miércoles, 17 de febrero de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 1 YA KWARESMA

ALHAMISI WIKA YA KWANZA YA KWARESMA

Somo: Est 14:1, 3-5, 12-14
Zab: 138: 1-2ab, 2cde, 7c-8
Injili: Mt 7:7-12
Nukuu:
“Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki. Utukumbuke, Ee Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu, unipe moyo thabiti, Ee Mfalme wa miungu na Bwana wa milki zote,” Est 14:4

“Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuze moyo wake apate kumchukia Yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye,” Est 14:13

"Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa." Mt 7:7-8

Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:11 

Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt 7:12 

TAFAKARI: “Kujiachia katika Sala: ‘Ee Bwana, Wewe ndiwe mwenye haki.’”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari namna ya "kujiachia katika sala." Masomo yetu ya leo yanatuelekeza katika fundisho hilo. Somo la kwanza, Malkia Esta anatupa mfano hai wa kujiachia kabisa katika sala. Kujiachia katika sala, kwanza kabisa ni kutokuwa na shaka kwa kile unachoomba. Pili, kutokuwa na shaka kwa yule unayejisalimisha kwake, yaani Mungu. Tatu, kuamini kuwa umeshapata hata kama bado. Atua hii ya tatu inaitwa "atua ya utakatifu katika sala."

Wengi wetu hatufiki hatua hii ya tatu kwa sababu zifuatazo; kwanza hatujiamini na hatuamini tuombacho. Pili, uhusiano wetu na Mungu ni wamashaka. Mungu wetu kwa mtazamo huu, ni yule ambaye, "labda inawezekana." Tatu, Hatuna utulivu wa ndani katika kuomba. Tunamuharakisha Mungu atende tunavyotaka. Hatumpi nafanya kutenda apendavyo na ifaavyo kwetu. Tunajilinganisha naye na kusahau kuwa sisi na yale tunayoomba ni mali yake na yanawezekana kwa uwezo wake.

Malkia Esta katika sala yake anatambua kabisa nje ya Mungu hakuna lolote na yeye si lolote. Esta anajisalimisha na kujiachia hivi, "Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe;  maana hatari yangu imo mikononi mwangu." Est 14:4

Kutawanya mawazo katika sala ni tatizo lingine la walio wengi. Mfano unamwomba Mungu akuwezeshe kununua gari, huku ukiwa na mashaka kama hilo gari litakuwa na "spare tyre,"-tairi la akiba.

Ndugu yangu, sala ya kujiachia ni kutotia shaka kabisa, na kumwambia Mungu atende kwa kadiri impendezavyo Yeye. Itakuwa vigumu kufaidi minofu ya nyanya ukiwa na kisu butu. Sala kama kisu, kinapaswa kuwa kikali ili kitimize kazi yake kama kisu. Ikiwa ndivyo sivyo, hatuwezi kupata yale tuombayo kama Mtume Yakobo anaposema, "hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu." Yak 4:3. Uimara huu wa sala wenye kubeba nia nzuri tunajifunza kutoka sala ya Malkia Esta. Naye anasali hivi, “Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuze moyo wake apate kumchukia Yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye,” Est 14:13.

Somo la Injili linatupa uhakikisho wa yale tuombayo, tutafutayo na tuyasalimishayo kwa Mungu. Uhakikisho huu wa kuyapata haya tuombayo ni pale tu tunapojiachia kwake. Hapa yatupasa kwenda zaidi ndani. Je, kuomba, kutafuta, na kujisalimisha/kubisha hodi katika sala kuna maanisha nini?

Wengi wetu katika jambo hili tunashindwa mara zote kufahamu maana yake. Mungu kamwe habariki utupu licha ya kwamba uwezo huo anao. Labda ni kukumbushe tu mifano miwili. Mfano wa kwanza ni muujiza wa kwanza kule Kana. Yesu anabadili maji kuwa divai (Yoh 2: 1-11). Kabla ya muujiza huu Yesu anawaambia, "jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu." Yoh 2:7. Kuna maanisha nini? Je, isingetosha Yesu kuinua mikono yake juu na mapipa ya divai kutondoka?

Muujiza mwingini ni ule wa mikate ambapo watu walikula mikate na samaki hadi wakasaza makapu 12. Kabla ya kufanya muujiza huu, Yesu anawauliza wanafunzi wake, "Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili," Mk 6:38. Kwa nini Yesu awaulize swali hili? Isingetosha kuinua tu mikono na mikate na samaki kudondoka kama mvua ya mawe?

Ndugu yangu, huku ndiko Yesu anapomaanisha, "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa." Mt 7:8

Ukweli ni kwamba Mungu habariki utupu. Yatupasa kufanya kitu. Hubariki yale tujitahidiyo kufanya na yale ambayo tuna malengo mathubuti nayo.

Haiwezekani kushinda shindano la Coca-cola ikiwa wewe ni mpenzi wa pepsi cola. Hata ungekesha kusali mwaka mzima utatoka pakavu. Yakupasa kunywa soda ya Coca-Cola ili upate fursa ya kubandua visoda vyake, ikiwa ni njia mojawapo ya kushinda shindano hilo. Unapoweka sala kwenye tendo hilo utakuwa umeshafanya yote matatu; kuomba, kutafuta na kubisha hodi/kujisalimisha. Hapa hakika baraka utapata kwani huku ndiko kujiachia. Na Yeye atakupa kadiri aonavyo inafaa. Kwani, "maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?" Lk 11:11

Pamoja na kujiachia katika sala kwa mtindo niliusema, yakupasa kufanya mambo makuu manne wakati Mungu anapoonekana kuwa mbali. Mambo hayo ni haya yafuatayo; mwambie Mungu ukweli unavyohisi, angalia zaidi Mungu ni nani, yaani asili yake isiyobadilika [wema na upendo wa Mungu, Mungu mwenye nguvu zote, Mungu ajuaye kila kitu katika maisha, Mungu mtawala wa kila kitu, Mungu ayeokoa], mwamini Mungu katika kutunza ahadi zake, na kumbuka yale Mungu ameshakutendea. Katika mambo haya manne, leo tutafakari hili la nne, “kumbuka yale Mungu ameshakutendea,” na haya matatu tutayatafakari kwa undani wakati mwingine.

Ndugu yangu, kama Mungu hajakufanyia chochote kamwe, bado anastahili sifa zako daima maisha yako yote kwa sababu ya alichokifanya Yesu msalabani. MWANA WA MUNGU ALIKUFIA! Hii ni sababu kubwa ya kuabudu. Kwa bahati mbaya, tunasahau mambo magumu ya kina ya sadaka ya maumivu makali aliyoitoa Mungu badala yetu. Mazoea huleta kutosheka. Hata kabla ya kusulubiwa kwake, Mwana wa Mungu alivuliwa nguo, akapigwa vibaya sana, akadhihakiwa na kuchekwa, akavikwa taji ya miiba, na akatemewa mate. Alidhalilishwa na kudhihakiwa na watu waovu,  akatendwa vibaya kuliko mnyama.

Kisha, akiwa karibu kuzimia kwa sababu ya kupoteza damu nyingi, alilazimishwa kubeba msalaba kwenda mlimani-[Golgotha-fuvu la kichwa(Mt 27:33, Mk 15:22, Lk 23:33, na Yoh 19:17)], alipigwa misumari juu yake, na aliachwa afe pole pole, kifo cha mateso ya kusulubishwa. Damu yake ya uhai ilipomwagika, watu wenye maudhi walisimama na kumtukana huku wakimpa changamoto ya kuhoji uhusiano wake na Mungu.

Akisha Yesu kuchukua dhambi ya binadamu na hukumu yake, Mungu alitazama pembeni mwa sehemu hiyo ovu, na Yesu alilia katika hali ya kulemewa sana, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Yesu angeweza kujiokoa mwenyewe lakini asingekuwa amekuokoa wala kuniokoa.

Maneno hayatoshi kueleza giza la wakati huo. Kwa nini Mungu aliruhusu na kuvumilia mateso maovu kiasi hicho. Kwa nini? Mungu aliyaruhusu na kuyafanya hayo yote ili wewe na mimi tuweze kuokolewa na kuzimu ya milele! Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye,” 2Kor 5:21. Yesu aliacha vyote ili wewe na mimi tupate vyote. Alikufa ili wewe na mimi tuishi milele. Jambo hilo tu linatosha kukufanya umshukuru na kumsifu daima. Usijiulize kamwe jambo la kushukuru.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka?” Mt 7:9-10


Ee Yesu tujalie sala ya utakatifu kwa kwa yale tukuombayo na utupe kadiri ya hitaji letu. Amina 

No hay comentarios:

Publicar un comentario