JUMATANO
WIKI YA 3 YA KWARESMA
Somo:
Kumb 4:1, 5-9
Zab:
148:12.13, 15-16, 19-20
Injili:
Mt 5:17-19
Nukuu:
“Na sasa, ee Israeli,
zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende, mpate kuishi na
kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu,” Kumb 4:1
“Msidhani ya kuwa
nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt
5:17
TAFAKARI:
“Sheria
ya Bwana ni kamilifu, nayo ni uhai wetu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo na tutafakari “sheria ya Bwana na ukamilifu wake.” Sheria ya Bwana ni
utaratibu wa kuyaishi yale yampendezayo Mungu, na kuwa na mahusiano mazuri naye
kwani Yeye ndiye uhai na uzima wetu. Wana wa Israeli walipewa sheria kama
mwongozo wa kutenda na kuwa na mahusiano mazuri na Mungu. “Bwana akamwambia Musa,
Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile
sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe,” Kut 24:12. Sheria hizi
zilipaswa kufuatwa kiaminifu na bila kuzichakachua. “Mioyo yenu na iwe kamili
kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake,
kama ilivyo leo.” 1Fal 8:61.
Ukamilifu na uaminifu
wa mtu ulipatikana katika kuzishika sheria za Bwana. Kwa sababu, “sheria ya
Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga
hekima.” Zab 19:7. Hivi ndivyo ilivyopaswa kuzishika sheria za Bwana. Na hilo
ndilo lililokuwa kusudi la sheria. Jambo la kushangaza wakati wa Yesu, Wayahudi
hawakuwa wanafuata Torati kama iliyokuwa mwanzo, yaani, nyakati za Musa.
Wayahudi walikuwa wanafuata tafsiri ya Torati ambayo iliendana na matamanio yao
na siyo ya Mungu. Huu ndio ugomvi uliokuwepo kati ya Yesu na Waandishi na
Mafarisayo.
Jambo muhimu sana la
kujua ni kwamba kipindi cha Yesu, Wayahudi na hasa mafarisayo na waandishi
hawakuwa wanaifuata Torati kama iliyokuwa, ila tafsiri yake (maisha ya dini na
matendo yake kupitia masimulizi), iliyojulikana kwa ujumla kama TALMUD. Talmud
ilibeba mambo mawili: MIDRASH (tafsiri ya mambo mbalimbali toka Torati), na
MISHNAH (marudio/waliyorudia au mafundisho)
Kwa mantiki hiyo hapo
juu ya TALMUD, vitabu vile vitano vya Torati vingewezwa kuandikwa kwa kurasa
350 tu; wakati TALMUD ilichukuwa hadi vitabu 523; vilivyo rudufiwa (printed)
katika mabando (volumes) 22. Haya ndiyo yanayonukuliwa na mafarisayo na waandishi
kama mapokeo ya wazee. Sehemu nyingi za mafundisho ya Yesu anapinga jambo hili
la kufuata mapokeo ambayo ni tafsiri kutoka Torati, (Mt 15:2-3, 6; Mk 7:3, 5,
8, 9, 13). Naye Yesu anawaambia, “Ninyi mwaiacha amri
ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu,” Mk 7:8. Mapokea haya ni
ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Mtume Paulo baada ya kuongoka na kuujua ukweli
kuhusu sheria ya Bwana anawaambia Wakolosai, “Angalieni
mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya
mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa
jinsi ya Kristo,” Kol 2:8. Ukweli ni kwamba, Mtume Paulo kama Mfarisayo kabla
ya kuongoka kwake aliyafuata mapokea haya ya wazee ambayo yalikuwa ni ‘ukweli
wa Mungu uliopotoshwa.’ Paulo anakiri jambo hili na kusema, “Nami
naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika
kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu,” Gal
1:14.
Kwenye jambo hili,
yaani kweli ya Sheria ya Bwana, Yesu anawakemea Mafarisayo na Waandishi na
kusema, “Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja
kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17. Hapa Yesu akubaliani nao kwa swala la
kuichakachua Torati kama walivyokwisha kufanya. Yesu anarudisha mpango mzima wa
Mungu katika safari nzima ya ukombozi wa mwanadamu. Yesu anatoa zaidi maana ya
sheria na ushikaji wa sheria hiyo. Yesu anawakosoa Mafarisayo kwa unafiki wao
katika sheria na kusema, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa
mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria,
yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine
msiyaache,” Mt 23:23
Utimilifu wa sheria
kadiri ya mpango mzima na mtazamo wa Yesu umebebwa katika upendo. Hii ndiyo
amri mpya. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi
mpendane vivyo hivyo,” Yoh 13:34. Mtakatifu Agustino anatuambia kwamba,
“ukipenda utafanya yote.” Ni katika mantiki hii kwamba, “mkipenda, mtazishika
amri zangu,” Yoh 14:15. Ndugu yangu, ukiona viongozi wetu serikalini au kwenye
taasisi yoyote ile wanang’ang’ana kubadili katiba kwa matamanio yao na vyama
vyao bila kujali maslahi ya wengi, ni wazi kabisa mwisho wake ni upotoshaji wa
kweli na kwenda kinyume na mpango wa Mungu kupitia watu wake.
Katika kweli hili
niliyosema kuhusu ung’ang’anizi wa kubadili mambo kadiri ya matamanio ya
wachache, bado tunao Mafarisayo na Waandishi katika jamii yetu kama ilivyokuwa
nyakati za Yesu. Leo tuna mkwamo mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar kwa sababu
tu ya wachache wenye kutanguliza matamanio yao ya kuenzi umilele katika
‘utawala’ bila hofu ya Mungu. Hiki ni kitu kisichowezekana hata kidogo. Katiba
haitafsiriwi kama ilivyo, bali inapewa tafsiri kadiri ya matamanio ya wachache
ili kukidhi tamaa na makusudi yao huku wengi wakiteseka pasipo sababu za
msingi. Yatupasa kila mmoja wetu kadiri ya Imani na itikadi zake aone hili ni
tatizo kubwa na linahitaji kutatuliwa haraka. Katiba ndio msahafu wetu sote
bila kujali Dini, Imani, na itikadi zetu. Katiba haipaswi kuhodhiwa na Chama
chochote kile cha siasa. Tukifanya hivyo tu, tujiandae kwa machafuko makubwa.
Ndugu yangu, nawe uliye
Mkristo, Ukristo wetu bila UPENDO wa kweli ni Ukristo MFU. Kwa Mkristo kuwa na
upendo wa dhati ni kuzishika amri za Mungu katika ukamilifu wake. “Yeye aliye
na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa
na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake,” Yoh 14:21. Na kukaa
katika pendo la Mungu ni kuzishika amri zake. “Mkizishika amri zangu, mtakaa
katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa
katika pendo lake,” Yoh 15:10
Ndugu yangu, ni wakati
wa kijitazama, na hasa tukianzia kwenye familia zetu, Jumuiya zetu ndogondogo
za Kikristo, na za kitawa, na dhamana tuliyopewa na umma kama viongozi kuishi
katika kweli na haki. Huwezi kutenda kweli na haki kama huwapendi wale unao
waongoza. Mwenye nafasi hii ya uongozi bila upendo kwa watu wake, ni rahisi
sana kusukumwa na ubinafsi wake, na matamanio ya wachache wasio na uchungu na
mateso ya wengi. Je, kama
kiongozi waishi upendo wa kweli na haki? Mt. Yohane wa Msalaba anasema hivi,
“When evening comes, you will be examined in love. Learn to love, as God
desires to be loved and abandon your own ways of acting.” Kunapokuwa na upendo
wa kweli, sheria ufanya kazi dogo sana, na wakati mwingine sheria hiyo hutoweka
kabisa.
Upendo wa kweli utusukuma kufanya zaidi ya yale
yanayohainishwa na sheria husika. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa
mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Huu ndio mfano wa
kuigwa kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tupendane! “The soul that walks in
love neither tires others nor grows tired,” Mt. Yohane wa Msalaba.
Tumsifu Yesu Kristo
“Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua
Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiza,” Mt 5:17
Ee Yesu, nijalie
Upendo wa kweli na kukuona kwa kila mmoja ninayekutana naye katika maisha yangu.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario