ALHAMISI WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo:
1Fal 2:1-4, 10-12
Zab:
1Nya 29:10, 11ab, 11d-12, 12acd
Injili:
Mk 6:7-13
Nukuu:
“Mimi
naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume,”
1Fal 2:2
“uyashike
mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na
amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika
torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako,” 1Fal
1:3
“ili
Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto
wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote,
na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha
Israeli,” 1Fal 2:4
“Basi
Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba yake; na ufalme wake ukawa
imara sana,” 1Fal 2:12
“akawakataza
wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala
pesa za bindoni; lakini
wajifungie viatu; akasema, Msivae kanzu mbili,” Mk 6:8-9
“Akawaambia,
Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali
pale,” Mk 6:10
“Na
mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko,
yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao,” Mk 6:11
“Wakatoka,
wakahubiri kwamba watu watubu,” Mk 6:12
“Wakatoa
pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza,” Mk 6:13
TAFAKARI:
“Kama Mzazi unawaachia urithi gani watoto wako?”
Wapendwa wana wa Mungu,
nachelea kusema kwamba leo malezi wayapatayo watoto wetu kutoka kwa wazazi wao
yamekuwa kama yale ya kuku huria, kujitafutia wenyewe. Malezi haya ni hatari
sana kama ilivyo kwa kuku hawa huria yalivyo hatarishi kwa ugonjwa wa
kideri. Hatari ya kwanza ni kwamba
wazazi wanakosa nguvu ya kimaadili katika kuonya, kukemea, kuagiza na kuongoza.
Wazazi hawawezi tena kuwa kwenye nafasi zao kwa sababu wanapigana vikumbo huko
mitaani na watoto wao katika ile hali ya kujiokotezea kama kuku huria.
Hatari ya pili ni aina
ya viongozi tunao wapata kutoka katika
jamii yetu leo. Si jambo la kushangaza leo kuwaona viongozi tena wenye nafasi
kubwa katika jambii wasiojishemu, na wasio na akiba ya maneno midomoni mwao.
Viongozi hao ni zao au tokeo la familia hizi huria. Na ninapoongelea viongozi
ninamaanisha pande zote, iwe taasisi za serikali au za kidini. Si jambo la
kushangaza kumwona kijana mdogo kabisa tena wa umri akimnasa makofu Babu au
mzazi wake wa kumzaa kwa vile tu nafasi na ofisi yake inaruhusu. Ulewi wa
madaraka na matumizi mabaya ya madaraka. Hiki ni kizazi cha nyoka! Je, tufanye
nini? Yatupasa kila mmoja wetu kadiri ya nafasi na wito wake kwenda kwenye
kiini cha tatizo, yaani, FAMILIA, na kuangali ni wapi tulipokosea au potoka.
Leo kwa namna ya pekee
Mama Kanisa anatutaka tujifunze kwa Mfalme Daudi na kwa Yesu mwenyewe. Wakati
wa siku zake za mwisho ulipotimia, Mfalme Daudi alimwita mtoto wake Sulemani na
kumwachia urithi wa kudumu. Kwanza, Daudi
anatambua uwezo wa mtoto wake na yale yatayomkabili huko mbele ya
maisha. Daudi anamwambia mwanaye, “Mimi
naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume,”
1Fal 2:2. Leo wazazi wetu wanafanya yale ya kawaida sana na ya mzunguko wa
kawaida. Wakati mwingine ni mtindo wa kuiga tu. Mfano, wajibu mkubwa wa mzazi
leo: Mtoto ameenda shule, amekula, amelala, na amevaa, basi. Hakuna muda wa kukaa na watoto wetu na kujadili
yale ambayo hatuyasemi kwa kuwahofia. Haya ambayo hatuyasemi ndiyo
wanayookoteza huko mitaani na mwisho wanaishia kwenye gonjwa la kideri kama
kuku huria.
Mfalme Daudi anamwambia
mtoto wake Sulemani, “uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume.” Haya maneno ni
mazito sana. Hii ndiyo jando ya watoto wa kiume. Je, wewe Baba unajua wajibu
huu muhimu kwa watoto wako wa kiume. Leo kuwaona watoto wa kiume kutoboa
masikio, kuvaa hereni, kusuka nywele, na kuvaa milegezo ni jambo la kawaida na
jambo la kusikitisha wapo wazazi wanao furahia hali hii na hata kuwashawishi
watoto wao kuwa hivyo. Ajabu na robo! Je, na wewe Mama una nafasi ya kukaa na
mtoto wako wa kike na kumwambia, “uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamke?” Hii
ndiyo unyago kwa watoto wa kike. Leo si jambo la ajabu kuwaona mabinti zetu
kuiga tabia za kiume na kutaka kuwa hivyo. Hivi Mungu alikosea kutuumba kama
tulivyo? La hasha! Wazazi wetu wapo likizo isiyo na ukomo.
Wapendwa wana wa Mungu,
shule ya kwanza na ya muhimu ni FAMILIA. Tukikosea hapa hatuna mtu katika
ukamilifu wake. Malezi ya mwili ni muhimu sana. Hili la mwili linaendana pili
na la kiroho. Wazazi na walezi mnawajibu wa kuwafundisha watoto wenu kuishi na
hofu ya Mungu. Nasi katika taasisi za kidini na serikali tunawajibu huo kadiri
ya nafasi na karisma ya taasisi. Hili nalo Mfalme Daudi analifanya kwa mtoto
wake Sulemani. Naye Daudi anamwambia Sulemani, “uyashike
mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na
amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika
torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako,” 1Fal
1:3
Jamii isiyokuwa na hofu
ya Mungu ni hatari sana. Leo kuona watu wanachinjwa kama kuku katika matukia
tofauti tofauti ni matukio ambayo yanaanza kuzoeleka. Mbaya zaidi ni pale
unapoona jamii kutoshitushwa na haya yanapotokea. Leo mtu kukwapua hela za umma
kwa kiasi kukubwa awezacho kinaonekana kama sifa na mafanikio. Tusiporudi
kwenye kiini cha tatizo yaani, FAMILIA, hata kama tukianzisha mahakama za
mafisadi kila mtaa haitakuwa tiba kwa tatizo la ufisadi kwa sababu hata hao
mahakimu tunaotegemea wasimamie sheria na kutenda haki wana Upungufu wa Kinga
ya Maadili-“UKIMA.” Huu UKIMA ni tatizo kubwa sana leo katika Familia zetu,
Taasisi zetu za kidini na hasa taasisi za kiserikali, na Taifa kwa ujumla wake.
Pasipo na hofu ya
Mungu, haki za wanyonge huporwa mchana kweupe. Pasipo na hofu ya Mungu,
waliopewa dhamana na umma huzikanyaka haki za watu bila kujali. Pasipo na hofu
ya Mungu, katiba ya nchi kama sheria mama uvunjwa bila kujali kila kukichwa.
Kinachoangaliwa hapa ni maslahi binafsi na ya kichama. Je, haya hamuyaoni?
Kwenye malezi mazuri ya
mwili na roho maisha yajayo huwa na matumaini. Kwenye malezi mazuri ya mwili na
roho, kuna urithishwaji mzuri wa maadili kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Leo walio wengi ukimuuliza kesho itakuaje hana jibu, zaidi ya ubabaishaji tu.
Kila mmoja anaishi kwa ujanja ujanja tu. Kila mmoja yupo kumuwahi mwingine,
tena kwa kumdhuru. Leo wote tunaishi kama tupo kwenye vituo vya treni, yaani,
kila mmoja anaushikilia mzigo wake akifikiri aliye jirani yake ni mwizi. Ajabu
na roho! Mfalme Daudi anamwachia mtoto wake Sulemani urithi wa maadili mema
akijua kuna matumaini hapo kesho. Naye anasema, “ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu,
akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa
kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika
kiti cha enzi cha Israeli,” 1Fal 2:4.
Wapendwa wazazi, walezi, na wale wote walio kwenye taasisi za kidini, na
kiserikali tuna kazi ya zaida kulitoa Taifa hapa lilipo na kulipeleka hapo
kesho kwenye mwanga wa kweli. Tuache mtindo wa kuishi kama vile kesho haipo. La
sivyo mbele huko ni giza tupu!
Matokeo ya malezi
mazuri ya mwili na roho aliyoyatoa Daudi kwa mtoto wake, ni kile alichokuwa
Mfalme Sulemani. “Basi Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Daudi baba
yake; na ufalme wake ukawa imara sana,” 1Fal 2:12. Je, tunaacha uhenga gani kwa
watoto wetu na familia zetu mara tuuachapo ulimwengu huu?
Alilolifanya Mfalme Daudi kwa mwanaye
Sulemani, ndilo analolifanya Yesu kwa wanafunzi wake ‘Thenashara,’ yaani, wale kumi na mbili, anapowatuma
wawili wawili. Fundisho la kwanza ni kwamba Yesu anawafundisha mitume wake
mshikamano akijua ‘umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.’ Jambo la pili, Yesu
anawapa angalizo la namna ya kuuendea ulimwengu ili wafanikishe lengo la msingi
ambalo lipo mbele yao, yaani, “wakahubiri kwamba watu watubu,” Mk
6:12. Ili lengo hili lifikiwe, yawapasa, “wasichukue kitu cha njiani isipokuwa
fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu; akasema,
Msivae kanzu mbili,” Mk 6:8-9. Ukweli ni kwamba
kadiri watakavyo jitenga na malimwengu haya ndiyo watakavyokuwa huru kulifikia
lengo hili Msingi, “kuhubiri habari njema, na kufanya toba ya kweli.”
Malezi hayo ayatoayo Yesu kwa hao
Thenashara yana lenga hasa mwili na ndiyo jando yao. Huwezi kuyafikia malengo
yako kama hautakuwa na kiasi katika maisha yako. Hili Yesu analiona vizuri
sana. Yesu anazidi kulikazia hili na kuwaambia, “Mahali
po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale,”
Mk 6:10. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, ili kuyafikia
malengo yako katika maisha unahitaji utulivu wa mwili na roho. Na hata pale
unapofanikiwa unahitaji utulivu wa mwili na roho kuyachambua kwa kina mafanikio
hayo. Huku ndiko Yesu anakokuita kwenda faraghani. “Basi
wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua,
akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida,” Lk 9:10. Maisha ya kutangatanga bila tafakari
ya kina kwa kile utakacho kukifanya ni vigumu kukifikia. Hili nalo Yesu
analiona.
Kwa upande wa kiroho, Yesu hakuacha
kuwafundisha wanafunzi wake ili walifikie lile lengo. Naye anawaambia wanafunzi
wake, “Na
mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko,
yakung'uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao,” Mk 6:11.
Anachokisema Yesu hapa ni hiki; ‘wanafunzi wake wasipoteze muda kwa kujihesabia
haki hata kama watathihakiwa kuliko wazi na kwa makusudi.’ Watu hawana uwezo wa
kuwahesabia haki isipokuwa Mungu mwenyewe. Hayo yakitokea yawapasa kuondoka wakiwa
na moyo mweupe bila kuchua lolote kutoka kwao. Ni Mungu tu mwenye kutuhesabia
haki na mastahii yetu, ndiye atakaye tenda haki hiyo. Hakuna sababu ya kuwabeba
watu vichwani mwao na mioyoni kwao kwa vile tu hawakutendewa haki kwa
kukaribishwa kwa heshima. Jambo la muhimu ni kulenga kwenye lengo msingi lilio
mbele yao. Muda kamwe hautawasubiri.
Matokeo ya mafundisho
haya ya Yesu kwa Mitume wake,
Thenashara, “Wakatoa pepo wengi, wakapaka
mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza,” Mk 6:13. Na huu ndio mpango
kazi wa Yesu, “Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza
mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Mpango kazi huu, Mitume wake na
wapelekwa wake Yesu wanaanza kuutekeleza. Na kauli mbiu ya mpango kazi huu ni
hii: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu
umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Ndugu yangu kwa kifupi hiki
ndicho mimi na wewe tupaswacho kukijua kuhusu siri ya wokovu wetu ambao kama
tulivyo mwili na roho hatutaweza kulifikia lengo hili kama tusipoyafanya yote
hayo mawili katika ukamilifu wake, na hatutaweza pia kulifikia lengo letu hili
kama tutadhara moja ya hayo mawili, yaani mwili na roho. Huu ndio urithi
tunaopaswa kuwarithisha watoto wetu leo. Maisha yetu ya umilele yanategemea
sana maandalizi mazuri leo hapa duniani.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mtu
mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye
haki,” Mit 13:22
NA
“Bwana
anazijua siku za wakamilifu, Na urithi wao utakuwa wa milele.” Zab 37:18
No hay comentarios:
Publicar un comentario