyojaa
wivu na chuki hawapotayari kuupokea ukweli huo na kubadilika. Kwa tendo hili,
Ufalme wa Mungu unaondolewa kwao na kupewa taifa lingine.
Je, hili la Yusufu na
Yesu linasema nini kuhusu Ukristo wako? Ndugu yangu, ni ukweli ulio wazi
kwamba, kuishi maisha ya kweli na ufuasi thabiti kwa Kristo, ndani ya Kristo,
na kwa ajili ya Kristo, ni kutangaza vita vya kudumu dhidi ya utawala wa giza.
Ni kutangaza vita pia dhini ya ndugu, jamaa na marafiki, na matamanio yako binafsi. Mashambulio haya ni
mtihani kwa ye yote yule aliye mwaminifu katika ufuasi wa Yesu Kristo. Katika
hili Yesu anasema, “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina
langu; lakini mwenye kuvumila hata mwisho, ndiye atakayeokoka,” Mt 10:22.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ndugu zake wakaona ya kuwa baba
yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye
kwa amani,” Mwa 37:4
Ee Yesu tujalie
ujasiri wa kuvishinda vita dhidi ya Imani yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario